Nenda kwa yaliyomo

Harakati ya Zayd bin Ali

Kutoka wikishia

Harakati ya Zayd bin Ali (Kiarabu: ثورة زيد بن علي) ni uasi dhidi ya serikali ya Bani Umayya uliokuwa ukiongozwa na Zayd bin Ali bin Hussein. Mapinduzi haya yalitokea mwezi Safar (Mfunguo Tano) mwaka wa 122 Hijiria wakati wa utawala wa Hisham bin Abdul Malik, yakiambatana na kipindi cha Uimamu wa Imamu Swadiq (a.s) na kusababisha kifo cha Zayd na wengi wa masahaba zake. Imamu Sadiq (a.s) hakufuatana na Zayd katika uasi huu. Kuna hitilafu baina ya wanachuoni wa Kishia katika uchanganuzi wa sababu na tafsiri ya utendaji wa Imam wa 6 wa Shia kuhusiana na uasi huu na iwapo msimamo wa Imamu ulikuwa wa kisiasa na busara, au kwa sababu ya kutokuridhishwa kwake na uasi huo au sababu nyinginezo.

Mwanzoni, watu wengi wa mji wa Kufa na mikoa mingine walitoa kiapo cha utii kwa Zayd bin Ali na wajumbe wake; lakini watu walipofungwa katika msikiti wa Kufa, ni watu 300 tu ndio walioandamana na Harakati ya Zayd. Kama ilivyotajwa katika historia ya Tabari, Harakati ya Zayd ilianza usiku wa Jumatano ya kwanza ya mwezi Safar 122 Hijria, na katika siku ya kwanza, jeshi la Zayd lilishinda, lakini siku ya pili, baada ya wapiga mishale kuongezwa kwa gavana wa jeshi la Kufa, Jeshi la Zayd lilishindwa na Zayd bin Ali pia alijeruhiwa. Zayd aliuawa shahidi mwezi tatu Mfunguo Tano Safar mwaka huo huo.

Kwa mujibu wa vyanzo, Zayd aliasi kwa nia ya kutaka damu ya Imamu Hussein (a.s), kuamrisha mema na kukataza maovu na kuchukua ukhalifa kutoka mikononi mwa Bani Umayya. Hatua ya Hisham bin Abd al-Mali Khalifa wa Bani Umayya kumtendea vibaya Zayd mbele ya watumishi wa baraza pia kunatajwa kama moja ya motisha na msukumo wa Zayd wa kuanzisha harakati. Uasi wake umechukuliwa kama utangulizi wa kuanguka kwa serikali ya Bani Umayya. Pia, ukosefu wa uungwaji mkono wa watu wa Kufa, nguvu za kijeshi za serikali ya Bani Umayya, na mawakala wenye ushawishi wa Bani Umayya vimezingatiwa kuwa sababu za kushindwa kwa harakati ya Zayd.

Kiongozi wa Harakati

Makala kuu: Zayd bin Ali

Zayd ni mtoto wa Imamu wa nne Waislamu wa madhehebu ya Mashia. Mama yake Zayd alikuwa Ummu Walad, ambaye Mukhtar Thaqafi alimnunua kwa dirihamu 30,000 na kumpa kama zawadi Imam Sajjad (a.s.).[1] Tarehe ya kuzaliwa Zayd haifahamiki kwa usahihi. Lakini kuuawa kwake shahidi kumetajwa kuwa ni mwaka 120,[2] 121 au 122.[3]

Kundi la Zaydiyya linamchukulia Zayd bin Ali kama Imamu wao wa tano, na madhehebu ya Zaydiyya inanasibishwa kwake.[4] Kwa hiyo Zayd alichukuliwa kuwa Imamu, na baada ya kufa shahidi Imamu Hussein (a.s), baadhi ya Alawiy waliona uasi wa kutumia silaha kama mojawapo ya masharti ya uimamu.[5] Na baada ya kifo cha kishahidi cha Zayd, Mashia waliokuwa na itikadi ya kufanya harakati kwa upanga na kutoka kwa ajili ya kukabiliana na kiongozi dhalimu, walimwita Imamu na hivyo kuondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Zaydiyyah.[6]

