Dua ya Arubaini na Tano ya kitabu cha Sahifa Sajjadiya
Dua ya Arubaini na Tano ya Sahifa Sajjadiya (Kiarabu: الدعاء الخامس والأربعون من الصحيفة السجادية) ni dua iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s), aliyokuwa akiitumia kama ni dua ya kuhitimishia na kuagia mwezi wa Ramadhani. Katika dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anachanganua neema za Mwenye Ezi Mungu juu ya viumbe Wake, huku akisisitiza dhana ya Mwenye Ezi Mungu ya kutohitajia waja Wake waja, pamoja na kuwasilisha shukrani kutokana na fadhila za Mola wake juu yake. Zaidi ya hayo, pia Imamu Zain al-Abidin (a.s.) ameitumia dua hii kwa ajili ya kuuaga mwezi wa Ramadhani wakati pamoja na kuorodhesha sifa bainifu za mwezi huo. Kupitia dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anamuomba Mola wake amuwafikishe kuushuhudia mwezi wa Ramadhani wa mwaka unaofuata. Maudhui ya toba pamoja na ulazima wa kutubia, ni maudhui nyengine iliyomo ndani ya muktadha wa dua hii. Ndani ya dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anasisitiza ulazima wa kuomba toba ndani ya Siku Kuu ya Idi al-Fitr, pamoja na umuhimu wa kuwaombea fanaka waja wengine, na kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Aali zake watoharifu.
Dua ya Arubaini na Tano imefasiriwa na kushereheshwa kupitia kupitia tafsiri kadhaa chambizi za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Kwa upande wa lugha ya Kiajemi, miongoni mwa vitabu vilivyotoa huduma hii ni kama vile; Diare Asheqan kazi ya Hussein Ansarian, na Shuhud wa Shenakht kazi ya Hassan Mamduhi Kermanshahi. Aidha, kwa upande wa lugha ya Kiarabu, tafsiri chambuzi ya dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, inapatikana katika kitabu kiitwacho Riyad as-Salikin kilichoandikwa na bwana Sayyid Ali Khan Madani.
Mafunzo ya Dua
Dua ya arobaini na tano kutoka kitabu cha Sahifa Sajjadiyya, ni mojawapo ya dua zilikuwa zikizisomwa na Imam Sajjad (a.s) wakati wa kuhitimisha na kuaga mwezi wa Ramadhani. Kulingana na mchambuzi wa dua za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya bwana Mamduhi Kermanshahi, katika maelezo yake kuhusu sala hii, ni kwamba; Imamu Sajjad ameonekana kutumia maneno ya mahuzuniko na yenye hisia za hali juu kabisa katika dua yake hii ya kuuaga mwezi wa Ramadhani. Aidha, amejitahidi ndani yake kutubainishia baadhi ya sifa maridadi za mwezi huu, pamoja na kutuwekea wazi wajibu wa muumini katika kipindi hicho. Amefanya hivyo ili aweze kutupa vigezo vya matendo mema vitakavyoweza kutumika kama ni mwongozo wa matendo yetu kwa kwa jili ya kujiandaa na Ramadhani ya mwaka unaofuata. [1] Mafunzo ya dua hii yameelezwa katika vifungu vifuatavyo:
- Mwenye Ezi Mungu kutotaka malipo: Mungu hawapi waja neema Zake ili alipwe.
- Sifa ya Mwenye Ezi Mungu ya kutohitaji: Mwenye Ezi Mungu hana haja na viumbe Vyake hata kidogo.
- Mungu kutojuta katika utoaji wake: Mwenye Ezi Mungu hajuti kamwe kwa fadhila anazowapa waja Wake (sifa ya majuto haipo katika dhati Yake).
- Kutokuwepo ukomo wa mipaka ya Mungu: Dhati ya Mwenye Ezi Mungu, na pia Majina na Sifa Zake, havina ukomo.
- Utoaji malipo uliopindukia mipaka: Mwenye Ezi Mungu huwapa waja malipo makubwa zaidi ya stahili ya matendo yao.
- Adhabu ya Mungu ni uadilifu mtupu: Adhabu anayoitoa Mungu inalingana na uadilifu Wake kamili.
- Msamaha wa Mungu ni fadhila: Mwenye Ezi Mungu husamehe dhambi za waja kwa fadhila Zake, si kwa kuwa wamestahiki.
- Utoaji neema bila masimango: Mungu huwaneemesha waja Wake bila kuwasimanga.
- Upole wa Mungu kwa waja wenye shukrani: Mungu huwaonyesha upole wa kipekee waja Wake wanaomshukuru.
- Kusitiriwa kwa dhambi za waja: Mwenye Ezi Mungu ni mwenye kuficha na kusitiri aibu na dhambi za waja Wake.
- Uvumilivu wa Mungu dhidi ya uasi: Mungu ni mvumilivu anapoasiwa na waja Wake.
- Ubora wa Ramadhani: Mwezi wa Ramadhani ni mbora kuliko nyakati zote za mwaka kutokana na kuteremshwa Qur'ani na nuru ya Kiungu ndani yake.
- Ramadhani, ni mwezi wa neema: Mwezi wa Ramadhani unabeba baraka na manufaa makubwa zaidi kwa walimwengu wote.
- Ramadhani ni Mwezi Mtukufu wa Mwenye Ezi Mungu: Huu ni mwezi mkuu zaidi wa Mwenye Ezi Mungu na ni sikukuu (Eid) kwa wapenzi Wake.
- Ramadhani, mwandani mtukufu: Ni mwandani na mgeni mtukufu ambaye usuhuba naye unapendeza na kutuliza moyo.
- Ramadhani, jirani mwema: Ni jirani ambaye uwepo wake hulainisha nyoyo za watu na kuwafanya wahurumiane.
- Ramadhani, mwezi wa kutimizwa haja: Ni mwezi ambao matumaini na haja za waja hutimizwa.
- Ramadhani, msaidizi dhidi ya Shetani: Mwezi huu ni msaada mkubwa katika vita dhidi ya Shetani (Saumu ni silaha bora ya kumshinda Shetani).
- Ramadhani, mwezi wa msamaha: Ni mwezi ambao dhambi nyingi husamehewa ndani yake.
- Athari ya Ramadhani kijamii na kiroho: Mwezi huu huondoa athari za dhambi na kuimarisha uhusiano baina ya watu.
- Athari ya Ramadhani katika safari ya kiroho: Mwezi huu huondoa vizuizi katika njia ya kumuelekea Mwenye Ezi Mungu.
- Ubora wa Waislamu kwa Ramadhani: Mwenyezi Mungu amewatukuza Waislamu juu ya mataifa mengine kwa kuwapa mwezi wa Ramadhani.
- Usiku wa Cheo (Lailatul-Qadr): Usiku mmoja ndani ya Ramadhani (Usiku wa Cheo) ni bora kuliko miezi elfu moja.
- Upendo kwa Ramadhani kabla ya kuja: Mwezi wa Ramadhani unapendwa na kutarajiwa kabla hata haujafika.
- Huzuni ya kuondokewa na Ramadhani: Kuondoka kwa mwezi huu huleta huzuni hata kabla haujamalizika.
- Haiba ya Ramadhani: Mwezi wa Ramadhani una haiba na heshima kubwa katika nyoyo za waumini.
- Ugumu wa Ramadhani kwa waovu: Kwa watu waovu, mwezi huu huonekana mrefu na mgumu.
- Kuiaga Ramadhani kwa huzuni: Kuagana na mwezi wa Ramadhani ni jambo zito na lenye kuhuzunisha.
- Kukiri mapungufu katika Ramadhani: Kukiri kwamba ni haki kidogo sana ya mwezi huu tuliyoweza kuitekeleza.
- Huzuni ya kupioteza Ramadhani: Kuomboleza na kuomba fidia kwa msiba wa kuondokewa na mwezi wa Ramadhani.
- Kutokuwepo mshindani wa Ramadhani: Hakuna siku wala mwezi unaoweza kushindana na hadhi ya Ramadhani.
- Wito wa Mungu kwa ajili ya Toba ya kweli: Mwenye Ezi Mungu anawaita waja Wake wafanye toba ya kweli (Tawbatan Nasuha).
- Mlango wa toba uko wazi: Mlango wa msamaha wa Mungu daima uko wazi kwa anayetubia.
- Kukosa udhuru kwa anayeghafilika: Mtu anayepuuza fursa ya kuingia katika uwanja wa msamaha hatakuwa na udhuru.
