Barua ya Imamu Hussein (a.s) kwa Wakuu wa Basra
Barua ya Imamu Hussein (a.s) kwa Wakuu wa Basra (Kiarabu: رسالة الإمام الحسين إلى وجوه البصرة) ilikuwa ni barua maalumu ya wito, iliyoandikwa na Imam Hussein (a.s.) kwa wakuu wa makabila ya Waarabu wa Basra, kabla ya janga la mauaji ya Karbala. Imam (a.s) katika barua hii aliwafikishia Warabu wa Basra ujumbe wake muhimu akiewaeleza kwamba; Ukhalifa ni haki pekee inayowastahikia Ahlul-Bait (a.s). Katika barua hii alifafanua akiwaambia kwamba; kukaa kimya kwa familia hii tukufu dhidi ya unyakuzi wa Ukhalifa, kulikuwa ni kwa ajili ya kuulinda umoja wa Waislamu, hatua ambayo ilikuwa ni muhimu kwa wakati huo. Katika barua yake Imamu (a.s) alizungumzia jinsi ya Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w) zilivyokuwa zikifutwa na badala yake, bidaa zikonekana kufufuka na kushika nafasi ya Sunna hizo. Kwa msingi huo, aliwataka wakuu wa mji wa Basra wajiunge naye ili kukomesha masuala hayo. Barua hii ilitumwa na kuwasilishwa mikononi mwa wakuu hao kupitia Sulaiman bin Razin.
Walengwa wa Barua na Mjumbe wa Imam Hussein (a.s)
Pale Imamu Hussein (a.s) alipokuwa akiishi Makka (mwaka wa 60 Hijria), aliwaandikia barua watu wa Basra [1] akiwataka wamsaidie katika jitihada zake za kusimama dhidi ya batili. [2] Barua hii ilitumwa na Imamu Hussein (a.s) kwa viongozi na viongozi wa makabila ya watu wa Basra [3] au kwa wafuasi maalumu wa Imamu (a.s) [4] waliokuwa wakiishi mjini Basra. Mwanahistoria maarufu ajulikanaye kwa jina la Tabari, mwanzoni anawataja viongozi watano wa Basra kuwa ndio walengwa wa barua hii, ila baadaye amewataja watu sita badala ya watano, [5] ambao pia majina yao yanapatikana katika baadhi ya vyanzo vingine vya historia. [6] Watu hao ni: Malik bin Mism'a Bakri, Ahnaf bin Qays, Mundhir bin Jarud, Masud bin Amr, Qays bin Haytham na Amr bin Ubaydullah bin Ma'mar. Hata hivyo, katika vyanzo vingine, pia anatajwa Yazid bin Masud Nahshali. [7]
Baadhi wamesema kwamba Imamu Hussein (a.s) alituma barua moja iliyokuwa na ujumbe mmoja, kisha ikafikishwa kwa kila mmoja katia ya walengwa hao. [8] Kama ilivyoandikwa katika taarifa nyingine ya kwamba; Imamu Hussein (a.s) aliordhesha majina ya wahusika hao katika barua moja iliyowataja baadhi ya watu hao kumpa msaada wao katika harakati zake dhidi ya dhulma. [9]
Vyanzo viaeleza kwamba; Mjumbe wa barua hiyo iama alikuwa ni Suleiman [10] au Salman [11] aliyefahamika kwa jina la «Abu Razin» [12] ambaye alikuwa ni miongoni mwa watumwa walioachwa huru na Imamu Hussein (a.s). [13] Abu Razin alifanya jitihada zote kufika Kufa kwa haraka na bila ya kuchelewa. [14] Vyanzo vyengine vimemtaja Dharra' Sadusi kuwa ndiye mjumbe wa Imamu (a.s) aliyewajibika kuwasilisha barua hiyo. [15]
- Pia soma: Sulaiman bin Razin
Yaliyomo katika Barua
Katika barua yake kwa watu wa Basra, Imamu Hussein (a.s) aliwataka watu wa Basra waisimamie uhuishaji wa kitabu cha Mungu na Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w). [16] Katika barua hii, Imamu (a.s) alieleza kwamba; nafasi ya ukhalifa ni haki ya Ahlul-Bait (watu wa nyumba ya bwana Mtume) (s.a.w.w) [17] na kufafanua kuhusiana na jitihada za Bani Umayya [18] za kuangamiza Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na harakati zao za kuanzisha uzushi ndani ya dini. [19]
