Tukio la Fakh

Kutoka wikishia

Tukio na harakati za Fakh au Mapinduzi ya Sahib Fakh (Kiarabu: واقعة فخّ) ni miongoni mwa harakati na mapinduzi yaliyofanywa na Maalawi, watu kutoka katika kizazi cha Imamu Ali dhidi ya utawala wa Bani Abbas. Harakati hii ilitokea mwaka 169 Hijiria. Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Jawadi (a.s) ni kwamba, baada ya tukio la Karbala, harakati ya Fakhkh ilikuwa tukio gumu zaidi la majaribu ya Ahlul-Bayt (a.s). Harakati hii iliongozwa na Hussein ibn Ali bin Hassan mashuhuri kwa lakabu ya Swahib Fakhkh. Yeye ni mmoja wa wajukuu wa Imamu Hassan (a.s) ambaye aliishi katika zama za Imamu Kadhim (a.s). Tukio hili lilitokea katika mji wa Madina na likaishia kwa kuuawa yeye pamoja na masahaba zake. Kutokana na kuwa tukio hili lilitokea katika kitongoji cha Fakhkh yapata kilomita nne kutoka Masjid al-Haram (msikiti mtakatifu wa Makka) limeondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Harakati ya Fakhkh au Harakati ya Swahib Fakhkh.

Kwa mujibu wa hadithi na riwaya mbalimbali, Imamu Mussa al-Kadhim (a.s) alikataa kumpa baia na kiapo cha utii Hussein Fakhkh na alibashiri na kutoa habari ya kutofanikiwa kwa harakati yake. Hata hivyo ripoti zinaonyesha kuwa, Swahib Fakhkh aliomba ushauri kutoka kwa Imamu na nukuu nyingine zinaonyesha kuwa, Imamu alimpa amri ya kuanzisha harakati hiyo; hata hivyo mkabala na hadithi hizo kuna hadithi nyingine ambazo zinasema kuwa, baada ya kuombwa ushauri, Imamu Kadhimu hakutoa jibu chanya kwa waliotaka kuanzisha harakati. Hata hivyo, baadhi ya watafiti wanaamini kwamba, katika hadithi, hakuna msimamo wa wazi wa Imamu Kadhim wa kuonyesha kuunga mkono au kupinga harakati hiyo. Baadhi ya watafiti pia wakitegemea baadhi ya hadithi, wametambua kwamba, Imamu Kadhim aliunga mkono shakhsia ya Swahib Fakh na kuunga mkono harakati yake; lakini baadhi ya wengine wamesema kuwa, hoja na dalili hii haitoshi.

Kwa mujibu wa waandishi wa historia harakati ya Swahib Fakhkh ilitokea kufuatia mashinikizo na mibinyo ya utawala wa Bani Abbas dhidi ya kizazi na ukoo wa Alawiyyun (kizazi cha Ali). Miezi kadhaa kabla ya tukio hilo, Hussein Fakhkh aliwaalika watu wengi kutoka miji tofauti kwa ajili ya harakati wakati wa msimu wa Hija na akachukua baia na kiapo cha utii kutoka kwao. Hata hivyo inaelezwa kkwamba, maudhi na mateso ya gavana wa Madina ndiyo yaliyomsukuma Hussein aanzishe harakati yake mwezi mmoja mapema zaidi ya alivyokuwa amekusudia. Alianzisha harakati hiyo mwezi Dhul-Qaadah badala ya Dhul-Hija katika mji wa Madina. Kwa muda mfupi tu wafanya mapinduzi na harakati hiyo walifanikiwa kudhibiti mji wa Madina na kuanza kuelekea Makka.

Baadhi ya maajenti na vibaraka wa serikali waliokuwa katika safari ya Hija walipambana na waasi hao kwa amri ya Hadi Abbasi. Katika vita hivi vilivyotokea tarehe 8 Dhul-Hijjah, Sahib Fakhkh na watu wake wengi waliuawa, na wengine walitekwa au kutoroka.