- Dua ni ibada: Kuomba dua ni aina ya ibada, na kuacha kuomba ni kiburi.
- Kuomba taufiki ya ibada za usiku: Kuomba msaada wa Mungu ili kuweza kukesha kwa ajili ya ibada ndani ya mwezi wa Ramadhani.
- Kuomba kufaidika na fadhila: Kuomba ili kupata fadhila na baraka za mwezi wa Ramadhani.
- Kuomba msamaha kwa mapungufu: Kumuomba Mungu radhi kwa uzembe na mapungufu yaliofanyika ndani ya mwezi wa Ramadhani.
- Kuomba kuidiriki Ramadhani ijayo: Kuomba kupata uhai na taufiki ya kuushuhudia mwezi wa Ramadhani wa mwaka ujao na kufanya ibada ipasavyo.
- Kuomba malipo mema: Kuomba malipo sawa na ya wale waliofunga na kutekeleza haki za mwezi huu kikamilifu.
- Kuomba jaala (taufiki) ya kuwa miongoni mwa waliobahatika: Kuomba kujumuishwa miongoni mwa watu waliofaulu na kupata heri nyingi za mwezi wa Ramadhani.
- Kuomba kuwa miongoni mwa wanaotubia: Kuomba kuwekwa katika kundi la waja wanaotubia ambao Mungu anawapenda.
- Dua kwa wazazi na Waislamu wote: Kuwaombea wazazi wote, na Waislamu wote, wa kiume na wa kike.
- Dua ya kuomba hali ya hofu na matumaini (Khawf na Rajaa): Kuomba kupata hadhi ya kumuogopa Mungu na kutarajia rehema Zake.
- Kuomba radhia na hifadhi: Kuomba kupata ladha ya yale tunayomuomba Mungu na kuhisi uzito wa yale tunayojilinda kwake.
- Chanzo cha wema na upungufu: Kunasibisha mema yote kwa Mwenyezi Mungu na mapungufu yote kwa mwanadamu mwenyewe.
- Hali za watu Siku ya Kiyama: Tofauti ya hali baina ya waumini na wakosefu wa imani Siku ya Hukumu.
- Biashara yenye faida na Mungu: Mema hulipwa mara kumi, ilhali malipo ya dhambi huandana na kiwango cheke tu.
- Uhuru wa mwanadamu kukua kiroho: Mwanadamu amepewa uwezo na hiari ya kukua na kufikia daraja za juu.
- Mipango wa Mungu na maumbile ya mwanadamu: Mipango ya Mungu inaendana na maumbile asilia ya mwanadamu (Fitra).
- Shukrani kwa neema ya Uislamu: Kumshukuru Mungu kwa kuongoza kwenye dini Yake teule.
- Mwongozo wa Mungu wa kuwaongoza waja Wake kwenye dini sahihi: Ni Mungu pekee ndiye anayeongoza kwenye dini kulingana na mwenendo anaouridhia.
- Kiburi ni kizuizi cha dua: Kujiona na kuwa kiburi humzuia mja kufanya ibada na maombi.
- Lugha ya Qur'ani ndio njia bora zaidi ya ulinganiaji: Qur'ani inatoa njia bora zaidi ya kuwaita watu kwa Mwenyezi Mungu.
- Wahyi ndio njia ya kuijua ghaibu: Ni kwa njia Wahyi tu, ndipo siri za ulimwengu usioonekana zaweza kufahamika.
- Hisani na Fadhila za Mwenye Ezi Mungu ni sababu ya sifa Zake: Wema na fadhila za Mungu ndizo sababu kuu za Yeye kusifiwa.
- Umuhimu wa kutumia umri: Ulazima wa kutumia rasilimali ya umri ili kufikia daraja za juu za ubinadamu.
- Toba ya Eid al-Fitr: Umuhimu wa kufanya toba isiyokuwa na marejeo ya dhambi katika siku ya Eid al-Fitr.
- Eid al-Fitr, siku ya furaha: Eid al-Fitr ni siku ya furaha na shangwe kwa waumini.
- Kutawakali kwa Mungu: Kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila jambo.
- Dua: Dua ya kuwatakia kheri wazazi wakiume na wakike pamoja na Waislamu kwa jumla
- Kumswalia Mtume (s.a.w.w) na Aali zake:
- Kumuombea rehema bwana Mtume (s.a.w.w): Kumuombea rehema na amani Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Aali zake, rehema ziendazo sawa na zile za Malaika waliokurubishwa mbele ya Mwenye Ezi Mungu.
- Kuomba baraka za Swala: Kuomba kupata baraka na manufaa yatokanayo na kumswalia Mtume na Aali zake. (s.a.w.w)
- Swala ni njia ya kujibiwa dua: Kuomba dua ikubaliwe kwa wasila wa (kwa nia ya) kumswalia Mtume na Aali zake. (s.a.w.w)
- Swala ni kumshukuru bwana Mtume (s.a.w.w): Kumswalia Mtume (s.a.w.w), ni njia ya kumshukuru na kuyahuisha mafundisho yake. [2]
Tafsiri Chambuzi za Dua ya Arubaina na Tano
Hakika, Dua ya 45 ya Sahifa Sajjadiya, ambayo ni dua ya kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni dua iliobahatika kufasiriwa na kuchambuliwa kwa lugha kadhaa kupitia wanazuoni mbali mbali ulimwenguni. Dua imefasiriwa sambamba na dua nyengine zilizomo ndani ya Kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa vitabu mashuhuri zilizoandikwa kwa lugha ya Kifarsi kuhusiana na kazi hiyo ni pamoja na: Kitabu kiitwacho "Diare Ashiqan", ambacho kazi ya mwanazuoni mashuhuri aitwaye Sheikh Hussein Ansarian. [3] Katika kazi yake hii kubwa, amefafanua kwa kina maana ya mafunzo yaliyomo ndani ya dua zote za Sahifa Sajjadiya, ikiwemo Dua hii ya 45. Cha pili ni kitabu kiitwacho "Shuhud wa Shinakht", kazi ya mwanachuoni ajulikanaye kwa jina la Hassan Mamdouhi Kermanshahi. [4] Kazi nyengi muhimu iliyoandikwa kwa lugha ya Kifarsi inapatikana katika kitabu kiitwacho "Sharhe wa Tarjumeye Sahife Sajjadiyyeh", kitabu kilichoandikwa na mwandishi aitwayr Sayyid Ahmad Fehri. [5]
Tafsiri chambuzi nyengine muhimu kuhusiana na Dua hii, inapatikana katika vitabu viliwili muhimu vilivyojitenga kwa ajili ya kuchambua dua za kuukaribisha pamoja na dua ya kuuaga mwezi wa Ramadhani zilizokuwa zikitumiwa na Imamu Sajjad (a.s). Vitabu viwili hivyo ni: "Simaye Ramadhan" kilichoandikwa na Ali Karimi Jahromi, [6] na "Suruush Ramadhan" (ufafanuzi wa dua za Imamu Sajjad mwanzoni na mwishoni mwa mwezi wa Ramadhani) kilichoandikwa na Sayyid Reza Bagherian Movahed na Ali Baqiri-Far. Katika vitabu hivi, waandishi wamechambua nyanja mbalimbali kuhusiana na mwezi wa Ramadhani. Pia, wamegusia baadhi ya fadhila za Eid al-Fitr na adabu za kutoka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Vitabu hivi vinatoa mwongozo wa kina kabisa kuhusiana na jinsi ya kuukaribisha na kuuga mwezi huu mtukufu, vikijikita katika mafundisho ya Imamu Sajjad kama yanavyopatikana katika Sahifa Sajjadiyya. [7]
Pia tafsiri ya dua ya 45 ya kitabu cha Sahifa Sajjadiya imefanyiwa kazi na wasomi mbalimbali kupitia lugha ya asili ya dua hiyo (Kiarabu). Miongoni mwa kazi hizo mashuhuri ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Riyadh as-Salikin’ cha Sayyid Ali-Khan Madani [8] na ‘Fi Dhilali as-Sahifat as-Sajjadiyya’ cha Muhammad Jawad Mughniya. [9] Vilevile, mchango wa Muhammad bin Muhammad Darabi katika kitabu ‘Riadhu al-Arifin’ [10] na wa Sayyid Muhammad Hussein Fadlallah katika kitabu kiitwacho ‘Afaq ar-Ruh’, [11] ni miongoni mwa muhimu zilizoandikwa kwa lugha ya Kiarabu kuhusiana na dua ya arubaini na tano sambamba na dua nyengine za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Aidha kuna vitabu maalumu vilivyoshughulikia upande wa istilahi na msamiati wa dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya. Wanazuoni walichukua jukumu hili ni pamoja na; Faidu Kashani katika kitabu chake ‘Ta'liqat 'ala as-Sahifat as-Sajjadiyya’ [12] na bwana Izzu ad-Din al-Jaza'iri katika kitabu chake ‘Sharhu as-Sahifatu as-Sajjadiyya’. [13]
Matini ya Dua ya Arubaini na Tano Pamoja na Maelezo Yake kwa Kiswahili
وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ فِی وَدَاعِ شَهْرِ رَمَضَانَ Na ifuatayo ilikuwa miongoni mwa dua zake (amani iwe juu yake) aliyokuwa akiiomba wakati wa kuuaga mwezi wa Ramadhani. اللَّهُمَّ يَا مَنْ لَا يَرْغَبُ فِي الْجَزَاءِ
Ewe Mwenye Ezi Mungu, Ewe ambaye huna raghba ya kupokea malipo. وَ يَا مَنْ لَا يَنْدَمُ عَلَى الْعَطَاءِ
Na Ewe ambaye kamwe hajutii utoaji Wako. (Na Ewe, Mpaji usiye na majuto juu ya fadhila Zako kwa viumbe Wako).