Kuanza Harakati na Kubadilika Wakati Wake

Kwa mujibu wa historia ya Tabari, Zayd aliuchagua usiku wa Jumatano tarehe 1 Safar 122 H kuwa wakati wa kuanza uasi na harakati yake hiyo na masahaba zake.[7] Lakini uasi ulitokea mapema zaidi ya muda uliopangwa. Yeye na masahaba zake waliondoka mjini humo siku ya Jumanne jioni na kujitayarisha kwa ajili ya vita;[8] kwa sababu Yusuf bin Omar, gavana wa Iraq, alifahamu kuhusu mienendo ya Zayd na masahaba zake wawili.[9] na akawaamuru maofisa hao wakamatwe. Pamoja na hayo, makachero hawakufanikiwa kumpata Zayd,[10] lakini kufahamu watawala kuhusiana na makazi ya Zayd na kukamatwa kwa washirika wake wawili wa karibu na uwezekano wa shambulio la adui vilimfanya Zayd na washirika wake kujiandaa kwa vita mapema zaidi ya walivyokuwa wamepanga.[11]

Watoa Kiapo cha Utiifu Wamgeuka Zayd

Wakati Zayd bin Ali alipofika Kufa kutoka safari yake ya Sham, alipokelewa na watu na matakwa ya kuanzisha harakati.[12] na kwa mujibu wa riwaya ya Sheikh Mufidu, wale waliokwenda kukutana naye walitoa kiapo cha utii kwake,[13] lakini siku moja kabla ya kutoka na kuanzisha harakati, gavana wa Iraq alimuamuru liwali wa Kufa kukusanya watu msikitini. Baada ya liwali kuwaita viongozi wa ukoo na wazee msikitini, akatangaza mjini kwamba yeyote ambaye hatafika msikitini, damu yake itakuwa halali kumwagwa.[14] Matokeo yake yakawa ni kwamba, ni watu 300 tu waliombatana na Zayd.[15] Imekuja katika vyanzo ya kwamba, katika usiku huo Zayd bin Ali na masahaba zake walikaa jangwani na wakapiga nara ya kuomba nusura.[16]

Kwa mujibu wa Tabari, siku iliyofuata, wakati Zayd alipokabiliana na idadi ndogo ya masahaba zake na akajua kuhusu kufungwa kwa wazee wa makabila kwenye msikiti wa Kufa, alionyesha huzuni na masikitiko na kutoukubali udhuru wa watoaji baiya.[17]na akawaita kuwa watu wa hadaa na wazembe.[18] Hata hivyo, kwa mujibu wa riwaya ya Tabari, wazee wa Kufa hapo awali walikuwa wamemkumbusha Zayd bin Ali juu ya kuvunja agano la watu wa Kufa dhidi ya Imam Ali (a.s), Imamu Hassan (a.s) na Imamu Hussein (a.s) na walikuwa wamemzuia asianzshe harakati hiyo.[19]

Wale waliotoa kiapo cha utii kwa Zayd bin Ali wanahesabiwa kuwa ni Makufi (wenyeji wa eneo la Kufa) wapatao 15,000.[20], ambapo miongoni mwao walikuwemo watu kutoka kwa wazee wa Kufa, akiwemo Salama hbin Kahil, Nasr bin Khuzaymah Absi, na Muawiyah bin Is’haq bin Zayd bin Haritha.[21] ] Fauka ya hayo, idadi ya watu huko Mada'in, Basra, Wasit, Mosul, Rey na Jurjan pia walitoa kiapo cha utii kwa wajumbe wa Zayd bin Ali.[22] Tukitegemea mazungumzo ya Zayd bin Ali na Salama bin Kahil, mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kufa, kuwa msingi wa idadi ya wale waliotoa kiapo cha utii, basi watu 40,000 walitia saini makubaliano naye.[23] Katika ripoti nyingine ya Abul Faraj Isfahani amezungumzia wapiganaji 100,000 kwamba, walitangaza kumuunga mkono Zayd.[24] Abul Faraj Esfahani pia alitoa habari kuhusu himaya na msaada wa kifedha wa Abu Hanifa, mwanachuoni wa Kisunni na mwanzilishi wa Madhehebu ya Hanafi, kwa Zayd bin Ali. [25].