Kufuatia vita hivi, gavana wa Madina alichoma moto nyumba na mali za kundi la waasi na kuwanyang'anya baadhi ya wengine. Alichukua vichwa vya mashahidi, pamoja na mateka na kuvipeleka kwa Khalifa. Kwa mujibu wa wanachuoni ni kwamba, kuanza harakati hiyo kabla ya wakati uliokuwa umepangwa, kutoungana baadhi ya wazee na shakhsia wakubwa wa Alawi na watu wa Makka na Madina kutokuwa pamoja na harakati ya Fakhkh zinatajwa kuwa sababu muhimu zaidi zilizopelekea kushindwa kwa harakati ya Fakh. Vitabu mbalimbali vimeandikwa juu ya suala la tukio la Fakh, ambapo "Akhbaru Fakhkh" kilichoandikwa na Ahmad bin Sahl Razi (aliaga mwa karne ya 4) ndicho cha zamani zaidi miongoni mwavyo ambacho kimeshughulikia na kuzungumzia suala hili kwa kujitegemea.

Harakati ya Fakhkh; tukio chungu kwa Mashia

Tukio la Fakhkh limetambulishwa kama moja ya matukio machungu zaidi katika historia ya Ushia, na riwaya kutoka kwa Mtume na Maimamu wa Shia [1] ni ushahidi wa madai haya. [2] Kwa mujibu wa riwaya kutoka kwa Imamu Jawadi (a.s), baada ya tukio la Karbala, tukio hili lilikuwa majaribu makubwa zaidi ya Ahlul-Bayt (a.s). [3] Kwa mujibu wa riwaya na hadithi iliyonukuliwa na Abu al-Faraj Isfahani, mwanahistoria wa karne ya 4 Hijiria ni kwamba, Mtume (s.a.w.w) na Imamu Swadiq (a.s) walitabiri kifo cha Hussein bin Ali (Swahib Fakhkh) katika eneo la Fakhkh na kubashiri kwamba atakuwa mtu wa peponi. [4] Kadhalika imepokewa kwamba Imamu Kadhim (a.s) alikuwa akiwalilia mashahidi wa Fakhkh na kuwaombea kifo kwa Mwenyezi Mungu wauaji wao. [5]. Vilevile Imamu Kadhim (a.s) alichukua jukumu la kuwa msimamizi wa mayatima na wajane wa mashahidi waliouawa katika tukio la Fakhkh. [6] Tukio la Fakhkh limeakisiwa na kuzungumziwa katika beti za mashairi za washairi mbalimbali yakiwemo mashairi yaliyotungwa na Di’bil al-Khuzai. [7]

Kiongozi wa Harakati

Makala kuu: Swahib Fakhkh

Hussein bin Ali, mashuhuri kwa jina la Swahib Fakhkh, ni katika wajukuu wa Imamu Hassan (a.s). [8] Baba yake ni Ali (aliyejulikana kama Ali mwema na mtukufu) na mama yake alikuwa Zainab (binti ya Abd Allah Mahdh) ambapo kutokana na kufanya sana kwao ibada walijulikana kama wanandoa wema [9]. Swahib Fakhkh alikuwa mashuhuri kama mtu shujaa na mkarimu [10], riwaya mbalimbali zimebainisha ukarimu wake [11]. Sheikh Tusi anamhesabu miongoni mwa masahaba wa Imamu Swadiq (a.s). [12] Swahib Fakhkh alifariki dunia Dhul-Hijjah 169 Hijiria akiwa na umri wa miaka 41. [13].