وَ يَا مَنْ لَا يُكَافِئُ عَبْدَهُ عَلَى السَّوَاءِ.
Na Ewe yule ambaye hamlipi mja wake malipo yanayolingana tu na tendo lake (bali daima malipo yake ni makubwa zaidi ya matendo yake)
مِنَّتُكَ ابْتِدَاءٌ، وَ عَفْوُكَ تَفَضُّلٌ، وَ عُقُوبَتُكَ عَدْلٌ، وَ قَضَاؤُكَ خِيَرَةٌ
Neema Zako ni za awali (zilizokuja bila ya kutanguliwa na amali fulani), msamaha Wako ni fadhila (za ziada), adhabu Yako ni uadilifu (kamilifu), na hukumu Yako ndiyo kheri (bora kabisa). إِنْ أَعْطَيْتَ لَمْ تَشُبْ عَطَاءَكَ بِمَنٍّ، وَ إِنْ مَنَعْتَ لَمْ يَكُنْ مَنْعُكَ تَعَدِّياً.
Unapotoa, huwa huuchafui (huuambatanishi) utoaji wako na masimango fulani; na pale unaponyima, kunyima kwako huwa si kitendo cha udhalimu (si hujuma fulani). تَشْكُرُ مَنْ شَكَرَكَ وَ أَنْتَ أَلْهَمْتَهُ شُكْرَكَ
Wewe wamkubali kwa malipo yule anayeshukuru, na hali ya kuwa ni Wewe Mwenyewe ndiye uliyemfunulia maarifa na kumpa msukumo wa kukushukuru. وَ تُكَافِئُ مَنْ حَمِدَكَ وَ أَنْتَ عَلَّمْتَهُ حَمْدَكَ.
Nawe humlipa yule anayekuhimidi, ilhali ni Wewe ndiye uliyempa uwezo na maarifa ya kukuhimidi.
تَسْتُرُ عَلَى مَنْ لَوْ شِئْتَ فَضَحْتَهُ، وَ تَجُودُ عَلَى مَنْ لَوْ شِئْتَ مَنَعْتَهُ، وَ كِلَاهُمَا أَهْلٌ مِنْكَ لِلْفَضِيحَةِ وَ الْمَنْعِ غَيْرَ أَنَّكَ بَنَيْتَ أَفْعَالَكَ عَلَى التَّفَضُّلِ، وَ أَجْرَيْتَ قُدْرَتَكَ عَلَى التَّجَاوُزِ.
Unamsitiri yule ambaye kama ungelitaka, ungemfedhehesha; na unamkirimu yule ambaye kama ungelitaka, ungemnyima. Na wote wawili, kwa haki kabisa, ni wenye kustahili kutoka Kwako fedheha pamoja na kunyimwa. Hata hivyo, Wewe umeujenga mwenendo wa matendo Yako juu ya fadhila (juu ya msingi wa hisani), na umeuelekeza uwezo Wako kwenye msamaha. وَ تَلَقَّيْتَ مَنْ عَصَاكَ بِالْحِلْمِ، وَ أَمْهَلْتَ مَنْ قَصَدَ لِنَفْسِهِ بِالظُّلْمِ، تَسْتَنْظِرُهُمْ بِأَنَاتِكَ إِلَى الْإِنَابَةِ، وَ تَتْرُكُ مُعَاجَلَتَهُمْ إِلَى التَّوْبَةِ لِكَيْلَا يَهْلِكَ عَلَيْكَ هَالِكُهُمْ، وَ لَا يَشْقَى بِنِعْمَتِكَ شَقِيُّهُمْ إِلَّا عَنْ طُولِ الْإِعْذَارِ إِلَيْهِ، وَ بَعْدَ تَرَادُفِ الْحُجَّةِ عَلَيْهِ، كَرَماً مِنْ عَفْوِكَ يَا كَرِيمُ، وَ عَائِدَةً مِنْ عَطْفِكَ يَا حَلِيمُ.
Nawe umewakabili (umewapokea) walio kuasi kwa sifa ya upole, na ukawapa muhula wale waliozidhulumu nafsi zao (kwa makusudi). Unawapa fursa (waja hao) kwa subira Yako ili wapate kurejea Kwako, na unaacha kuwapatiliza kwa adhabu ya haraka, ili waelekee kwenye toba (Yako). Lengo ni kwamba; asiangamie mwenye kuangamia miongoni mwao, kwa ajili Yako, na wala asije hasirika mwenye kuhasirika miongoni mwa waovo wao, kwa neema Yako (kupitia neema Yako), isipokuwa baada ya kupewa visingizio (mbali mbali vya kumrejesha kwako) kwa kipindi kirefu, na baada ya kusimamishwa mfululizo wa hoja thabiti dhidi yake. Hili latokana na ukarimu unaochipua (unaomea) kutoka kwenye msamaha Wako, Ewe Mkarimu, na hili larejea kwenye (chimbuko la) huruma Yako, Ewe Mpole.
أَنْتَ الَّذِي فَتَحْتَ لِعِبَادِكَ بَاباً إِلَى عَفْوِكَ، وَ سَمَّيْتَهُ التَّوْبَةَ، وَ جَعَلْتَ عَلَى ذَلِكَ الْبَابِ دَلِيلًا مِنْ وَحْيِكَ لِئَلَّا يَضِلُّوا عَنْهُ، فَقُلْتَ- تَبَارَكَ اسْمُكَ-: «تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَصُوحاً عَسى رَبُّكُمْ أَنْ يُكَفِّرَ عَنْكُمْ سَيِّئاتِكُمْ وَ يُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهارُ
Wewe ndiye uliyefungua mlango wa msamaha (Wako) kwa ajili ya waja wako, na ukaupa jina la 'Toba'. Na uliweka mwongozo maalumu kwa ajili ya mlango huo ndani ya ufunuo Wako, ili (waja Wako) wasije kuupoteza (mlango huo). Kisha ukasema—Jina lako litukuke—: "Mgeukieni (mwelekeeni) Mwenye Ezi Mungu kwa toba ya kweli, huenda Mola wenu akakufutieni makosa yenu na kukuingizeni kwenye bustani zipitwazo mito (ya fakhari) chini yake... يَوْمَ لا يُخْزِي اللَّهُ النَّبِيَّ وَ الَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ، نُورُهُمْ يَسْعى بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَ بِأَيْمانِهِمْ، يَقُولُونَ: رَبَّنا أَتْمِمْ لَنا نُورَنا، وَ اغْفِرْ لَنا، إِنَّكَ عَلى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ» فَمَا عُذْرُ مَنْ أَغْفَلَ دُخُولَ ذَلِكَ الْمَنْزِلِ بَعْدَ فَتْحِ الْبَابِ وَ إِقَامَةِ الدَّلِيلِ!