Ushindi Mwanzoni na Kushindwa Mwishoni

Kwa mujibu wa Tabari, katika siku ya kwanza ya mwezi Safar 122 Hijria, Zayd aliwateua masahaba zake wawili kwenda Kufa ili kuwajulisha watu kuhusu mwanzo wa harakati hiyo. Lakini watu hawa wawili waliuawa karibu na Kufa na makachero wa mtawala.[26] Kwa msingi huo, Zayd akamtuma mtu mwingine aliyejuliakana kwa jina la Said bin Khaytham.[27] Ingawa jeshi la Zayd bin Ali awali lilipata mafanikio na lilijaribu kuwakomboa watu waliofungiwa msikitini[28] na likashinda vita vya kuzunguka msikiti na soko,[29] lakini siku ya pili, kwa kujiunga idadi ya askari warushaji mishale na Yusuf bin Omar, mtawala wa Umayya wa Iraq, baadhi ya masahaba wa karibu wa Zayd waliuawa[30] na yeye mwenyewe alijeruhiwa vibaya sana.[31]

Siku ya Kwanza: Ushindi

Mapigano kati ya vikosi vya Zayd bin Ali na askari wa Gavana wa Kufa yalianza siku ya kwanza ya Safar katika mwaka wa 122 Hijria. Zayd alilisogeza jeshi lake kuelekea mjini na alikuwa akiwahimiza kupigana. Mapambano ya kwanza yalitokea karibu na Kufa katika eneo la Sayadin (Saidin) na kupelekea ushindi wa washirika wa Zayd, na kisha vita vikaendelezwa hadi Kufa.[32] Baada ya Zayd kuwaona masahaba wake ni wachache, aliingiwa na wasiwasi kwamba watu wa Kufa wangemuacha peke yake kama walivyomfanyia Imamu Hussein (a.s).[33]

Zayd bin Ali akiwa pamoja na Nasr bin Khuzaymah, Muawiya bin Is’haq na baadhi ya masahaba zake walikwenda msikitini kuwaokoa watu waliokuwa wakishikiliwa kutokana na kuzingirwa na askari wa Bani Umayya. Ingawa waliweza kufika msikitini na kutundika bendera zao msikitini,[34] lakini maajenti wa Bani Umayya waliwazuia kusonga mbele na kwa kuwasili kwa jeshi lililokuwa na nguvu mpya la Yusuf bin Omar, vita vikali vilizuka kuzunguka msikiti na soko. Hatimaye, vita na mzozo vilihamia kwenye kitongoji kiitwacho Dar al-Rizq, na Zayd na washirika wake wakashinda katika siku ya kwanza ya vita.[35]

Siku ya Pili: Kushindwa

Mwanzoni mwa siku ya pili ya vita, Nasr bin Khuzaymah aliuawa na Nayl bin Farwah.[36] Kifo chake kilimuathiri sana Zayd.[37] Pamoja na hayo vita vikali vya Zayd na masahaba zake katika asubuhi ya siku hii vilimalizika kwa wao kupata ushindi.[38]Yusuf bin Omar alitayarisha jeshi lingine kuwashambulia washirika wa Zayd, lakini Zayd na washirika wake walilisambaratisha. Lakini kwa kuongezwa wapiga kwenye jeshi la Yusuf bin Omar, ikawa kibarua kigumu kwa jeshi la Zayd, na ni katika hali hii ambapo, Mu’awiya bin Is’haq, kamanda mwingine wa Zayd, naye aliuawa. Magharibi ya siku hii pia Zayd alijeruhiwa sana baada ya kulengwa na mshale katika paji lake la uso [39] na kisha katika siku ya tatu ya mwezi Safar mwaka 122 Hijria akafa shahidi.[40]

