Kusindikizwa na kuzikwa Fatima (a.s)

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na kusindikizwa na kuzikwa Bibi Fatima Zahra (a.s). Ili kujua juu ya matukio yanayohusiana angalia makala ya Mahali alipozikwa Bibi Fatima (a.s) na Kufariki kishahidi kwa bibi Fatima (s.a).

Kusindikizwa na kuzikwa Bibi Fatima (Kiarabu: تشييع السيدة فاطمة الزهراء (ع) ودفنها) kunaashiria kusindikizwa na kuzikwa binti huyu wa Mtume usiku na kwa siri katika mwaka wa 11 Hijiria. Fatima (a.s) aliusia kwamba, hataki watu waliomdhulumu Fadak, waliomuudhi na kupora ukhalifa akiwemo Abu Bakr bin Abi Quhafa na Omar bin al-Khattan wausalie mwili wake na kuhudhuria mazishi yake. Kwa hiyo, aliusia mazishi yake yafanyike kwa siri, na mahali pa kaburi lake pia pawe ni sehemu ya siri na pasipojulikana. Wasia huu ni ishara ya kutoridhia na kuonyesha upinzani kwa Khalifa na matukio yaliyotokea baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w).

Mwili wa Fatima ulisindikizwa na kuzikwa na watu wachache kama vile Imam Ali (a.s), Hassanein (Hassan na Hussein), Aqil bin Abi Talib, Abbas bin Abdul Muttalib, Ammar Yasir, Miqdad bin Aswad, Zubair bin Awam, Abu Dhar al-Ghiffari na Salman Farsi na bila ya Abu Bakr na Omar. Mahali alipozikwa Bibi Fatima (a.s) hapafahamiki. Baada ya watu kufahamu kwamba, Fatima amezikwa usiku, Omar bin al-Khattab alichukua uamuzi wa kufukua makaburi ili amswalie Sala ya maiti Bibi Fatima; lakini alilazimika kuachana na uamuzi huo baada ya tishio la Imamu Ali (a.s).

Kufa shahidi Bibi Fatima (a.s)

Makala asili: Kufariki kishahidi kwa bibi Fatima (s.a)

Fatima (a.s), binti ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alifariki dunia mwaka wa 11 Hijiria baada ya muda mfupi wa ugonjwa uliotokana na majeraha ya kimwili yaliyosababishwa na matukio ya baada ya kifo cha Mtume. [2] Kuhusu tarehe ya kufa kwake shahidi kuna hitilafu baina ya wanahistoria ambapo inaelezwa kuwa ni siku arubaini na miezi minane baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). [3] Siku 95 baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) [4] yaani tarehe 3 Jumadi al-Thani [5] inatambulika kuwa kauli maarufu zaidi kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia [6] na siku 75 baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) yaani 13 Jumadi al-Awwal [7] ni miongoni mwa nukuu nyinginezo.

Kukusanyika watu kwa ajili ya kusindikiza mwili wa Fatima

Bibi Fatima alifariki dunia baada ya kuzama kwa jua. [8] Kwa mujibu wa kitabu cha Fattal Nishabouri, watu wa Madina walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (a.s) na wakangojea kuuswalia mwili wake. Lakini Abu Dharr aliwaendea watu na kuwatangazia kwamba mazishi ya binti ya Mtume yameakhirishwa na watu wakatawanyika. [9]

Abbas bin AbdulMutalib, ami yake Mtume (s.a.w.w) alimtaka Imamu Ali (a.s) awakusanye Muhajirina na Ansari kwa ajili ya mazishi na Sala ya maiti, kwani hili ni jambo zuri kwa dini. Kwa kujibu Imam Ali (a.s) alisema kwamba, hawezi kufuata ushauri wake, kwa sababu Fatima (a.s) aliacha wasia kwamba Sala yake na mazishi yake yawe ya siri. [10] Kwa mujibu wa nukuu ya Salim bin Qays, katika usiku wa kuaga dunia Bibi Fatima, walimuomba Imam Ali (a.s) asiwatangulie kuswalia maiti ya Fatima (a.s). [11]

Kumuosha, kumkafini na kumsalia

Fatima (a.s) aliusia kwamba mumewe Imamu Ali (a.s) amuoshe. [13] Pia alimuomba Asma bint Umais amsaidie Imam Ali (a.s) katika kuuosha mwili wake. [14] Imam Ali na Asma walimuosha Fatima kwa mujibu wa wasia wake [15] na kumvisha sanda (kumkafini). [16]