Siku ambayo (katu) Mwenye Ezi Mungu hatamfedhehesha (hatomshusha hadhi) Mtume (Wake pamoja) na waumini walioandamana naye; nuru yao itang'ara (ikiangaza) mbele yao na kuliani mwao, (wanatembea huku) wakisema: 'Ee Mola wetu, kamilisha (tutimizie) nuru yetu na utusamehe (makosa yetu), kwa hakika wewe ni muweza juu ya kila jambo.' Hivyo basi, ni hoja gani ya msingi anayoweza kuitoa mtu anayepuuza kuingia katika makazi hayo tukufu, ilhali mlango umekwisha funguliwa na hoja (dalili) zimethibitishwa? وَ أَنْتَ الَّذِي زِدْتَ فِي السَّوْمِ عَلَى نَفْسِكَ لِعِبَادِكَ، تُرِيدُ رِبْحَهُمْ فِي مُتَاجَرَتِهِمْ لَكَ، وَ فَوْزَهُمْ بِالْوِفَادَةِ عَلَيْكَ، وَ الزِّيَادَةِ مِنْكَ، فَقُلْتَ- تَبَارَكَ اسْمُكَ وَ تَعَالَيْتَ-: «مَنْ جاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثالِها، وَ مَنْ جاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلا يُجْزى إِلَّا مِثْلَها«.
(Ewe Mola), na ni Wewe ndiye uliyejipandishia thamani (bei) (kusiana na malipo ya wema) kwa ajili ya waja Wako, ukitaka wapate faida katika biashara yao Kwako, na ili waweze wafuzu wakati wa kuwasili kwao mbele Yako (wakati wa kuja mbele Yako), pia ukawapa nyongeza ya ziada itokayo kwako. Na ulisema – (Ewe Mola ambaye) jina Lako limebarikiwa na Uliyetukuka: “Atakayeleta (atakayekuja na) jema moja, atalipwa (thawabu) mara kumi ya mfano wa jema lake (hilo), na atakayeleta (atakayekuja na) ovu moja, hatalipwa ila mfano wake tu (kwa kiwango cha uvu hilo tu).
وَ قُلْتَ: «مَثَلُ الَّذِينَ يُنْفِقُونَ أَمْوالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنْبَتَتْ سَبْعَ سَنابِلَ فِي كُلِّ سُنْبُلَةٍ مِائَةُ حَبَّةٍ، وَ اللَّهُ يُضاعِفُ لِمَنْ يَشاءُ» وَ قُلْتَ: «مَنْ ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّهَ قَرْضاً حَسَناً فَيُضاعِفَهُ لَهُ أَضْعافاً كَثِيرَةً» وَ مَا أَنْزَلْتَ مِنْ نَظَائِرِهِنَّ فِي الْقُرْآنِ مِنْ تَضَاعِيفِ الْحَسَنَاتِ. Nawe ukasema: 'Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenye Ezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyootesha (iliyozalisha) mashuke saba; katika kila shuke moja kukawa na punje mia. Na Mwenye Ezi Mungu humzidishia amtakaye.' (Qur'an, 2:261). Nawe ukasema: 'Ni nani atakayemkopesha (aliyekuwa tayari kumkopesha) Mwenye Ezi Mungu mkopo mwema, ili amuongezee ongezo la nyongeza nyingi (zilioje)?' (Qur'an, 2:245). Pamoja mengineyo uliyoyateremsha katika Qur'ani (Yako) yanayofanana na hayo, kuhusiana na ungezeko la kuongezeka kwa mema.
وَ أَنْتَ الَّذِي دَلَلْتَهُمْ بِقَوْلِكَ مِنْ غَيْبِكَ وَ تَرْغِيبِكَ الَّذِي فِيهِ حَظُّهُمْ عَلَى مَا لَوْ سَتَرْتَهُ عَنْهُمْ لَمْ تُدْرِكْهُ أَبْصَارُهُمْ، وَ لَمْ تَعِهِ أَسْمَاعُهُمْ، وَ لَمْ تَلْحَقْهُ أَوْهَامُهُمْ، فَقُلْتَ: «فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ، وَ اشْكُرُوا لِي وَ لا تَكْفُرُونِ»وَ قُلْتَ: «لَئِنْ شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ، وَ لَئِنْ كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذابِي لَشَدِيدٌ «.
Nawe (Ewe Mwenyezi Mungu) ndiye Uliyewadhihirishia waja Wako kwa kauli Yako tukufu itokayo katika elimu Yako ya ghaibu, na kuwahimiza kwa nasaha Zako ambazo ndani yake mna heri na fanaka zao. Umewajulisha yale ambayo lau Ungeliwasitiria, kamwe macho yao yasingeweza kuyaona, wala masikio yao yasingeweza kuyaelewa, na wala akili na fikra zao zisingeweza kuyadiriki. Hivyo, Ukasema (uliwajulisha kwa kusema): "Basi nikumbukeni, Nami nitakukumbukeni. Na nishukuruni, wala msinikufuru.” Na Ukasema tena: “Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi akisema: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali. »
وَ قُلْتَ: «ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ، إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ داخِرِينَ»، فَسَمَّيْتَ دُعَاءَكَ عِبَادَةً، وَ تَرْكَهُ اسْتِكْبَاراً، وَ تَوَعَّدْتَ عَلَى تَرْكِهِ دُخُولَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ.
Na (uliwambia) ulitamka wazi kabisa ukasema: "Niombeni, nami nitayaitikia maombi yenu. Hakika, ya wale wanokataa kuniabudu kutoka na jeuri na kiburi chao, bila shaka (hao) wataingia katika moto wa Jahannamu wakiwa katika hali ya udhalili na unyonge (wa hali ya juu)." Kwa mantiki hii, umelifanya tendo la kukuomba (dua), kuwa na hadhi sawa na ibada kamilifu, na ukakieleza kitendo cha kutokuomba, kuwa ni dhihirisho (au akisiko) la majivuno na kiburi. Vilevile, umetoa onyo kali na ahadi ya adhabu kwa wale wanaopuuza amali hiyo, na ukawaahidi kuwatupa ndani ya moto wa Jahannamu huku wakiwa wamedharauliwa na kufedheheshwa.
فَذَكَرُوكَ بِمَنِّكَ، وَ شَكَرُوكَ بِفَضْلِكَ، وَ دَعَوْكَ بِأَمْرِكَ، وَ تَصَدَّقُوا لَكَ طَلَباً لِمَزِيدِكَ، وَ فِيهَا كَانَتْ نَجَاتُهُمْ مِنْ غَضَبِكَ، وَ فَوْزُهُمْ بِرِضَاكَ.
Basi (waja Wako) wakakukumbuka kwa hisani Yako, na wakakushukuru kwa fadhila Zako, na wakakuomba kwa amri Yako, na wakatoa sadaka kwa ajili Yako, wakitafuta ziada (nyongeza) Yako. Na ndani ya hayo ndimo mlimokuwa ukombozi wao wa kuepukana na ghadhabu Zako, pamoja na kufaulu kwao kwa kupata radhi Zako.
وَ لَوْ دَلَّ مَخْلُوقٌ مَخْلُوقاً مِنْ نَفْسِهِ عَلَى مِثْلِ الَّذِي دَلَلْتَ عَلَيْهِ عِبَادَكَ مِنْكَ كَانَ مَوْصُوفاً بِالْإِحْسَانِ، وَ مَنْعُوتاً بِالامْتِنَانِ، وَ مَحْمُوداً بِكُلِّ لِسَانٍ، فَلَكَ الْحَمْدُ مَا وُجِدَ فِي حَمْدِكَ مَذْهَبٌ، وَ مَا بَقِيَ لِلْحَمْدِ لَفْظٌ تُحْمَدُ بِهِ، وَ مَعْنًى يَنْصَرِفُ إِلَيْهِ.
Na lau kiumbe mmoja angelimwongoza kiumbe (mwenziwe) kulingana na (akiitegea) nafsi yake (katika muongozo huo), kisha wake ukawa sawa (ukafanana) na ule ambao umewaongozea waja wako (kutoka) kwako, basi (bila shaka kiumbe huyo) angelisifiwa kwa wema (wake), na angetajwa kwa fadhila (zake), na angehimidiwa kwa kila lugha (kwa mifumo ya lugha mbali mbali). Basi sifa njema zote ni zako (Ewe Mwenye Ezi Mungu) madhali badu kuna nafasi (mahala) ya kuingia sifa Zako hizo, na madhali bado kumebakia lugha (neno) linaloweza kutumika kwa ajili ya kukusifia sifa hizo, na madhali bado kuna nafasi maana inayoweze kuelekea kwenye kazi ya kumsifu na kumhidi Yeye.
يَا مَنْ تَحَمَّدَ إِلَى عِبَادِهِ بِالْإِحْسَانِ وَ الْفَضْلِ، وَ غَمَرَهُمْ بِالْمَنِّ وَ الطَّوْلِ، مَا أَفْشَى فِينَا نِعْمَتَكَ، وَ أَسْبَغَ عَلَيْنَا مِنَّتَكَ، وَ أَخَصَّنَا بِبِرِّكَ!