Kaburi linalohusishwa na Zayd bin Ali huko Kufa

Ili mwili wake usiangukie mikononi mwa maafisa wa Bani Umayya, masahaba wa Zayd walibadilisha njia na wakauzika lakini mtumwa aliokuwa nao akamjulisha Hakam Ibn Salt.[41]Bani Umayya walifukua na kutoa mwili wa Zayd na, wakautundika kwa amri ya Yusuf bin Omar, na kupeleka kichwa chake kwa Hisham bin Abdul Malik, khalifa wa Bani Umayya.[42]

Msimamo wa Imamu Swadiq (a.s)

Uasi na harakati ya Zayd bin Ali ilitokea katika zama za Uimamu wa Imam Sadiq (a.s), Imamu wa sita wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, lakini Imamu Sadiq hakushiriki katika harakati hiyo.[43] Kuna hadithi na maoni mbalimbali kuhusu Zayd na harakati yake, lakini kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) hakuna msimamo wa wazi ulioripotiwa kuhusiana na harakati hiyo ya Zayd. Mwandishi wa kitabu Kifayat al-Athar ameripoti kwamba kundi la Mashia wanaamini kwamba hatua ya Imam Sadiq (a.s) ya kutoandamana na uasi na harakati ya Zayd ilitokana na upinzani wake kwa Zayd. Hata hivyo mwandishi wa kitabu hicho anaamini kwamba, hatua ya Imamu ya kutokuwa pamoja na Zayd katika harakati hiyo yenyewe hiyo ni aina ya sera, busara na mipango yake.[44]

Baadhi ya wanachuoni wa Kishia, akiwemo Shahid Al-Awwal,[45] Ayatullah Khui,[46] na Mamaqani[47] wanaamini kwamba, Zayd bin Ali alikuwa na ruhusa kutoka kwa Imam Sadiq (a.s). Pia, baadhi ya watafiti, sambamba na kauli za wanavyuoni watatu waliotajwa hapo juu, wamenukuu riwaya kutoka kwa Imamu Ridha (a.s) na kuichukulia harakati ya Zayd kwamba, ilifanyika kwa idhini ya Imamu Sadiq.[48] Kwa mujibu wa riwaya iliyotajwa, Zayd bin Ali alishauriana na Imamu Sadiq, na Imamu huyo wa sita wa Waislamu wa ya Shia akamwambia: “Kama unataka kuwa mtu ambaye ametundikwa kwenye sinagogi la Kufa, hii ndiyo njia”.[49] Watafiti wengine wakitumia riwaya hiyo hiyo, wamesema kwamba pamoja na kwamba Zayd alikuwa mkweli katika mapinduzi na harakati yake na lau angeshinda, angelikabidhi ukhalifa kwa wanaostahiki, lakini Imamu Sadiq alimkataza kufanya harakati hiyo.[50] Allama Tehrani pia akitumia riwaya ya Aban bin Othman kutoka kwa Muumin al-Taq ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi[51] ameitambua harakati ya Zayd kwamba, ilifanyika bila ya idhini ya Imamu Sadiq.[52]

Kwa kuzingatia baadhi ya riwaya zilizosimuliwa kutoka kwa Imam Sadiq[53] na Imam Ridha[54], Zayd bin Ali alikusudia kukabidhi ukhalifa kwa Imam Sadiq (a.s) endapo atashinda. Kwa mujibu wa Sheikh Mufid, kaulimbui ya Zayd bin Ali ilikuwa “ al-Ridha min Aal Muhammad” (Ridhaa ya Ahlul-Bayt wa Mtume) na kinyume na imani ya watu, hakutaka ukhalifa kwa ajili yake mwenyewe, bali baada ya ushindi angeukabidhi kwa mstahiki wake.[55] Allama Majlisi ameinasibisha kauli hii na akthari ya wanazuoni wa Kishia na kusema bayana kwamba, yeye hajui kauli nyingine yoyote kutoka kwao kuhusiana na kadhia hii, isipokuwa kauli hii.[56] Kwa mujibu wa Sheikh Mufid, Imamu Sadiq alipopata habari za kuuawa shahidi Zayd, aliathirika sana na akaamrisha kugawanya mali miongoni mwa familia za wale waliouawa shahidi katika harakati yake.[57]