Hussein bin Abdul Wahhab katika kitabu cha Uyun al-Mu’jizat [17] na Muhammad bin Jarir Tabari katika kitabu cha Dalail al-Imamah, [18] mmoja wa wanazuoni wa Kishia katika karne ya tano Hijiria, wamenukuu kwamba Imam Ali (a.s) pekee akiwa pamoja na Imamu Hassan (a.s) na Imamu Hussein (a.s) ndio waliouswalia mwili wa Fatima (s.a.w.w). Katika baadhi ya vyanzo, idadi ya washiriki wametajwa kuwa ni zaidi, kama vile Fattal Nishabouri, mwanachuoni wa Kishia wa karne ya tano na sita Hijiria, katika Rawdhat al-Waidhin, [19] na Fadhl bin Hassan Tabarsi, mwanazuoni wa karne ya sita, katika kitabu cha I’lam Al-Waraa [20] amenukuu kwamba, Imam Ali (a.s) na Hasnain (a.s), Aqeel kaka yake Imam Ali (a.s), Ammar, Miqdad, Zubair, Abu Dharr, Salman, Buraydah bin Husayb na baadhi ya Bani Hashim pia waliuswalia mwili wa Fatima (a.s) na wakamzika. Allama Majlisi amesimulia riwaya katika Bihar al-Anwar kwamba, watu waliokuwepo kwenye shughuli ya kumzika Fatima (a.s) walikuwa Salman Farsi, Miqdad, Abu Dhar Ghafari, Abdullah bin Masoud, Abbas bin Abdul Muttalib na Zubair bin Awam. [21] Imeelezwa katika kitabu cha Salim bin Qays kwamba, Abbas, ami yake Mtume, alikuwa ndiye mwenye kusalisha Sala ya maiti ya Fatima (a.s). [22]

Sababu ya kutowajulisha watu

Sababu ya kufanyika kwa siri mazishi ya Fatima (a.s) ni wasi wake; kwa mujibu wa riwaya ya Fattal Nishabouri, Fatima (a.s) alimuusia Imam Ali (a.s) kwamba, hakuna hata mtu mmoja katika watu waliomdhulumu na kumnyang'anya haki yake anayepaswa kumsalia na kushiriki katika mazishi yake [23]. Kadhalika aliusia kwamba, azikwe katika usiku wa giza wakati watu watakapokuwa wamelala. [24]

Sheikh Saduq pia amenukuu kwamba Imam Ali (a.s) alipoulizwa sababu ya kumzika Fatima (a.s) kwa siri wakati wa usiku, Imam alijibu: Fatima alikuwa na hasira na kundi fulani la watu na hakupenda washiriki katika mazishi yake. [25] Ibn Qutaybah Dinawari, mwanachuoni na mtaalamu wa hadithi wa Kisunni katika karne ya tatu ya Hijiria, pia alinukuu kwamba, Fatima aliusia azikwe usiku ili Abu Bakr asihudhurie mazishi yake. [26]

Mazishi

Makala asili: Mahali alipozikwa Bibi Fatima (a.s)

Katika kitabu cha Tarikh Yaqoubi, miongoni mwa vyanzo vya kihistoria vya karne ya tatu, imeelezwa kwamba mwili wa Fatima (a.s) ulizikwa usiku, na ni Salman, Abu Dhar na Miqdad pekee nduio waliohudhuria mazishi hayo. [29] Ibn Shahrashub amenukuu katika kitabu chake cha Manaqir hadith Mursal (hadithi ambayo ndani yake hakujatajwa jina la mpokezi katika sanadi na mapokezi ya hadithi) kwamba, wakati Imamu Ali (a.s) alipouleta mwili wa Fatima jirani na kaburi, ulitoka nje mkono kutoka kaburini na kupokea mwili wa Fatima na kisha ukapotea. [30] Baada ya Imamu Ali (a.s) kumzika Fatima alipoteza athari za kaburi hilo ili lisifahamike. [31]

Kumenukuliwa hadithi na nukuu mbalimbali husiana na mahali alipozikwa Bibi Fatima (a.s). [32] Miongoni mwazo:

Matukio ya baada ya kuzikwa Fatima

Kadhalika angalia: Kujenga makaburi kwa ajili ya kuficha kaburi la Fatima (a.s)

Ili kuficha kaburi la Fatima (a.s) na kulizuia lisipatikane, sambamba na kuharibu athari za kaburi hilo Imam Ali (a.s) alitengeneza makaburi saba [40] na, kwa kauli na nukuu nyingine alitengeneza makaburi arobaini [41]

Imeelezwa katika kitabu cha Salim bin Qays, kwamba asubuhi baada ya kuzikwa kwa Fatimah (a.s), Abu Bakr na Umar bin Khattab, pamoja na watu walikwenda kumswalia maiti, na Miqdad akawaambia kwamba walikuwa wamezika maiti jana usiku. [42]