Msimamo wa Imamu Kadhim mkabala wa harakati ya Fakhkh

Kulingana na hadithi iliyonukuliwa na Kulayni katika kitabu cha al-Kafi, wakati Swahib Fakh alipoanzisha uasi na harakati alimtaka Imamu Kadhim ampe kiapo cha utii. Lakini Imamu Kadhim alikataa kutoa kiapo cha utii, na akamtaka asimlazimishe kutoa kiapo hicho, na yeye alifanya hivyo hivyo. [14] Abdullah Mamaqani anaamini kwamba, takwa la kiapo cha utii cha Swahib Fakhkh kwa Imamu Kadhim halikuwa na uhalisia na ilikuwa ni utaratibu wa kawaida ili kwamba, ikifaulu, amkabidhi ukhalifa; kwa hiyo, Imamu alitumia taqiyyah kukamkataza Hussein asianzishe harakati; lakini ndani ya moyo wake aliridhika na kitendo chake; kama ambavyo baada ya kuuawa kwake shahidi alimuombea rehema na maghufira. [15]

Katika riwaya na hadithi ya Abul Faraj Esfahani, imeelezwa kwamba Hussein alishauriana na Imamu Kadhim (a.s.) kwa ajili ya kuanzisha mapinduzi na harakati hiyo na kwamba, harakati hiyo ilifanyika kwa amri ya Imamu [16]. Kadhalika kwa mujibu wa Sayyid Ibn Tawus alivyonukuu kutoka kwa wanachuoni wa Kishia katika karne ya 7 Hijiria ni kwamba, Hadi Abbasi aliitambua harakati ya Hussein Fakhkh kwamba, ilifanyika kwa amri ya Imamu Kadhim. [17] Hata hivyo, kwa mujibu wa hadithi kutoka katika kitabu cha al-Kafi, Yahya bin Abdullah alilalamika na kuonyesha manung’uniko katika barua yake kwa Imamu Kadhim kuhusu jibu hasi la Imamu kwa ombi lao la ushauri katika harakati ya Fakhkh.[18]

Ahmad bin Ibrahim Hassani na Ahmad bin Sahl, wanahistoria wawili wa madhehebu ya Zaydiyyah wa karne ya 4 Hijiria wanasema, wakati wa kutokea harakati ya Fakhkh, Imamu Kadhim alikuwa Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija. [19] Kwa mujibu wa riwaya ya wawili hawa, Musa bin Issa, mmoja wa watendaji na makachero wa ukhalifa wa Bani Abbas alimuita Imamu wakati wa vita, na Imamu akaenda huko na kukaa naye hadi mwisho wa vita [20]. Kwa mujibu wa ripoti hii, baada ya vita wakati Imamu alipokwenda katika ardhi ya Mina, walimletea vichwa vilivyokatwa [21]. Kwa mujibu wa nukuu ya Abul Faraj Isfahani, Imamu Kadhim, alipoona kichwa cha Husein bin Ali, alisoma Aya ya marejeo kwa Mola (Inna Lilahi Wainna Ilayh Rajiuun) na kwa kutaja fadhila zake, alimtambulisha kama mtu mwaminifu. [22]

Allama Majlisi, mwandishi wa kitabu Bihar Al-Anwar, ingawa ameisifu shakhsia ya Hussein Fakhkh, lakini anaamini kwamba, kuna ukosoaji uliobainishwa kuhusu shakhsia yake. [23] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba, ingawa kuna riwaya zinazothibitisha shakhsia ya Swahib Fakhkh, lakini hakuna uthibitisho kutoka kwa Maimamu wa Kishia wa kuthibitisha harakati yake. [24] Rasul Jaafariyan, mtafiti wa masuala ya historia, licha ya kuwa anaichukulia harakati ya Fakhkh kuwa ni miongoni mwa harakati salama kabisa zilizofanywa na watu wa Alawi dhidi ya Bani Abbas, lakini anaandika kwamba, hakuna uhakika kwamba harakati hii ilitekelezwa kwa amri ya Imamu Kadhim (a.s). Bali, inaweza kusemwa kwamba, Mashia Imamiyyah hawakuwa ni wenye kukubaliana na harakazi hizi; kwa sababu katika suala hili, walikuwa na mizozo na Alawi na kulikuweko na hitilafu baina yao. [25]