Msukumo na Mazingira ya Harakati

Sheikh Mufidu alichukulia motisha na msukumo mkuu wa Zayd bin Ali wa kuanzisha harakati dhidi ya serikali ya Bani Umayya kuwa ni kulipiza kisasi cha damu ya Imamu Husein (a.s).[58] Pia amelitaja suala la kuamrisha mema na kukataza maovu kuwa ni moja ya dhamira na msukumo wa Zayd wa kuanzisha harakati hiyo na akasema kwamba, muamala usiofaa Hisham bin Abd al-Malik, khalifa wa Bani Umayya dhidi yake mbele ya watumishi wa baraza pia kunatajwa kama moja ya motisha na msukumo wa Zayd wa kuanzisha harakati yake hiyo.[59]

Pia, baadhi ya watafiti wamezingatia kutusiwa na kutukanwa Imam Ali (a.s) katika mimbari katika kipindi cha Hisham bin Abdul Malik,[60] dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya dhidi ya familia ya Mtume, na hatimaye ukafiri na ulahidi wa Bani Umayyah kwa maoni ya Zayd bin Ali kama sababu za uasi na harakati ya Zayd.[61] Muhammad bin Jarir al-Tabari amezungumza kuhusu tofauti kuhusiana na sababu ya uasi wake[62] ambapo ametaja mambo kama vile tuhuma za kifedha, kutokubaliana kwake na Abdullah Mahdh kuhusiana na wakfu za Imam Ali (a.s) hapo Madina, ambako kulipelekea kwenye usuluhishi wa Khalid bin Abdul Malik na pia, tuhuma za kifedha zilizokuwa zikitolewa dhidi ya Zayd wakati wa utawala wa Yusuf bin Omar na mwaliko wa watu wa mji wa Kufa kwake kuwa ni miongoni mwa sababu zilizotambuliwa kuwa zilipelekea kuibuka harakati ya Zayd.[63] Kwa mujibu wa vyanzo, katika kiapo cha utii ambacho Zayd alipatiwa na watu kulitiliwa mkazo masuala kama kugawanya ngawira kwa usawa, kuwakataa madhalimu na kuwasaidia Ahlu al-Bayt (a.s) dhidi ya wapinzani wao.[64] Mamaqani analichukulia lengo la Zayd katika harakati hiyo kuwa ni kuuchukua ukhalifa kutoka mikononi mwa Bani Umayya na kuukabidhi kwa Imam Sadiq (a.s.) na anaamini kwamba Zayd hakuwa akibainisha wazi lengo lake hili ili Imam Sadiq (a.s) asidhuriwe.[65]

Matokeo ya Harakati

Kumebainishwa matokeo ya harakati ya Zayd bin Ali na miongoni mwayo ni: Harakati ya Zayd na baada ya hapo, iliandaa mazingira ya kutokea harakati ya Yahya na hilo kuwa utangulizi wa kuanguka kwa serikali ya Bani Umayya[66] na kupanua wigo wa harakati za Shia hadi Khorasan.[67] Kiasi kwamba, imekuja katika Tarikh Ya’qubi kwamba, kuuawa Zayd bin Ali kuliwafanya Mashia wa Khorasan kuanzisha harakati ya kubainisha dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya dhidi ya familia ya Mtume (s.a.w.w), na kwa muktadha huo hapakuwa na mahali ambapo watu hawakuwa wakifahamu jinai za Bani Umayya[68] Vile vile imepokewa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) kwamba, Hisham bin Abdul Malik alimuua Zayd bin Ali, na badala yake Mwenyezi Mungu akaondoa utawala wake.[69] Katika nukuu nyingine kutoka kwa Imamu wa sita (Imam Ja’far Sadiq) imeelezwa kuwa, siku saba baada ya Bani Umayya kuchoma mwili wa Zayd Mwenyezi Mungu akaazimia kuwaangamiza.[70] Moja ya matokeo mengine ya harakati ya Zayd bin Ali ni kupungua kwa unyeti wa serikali kwa Ahlul-Bayt (a.s), na matokeo yake kukapatikana fursa kwa Imam Sadiq (a.s) ya kueneza madhehebu ya Shia.[71]