Ewe Yule ambaye amejisifisha kwa waja wake kupita wema (hisani) na fadhila (Zake), na akawafunika (waja Wake) kwa hisani na ukarimu, ni kiasi gani umeeneza ndani yetu neema Zako, na umetimiza juu yetu hisani Zako, na umetuhusisha (umetuchagua) na wema wako (kwa kutufadhili kwa wema wako)!
هَدَيْتَنَا لِدِينِكَ الَّذِي اصْطَفَيْتَ، وَ مِلَّتِكَ الَّتِي ارْتَضَيْتَ، وَ سَبِيلِكَ الَّذِي سَهَّلْتَ، وَ بَصَّرْتَنَا الزُّلْفَةَ لَدَيْكَ، وَ الْوُصُولَ إِلَى كَرَامَتِكَ
Umetuongoza kwenye Dini Yako tukufu uliyoichagua (kwa ajili yetu), na katika njia Yako ya imani uliyoikubali na kuiridhia. Umeirahisisha Sabili (njia) Yako adhimu kwa ajili, na pia umetufumbulia na kutuonyesha fursa adhimu ya kukaribia Kwako, pamoja na kutuwezesha kufikia utukufu na neema Zako tukufu. اللَّهُمَّ وَ أَنْتَ جَعَلْتَ مِنْ صَفَايَا تِلْكَ الْوَظَائِفِ، وَ خَصَائِصِ تِلْكَ الْفُرُوضِ شَهْرَ رَمَضَانَ الَّذِي اخْتَصَصْتَهُ مِنْ سَائِرِ الشُّهُورِ، وَ تَخَيَّرْتَهُ مِنْ جَمِيعِ الْأَزْمِنَةِ وَ الدُّهُورِ، وَ آثَرْتَهُ عَلَى كُلِّ أَوْقَاتِ السَّنَةِ بِمَا أَنْزَلْتَ فِيهِ مِنَ الْقُرْآنِ وَ النُّورِ، وَ ضَاعَفْتَ فِيهِ مِنَ الْإِيمَانِ، وَ فَرَضْتَ فِيهِ مِنَ الصِّيَامِ، وَ رَغَّبْتَ فِيهِ مِنَ الْقِيَامِ، وَ أَجْلَلْتَ فِيهِ مِنْ لَيْلَةِ الْقَدْرِ الَّتِي هِيَ خَيْرٌ مِنْ أَلْفِ شَهْرٍ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, na Wewe umejaalia (umetuchagulia) mwezi wa Ramadhani, miongoni mwa yale majukumu (Yako), na miongoni mwa faradhi hizo (Zako), mwezi ambao ni chaguo maalumu miongoni mwa miezi (Yako) yote, na ukaupa hadhi (ukauboresha) kuliko zama na nyakati nyengine zote, na kuutukuza kuliko nyakati zote za mwaka mzima, kupitia yale uliyoteremsha ndani yake miongoni mwa Qur'ani na Nuru (Yako), na ukaongeza ndani yake kiwango cha Imani maradufu, na ukafaradhisha ndani yake Saumu, na ukapendekeza ndani yake visimamo (vya usiku), na ukauadhimisha (ukajaalia) ndani yake usiku wa Cheo (Lailatul Qadr) ambao ni bora kuliko miezi elfu. ثُمَّ آثَرْتَنَا بِهِ عَلَى سَائِرِ الْأُمَمِ، وَ اصْطَفَيْتَنَا بِفَضْلِهِ دُونَ أَهْلِ الْمِلَلِ، فَصُمْنَا بِأَمْرِكَ نَهَارَهُ، وَ قُمْنَا بِعَوْنِكَ لَيْلَهُ، مُتَعَرِّضِينَ بِصِيَامِهِ وَ قِيَامِهِ لِمَا عَرَّضْتَنَا لَهُ مِنْ رَحْمَتِكَ، وَ تَسَبَّبْنَا إِلَيْهِ مِنْ مَثُوبَتِكَ، وَ أَنْتَ الْمَلِيءُ بِمَا رُغِبَ فِيهِ إِلَيْكَ، الْجَوَادُ بِمَا سُئِلْتَ مِنْ فَضْلِكَ، الْقَرِيبُ إِلَى مَنْ حَاوَلَ قُرْبَكَ.
Kisha, ukatufadhilisha kwa mwezi huu mtukufu (Ramadhani) juu ya mataifa mengine yote, na kwa fadhila zake ukatuteua sisi miongoni badala ya kaumu nyengine zote za mila (dini) mbali mbali. Hivyo, kwa amri yako tukafunga mchana wake, na kwa msaada wako tukasimama (kwa ibada) usiku wake. (Tumefanya ibada hizo) Tujikurubisha Kwako kupitia saumu na kisimamo chake, tukitaraji rehema Zako ulizotuandalia kupita mwezi huo, na tukatumia mwezi huo kama nyenzo ya tafuta thawabu Zako. Nawe ndiwe hazina wa yale matilaba yatafutwayo kupitia Kwako, Mwingi wa ukarimu kwa yale uombwayo miongoni mwa fadhila Zako, na ndiye uliye karibu mno kwa yeyote yule anayejaribu kujikurubisha Kwako. وَ قَدْ أَقَامَ فِينَا هَذَا الشَّهْرُ مُقَامَ حَمْدٍ، وَ صَحِبَنَا صُحْبَةَ مَبْرُورٍ، وَ أَرْبَحَنَا أَفْضَلَ أَرْبَاحِ الْعَالَمِينَ، ثُمَّ قَدْ فَارَقَنَا عِنْدَ تَمَامِ وَقْتِهِ، وَ انْقِطَاعِ مُدَّتِهِ، وَ وَفَاءِ عَدَدِهِ.
Na kwa kweli mwezi huu umekaa nasi kwa kwa makazi ya heshima na taadhima (kwa makazi ya kuhimidiwa), na umeandamana nasi kwa ushirika ulio mwema, na umetupatia faida bora zaidi kuliko faida za walimwengu wote. Kisha, umeachana nasi pale wakati wake ulipotimia, na baada ya kumazika kwa muda wake, na baada ya kuhitimika (kukamilika) idadi ya siku zake. فَنَحْنُ مُوَدِّعُوهُ وِدَاعَ مَنْ عَزَّ فِرَاقُهُ عَلَيْنَا، وَ غَمَّنَا وَ أَوْحَشَنَا انْصِرَافُهُ عَنَّا، وَ لَزِمَنَا لَهُ الذِّمَامُ الْمَحْفُوظُ، وَ الْحُرْمَةُ الْمَرْعِيَّةُ، وَ الْحَقُّ الْمَقْضِيُّ، فَنَحْنُ قَائِلُونَ: السَّلَامُ عَلَيْكَ يَا شَهْرَ اللَّهِ الْأَكْبَرَ، وَ يَا عِيدَ أَوْلِيَائِهِ.
Basi, sisi ni waagaji tunaoaga muago wenye sifa ya muago anaoagwa nao yule ambaye; ni jambo zito na la huzuni kubwa kwetu kuweza kutengana naye, na kuondoka kwake kumetugharikisha kwenye (mkondo wa) majonzi na upweke. Nasi kwa ajili yake, tunalazimika kutunza ahadi iliyohifadhiwa (baina yetu), na kutunza ile heshima iliyozingatiwa (baina yetu), pia kutunza ile haki ambayo tayari imekwisha timizwa (baina yetu). Hivyo basi, tunatamka tukisema: Amani iwe juu yako, Ewe Mwezi mkuu wa Allah, na Ewe Sikukuu ya vipenzi vyake. السَّلَامُ عَلَيْكَ يَا أَكْرَمَ مَصْحُوبٍ مِنَ الْأَوْقَاتِ، وَ يَا خَيْرَ شَهْرٍ فِي الْأَيَّامِ وَ السَّاعَاتِ.
Amani iwe juu yako, ewe mwandani mtukufu (miongoni mwa nyakati) kuliko nyakati zote, na ewe mwezi ulio bora katika siku na saa (kuliko siku na nyakati zote). السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ شَهْرٍ قَرُبَتْ فِيهِ الْآمَالُ، وَ نُشِرَتْ فِيهِ الْأَعْمَالُ.
