Badr al-Din al-Houthi
Badr al-Din al-Houthi (Kiarabu: بدرالدين الحوثي) (1431-1345 H) ni mwanazuoni wa Kizaydiyyah na kiongozi wa kiroho wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen. Ni baba wa Hussein Badreddin al-Houthi, mwanzilishi wa Harakati ya Ansarullah. Baada ya Hussein kuuawa, Abdul-Malik al-Houthi, mtoto mwingine wa Badr al-Din, alichukua uongozi wa harakati hiyo.
Badr al-Din Houthi alikuwa mmoja wa waungaji mkono wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, waungaji mkono wa umoja wa Kiislamu na muungaji mkono wa Palestina. Ameandika vitabu kadhaa, ikiwemo al-Taysir fi al-Tafsir. Kazi zilizoandikwa za Badr al-Din kuhusu Uwahabi zimekusanywa katika mjumuiko unaojulikana kama al-Silsal al-Dhahabiyyah fi al-Radd Alaa al-Wahhabiyyah. Abdul-Malik al-Houthi ambaye ni kiongozi wa tatu wa Harakati ya Ansarullah ni mtoto wake wa tatu.
Nafasi na Umuhimu
Badr al-Din Houthi, ni kiongozi wa kiroho wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen na anahesabiwa kuwa mmoja wa viongozi wa kidini wa madhehebu ya Zaidiyyah Jarudiyya. [1] Anatambulika kwa lakabu kama Allamah, Mujahidi [2], mfasiri wa Qur'an na Mujitahidi. [3]
Al-Houthi alikuwa mmoja wa watetezi wa umoja wa Kiislamu. [4] Alikuwa amilifu katika kukabiliana na fikra na imani dhidi ya Uislamu na dini ya Ahlul-Bayt. [5] Ana athari pia katika uga wa elimu mbalimbali za Kiislamu na ameandika kitabu kupinga kundi la Uwahabi. [6]
Fikra
Badr al-Din al-Houthi alizingatia na kutoa kipaumbele kwa suala la Palestina na kukabiliana na Israel na aliona kuwa ni jambo la lazima kuwaunga mkono wanyonge. [7] Aliunga mkono msimamo na hatua za mwanawe Hussein katika kukabiliana na Marekani kwa kutoa kaulimbiu ya Sarkha na kususia bidhaa za Marekani na Israel. [8]
Badr al-Din alikuwa akiuona umoja wa Kiislamu kuwa ni jambo muhimu na la dharura kwa ajili ya kukabiliana na hatari kubwa ambazo Waislamu wanakabiliwa nazo. [9] Aidha alikuwa akitaka kuchukuliwa misimamo mwafaka katika uwanja huo. [10]
Itikadi za al-Houthi zinachukuliwa kuwa karibu na Shia Imamiyyah. [11] Yeye anawatambua kuwa makafiri wale maadui wa Imamu Ali (a.s) ambao walikuwa wakijua kwamba, haki ipo pamoja na Imamu Ali lakini wakasimama kupigana naye. [12]
Himaya na Kuathirika Kwake na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Badr al-Din al-Houthi alikuwa mmoja wa wafuasi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. [13] Inasemekana kwamba alisherehekea mafanikio ya kijeshi ya Iran katika vita vya Iran na Iraq na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kufyatua risasi hewani. [14] Kadhalika mwamko wa fikra za Harakati ya Ansarullah ya Yemen ambayo inamtambua kama baba yake wa kimanaawi chimbuko lake ni Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. [15] Sera zake na za watoto wake pia zinazingatiwa kuwa zinalingana na sera za Iran. [16]
Badr al-Din alisafiri hadi Iran na mwanawe Hussein mwaka 1994. [17] Wengine wamesema kwamba alirudi Yemen mwaka wa 2002 [18] na wengine wamesema kwamba alikaa Iran kwa mwaka mmoja. [19]. Baadhi wamedai kwamba, akiwa Iran yeye na mwanawe waliathirika na Madhehebu ya Shia Ithnaasharia. Na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Ansarullah imechukuliwa kuwa ni harakati ya Maimamu Kumi na Mbili wa Shia; lakini Wahouthi wanakataa dai hili na kusisitiza utambulisho wao kwamba, ni Zaydiyyah. [20]
Harakati za Kisiasa
Baada ya kifo cha kishahidi cha mwanawe Hussein Badreddin al-Houthi alichukua uongozi wa Harakati ya Ansarullah. [21] Kwa msaada wa baadhi ya wanachuoni wa Kizaydiyyah, alianzisha Hizb al-Haq. [22] Al-Houthi alikuwa miongonii mwa wanachama muhimu wa chama hiki [23] ambaye kutokana na kuibuka hitilafu ndani ya chama hicho, alijitenga na kuanzisha chama cha Shabab al-Mu'min. [24]
Ufisadi, serikali kutokuwa na utendaji unaofaa na ushawishi na uingiliaji kati wa wageni, hasa Marekani, nchini Yemen ulisababisha Badr al-Din al-Houthi kuwatolea wito wanafunzi wake kupigana na serikali. [25] Mgogoro na makabiliano hayo yalifikia hatua ya vita vya kijeshi na na Badr al- Din akalazimika kuondoka Yemen [26].