Pamoja na kuchambua natija na matokeo ya harakati ya Zayd bin Ali, baadhi ya watafiti pia wameeleza sababu za kushindwa kwa kwa harakati hiyo ambazo ni pamoja na; nguvu ya kijeshi ya serikali ya Bani Umayya,[72] kuwepo kwa majasusi na mawakala wenye ushawishi ambao walifichua mambo wakati wa harakati hiyo, hatua ya Imam Sadiq (a.s) ya kutounga mkono waziwazi harakati hiyo na hatimaye kutounga mkono harakati hiyo watu wa mji wa Kufa.[73]

Masuala Yanayo Husiana

Rejea

  1. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 124, 1419 H.
  2. Sheikh Mufid, al-Irshad, juz. 2, uk. 174, 1413 H.
  3. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 160, 1967 M.
  4. Subhi, Fi Ilm al-Kalam, juz. 3, uk. 48, 1411 H.
  5. Subhi, Fi Ilm al-Kalam, juz. 3, uk. 48-52, 1411 H, Khazzaz Qummi, Kifayah al-Athar, uk. 305, 1401 H.
  6. Khazzaz Qummi, Kifayah al-Athar, uk. 305, 1401 H.
  7. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 181, 1967 M.
  8. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 181-182, 1967 M, Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 132, 1419 H.
  9. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 180, 1967 M.
  10. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 180, 1967 M.
  11. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 180, 1967 M, Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 132, 1419 H.
  12. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 162-166, 1967 M.
  13. Sheikh Mufid, al-Irshad, juz. 2, uk. 173, 1413 H.
  14. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 181, 1967 M.
  15. Balazuri, Ansab al-Ashraf, juz. 3, uk. 244, 1977 M.
  16. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 182, 1967 M.
  17. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 182, 1967 M.
  18. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 182-183, 1967 M, Ibnu A'tham Kufi, al-Futuh, juz. 8, uk. 290, 1991 M.
  19. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 166-168, 1967 M.
  20. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 181, 1967 M.
  21. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 167, 1967 M.
  22. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 132, 1419 H.
  23. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 168, 1967 M.
  24. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 131, 1419 H.
  25. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 141, 1419 H, Balazuri, Ansab al-Ashraf, juz. 3, uk. 239, 1977 M.
  26. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 182, 1967 M.
  27. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 133, 1419 H
  28. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 184-185, 1967 M.
  29. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 184, 1967 M.
  30. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 185-186, 1967 M.
  31. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 186, 1967 M.
  32. Ibnu Maskawaih, Tajarub al-Umam, juz. 3, uk. 142-144, 1379 S.