Amani iwe juu yako, ewe mwezi ambao ndani yake matumaini hukaribia (kutimia), na (mwezi ambao tayari ndani yake) matendo mema yameshasambazwa. السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ قَرِينٍ جَلَّ قَدْرُهُ مَوْجُوداً، وَ أَفْجَعَ فَقْدُهُ مَفْقُوداً، وَ مَرْجُوٍّ آلَمَ فِرَاقُهُ.
Amani iwe juu yako, Ewe Mwandani ambaye cheo chake hutukuka pale anapokuwepo, na msiba mchungu huwadia pale anapokosekana, na maumivu huwa ndiyo yenye kutarajiwa kutokana na kuachana naye. السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ أَلِيفٍ آنَسَ مُقْبِلًا فَسَرَّ، وَ أَوْحَشَ مُنْقَضِياً فَمَضَّ
Amani iwe juu yako, ewe kipindi jirani ambacho ujio wake uliziburudisha nyoyo na kuzipa furaha, na kutoweka kwake kukasababisha hisia za ukiwa na maumivu ya kihisia. السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ مُجَاوِرٍ رَقَّتْ فِيهِ الْقُلُوبُ، وَ قَلَّتْ فِيهِ الذُّنُوبُ.
Amani iwe juu yako ewe jirani ambaye nyoyo zililainika ndani yake, na dhambi zikapunguka ndani ya kipindi chake.
السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ نَاصِرٍ أَعَانَ عَلَى الشَّيْطَانِ، وَ صَاحِبٍ سَهَّلَ سُبُلَ الْإِحْسَانِ
Salamu iwe juu yako, ewe msaidizi aliyekuwa nguzo dhidi ya nguvu hasi, na mwenza aliyeandaa mazingira (njia) wezeshi kwa ajili ya matendo mema (kwa ajili ya hisani).
السَّلَامُ عَلَيْكَ مَا أَكْثَرَ عُتَقَاءَ اللَّهِ فِيكَ، وَ مَا أَسْعَدَ مَنْ رَعَى حُرْمَتَكَ بِكَ!
Amani iwe kwako! Ni watu wengi walioje wanaokombolewa na Mwenye Ezi Mungu ndani yako (kupitia wewe), na ni wenye furaha ilioje wale wanaoiheshimu hadhi yako adhimu! السَّلَامُ عَلَيْكَ مَا كَانَ أَمْحَاكَ لِلذُّنُوبِ، وَ أَسْتَرَكَ لِأَنْوَاعِ الْعُيُوبِ!
Amani iwe juu yako, ni kiasi kikubwa kilioje cha dhambi unazozifuta, (ni uwezo mkubwa ulioje ulio nao katika kufuta dhambi) na kiwango kikubwa cha aibu unazozisitir (na ni uwezo mkubwa ulioje ulio nao katika kisitiri aibu).
السَّلَامُ عَلَيْكَ مَا كَانَ أَطْوَلَكَ عَلَى الْمُجْرِمِينَ، وَ أَهْيَبَكَ فِي صُدُورِ الْمُؤْمِنِينَ!
Amani iwe juu yako, ni kwa kiasi gani muda wako huwa ni mfrefu kwa wahalifu, na (ni kwa kiasi gani) haiba yako huwa ni adhimu vifuani mwa waaminifu!
السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ شَهْرٍ لَا تُنَافِسُهُ الْأَيَّامُ.
Amani iwe iwe juu yako, ewe mwezi ambao hakuna siku iwezayo kushindana nao.
السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ شَهْرٍ هُوَ مِنْ كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ Amani iwe juu yako, Ewe Mwezi ambao ndani yake mna usalama (amani) kutokana na kila jambo.
السَّلَامُ عَلَيْكَ غَيْرَ كَرِيهِ الْمُصَاحَبَةِ، وَ لَا ذَمِيمِ الْمُلَابَسَةِ
Amani iwe juu yako, (ewe yule) ambaye ushirika wetu naye haukuwa ni wenye kukirisha, wala mwingiliano wetu naye haukua ni wenye lalama. السَّلَامُ عَلَيْكَ كَمَا وَفَدْتَ عَلَيْنَا بِالْبَرَكَاتِ، وَ غَسَلْتَ عَنَّا دَنَسَ الْخَطِيئَاتِ
Amani iwe juu yaako, kama vile ulivyotujia kwa baraka mbali mbali, na wakati huohuo, ukatusafisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili. السَّلَامُ عَلَيْكَ غَيْرَ مُوَدَّعٍ بَرَماً وَ لَا مَتْرُوكٍ صِيَامُهُ سَأَماً.
Amani iwe juu yako, hatukuagi kwa kuwa tumekuchoka, wala hatuachi kufunga (ndani yake) kwa sababu ya kuchoshwa. السَّلَامُ عَلَيْكَ مِنْ مَطْلُوبٍ قَبْلَ وَقْتِهِ، وَ مَحْزُونٍ عَلَيْهِ قَبْلَ فَوْتِهِ.
Amani iwe juu yako, ewe (mwezi) unaotamaniwa kabla ya wakati wake (kabla ya kuwadia kwa wakati wake), na unaohuzunikiwa kabla ya kuondoka kwake.
السَّلَامُ عَلَيْكَ كَمْ مِنْ سُوءٍ صُرِفَ بِكَ عَنَّا، وَ كَمْ مِنْ خَيْرٍ أُفِيضَ بِكَ عَلَيْنَا
Amani iwe juu yako, ni maovu mangapi yaliyotuepuka kwa sababu yako, na ni mema mangapi yaliyotumiminikia kupitia kwako (kutokana na uwepo wako). السَّلَامُ عَلَيْكَ وَ عَلَى لَيْلَةِ الْقَدْرِ الَّتِي هِيَ خَيْرٌ مِنْ أَلْفِ شَهْرٍ
Amani iwe juu yako na juu ya Usiku wa Cheo (Lailatu Al-Qadri), ambao ni bora kuliko miezi elfu.
السَّلَامُ عَلَيْكَ مَا كَانَ أَحْرَصَنَا بِالْأَمْسِ عَلَيْكَ، وَ أَشَدَّ شَوْقَنَا غَداً إِلَيْكَ.
Amani iwe juu yako, ni shauku (hamu) ilioje tuliyokuwa nayo jana juu yako, na kali ilioje ile shauku yetu ya kukutana nawe hapo kesho.
السَّلَامُ عَلَيْكَ وَ عَلَى فَضْلِكَ الَّذِي حُرِمْنَاهُ، وَ عَلَى مَاضٍ مِنْ بَرَكَاتِكَ سُلِبْنَاهُ.
Amani iwe juu yako na juu ya fadhila zako ambazo tunazikosa kwa hivi sasa (katika kipindi cha kutokuwepo kwako), na juu ya zile baraka zako zilizopita ambazo sasa hatunazo tena.
اللَّهُمَّ إِنَّا أَهْلُ هَذَا الشَّهْرِ الَّذِي شَرَّفْتَنَا بِهِ، وَ وَفَّقْتَنَا بِمَنِّكَ لَهُ حِينَ جَهِلَ الْأَشْقِيَاءُ وَقْتَهُ، وَ حُرِمُوا لِشَقَائِهِمْ فَضْلَهُ.
Ewe Mwenyezi Mungu, hakika sisi ni watu wa mwezi huu ulitupa heshima kupitia kwake, na kwa fadhila zako ukatuwezesha kutekeleza wajibu wetu (ndani yake), wakati ambapo waovu waliupuuza muda wake (uwepo wake) na wakanyimwa baraka zake kwa sababu ya uovu wao.
أَنْتَ وَلِيُّ مَا آثَرْتَنَا بِهِ مِنْ مَعْرِفَتِهِ، وَ هَدَيْتَنَا لَهُ مِنْ سُنَّتِهِ، وَ قَدْ تَوَلَّيْنَا بِتَوْفِيقِكَ صِيَامَهُ وَ قِيَامَهُ عَلَى تَقْصِيرٍ، وَ أَدَّيْنَا فِيهِ قَلِيلًا مِنْ كَثِيرٍ.
Wewe ndiye Msimamizi (Mwenye mamlaka kali) wa ule welewa uliyotutunukia katika kuelewa fadhila zake, na (Ndiye wwenye mamlaka kali wa ule) mwongozo uliotuongoza kuhusiana na mfumo wake (sunna zake). Na ukatuwezesha kwa uwezesho wako (kwa taufiki Yako), kufunga saumu yake na kutekeleza ibada zake za usiku, licha ya mapungufu yetu, nasi tumeweza tumetimiza machache ndani yake, kati ya mengi miongoni mwa majukumu yake.
