Nenda kwa yaliyomo

Islah Dhat al-Bayn

Kutoka wikishia

Makala hii inahusiana na mafuhumu ya Islah Dhat al-Bayn. Ili kujua kuhusiana na Aya yenye jina hili hili, angalia makala ya Aya ya Islah Dhat al-Bayn.

Islah Dhat al-Bayn (Kiarabu: اإصلاح ذات البين) ni kusuluhisha jambo na kuleta upatanishi na marekebisho ya uhusiano baina ya watu waliohasimiana na kugombana. Islah Dhat al-Bayn ni miongoni mwa tabia njema na fadhila za kimaadili na mkabala wake ni kutoa maneno machafu, kusengenya, kuleta mfarakano na uadui baina ya watu ambapo hii ni mifano ya wazi ya tabia mbaya na chafu za kimaadili.

Katika Aya na hadithi mbalimbali kumependekezwa mbinu na njia za kuleta upatanishi na kuhitimisha mizozo na mivutano; miongoni mwazo ni kuchaguliwa mpatanishi na muamuzi na pande mbili katika hitilafu na magomvi ya kifamilia, kuzuia kuibuka hitilafu kwa kutoa nasaha kwa njia sahihi na kuchochea huba na hisia za kidini. Inaelezwa katika mafundisho ya dini kwamba, kuwa na sifa mbaya kama ubakhili, kumfuata shetani na kupenda dunia ni miongoni mwa vikwazo na vizingiti vya kuleta upatanishi.

Utambuzi wa maana

Islah Dhat al-Bayn ni kupatanisha waliogombana na wasioelewana na kurekebisha (kuboresha) mahusiano mabaya baina ya watu au kundi, [1] uhusiano ambao umevurugika kutokana na ugomvi, mzozo, uadui, uhasama na kadhalika. [2] Neno hili limechukuliwa katika Aya ya kwanza ya Surat al-Anfal [3] ambayo inasema: …na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.

Islah Dhat al-Bayn inajumuisha kupatanisha watu wawili na makundi mawili.

Islah Dhat al-Bayn ni katika fadhila njema za kimaadili sifa ambayo iko mkabala na sifa mbaya za kimaadili kama kutoa maneno machafu, kusengenya, kuleta mfarakano na uadui baina ya watu. [4]

Umuhimu na nafasi

Qur’ani Tukufu imetaja na kuzungumzia katika Aya kadhaa suala la kuleta suluhu na upatanishi na imeagiza na kutoa amri ya kufanywa hilo. [5] Kadhalika Imamu Ali (a.s) katika wasia wake kwa Hassan na Hussein (a.s) aliwataka wafanye islah dhat al-bayn. [6] Kadhalika kwa mujibu wa Aya za Qur’an watu ambao wanafanya suhulku na upatanishi baina ya watu wamo katika rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu. [7] Katika baadhi ya hadithi suala la kuleta upatanishi na maelewano baina ya watu limetajwa kuwa bora zaidi na lenye fadhila kuliko Sala, Saumu, [8] na sadaka. [9] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi mtu ambaye anachukua hatua ya kuleta upatanishi baina ya watu wawili anaswaliwa na Mailaka na Mwenyezi Mungu anampa ujira na thawabu za Laylatul-Qadr (usiku mteule na wenye heshima). [10]

Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ni kwamba, inajuzu kusema uwongo kwa ajili ya kuleta upatanishi baina ya watu. Kadhalika Qur’ani Tukufu imeruhusu minong’ono [11] (najwa) kwa ajili ya kuleta suluhu na upatanishi. [12] Pamoja na hayo katika sehemu nyingine hilo linatambuliwa kuwa ni amali ya shetani. [13] [14]. Qur’ani tukufu haitambui kiapo kinachotolewa kwa ajili ya kuacha kuleta suluhu baina ya watu. [15]

Kwa mujibu wa hadithi Mufadhal bin Omar alikuwa na kiwango fulani cha fedha kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) na akaitumia kwa ajili ya kuleta upatanishi baina ya Mashia. Kwa mfano, alitumia fedha hizo kwa ajili ya kuondoa hitilafu baina ya Abu Hanifa Sabiq al-Hajj na mkwewe. [16]

Mikakati na vizingiti

Kuna mbinu na mikakati ambayo imebainisha kwa ajili ya kuleta suluhu na upatanishi baina ya watu:

  • Kuzuia kutokea hitilafu: Kwa mujibu wa rai ya wafasiri, kuzuia kutokea hitilafu na mivutano baina ya warithi ni madhumuni ya Aya ya 182 ya Surat al-Baqarah [17] ambapo ni lazima anayeusia achunge uadilifu na kutolewa maagizo ya kutekelezwa majukumu ili kuzuia wasia ambao unapelekea kutokea hitilafu. [18]
  • Kuchaguliwa muamuzi upande wa jamaa za mke na upande wa jamaa za mume katika hitilafu za kifamilia: Ili kutatua mizozo na mivutano ya kifamilia endapo kutatokea wasiwasi na woga wa uwezekano wa kuchana mume na mke inapendekezwa kuchagua muamuzi kutokana na jamaa za mume na muamuzi kutokana na jamaa za mke kwa ajili ya kuleta upatanishi na maridhiano. [19]