Watu walipopata habari ya kuzikwa kwa Fatimah (a.s) walisikitika na kulaumiana kwa kushindwa kuhudhuria mazishi na kumswalia mtoto wa pekee wa Mtume (s.a.w.w). Kwa mujibu wa nukuu ya Salim bin Qays, baada ya Omar kupata habari ya kusaliwa na kuzikwa siri Fatima alimwambia Abu Bakr: Nilikwambia kwamba watafanya hivi.” [44] Omar pia alibishana na Abbas bin Abd al-Muttalib na akawashutumu Bani Hashim kwa husuda. Abbas pia alilichukulia hili kuwa ni wasia wa Fatima na akasema kwamba aliacha wasia kwamba ninyi wawili msimswalie yeye. [45]

Kwa mujibu wa kile kilichotajwa katika Bihar al-Anwar, Omar bin Khattab alisema, “waleteni baadhi ya wanawake wa Kiislamu wafukue makaburi haya na watafute mwili wa Fatima, ili tuuswalie na kuuzika tena na kulizuru kaburi lake. [46] Habari hizi zilipomfikia Imam Ali (a.s) alikasirika sana na akachukua upanga wake na akaenda Baqi’ [47] na baada ya kupamba moto mabishano baina yake na Omar, [48] alimwambia Omar: Kama nikitoa upanga wangu kutoka kwenye ala yake, sitairudisha isipokuwa nimekuua. [49] Vile vile aliwaambia watu waliotaka kuyafukua makaburi hayo kwamba mtu yeyote akihamisha jiwe moja kutoka kwenye makaburi haya, atamuua. [50] Baada ya tishio hilo Omar aliachana uamuzi wake. [51] Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, baada ya mazungumzo hayo, Abu Bakr alimtuliza Imam Ali (a.s) kwa kusema kwamba, yeye hatafanya jambo lolote ambalo Ali (a.s) halipendi. [52]

Vyanzo

  • Fattāl al-Nayshābūrī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Rawḍat al-wāʿiẓīn wa baṣīrat al-muttaʿzīn. 1st edition. Qom: Intishārāt-i al-Raḍī, 1375 Sh.
  • Hilālī, Sulaym b. Qays. Kitāb Sulaym b. Qays al-Hilālī. Edited by Muḥammad Anṣārī Zanjānī. 1st edition. Qom: Al-Ḥadī Publication, 1405 AH.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad. Al-Ṭabaqāt al-kabīr. Edited by ʿAbd al-Qādir Aḥmad ʿAṭā. 1st edition. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1410 AH/1990.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. 1st edition. Qom: Intishārāt-i ʿAllāma, 1379 AH.
  • Ibn ʿAbd al-Wahhāb, Ḥusayn. ʿUyūn al-muʿjizāt. 1st edition. Qom: Maktabat al-Dāwarī, [n.d].
  • Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allāh b. Muslim . Taʾwīl mukhtalaf al-ḥadīth. [n.p]: Al-Ishrāq, 1999.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. 4th edition. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Nahj al-balāgha. Translated to Farsi by ʿAbd al-Muḥammad Āyatī. Tehran: Nashr wa Pazhūhish Farzān Rūz, 1377 Sh.
  • Najmī, Muḥammad Ṣādiq. Qabr Fāṭima (a) yā qabr Fāṭima bnt. Asad (The grave of Fatima (a) or the grave of Fatima bnt. Asad). Miqāt-i Haj Journal. No 7, Spring 1373 Sh.
  • Majmūʿa āthār-i ustād Riḍā Badr al-Samāʾ barāyi Ḥaḍrat-i Fāṭima Zahrā (a) (Collection of works by Rida Badr al-Samaʾ for Lady Fatima al-Zahra (a)). Rahyāfta Website. Accessed: 2022/5/21.
  • Shubayrī, Sayyid Muḥammad Jawād. Shahādat-i Fāṭima (a), Dānishnāma-yi Fāṭimī. volume 1. 1st edition. Tehran: Pazhūhishgāh-i Farhang wa Andīsha-yi Islāmī, 1393 Sh.
  • Shahīdī, Sayyid Jaʿfar. Zindigānī-yi Fāṭima Zahrā (a). Tehran: Daftar-i Nashr-i Farhang Islāmī, 1363 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Amālī. 5th edition. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī, 1400 AH.
  • Ṭūsī, Muḥamamd b. al-Ḥasan al-. Miṣbāḥ al-mutahajjid wa silāḥ al-mutaʿabbid. 1st edition. Beirut: Muʾassisat Fiqh al-Shīʿa, 1411 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Amālī. 1st edition. Qom: Dār al-Thiqāfa, 1414 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Iʿlām al-warā bi-aʿlām al-hudā. 1st edition. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1417 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Dalāʾil al-imāma. 1st edition. Qom: Nashr-i Biʿthat, 1413 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-.Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abu l-faḍl Ibrāhīm. 2nd edition. Beirut: Dar al-Turāth, 1387 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. 1st edition. Beirut: Dār Ṣādir, [n.d].