اللَّهُمَّ فَلَكَ الْحَمْدُ إِقْرَاراً بِالْإِسَاءَةِ، وَ اعْتِرَافاً بِالْإِضَاعَةِ، وَ لَكَ مِنْ قُلُوبِنَا عَقْدُ النَّدَمِ، وَ مِنْ أَلْسِنَتِنَا صِدْقُ الِاعْتِذَارِ، فَأْجُرْنَا عَلَى مَا أَصَابَنَا فِيهِ مِنَ التَّفْرِيطِ أَجْراً نَسْتَدْرِكُ بِهِ الْفَضْلَ الْمَرْغُوبَ فِيهِ، وَ نَعْتَاضُ بِهِ مِنْ أَنْوَاعِ الذُّخْرِ الْمَحْرُوصِ عَلَيْهِ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, sifa zote njema ni Zako, tukikiri makosa yetu na kuungama kupoteza kwetu (fursa). Na kutoka nyoyoni mwetu tunakutolea azimio la majuto, na kutoka ndimi zetu, maombi ya dhati ya msamaha. Hivyo, tulipe malipo kwa uzembe uliotupata (katika mwezi huu); malipo ambayo kwayo tutaipata tena fadhila iliyotamaniwa, na yawe badali ya hazina za kila aina tulizokuwa tukizihifadhi.
وَ أَوْجِبْ لَنَا عُذْرَكَ عَلَى مَا قَصَّرْنَا فِيهِ مِنْ حَقِّكَ، وَ ابْلُغْ بِأَعْمَارِنَا مَا بَيْنَ أَيْدِينَا مِنْ شَهْرِ رَمَضَانَ الْمُقْبِلِ، فَإِذَا بَلَّغْتَنَاهُ فَأَعِنِّا عَلَى تَنَاوُلِ مَا أَنْتَ أَهْلُهُ مِنَ الْعِبَادَةِ، وَ أَدِّنَا إِلَى الْقِيَامِ بِمَا يَسْتَحِقُّهُ مِنَ الطَّاعَةِ، وَ أَجْرِ لَنَا مِنْ صَالِحِ الْعَمَلِ مَا يَكُونُ دَرَكاً لِحَقِّكَ فِي الشَّهْرَيْنِ مِنْ شُهُورِ الدَّهْرِ.
Na utuwajibishie udhuru wako juu ya yale tuliyopunguza ndani yake katika haki Zako (na utukubalie udhuru wetu kwa mapungufu yetu katika kutekeleza haki Yako), na turefushia umri wetu ule ulio mbele yetu ili tuweza kuudiriki mwezi wa Ramadhani ijao, na utakapotufikisha ndani yake, basi tusaidie juu ya kuitekeleza ibada Yako kwa haki kama inavyokustahilikia, na utuongoze (utupe taufiki) ya kutekeleza ibada kwa kiwango kinachoustahikia mwezi huo, na utupitishie (nyoyoni mwetu) miongoni matendo mwa mema, yale yatakayokuwa ni nyenzo ya kufikia haki Yako katika miezi miwili miongoni mwa miezi ya dahari.
اللَّهُمَّ وَ مَا أَلْمَمْنَا بِهِ فِي شَهْرِنَا هَذَا مِنْ لَمَمٍ أَوْ إِثْمٍ، أَوْ وَاقَعْنَا فِيهِ مِنْ ذَنْبٍ، وَ اكْتَسَبْنَا فِيهِ مِنْ خَطِيئَةٍ عَلَى تَعَمُّدٍ مِنَّا، أَوْ عَلَى نِسْيَانٍ ظَلَمْنَا فِيهِ أَنْفُسَنَا، أَوِ انْتَهَكْنَا بِهِ حُرْمَةً مِنْ غَيْرِنَا، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ اسْتُرْنَا بِسِتْرِكَ، وَ اعْفُ عَنَّا بِعَفْوِكَ، وَ لَا تَنْصِبْنَا فِيهِ لِأَعْيُنِ الشَّامِتِينَ، وَ لَا تَبْسُطْ عَلَيْنَا فِيهِ أَلْسُنَ الطَّاعِنِينَ، وَ اسْتَعْمِلْنَا بِمَا يَكُونُ حِطَّةً وَ كَفَّارَةً لِمَا أَنْكَرْتَ مِنَّا فِيهِ بِرَأْفَتِكَ الَّتِي لَا تَنْفَدُ، وَ فَضْلِكَ الَّذِي لَا يَنْقُصُ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, na yale tuliyoyakaribia katika mwezi wetu huu miongoni mwa makosa madogo au dhambi fulani, au tuliliotumbukia ndani yake miongoni mwa kosa, na tuliyochuma ndani yake miongoni mwa hatia tulizotenda kwa makusudi, au (yale tuliyotenda) kwa kusahau, ambapo tulijudhulumu nafsi zetu (kwa matendo hayo), au ikapelekea kuvunja heshima za wengine kwa makosa hayo, basi (kwanza kabisa twakuomba) umswalie Muhammad na Aali zake, na (kisha) utusitiri kwa sitara yako, na utusamehe kwa msamaha wako, na usitusimamishe mbele ya macho ya wanaofurahia mabaya yetu, na usitukunjulie ndimi za wanaotulaumu (watakaotulaumu kwa makosa yetu), na (twakuomba) ututumikishe (utuajiri) kwa yale yatakayokuwa ni sababu ya msamaha, na ni kafara kwa yale uliyoyachukia kutoka kwetu, (twakuomba ututakabalio matilaba yetu) kwa upole wako usioisha, na kwa fadhila Zako zisizopungua.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ اجْبُرْ مُصِيبَتَنَا بِشَهْرِنَا، وَ بَارِكْ لَنَا فِي يَوْمِ عِيدِنَا وَ فِطْرِنَا، وَ اجْعَلْهُ مِنْ خَيْرِ يَوْمٍ مَرَّ عَلَيْنَا أَجْلَبِهِ لِعَفْوٍ، وَ أَمْحَاهُ لِذَنْبٍ، وَ اغْفِرْ لَنَا مَا خَفِيَ مِنْ ذُنُوبِنَا وَ مَا عَلَنَ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mshushie rehema Zako Muhammad na Aali zake, na utufidie hasara zetu za mwezi huu, na utubarikie siku yetu ya Idi na ya futari yetu (chakula chetu cha siku ya Idi). Ijaalie (Idi yetu) iwe ni miongoni mwa siku bora zaidi miongoni mwa siku zilizotupitia maishani mwetu, (ijaalie) iwe ni yenye kutukaribisha zaidi kwenye msamaha (Wako), na (ifanye iwe ni) yenye kuondoa (kufuta zaidi) makosa (yetu), na (twakuomba) utughufurie madhambi yetu yaliyofichikana pamoja na yaliyodhihirika.
اللَّهُمَّ اسْلَخْنَا بِانْسِلَاخِ هَذَا الشَّهْرِ مِنْ خَطَايَانَا، وَ أَخْرِجْنَا بِخُرُوجِهِ مِنْ سَيِّئَاتِنَا، وَ اجْعَلْنَا مِنْ أَسْعَدِ أَهْلِهِ بِهِ، وَ أَجْزَلِهِمْ قِسْماً فِيهِ، وَ أَوْفَرِهِمْ حَظّاً مِنْهُ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, tuchunie (tupigie msasa/tusafishie) makosa yetu, kwa jinsi ya mwezi huu unavyomalizika (yafifishe makosa yetu kwa jinsi ya kufifia kwa mwezi wa ramadhani), Na tuondolee (yatoeshe) makosa yetu, na kwa jinsi ya kuondoka (kutoweka) kwake (Ramadhani). Tufanye tuwe ni miongoni mwa watu wake walio na furaha zaidi kutokana na kufaidika kwao na mwezi huu, (tujaalie tuwe ni) wenye fungu kubwa zaidi ndani yake, na (ni) wenye bahati nyingi zaidi kutoka kwake. اللَّهُمَّ وَ مَنْ رَعَى هَذَا الشَّهْرَ حَقَّ رِعَايَتِهِ، وَ حَفِظَ حُرْمَتَهُ حَقَّ حِفْظِهَا، وَ قَامَ بِحُدُودِهِ حَقَّ قِيَامِهَا، وَ اتَّقَى ذُنُوبَهُ حَقَّ تُقَاتِهَا، أَوْ تَقَرَّبَ إِلَيْكَ بِقُرْبَةٍ أَوْجَبَتْ رِضَاكَ لَهُ، وَ عَطَفَتْ رَحْمَتَكَ عَلَيْهِ، فَهَبْ لَنَا مِثْلَهُ مِنْ وُجْدِكَ، وَ أَعْطِنَا أَضْعَافَهُ مِنْ فَضْلِكَ، فَإِنَّ فَضْلَكَ لَا يَغِيضُ، وَ إِنَّ خَزَائِنَكَ لَا تَنْقُصُ بَلْ تَفِيضُ، وَ إِنَّ مَعَادِنَ إِحْسَانِكَ لَا تَفْنَى، وَ إِنَّ عَطَاءَكَ لَلْعَطَاءُ الْمُهَنَّا.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, na (kama kuna) yule aliyezingatia mwezi huu kwa uzingativu stahiki, na akailinda heshima yake kwa ulinzi hakikifu, na akasimamia kanuni (sheria) zake kwa usimamizi timilifu, na akajihadhari na maasi yake kwa tahadhari ya kweli, au akasogea karibu Nawe kwa kitendo cha ibada kilichosababisha ridhaa Yako kwake, na kikapelekea kuzielekeza huruma Zako juu yake; basi (nasi twakuomba), utukirimu kutoka katika ukarimu Wako (hazina yako mkuu) kwa mfano wa malipo yake (malipo ya mtu huyo), na utupe ziadia maradufu yake kutoka katika (hazina ya) fadhila Zako. Hakika fadhila Zako hazipungua (hazikauki), na wala hazina Zako hazikupwi bali hufurika, na migodi (hazina) ya za ihsani Zako haifilisiki, na hakika kipawa Chako ndicho kipawa kiletacho kitulivu (tunuku Yako ndiyo tunuku iletayo utulivu wa moyo).