  33. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 184, 1967 M.
  34. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 184-185, 1967 M.
  35. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 184, 1967 M.
  36. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 184-185, 1967 M.
  37. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 136, 1419 H
  38. Ibnu Athir, al-Kamil fi al-Tarikh, juz. 5, uk. 135, 1965 M.
  39. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 185-186, 1967 M.
  40. Abu al-Faraj Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 139, 1419 H
  41. Tabari, Tarikh al-Umum wa al-Muluk, juz. 7, uk. 186-187, 1967 M.
  42. Ibnu Maskawaih, Tajarub al-Umam, juz. 3, uk. 147, 1379 S.
  43. Khazzaz Qummi, Kifayah al-Athar, uk. 305, 1401 H.
  44. Khazzaz Qummi, Kifayah al-Athar, uk. 305, 1401 H.
  45. Shahid Awal, al-Qawaid, juz. 2, uk. 207,1400 H.
  46. Khui, Mu'jam Rijal al-Hadith, juz. 7, uk. 365, 1410 H
  47. Mamaqami, Tanqih al-Maqaal, juz. 9, uk. 261,1431 H.
  48. Ridhawi Ardakani, Shakhsiyat wa Qiyam Zaid bin Ali, Daftar intesharat Islami, uk. 122-123
  49. Sheikh Saduq, U'yun Akhbr al-Ridha (as), juz. 1, uk. 2, 1378 H.
  50. Rajabi «[Muwajahah Imam Sadiq (as) ba Nihdhat Tarjuma/Chera Imam az Qiyam Zaid Hemayat nakarde», Tovuti Mehr.
  51. Kulaini, al-Kafi, juz. 1, uk. 174, 1407 H.
  52. Tehrani, Imam Shenasi (mengenal Imam), juz.1, uk. 204-205, 1426 H.
  53. Kulaini, al-Kafi, juz. 8, uk. 264, 1407 H.
  54. Sheikh Saduq, U'yun Akhbar al-Ridha (as), juz. 1, uk. 249, 1378 H.
  55. Sheikh Mufid, al-Irshad, juz. 2, uk. 173, 1413 H.
  56. Majlisi, Mr'atul Uqul, juz. 4, uk. 118, 1404 H.
  57. Sheikh Mufid, al-Irshad, juz. 2, uk. 173, 1413 H.
  58. Sheikh Mufid, al-Irshad, juz. 2, uk. 171-172, 1413 H.
  59. Sheikh Mufid, al-Irshad, juz. 2, uk. 173, 1413 H.
  60. Ibnu Abil Hadid, Sharh Nahjul Balaghah, juz. 4, uk. 57,1404 H.
  61. Kariman, Sirah wa Qiyami Zaid bin Ali, uk. 260-268, 1404 H.
  62. Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 7, uk. 160, 1967 M.
  63. Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 7, uk. 160-167, 1967 M.
  64. Baladhuri, Ansab al-Ashraf, juz. 3, uk. 237-238, 1977 M, Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Mulk, juz.7, uk. 172-173, 1967 M.
  65. Mamaqami, Tanqih al-Maqal, juz. 9, uk. 233-234, 1431 H.
  66. Ridhawi Ardakani, Shakhsiyat wa Qiyam Zaid bin Ali, Daftar intesharat Islami, uk. 280-281
  67. Kazimi, Qiyami Zaid bin Ali wa Yahya bin Zaid wa Asbab Shikast wa Ta'thirati on dar Mubarezat Dhiddi Umawi, uk. 199
  68. Yakubi, Tarikh al-Ya'qubi, juz. 2, uk.326.
  69. Majlisi, Bihar al-Anwar, juz. 45, uk. 309, 1403 H.
  70. Kulaini, al-Kafi, juz. 8, uk. 161, 1407 H.
  71. Kariman, Sirah wa Qiyami Zaid bin Ali, uk. 361-362, 1364 S.
  72. Nuri, Zaid bin Ali wa Mashruiyat al-Thaurah Inda Ahlilbait, uk. 313, 1416 H.
  73. Ridhawi Ardakani, Shakhsiyat wa Qiyam Zaid bin Ali, Daftar intesharat Islami, uk. 263-279