Kutafuta mzizi wa hitilafu, kutumia masuala ya hisia za kihuba, kuwa na subira na kujiepusha na kupendelea upande wowote ni katika mbinu na mikakati ya kuleta suluhu na upatanishi baina ya watu wawili au makundi mawili. [20] Usengenyaji na kuzusha mifarakano ni miongoni mwa sababu muhimu za kusambaratika suluhu na mapatano baina ya watu na mbinu na mikakati ya kukabiliana na hilo ni kutuomuamini mzushaji na mbea na kumfukuza. [21]

Hatua na mbinu

Kuondoa hitilafu baina ya watu ni jukumu la utawala na waumini. Imekuja katika kitabu cha Tafsir Nemooneh kwamba, endapo upatanishi na usuhishaji utafanyika kupitia njia ya mazungumzo, hauhitajii mtawala wa kisheria (Haakim Shari’) lakini kama hilo litahitajia vitendo, ni lazima kupata idhini kutoka kwa mtawala wa kisheria. [22] Kadhalika Aya ya 9 ya Surat al-Hujuraat inasema: Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki.Kwa mujibu wa Aya hii ni kwamba, katika hatua ya awali inapaswa kutumika njia ya nasaha na kulingania Qur’ani na hukumu ya Mwenyezi Mungu wakati wa kuleta maridhiano na upatanishi baina yao. Lakini kama kundi mojawapo litakataa pendekezo la upatanishi basi ni lazima kupigana nalo mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. [23]

Vizingiti

Katika vitabu vya tafsiri kumetambulishwa masuala kama kumfuata shetani, [24], kuipenda dunia [25] na ubakhili [26] kama vizingiti vya islah Dhat al-Bayn.

Hukumu za kifiq’h

Chini ya anuani ya kuleta upatanishi mafakihi wamebainisha matawi kadhaa na hukumu za kifiq’h:

  • Ni mustahabu kuleta suluhu na upatanishi baina ya watu wawili au watu kadhaa ambao wana hasama na chuki baina yao na ni wajibu inapotokea kwamba, kuna suala la kulinda roho ya muumini kupitia upatanishi huo. [27] Ayatullah Makarim Shirazi mmoja wa Marajii wa Kishia anasema: Kupatanisha makundi mawili ya Waislamu ambayo yana uadui baina yao ni wajib kifai. [28]
  • Inajuzu kutumia Zaka kwa ajili ya kuleta suluhu na upatanishi. [29]
  • Ni mustahabu kwa hakimu kabla ya kutoa hukumu azitake pande zinazozozana kufanya suhulu baina yao na endapo zitakataa maridhiano na mapatano basi wakati huo atoe hukumu. [30]
  • Sahib al-Jawahir anasema, ili kuleta maridhiano na upatanishi baina ya mke na mume ni wajibu kuchaguliwa muamuzi kutoka upande wa jamaa za mke na muamuzi kutoka upande wa jamaa za mume. Hata hivyo imenukuliwa katika kitabu cha Tahrir cha Allama Hilli kwamba, jambo hili ni mustahabu. [31]

Rejea


Vyanzo

  • Daylamī, Ḥasan b. Abī l-Ḥasan al-. Aʿlām al-dīn fī ṣifāt al-muʾminīn. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1408 AH.
  • Dihkhudā, ʿAlī Akbar. Lughatnāma. Tehran: Dānishgāh-i Tehran, 1377 Sh.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. al-ʿUmar al-.Al-Tafsīr al-Kabīr. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Fayḍ al-Kāshānī, Muḥammad b. al-Murtaḍā al-. Tafsīr al-Ṣāfī. Tehran: Maktabat al-Ṣadr, 1415 AH.
  • Ḥāshimī Rafsanjānī, Akbar. Tafsīr-i rāhnamā. Qom: Būstān-i Kitāb, 1386 Sh.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1409 AH.
  • Kāshif al-Ghitāʾ, Muḥammad Ḥusayn. Wajīzat al-aḥkām. Najaf: Muʾassisa Kāshif al-Ghitāʾ, 1366 AH.
  • Kulaynī, Muḥmmad b. Yaʿqub al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Ahklāq dar Qurʾān. Qom: Madrisat al-Imām ʿAlī b. Abī Ṭālib (a), 1377 Sh.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1371 Sh.
  • Mughnīya, Muḥammad Jawād al-. Tafsīr al-Kāshif, Qom: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1424 AH.
  • Najafī, Muḥammad al-Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharḥ sharāʾiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Thawāb al-aʿmāl wa ʿiqāb al-aʿmāl. Qom: Dār al-Sharīf al-Raḍī, 1406 AH.
  • Sayyid Raḍī, Muḥammad Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣaliḥ. Qom: Hijrat, 1413 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʾ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Maʾrifa, 1412 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1390 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Nāsir Khusru, 1372 Sh.
  • Ṭurayḥī, Fakhr al-Dīn b. Muḥammad al-. Majmaʿ al-baḥrayn. Tehran: Wizārat-i Farhang wa Irshād-i Islāmī, 1367 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Mabsūṭ fī fiqh al-imāmīyya. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya li Iḥyāʾ al-Āthār al-Jaʿfarīyya, 1387 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Aḥmad Ḥabīb al-ʿĀmilī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].