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ اكْتُبْ لَنَا مِثْلَ أُجُورِ مَنْ صَامَهُ، أَوْ تَعَبَّدَ لَكَ فِيهِ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mbariki Muhammad na Aali zake, na utuandikie malipo yanayolingana na ya wale waliofunga au (wale) waliofanyia ibada kwa ajili katika kipindi hichi (cha Ramadhani kisha wakaendeleza ibada yao) hadi Siku ya Kiama. اللَّهُمَّ إِنَّا نَتُوبُ إِلَيْكَ فِي يَوْمِ فِطْرِنَا الَّذِي جَعَلْتَهُ لِلْمُؤْمِنِينَ عِيداً وَ سُرُوراً، وَ لِأَهْلِ مِلَّتِكَ مَجْمَعاً وَ مُحْتَشَداً مِنْ كُلِّ ذَنْبٍ أَذْنَبْنَاهُ، أَوْ سُوءٍ أَسْلَفْنَاهُ، أَوْ خَاطِرِ شَرٍّ أَضْمَرْنَاهُ، تَوْبَةَ مَنْ لَا يَنْطَوِي عَلَى رُجُوعٍ إِلَى ذَنْبٍ، وَ لَا يَعُودُ بَعْدَهَا فِي خَطِيئَةٍ، تَوْبَةً نَصُوحاً خَلَصَتْ مِنَ الشَّكِّ وَ الِارْتِيَابِ، فَتَقَبَّلْهَا مِنَّا، وَ ارْضَ عَنَّا، وَ ثَبِّتْنَا عَلَيْهَا.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, tunawasilisha toba yetu mbele yako katika siku hii ya Fitri yetu (Idi yetu), ambayo umeiteua kuwa ni sherehe na chanzo cha furaha kwa jamii ya waumini, na (ukaifanya) kuwa ni jukwaa la umoja na mkusanyiko kwa ajili ya wafuasi wa mila Yako. (Twatubia) toba hii kila kosa tulilotenda, au kitendo kiovu tulichokifanya tulichokitanguliza, au dhana potofu tuliyoificha ndani ya dhamira zetu. (Twatubia) toba ya mtu asiye na azma ya kurejelea tena makosani (mwake), na wala hana dhamira ya kurudia tena kwenye uovu (wake) baada ya hapa (baada ya toba hii). (Toba yetu hii) ni toba ya kweli na ya dhati iliyoepukana na kila shaka na wasiwasi ndani yake. Hivyo basi, tunakuomba uipokee (toba yetu hii) kutoka kwetu, uturidhie, na utudumishe katika msimamo (wetu) huu.
اللَّهُمَّ ارْزُقْنَا خَوْفَ عِقَابِ الْوَعِيدِ، وَ شَوْقَ ثَوَابِ الْمَوْعُودِ حَتَّى نَجِدَ لَذَّةَ مَا نَدْعُوكَ بِهِ، وَ كَأْبَةَ مَا نَسْتَجِيرُكَ مِنْهُ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, tunakuomba uturuzuku neema ya kuwa na khofu dhidi ya adhabu (Yako) iliyoiahidiwa (ndani ya maandiko Yako), na (twakuomba utujaalie) tuwe na hamu kubwa ya kupokea malipo mema uliyoahidi. Lengo letu ni kufikia ladha halisi ya ibda tunayoitumia katika kukuomba (maombi yetu), pia tuhisi uzito (wa kutenda) yale mambo tunayokuomba utukinge nayo.
وَ اجْعَلْنَا عِنْدَكَ مِنَ التَّوَّابِينَ الَّذِينَ أَوْجَبْتَ لَهُمْ مَحَبَّتَكَ، وَ قَبِلْتَ مِنْهُمْ مُرَاجَعَةَ طَاعَتِكَ، يَا أَعْدَلَ الْعَادِلِينَ.
Na utujumuishe (Kwako tuwe) miongoni mwa waja wako wenye kutubia, uliowawajibishi juu yao mapenzi Yako, na ukauridhia urejeo wao (kurudi kwao) katika taa yako (katika utiifu Wako), Ewe Hakimu Mwadilifu kuliko waadilifu wote. اللَّهُمَّ تَجَاوَزْ عَنْ آبَائِنَا وَ أُمَّهَاتِنَا وَ أَهْلِ دِينِنَا جَمِيعاً مَنْ سَلَفَ مِنْهُمْ وَ مَنْ غَبَرَ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, twakuomba uwaghufirie wazazi wetu wa kiume na wa kike, pamoja na jamii nzima ya waumini (wenzetu); wale waliotangulia katika vizazi vilivyopita na wale watakaofuata katika vizazi vijavyo, hadi Siku ya Kiyama.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ نَبِيِّنَا وَ آلِهِ كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى مَلَائِكَتِكَ الْمُقَرَّبِينَ، وَ صَلِّ عَلَيْهِ وَ آلِهِ كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى أَنْبِيَائِكَ الْمُرْسَلِينَ، وَ صَلِّ عَلَيْهِ وَ آلِهِ كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ، وَ أَفْضَلَ مِنْ ذَلِكَ يَا رَبَّ الْعَالَمِينَ، صَلَاةً تَبْلُغُنَا بَرَكَتُهَا، وَ يَنَالُنَا نَفْعُهَا، وَ يُسْتَجَابُ لَهَا دُعَاؤُنَا، إِنَّكَ أَكْرَمُ مَنْ رُغِبَ إِلَيْهِ، وَ أَكْفَى مَنْ تُوُكِّلَ عَلَيْهِ، وَ أَعْطَى مَنْ سُئِلَ مِنْ فَضْلِهِ، وَ أَنْتَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ. Ewe Mwenye Ezi Mungu, mrehemu Nabii wetu Muhammad na Aali zake, kwa namna (kama vile) ulivyowarehemu Malaika wako waliokurubishwa (walio karibu Nawe). Na mrehemu yeye pamoja na Aali zake, kama ulivyowarehemu (unavyo warehemu) Manabii wako waliotumwa (aridhini mwako). Na mrehemu yeye pamoja na Aali zake, kama ulivyowarehemu (unavyo warehemu) waja wako wema. Na umrehemu kwa rehema bora zaidi kuliko huzo, Ewe Mlezi wa walimwengu wote. Na (twakuomba umrehemu) rehema ambazo baraka zake zitukwa ni zenye kutufikie, na (umrehemu kwa rehema) tutakazonufaika nazo kwa manufaa yake, na (umrehemu kwa rehema) zitakazopelekea kukubaliwa kwa maombi yetu. Hakika, Wewe Ndiye Mbora (Mtukufu) zaidi uliye tarajiwa, na (Ndiye) Mtimizaji (Mtoshelezaji) zaidi uliyetegemewa, na Ndiye mkarimu zaidi wa kuombwa fadhila zake. Nawe ni Mueza juu ya kila jambo.