Dainawiy, mwandishi wa kitabu Akhbar al-Tiwal, ametoa nakala fupi ya barua hii ambayo kwa mujibu wake; Baada ya Imamu Hussein (a.s), kuwataja kwa majina waliokuwa wakilengwa ndani ya barua hiyo, aliwataka walengwa hao wasimamie urejeshawaji wa nembo za haki na kuondoa uzushi na nembo zake. Na kwamba kufanya kwao hivyo, katawapelekea kuongoka na kuelekea kwenye njia sahihi. [20] Vyanzo mbalimbali vimeeleza yaliyomo ndani ya barua hii kwa tofauti ndogo tu katika matini yake (ibara zake). [21] Tabari naye ameeleza nakala ndefu kuhusiana na barua hii, ingawa baadhi ya watafiti wameitilia shaka na kuona kwamaba; sehemu ya barua hiyo ni ongezeko lilioongezwa na wapokezi wa tukio hilo. [22] Yaliyomo katika barua, kulingana na nukuu za Tabari, ni kama ifuatavyo:
Matini ya Kiarabu
أَمَّا بَعْدُ: فَإِنَّ اَللَّهَ اِصْطَفَی مُحَمَّداً صَلَّی اَللَّهُ عَلَیْهِ [وَ آلِهِ] وَ سَلَّمَ عَلَی خَلْقِهِ، وَ أَکْرَمَهُ بِنُبُوَّتِهِ، وَ اِخْتَارَهُ لِرِسَالَتِهِ، ثُمَّ قَبَضَهُ اَللَّهُ إِلَیْهِ وَ قَدْ نَصَحَ لِعِبَادِهِ وَ بَلَّغَ مَا أُرْسِلَ بِهِ، وَ کُنَّا أَهْلَهُ وَ أَوْلِیَاءَهُ وَ أَوْصِیَاءَهُ وَ وَرَثَتَهُ وَ أَحَقَّ اَلنَّاسِ بِمَقَامِهِ فِی اَلنَّاسِ، فَاسْتَأْثَرَ عَلَیْنَا قَوْمُنَا بِذَلِکَ، فَرَضِینَا وَ کَرِهْنَا اَلْفُرْقَه وَ أَحْبَبْنَا اَلْعَافِیَه، وَ نَحْنُ نَعْلَمُ أَنَّا أَحَقُّ بِذَلِکَ اَلْحَقِّ اَلْمُسْتَحَقِّ عَلَیْنَا مِمَّنْ تَوَلاَّهُ وَ قَدْ أَحْسَنُوا وَ أَصْلَحُوا وَ تَحَرَّوْا اَلْحَقَّ، فَرَحِمَهُمُ اَللَّهُ، وَ غَفَرَ لَنَا وَ لَهُمْ وَ قَدْ بَعَثْتُ رَسُولِی إِلَیْکُمْ بِهَذَا اَلْکِتَابِ، وَ أَنَا أَدْعُوکُمْ إِلَی کِتَابِ اَللَّهِ وَ سُنَّه نَبِیِّهِ ص فَإِنَّ اَلسُّنَّه قَدْ أُمِیتَتْ، وَ إِنَّ اَلْبِدْعَه قَدْ أُحْیِیَتْ، وَ إِنْ تَسْمَعُوا قَوْلِی وَ تُطِیعُوا أَمْرِی أَهْدِکُمْ سَبِیلَ اَلرَّشَادِ، وَ اَلسَّلاَمُ عَلَیْکُمْ وَ رَحْمَه اَللَّه
Ama baada ya hayo: Hakika Mwenye Ezi Mungu alimteua Muhammad (s.a.w.w) miongoni mwa viumbe wake, akamkirimu kwa unabii wake, na akamchagua kwa kumpa utume wake. Kisha Mwenye Ezi Mungu akamchukua na kumrejesha kwake (akafariki), baada ya kuwanasihi waja wake na kufikisha aliyoletwa nayo. Sisi ndio watu wake wa karibu yake, marafiki zake, wasii wake, na warithi wake; nasi ndiwo tunaostahili zaidi miongoni mwa watu wote katika kurithi nafasi yake. Lakini watu wetu (wanajamii) walijichukulia watakavyo (ukhalifa) badala yetu. Tukaridhia, kwa kuwa tulichukia kutokea mifarakano, na tukapenda usalama na amani. Huku tukijua kwamba sisi ndiwo tunaostahili zaidi haki hiyo, ambayo ni haki yetu inayotustahilia sisi badala ya wale waliyoichukua, ambao walifanya vyema, na wakaleta marekebisho, na wamejitahidi kuleta haki; Mwenye Ezi Mungu awarehemu wao pamoja nasi. Sasa, nimemtuma mjumbe wangu kwenu na barua hii, nami ninakuitani kwenye kitabu cha Mungu na Sunna za Nabii wake (s.a.w.w). Bilas haka tayari Sunna zimefutwa, na bdala yake uzushi ndio uliohuishwa. Hivyo basi, kama mtayasikiliza maneno yangu na kutii amri yangu, nitakuongozeni kwenye njia ya uongofu. Baada ya hayo, ninakutakieni amani na rehema za Mwenye Ezi Mungu ziwe juu yenu.