Mazingira ya harakati

Kwa mujibu wa Yaqoubi, mwanahistoria wa karne ya tatu ya Hijiria ni kwamba, wakati Hadi Abbasi alipoingia madarakani mwaka wa 169 Hijiria, alizidisha mashinikizo kwa ukoo wa Alawi. [26] Alianzisha anga na mazingira ya hofu na wahaka dhidi ya kizazi cha Ali (a.s) na aliondoa sheria na mambo ambayo Alawi walikuwa wamesamehewa na baba yake yaani Mahdi Abbasi. [27] Aidha aliamuru maajenti wake katika sehemu mbalimbali kuwakamata na kuwapeleka kwake. [28]

Vile vile mtawala Hadi Abbasi alimteua mmoja wa wajukuu Omar bin al-Khattab, aitwaye Abdul Aziz bin Abdullah, kuwa gavana wa Madina [29], ambaye pia alifanya mambo mabaya dhidi ya Alawi na kila siku alikuwa akiwataka waje katika makao makuu ya utawala. [30]

Wengine wametumia baadhi ya ripoti na kusema kwamba Shahidi Fakhkh alikuwa akifikiria kufanya mapinduzi na harakati tangu wakati wa utawala wa Mahdi Abbasi; [31] kwa sababu kwa mujibu wa ripoti ya Razi, karibu watu elfu thelathini kutoka miji mbalimbali walikuwa wametoa bai na kiapo cha utii kwake ili waanzishe harakati wakati wa msimu wa ibada ya Hija katika jangwa la Arafa. [32] Vile vile walikuwa wamewajulisha kkwa njia ya barua watu wao wanaoaminika huko Khorasan na maeneo mengine kuhusu uamuzi wao huo [33]. Baada ya vitisho vya gavana wa Madina na kukamatwa kwa masahaba kadhaa wa Hussein, waliamua kuanzisha harakati yao mapema kabla ya muda waliokuwa wamepanga.[34]

Kuanza harakati Madina

Hussein Fakhkh alianzisha harakati katika mji wa Madina Mfunguo pili Dhul-Qa'dah mwaka 169 Hijiria. [35] Yeye na baadhi ya masahaba wake waliingia Msikiti wa Mtume (s.a.w.w) wakiwa na kaulimbiu "Ahad Ahad" wakati wa Swala ya Alfajiri, na wakamlazimisha muadhini aadhini kama Mashia ana ataje ibara ya “Hayy Ali Khair al-Amal” katika adhana. [36] Gavana wa Madina aliingiwa na hofu kubwa aliposikia adhana ya Mashia na akakimbia kutoka Madina [37]. Watu waliswali chini ya Uimamu wa Hussein na baada ya Swala, Hussein bin Ali alitoa khutba na kuwalingania watu kutoa kiapo cha utii kwake ili watu wawe pamoja naye kwa kuzingatia Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na kumridhia mtu ambaye ameridhiwa na familia ya Muhammad. [38] Hata hivyo, zipo riwaya zinazoonyesha kwamba watu wa Madina hawakufuatana nao. [39]

Juhudi za maajenti wa serikali huko Madina kukabiliana na Hussein Fakhkh hazikufua dafu na kusababisha kushindwa na kuuawa kwa baadhi yao. [40] Pia waliomba msaada kutoka kwa Mubarak Turki (mmoja wa makamanda wa ukhalifa) ambaye alikuwa ameingia Madina kwa nia ya kwenda kufanya ibada ya Hija. [41] Hata hivyo, kwa mujibu wa riwaya ya Abul Faraj Isfahani, Mubarak, ambaye hakutaka kupigana na Hussein, alimuomba Husein kupitia ujumbe wa siri amshambulie ili imlazimu kukimbia. [42] Hussein naye alifanya hivyo, na Mubarak akakimbia kuelekea Makka. [43] Kwa muktadha huo, mji wa Madina ukawa katika mamlaka na udhibiti wa Hussein, Kudhibiti kwake mji wa Madina kulidumu kwa muda wa siku 11. [44] Hussein Fakhkh alimteua Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Dinar (Dirbas) [45] al-Khuzai, kuwa gavana wa Madina na yeye akiwa na wafuasiu wake 300, [46] walianza safari tarehe 24 Dhul-Qaadah kuelekea Makka, [47].