Inasemekana kuwa, Badr al-Din amelengwa mara kadhaa na njama za kumuua bila mafanikio baada ya kusurika kifo mara zote hizo. Alipolengwa katika kijiji cha Al-Kharb, idadi kadhaa ya watu wa familia yake waliuawa. [27] Pia, operesheni ya jaribio la kumuua iliyofeli mnamo 2005 ilipelekea kuanza vita vya pili kati ya al-Houthi na serikali ya Yemen, na vita vilisimamishwa wakati ilipodhaniwa kuwa Badr al-Din ameuawa [28].
Sifa Maalumu za Kiakhlaqi
Wanazuoni wa zama za Badr al-Din al-Houthi, wamejitokeza na kumsifu sana. [29] Majd al-Din Muayidi amemchukulia kuwa ni mwanachuoni mwenye bidii na akasifu fikra yake. [30] Hussein bin Hassan alimuelezea kuwa ni mchamungu, mwenye kujinyima (kukinai na kuipa mgongo dunia), mnyenyekevu na mwenye kushikamana na ibada na akamtambulisha kama mtetezi wa shule (maktaba ya kifikra) ya Ahlul-Bayt. [31] Pia, kwa mujibu wa Abdul-Malik al-Houthi, alikuwa anaifahamu Qur'ani, alishikamana nayo na aliizingatia sana [32] Qur'ani. [33]
Athari
- Makala Kuu: Fahasara ya athari za Badr al-Din al-Houthi
Badr al-Din al-Houthi ana athari kadhaa, ambazo idadi yake ni karibu kazi 100. [34] Katika kitabu chake Al-Taysir fi al-Tafsir, ametumia mbinu ya kufasiri Qur'ani kwa Qur'ani na tafsiri ya hadithi kwa kuzingatia hadithi za Mtume (s.a.w.w) na Imam Ali (a.s). [35] Katika kitabu cha al-Majmuat al-Wafiyah Fi al-Fiat al-Baghiyah, amechambua kisa cha Ammar bin Yasir cha kuuawa na kundi la wavamizi. [36]
Ameandika vitabu vya Fadhail Aal-Muhammad (a.s), Ahadith Mukhtarah fi Fadhail Aal Bayt na Ayat al-Mawadah kuhusu Ahlul-Bayt (a.s). [37] Kazi zake kuhusu Aidha ameandika vitabu kama: Man hum al-Wahabiyyah na al-Ijaz fi radd ala fatawa al-Hijaz vitabu ambavyo vinauokosoa na kuupinga Uwahabi. Athari yake ya majibu dhidi ya Uwahabi imechapishwa ikiwa katika majimui ya al-Silsilat al-Dhahbiya Fi Radd alal-Wahabiyyah. [38]
Historia Yake
Alizaliwa tarehe 17 Jumadi al-Awwal mwaka 1345 Hijria huko Dhahyan, Yemen, na akakulia Sa'dah, iliyokuwa kituo kikuu cha Zaidiyyah huko Yemen. [39] Nasaba na ukoo wake unarejea nyuma na kufika kwa Hassan Muthanna, mtoto wa Imamu Hassan (a.s). [40] Nasaba ya familia ya Houthi inayoishi Sa'dah inarudi na kufika kwa Hussein bin Muhammad, ambaye alihama kutoka mji wa Houth hadi Dhahyan. [41]
Masomo
Badruddin al-Houthi alisoma elimu yake huko Sa’dah na baba yake Amiruddin Hussein Houthi (aliyefariki: 1394 H) na ami yake Hassan bin Hossein Houthi (aliyefariki: 1388 H. [42] Pia alinufaika na Abdul Aziz Ghalibi na Yahya bin Hussein Houthi. [43] Badr al-Din alipata ruhusa ya ijtihadi kutoka kwa baadhi ya wanachuoni ambao majina yao yametajwa katika Miftah Asanid Al-Zaydiyyah. [44]
Kifo
Badr al-Dudin al-Houthi alikufa mwishoni mwa 2010. Wahouthi waliripoti sababu ya kifo chake kuwa ni ugonjwa wa mapafu. Kundi la Al-Qaeda nchini Yemen lilidai kumuua wakati wa operesheni. [45] Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa havikukubali madai ya kundi la Al-Qaeda ya kuuawa Badr al-Din. [46]
Watoto
Kulingana na baadhi ya ripoti, Badr al-Din al-Houthi alikuwa na wake wanne [47] na alikuwa na binti saba na watoto 13 wa kiume. [48] Hussein, Yahya, Abdul Qadir, Muhammad, Ahmad, Hamid, Amiruddin, Ibrahim, Abdul-Malik, Ali, Abdul Khaliq, Abdul Salam na Najmuddin ni watoto wake wa kiume. [49] Hussein, mwanzilishi wa Ansarullah ya Yemen, Abdul Qadir na Ali waliuawa katika vita [50] na Ibrahim aliuawa katika tukio la njama ya mauaji. [51] Abdul Malik pia ni kiongozi wa tatu wa Yemen Harakati ya Ansarullah.