Vyanzo

  • Ibnu Abil Hadid, Abdul Hamid Hibatullah. Sharh Nahjul Balaghah. Tas-hih: Ibrahim Muhammad Abul Fadhl. Qom: Maktabah Ayatullah Mar'ashi an-Najafi, 1404 H.
  • Ibnu Athir, Ali bin Muhammad. Al-Kamil fi at-Tarikh. Beirut: Dar Sadir wa Dar Beirut, 1965 M.
  • Ibnu A'tham Kufi, Muhammad bin Ali. Al-Futuh. Tahqqiq: Ali Shiri. Beirut: Dar al-Adhwa, 1991 M.
  • Ibnu Maskawaih, Ahmad bin Muhammad. Tajarub al-Umam wa Ta'aqub al-Himam. Tahqqiq Abul Qasim Imami. Tehran: Intisharat Surush, 1379 HS.
  • Abul Faraj Isfahani, Ali bin Husain. Maqatil at-Talibiyyin. Tahqqiq: Ahmad Saqr. Beirut: Muassasah al-A'lami li al-Matbu'at, 1419 H.
  • Balazuri, Ahmad Yahya. Ansab al-Ashraf. Tahqqiq: Muhammad Baqir Mahmudi. Beirut: Dar at-Ta'aruf, 1977 M.
  • Husaini Tehrani, Sayid Muhammad Hussein. Imam Shenasi. Mashhad: Allamah Tabatabai, 1426 H.
  • Khazzaz Qummi, Ali bin Muhammad. Kifayah al-Athar. Tahqqiq: Sayid Abd. Latif Hassani. Qom: Intisharat Bidar, 1401 H.
  • Khui, Sayid Abul Qasim. Mu'jam Rijal al-Hadith. Qom: Markaz Nashre Athare Shiah, 1401 H / 1369 S.
  • Rajabi «[Muwajahah Imam Sadiq (as) ba Nihdhat Tarjuma/Chera Imam az Qiyam Zaid Hemayat nakarde», Tovuti Mehr. Tarikh Darj Matalib: 24 Shahrivar 1391 S, Tarikh Bazdid: 19 Tir 1397 S.
  • Ridawi Ardakani, Sayid Abul Fadhl. Shakhsiyat wa Qiyami Zaid bin Ali. Qom: Daftare Intisharate Islami, Bita.
  • Shahid Awal, Muhammad Makki. Al-Qawaid wa al-Fawaid. Tas-hih: Sayid Abdul Hadi Hakim. Qom: Kitabfurushi Mufid, (ofset Najaf, 1400 H).
  • Sheikh Saduq, Muhammad bin Ali. U'yun Akhbar ar-Ridha (as). Tas-hih: Mahdi Lajuwardi. Tehran: Intisharate Jahan, 1378 HS.
  • Sheikh Mufid, Muhammad bin Muhammad. Al-Irshad fi Ma'rifati Hujajillah ala al-Ibad. Qom: Kongres Sheikh Mufid, 1413 H.
  • Subhi, Ahmad Mahmud. Fi Ilm al-Kalam Dirasat Falsafiyah li Ara' al-Firaq al-Islamiyah fi Usul ad-Din. Beirut: Dar al-Nihdhat al-Arabiyah, 1411 H/1991 M.
  • Tabari, Muhammad bin Jarir. Tarikh al-Umam wa al-Muluk. Tahqqiq: Muhammad Abul Fadhl Ibrahim. Beirut: Dar at-Turath, 1967 M.
  • kazhimi, Muhmmad Hussein «Qiyam Zaid bin Ali wa Yahya bin Zaid wa Asbabe Shekast wa Ta'thirate an dar Mubarazate dhiddi Umawi» Dar majalah Tarikh Nu. juz. 12, Payiiz 1394.
  • Kariman, Hussein. Sirah wa Qiyam Zaid bin Ali. Shirkate Intisharate Ilmi wa Farhanggi, 1364 S.
  • Kulaini, Muhammad bin Ya'qub. Al-Kafi. Tas-hih: Ali Akbar Ghaffari va Muhammad Akhundi. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiyah, 1407 H.
  • Mamaqami, Abdullah. Tanqih al-Maqal fi Ilm ar-Rijal. Tahqqiq: Muhyiddin va Muhammad Ridha Mamaqami Qom: Muassasah Al al-Bait li Ihya at-Turath, 1431 H.
  • Majlisi, Muhammad Baqir. Bihar al-anwar. Beirut: Dar Ihya at-Turath al-Arabi, 1403 H.
  • Majlisi, Muhammad Baqir. Mir'at al-Uqul fi Sharh Akhbar Al ar-Rasul. Tas-hih: Said Hashim Rasuli Mahallati. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiyah, 1404 H.
  • Nuri, Hatim. Zaid bin Ali wa Mashruiyyat Thaurah Inda Ahli al-Bait. Markaz al-Ghadir li ad-Dirasat al-Islamiyah, 1416 H/1995 M.
  • Ya'qubi, Ahmad bin Is-haq. Tarikh al-Ya'qubi. Beirut: Dar Sadir. Bita.