Vita vya Fakhkh

Hadi Abbasi aliwaamuru baadhi ya shaksia wakubwa katika utawala waliokwenda Hija kukabiliana na Hussein na akamfanya kamanda wa vita hivyo kuwa Muhammad bin Suleiman [48]. Bani Abbas wakiwa na jeshi la watu elfu nne mnamo tarehe 8 Dhui-Hijjah (Siku ya Tarwiyah) walikabiliana ana kwa ana na jeshi la Hussein katika sehemu inayoitwa "Fakhkh" [49]. Kamanda wa Kiabbasi alimpa amani Hussein; lakini Hussein alikataa na wakati vita vilipoanza, Hussein na wenzake wengi waliuawa shahidi. [50] Kadhalika, kundi la masahaba wa Hussein walitekwa nyara na wengine wakatoroka. [51] Baadhi ya mateka waliuawa [52] na baadhi yao pamoja na vichwa vya mashahidi walipelekwa Baghdad kwa mtawala Hadi Abbasi. [53] Hadi alitundika kichwa cha Hussein katika daraja la Baghdad kwa muda, kisha akakipeleka Khorasan. [54] Miili ya watu waliouawa ilibakia juu ya ardhi kwa muda wa siku tatu na wanyama na ndege walikuwa wakiila. [55]

Kinyume na usemi maarufu kwamba vita hivi vilitokea mnamo tarehe 8 Dhul-Hija mwaka wa 169 Hijria, [56] katika baadhi vyanzo vingine, inaripotiwa kwamba, vilitokea mnamo tarehe 7 Dhul-Hija [57] na katika vyanzo vingine inaelezwa kuwa, vilijiri katika siku ya Arafa (tarehe 9 Dhul-Hija) mwaka wa 167 Hijria. [58] Kwa mujibu wa ripoti ya Bayhaqi katika "Lubab al-Ansab", baada ya kifo cha Sahib Fakhkh, Imamu Kadhim aliuswalia mwili wake. [59]

Matokeo

Baada ya harakati ya Sahib Fakhkh, gavana wa Madina, alichoma nyumba na mashamba na mitende ya Hussein na kundi la familia yake na kuwanyang'anya sehemu nyingine ya mashamba na mali zao. [60] Musa Ibn Issa, mmoja wa mawakala wa Bani Abbas, pia alikwenda Madina na kwa kuwaita watu wa mji huo msikitini kuwalazimisha wamseme vibaya na hadharani Hussein pamoja na masahaba zake. [61]

Kuna taarifa zinazokinzana kuhusu radiamali ya Hadi Abbasi kwa tukio la Fakhkh. [62] Kwa mujibu wa ripoti ya Razi, wakati Qassim bin Muhammad bin Abdullah alipokamatwa na kupelekwa kwa Hadi, mtawala huyo aliamuru viungo vyake vyote vya mwili vikatwe vipande vipande kwa msumeno. [63] Pia, kwa amri yake, vichwa vya baadhi ya mateka vilitenganishwa na mwili. [64] Kwa upande mwingine, kuna ripoti zingine. Kulingana na baadhi ya ripoti hizo, aliwashughulikia na kukabilian avibaya na wauaji wa tukio la Fakhkh na akaamuru mali zao ziporwe. [65] Kwa mujibu wa riwaya nyingine, Hadi Abbasi alilia alipoona vichwa vya mashahidi wa Fakhkh na kuwanyima wauwaji ujira wao na alihesabu kuwa hiyo ni adhabu ndogo zaidi wabayoweza kupatiwa. [66] Baadhi ya waandishi wanaamini kwamba, Hadi Abbasi, ili kuwatuliza wapinzani na kutuliza hali ya mambo katika jamii alijionyesha kuwa amechukizwa na matukio hayo ilihali si kweli. [67]