Majibu (Mwitikio)
Kuna taarifa tofauti zilizoelezwa kuhusiana na majibu ya viongozi wa Basra, baada ya wao kupokea barua hiyo itokayo kwa Imamu Hussein (a.s). Kwa ujumla ni kwamba, wao hawakukubaliana na ombi la Imamu Hussein (a.s), na badala yake waliamua kumjulisha gavana wa Basra kuhusiana na azma yake (a.s). Ila pia kulitokea baadhi yao, walioitikia wito huo wa Imamu na hata kujiunga naye.
Kufichuliwa kwa Barua na Kukamatwa kwa Mjumbe
Kulingana na vyanzo vilivyozungumizia tukio hili, baada ya vingozi hao kupokea barua hiyo, wengi miongoni mwa viongozi hao wa Basra waliamua kuificha barua ya Imamu Hussein (a.s) na kubaki kimya. [24] Lakini Mundhir bin Jarud, ambaye binti yake alikuwa ni mke wa Ubaidullah bin Ziyad, [25] aliichukua barua hiyo na kuipeleka kwa Ubaidullah. [26] Wakati huo, Ubaidullah alikuwa ni gavana wa mji Basra akimwakilisha Yazid mjini humo. Uongozi ambao alipewa na Yazid, kutokana na hali ya Kufa ya wakati huo. [27] Kulingana na mwanahistoria Baqir Sharif Qarashi (aliyefariki 1433 Hijria), Mundhir aliikabidhi barua ya Imamu Hussein (a.s) kwa Ubaidullah ili kuonyesha utii wake. [28]
Vyanzo vingine vimeandika vikisema kwamba; Mundhir alifanya hivyo kwa kuogopa kwamba, yawezekana barua hiyo hakuwa ikitoka kwa Imamu Hussein (a.s), bali ni njama kutoka kwa Ubaydullah [29] na ni njia ya kuupima uaminifu wake. [30] Baada ya Ibn Ziyad kuiona barua hiyo, alikasirika mno, na akatoa amri ya kukamatwa mjumbe wa barua haraka iwezekenavyo. [31] Mjumbe wa Imamu (a.s), ambaye alikuwa amejificha kati ya Washia walioko mjini Basra, [32] alikamatwa kupitia Mundhir [33] au watu wengine [34] na hatimae kupelekwa kwa Ubaidullah. Ubaydullah bin Ziyad naye alimkata shingo mjumbe huyo, kisha akautundika mwili wake mbele ya mlango wa mji. [35] Papo hapo Ubaidullahi alikwenda msikiti mkuu wa mji, akasimama kwenye membari ya msikiti huo [36] na akawaonya watu dhidi ya kumpingana naye, huku akitangaza utayari wake wa kwenda mji wa Kufa, wakati ambao alikuwa tayari ameshamteua ndugu yake, Uthman, kama mrithi wake wa kushika nafasi katika kipindi cha kutokuwepo kwake. [37]
Jibu Hasi
Ahnaf bin Qais, mmoja wa walengwa wa barua ya Imamu Hussein (a.s.), alijibu barua ya Imamu kwa kutaja Aya ya 60 ya Surat Ar-Rum isemayo: «فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللهِ حَقٌّ وَ لا يَسْتَخِفَّنَّكَ الَّذينَ لا يُوقِنُونَ ; Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenye Ezi Mungu ni ya kweli, wala usiwape nafasi ya kukushusha thamani wale wasio na yakini». [38] Hii ilifasiriwa kama ni kauli ya kukataa kumpa msaada Imamu Hussein (a.s) na kumwonya dhidi ya kuwaamini watu wa Basra katika kuanzisha harakati zake. [39]
