Kumlilia Hussein (a.s)

Kutoka wikishia
Kulia katika maombolezo ya Imamu Hussein (a.s)

Kumlilia Hussein (a.s) (Kiarabu: البكاء على الحسين (ع)) ni kulia kutokana na kudhulumiwa na masaibu yaliyomkumba Hussein bin Ali (a.s) pamoja na masahaba zake katika jangwa la Karbala. Katika hadithi za Maimamu (a.s) kumlilia Imamu Hussein (a.s) kumetiliwa mkazo na kufanya hivi kuna ujira na thawabu kama vile kusamehewa dhambi na kuingizwa peponi. Imenukuliwa pia katika baadhi ya hadithi ya kwamba, malaika na Mitume pia walilia kwa ajili ya msiba na masaibu yaliyompata mjukuu wa Mtume Imamu Hussein (a.s).

Wanazuoni wa Kishia wametambua sababu ya kusisitizwa kumlilia Imamu Hussein ni kuhakikisha kwamba, fikra na harakati ya kupigania uhuru na kupinga dhulma daima inabakia kuwa hai. Pia, manufaa yake ni kuonyeshwa huba na mapenzi kwa Imamu Hussein na kujadidisha baia na utii kwake pamoja na malengo yake, ikiwa ni pamoja na kutafuta kifo cha kuuawa shahidi, na hili linahesabiwa kuwa ndiyo sababu ya kuendelea kuwepo kwa Uislamu.

Fadhila za kumlilia Hussein

Kumlilia Hussein (a.s) ni kulia kutokana na kudhulumiwa na masaibu yaliyomkumba Hussein bin Ali (a.s) pamoja na masahaba zake katika tukio la Karbala. [1] Kumenukuliwa hadithi nyingi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s) zinazohusiana na fadhila za kumlilia Imamu Hussein (a.s) ambamo ndani yake kumesisitizwa juu ya kulia kwa ajili ya msiba na masaibu ya Imamu Hussein (a.s) [2] na kwamba, kufanya hivyo kuna ujira na thawabu nyingi. [3]

Sheikh Saduq, mmoja wa wataalamu wa elimu ya hadithi wa Kishia amenukuu kutoka kwa Rayyan bin Shabib kwamba, alikwenda kwa Imamu Ridha (a.s) mwanazuoni mwa Muharram ambapo sambamba na kumkumbusha kuhusiana na masaibu ya babu yake alimwambia:


((یَا ابْنَ شَبِیبٍ إِنْ کُنْتَ بَاکِیاً لِشَیْءٍ فَابْکِ لِلْحُسَیْنِ بْنِ عَلِیِّ بْنِ أَبِی طَالِبٍ(ع)


فَإِنَّهُ ذُبِحَ کَمَا یُذْبَحُ الْکَبْشُ وَ قُتِلَ مَعَهُ مِنْ أَهْلِ بَیْتِهِ ثَمَانِیَةَ عَشَرَ رَجُلًا مَا لَهُمْ فِی الْأَرْضِ شَبِیهُون‏


Ewe mwana wa Shabib! Ukitaka kulia kwa ajili ya jambo fulani, basi lia kwa ajili ya Hussein bin Ali bin Abi Talib (a.s), kwani kwa hakika ameuawa kwa kuchinjwa kama anavyochinjwa kondoo na ameuawa shahidi pamoja naye watu 18 wa familia yake ambao hawakuwa na mfano wao katika ardhi.

Aidha alimwambia: Ewe mwana wa Shabib! Kama utalia kwa ajili ya Hussein (a.s) na machozi yako yakatiririka katika mashavu yako, Mwenyezi Mungu atakusamehe dhambi zako ziwe ndogo, au kubwa, kidogo au nyingi.” [4]

Imenukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) ya kwamba amesema, Ali bin Hussein (a.s) alilia kwa ajili ya msiba wa baba yake kwa muda wa miaka 20 na kila wakati alipokuwa akiwekewa chakula mbele yake alikuwa akilia. [5] Imekuja katika baadhi ya hadithi ya kwamba, malaika, Mitume, ardhi, mbingu, wanyama, majangwa na bahari vyote viliomboleza na kumlilia Hussein (a.s). [6]

Kadhalika katika kitabu cha Kamil al-Ziyarat imenukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) kwamba, machozi kwa ajili ya Imamu Hussein (a.s) hata yakiwa na ukubwa wa bawa la nzi, malipo yake yako kwa Mwenyezi Mungu na hatatosheka na chochote kidogo kwa kazi hii ghairi ya pepo. [7]

Hata sharti la kunufaika na kupata thawabu na ujira huu mkubwa ni kuwa na imani na maarifa na Imamu Hussein, malengo yake [8] na vilevile kuchunga halali na haramu za Mwenyezi Mungu. [9]

Sababu ya kusisitizwa kumlilia Imamu Hussein (as)

Murtadha Mutahhari, mmoja wa wanazuoni wa Kishia, anauzingatia msisitizo mkubwa wa Maimamu wa kumlilia Imamu Hussein kuwa ulikuwa ni kuhakikisha kwamba, maktaba (fikra) na harakati ya kupigania uhuru na kupinga dhulma daima inabakia kuwa hai. Kwa mujibu wake ni kuwa, msisitizio huu wa Maimamu ulipelekea katika zama zao harakati hii ibakie kuwa hai na kutokea mapinduzi na jina la Imamu Hussein likawa kauli mbiu dhidi ya dhulma. [10]

Pia, kulia na maombolezo kwa ajili ya Imamu Hussein na mashahidi wa Karbala ni kujadidisha baia na utii kwa harakati ya Ashura na utamaduni wa kufa shahidi na ni lishe ya kiakili na kiroho kupitia shule na njia hii, na imesemwa kwamba kilio hiki ni ishara ya mfungamano wa kimoyo na Ahlul-Bayt (a.s) na ni aina ya makubaliano na mkataba wa huba na Imamu Hussein (a.s). [11] Imamu Khomeini (ra) amekitambulisha kilio na maombolezo kwa ajili ya Imamu Hussein kuwa ni sababu ya kuhifadhiwa Uislamu. [12]

Kulia na kujiliza

Maimamu wa madhehebu ya Shia mbali na kusisitiza juu ya kulia katika maombolezo ya Imamu Hussein (a.s) wameusia pia juu ya kujiliza na wamebainisha kwamba, hilo lina ujira. Sheikh Saduq amenukuu kutoka kwa Imamu Ridha (a.s): Kila ambaye atakumbuka msiba wetu (Ahlul-Bayt), siku ambayo macho yatalia, (siku ya Kiyama) macho yake hayatalia. [13] Kadhalika imenukuliwa kutoka kwa Imam Baqir na Imamu Sadiq (a.s) kwamba: “Kila ambaye atalia katika msiba na maombolezo ya Imamu Hussein (a.s) au atamliza mwingine hata kama ni mtu mmoja, sisi tutamdhaminia pepo na kila ambaye hatalia, lakini akawa na hali ya huzuni na maombolezo, atapata ujira na malipo haya haya. [14]

Kwa mujibu wa Sheikh Abbas Qumi mmoja wa Maulamaa wa karne ya 14 Hijria ni kwamba,, makusudio ya kujiliza sio ria na kujionyesha; kwani kumlilia Imamu Hussein (a.s) ni ibada na haijuzu kufanya ria na kujionyesha katika ibada. [15] Kujiliza ni kujishabihisha na wanaolia na kuwa pamoja nao katika hilo, [16] katika hali ambayo, ria ni mtu kujionyesha kwa wengine kwamba, anafanya jambo jema. [17]