Watoto wa Abdullah Mahdh, yaani Suleiman, Idris na Yahya, walikuwepo kikamilifu katika tukio hili. [68] Suleiman bin Abdullah na Hassan bin Muhammad bin Abdullah Mahadh waliuawa katika tukio hili. [69] Idris bin Abdullah alinusurika katika tukio la Fakhkh na kubakia hai. Alikimbilia Maghrib. na kuanzisha serikali ya Idrisia huko. [70]. Yahya bin Abdullah pia alinusurika kwenye vita vya Fakhkh na akakimbilia Deylam. [71] Harun al-Rashid alimwita Baghdad baada ya kumuandikia barua ya kumpa amani; lakini alimtia mbaroni na kumtia gerezani na hatimaye akaaga dunia akiwa kifungoni. [72]

Sababu ya kushindwa

Baadhi ya watafiti wamezingatia masuala yafuatayo kama sababu za kushindwa kwa harakati ya Sahib Fakh:

  • Kuanzishwa harakati kabla ya wakati uliokuwa umepangwa na kabla ya kuandaa vikosi.
  • Kutokuwa pamoja na harakati hiyo baadhi ya shakhsia wakubwa wa Alawi.
  • Kukiuka ahadi baadhi ya masahaba.
  • Kuanzishwa harakati katika masiku ya ibada ya Hija, kutokana na watu wa Makka na Madina kushughulishwa na masuala ya kiuchumi.
  • Kutokuwa pamoja na harakati hiyo shaksia wakubwa wa Makka.
  • Kutokuwa pamoja na harakati hiyo shaksia wakubwa wa Madina.
  • Kutokuwa mwafaka anga ya Hijaz kwa ajili ya harakati. [73].

Eneo la Fakhkh

Eneo la Fakh au kitongoji cha Mashahidi wa Makka liko kwenye mlango wa kaskazini wa Makka na liko umbali wa kilomita nne kutoka Masjid al-Haram. [74] Eneo hili lilikuwa makakaburi ya baadhi ya masahaba. [75] Kulingana na watafiti, makaburi ya mashahidi wa Fakhkh katika kitongoji cha mashahidi wa Makka yanagawanyika katika sehemu mbili; [76] Baadhi ya mashahidi wa harakati ya fakhkh wamezikwa katika eneo la moja ambalo lina bango ukutani ambalo limeandikwa “Makaburi ya Abdallah bin Omar, namba 2”. Makabauri mengine yapo mkabala wake katika eneo la jirani kabisa na mlima Fakhkh (Jabal al-Burud) au Jabal al-Shahid. [77] Hapo ndipo yanapopatikana makaburi hayo mengine. [78] Mwaka 601 Hijria, eneo la ziara la Swahib Fakhkh lilijengewa. [79]. Kando ya mlima Fakhkh, kuna eneo linalojulikana kwa jina la Dhi-Tuwa ambapo inaelezwa kwamba, ilikuwa sehemu ya vikao vya kabila la Qureshi katika tukio la Sulh al-Hudaybiyah. [80]

Monografia

Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa kuhusiana na maudhui ya tukio la Fakhkh ni:

  • Akhbar Fakhkh, (Habari za Fakhkh) mwandishi: Ahmad bin Sahl Razi. Kitabu hiki kiliandikwa katika karne ya 4 Hijria na kinahesabiwa kuwa kitabu kikongwe na cha kale zaidi kuhusiana na tukio la Fakhkh. [81] Inaelezwa kuwa, katika kitabu hiki kuna nyaraka ambazo hazipatikana katika vyanzo na vitabu vingine. [82]
  • Mahiyat Qiyam Shahid Fakhkh, (Utambulisho wa Harakati ya Fakhkh) mwandishi: Abul-Fadh Radhawi Ardekani. [84]
  • Batwal Fakhkh (Shujaa wa Fakhkh); mwandishi: Muhammad Hadi Amini. [86]