Juhudi za Kujiunga na Imamu
Imesemekana kwamba; ingawa Ubaidullah bin Ziyad alitoa amri ya kufungwa kwa njia za kutoka Basra kelekea Kufa, ili mtu yeyote yule asifanikiwe kumsaidia Imamu Hussein (a.s), ila baadhi ya viongozi wa Basra walifanikiwa kukimbia na kutoka katika mji huo. Miongoni mwa walifanikiwa kufanya hivyo ni Yazid bin Nabit, aliyekimbia yeye pamoja na watoto wake wawili, Abdullah na Ubaidullah, na hatimae wakafanikiwa kujiunga na Imamu Hussein huko Makka, na mwishowe wakafariki kupitia kifo cha kishahidi huko Karbala. [40]
Yazid bin Mas’ud Nahshali, miongoni mwa viongozi wengine wa Basra, alipopokea barua ya Imamu Hussein (a.s), aliwakusanya Waarabu wa makabila ya Bani Tamim, Bani Handhala, na Bani Sa’ad, kisha akawapasha habari kuhusiana na wito wa Imamu Hussein (a.s), akiwaeleza kwamba; hata yeye mwenyewe pia alikuwa tayari amesha jiandaa kwa ajili kwenda kumsaidia Imamu Hussein (a.s). Katika maelezo yake, aliwataka Waarabu hao watoe maoni yao kuhusana na jambo hilo. Papo hapo wote kwa pamoja walikubaliana na mawazo yake, isipokuwa Kabila la Bani Sa’ad, ambalo liliomba muda wa kushauriana baina yao ili kutoa uamuzi wao kamili. Yazid bin Mas’ud aliamua kuandikia barua Imamu Hussein (a.s), akimjulisha kuwa yeye na kabila lake wako tayari kumsaidia katika juhudi zake. Baada ya Imamu Hussein (a.s) kuiona barua hiyo, alimuombea dua njema Yazid bin Mas’ud. [41] Hata hivyo, baadhi ya watafiti wamesema kwamba; barua hii ilimfikia Imamu siku ya kumi ya Muharram, baada ya kujiri mauaji dhidi ya masahaba na familia ya Imamu Hussein (a.s). [42] Pale Yazid bin Mas’ud alipokuwa akijiandaa kuondoka, kwa ajili ya kuungana na Imamu Hussein (a.s), alipata habari ya Kufa shahidi kwa Imamu, jambo ambalo lilimpa masikitiko na huzuni kubwa mno. [43]
Malengo ya Barua ya Imamu
Baadhi ya waandishi wanasema kwamba; Kiuhalisia hakuna hata mmoja wa walengwa wa barua ya Imamu Hussein (a.s) aliyekuwa na mwelekeo wa kumjibu Imamu (a.s) ipasavyo, [44] bali mwelekeo wao wa kisiasa ulikuwa ni kinyume na siasa za Ahlul-Bait, [45] Ila Imamu alikuwa na malengo maalumu ya kuandikia barua wahusika hawa. Miongoni mwa malengo ya Imamu Hussein yaliyotajwa na waandishi hawa ni kama ifuatavyo:
- Kujaribu kuwahamasisha watu wa kawaida kupitia viongozi na wasomi wao.
- Kuwasiliana na watu wa Basra ili kuondoa kisingizio cha kutokuwa na ufahamu wa harakati za Imamu Hussein (a.s).
- Kuzuia viongozi ambao walikuwa wanasitasita kumsaidia Imamu, ili wasijiunge na safu ya maadui wa Imamu Hussein (a.s).
- Kutoa taarifa kuhusiana na kuanza kwa harakati za wapenzi wa Ahlul-Bait huko Basra, kama vile Yazid bin Mas’ud Nahshali na wengineo. [46]