Nenda kwa yaliyomo

Aya ya al-Tabligh

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Ayat al-Tabligh)
Ayat al-Tabligh

Ayat al-Tabligh (Kiarabu: آية التبليغ) (al-Maida: 67) ni miongoni mwa Aya za mwisho alizoshushiwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na Mwenyezi Mungu (s.w.t). Kwa mujibu wa Aya hii Mtume (s.a.w.w) alitakiwa kufikisha kwa watu ujumbe na yale aliyoteremshiwa na Mwenyezi Mungu, ambapo kama hakufanya hivyo, basi atakuwa hajafikisha ujumbe wake.

Waislamu wa madhehebu ya Shia na baadhi ya Waislamu wa Ahlu-Sunna wanaamini ya kwamba, Aya ya Tablighi ilishuka katika Hajjatul-Wida’ (Hija ya kuaga) kabla ya tarehe 18 Dhul-Hija (Mfunguo Tatu) mwaka wa 10 Hijiria. Katika itikadi na imani za Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kwamba, maudhui ya Aya hii ni ujumbe wa Ukhalifa na Uwasii wa Imamu Ali bin Abi Talib (a.s) na baada ya Mtume kushushiwa Aya hii alitekeleza amri hiyo kwa kumtangaza rasmi Imamu Ali (a.s) kuwa Khalifa na kiongozi wa Waislamu baada yake.

Andiko na tarjumi ya Aya

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ وَاللَّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ إِنَّ اللَّهَ لاَ يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ
Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi, na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake, na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu, hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
(Quran: 5: 67)

Sababu ya kushuka kwake

Makala kuu: Tukio la Ghadir

Wafasiri wa Qur’an Tukufu wamesema wazi na bayana kwamba, Aya ya Tablighi (kufikisha na kutangaza ujumbe) ilishuka baada ya Bwana Mtume (s.a.w.w) kurejea kutoka katika Hija yake ya mwisho (Hijjatul-Wida’) katika eneo la Ghadir Khum. Ilikuwa ni tarehe 18 Dhul-Hija (Mfunguo Tatu) mwaka 10 Hijiria. [1] Katika vyanzo na vitabu vya Ahlu-Sunna pia, kuna hadithi ambazo zinabainisha na kuweka wazi zama na sehemu iliposhuka Aya hii kwamba, ni katika eneo la Ghadir Khum. [2] Wanazuoni na Maulamaa wa Kishia wakitegemea hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu wa Kishia na baadhi ya Masahaba, wanatambua sababu ya kushuka Aya ya hii ya tangazo na kufikisha ujumbe kwamba ni kuhusiana na tukio la Ghadir na kutangazwa ukhalifa na uongozi wa Imamu Ali (a.s) kwa Waislamu baada ya Mtume (s.a.w.w). [3] Wanazuoni wa Ahlu-Sunna pia wanaamini kuwa, sababu ya kushuka Aya hii ni kuanza risala ya Mtume (s.a.w.w) au kutakiwa Mtume kuutangaza Uislamu. [4]

Kwa mujibu wa vyanzo vya Kishia, awali Jibril (a.s) alimshukia Mtume (s.a.w.w) wakati wa msimu wa Hija katika Hajjatul-Wida’ na akamtaka achukue baia na kiapo cha utii kutoka kwa watu kuhusiana na ukhalifa na uongozi wa Imamu (a.s) baada yake. Hata hivyo, Bwana Mtume (s.a.w.w) kutokana na ufahamu aliokuwa nao kuhusiana na udui wa makureshi na wanafiki pamoja na chuki na adawa yao kwa Amirul-Muuminina (a.s), aliona kutakuwa na hatari ya kuibuka mpasuko na mfarakano na watu kurejea katika zama za ujahilia hivyo akamtaka Mwenyezi Mungu awalinde na kuwahifadhi watu. Malaika Jibril akamshukia Mtume kwa mara ya pili katika Msikiti wa al-Khayf na akamfikishia tena agizo na amri ileile bila ya kumpa ahadi Mtume ya kuwalinda watu na hatari. Malaika wa Wahyi alimshukia Mtume (s.a.w.w) kwa mara ya tatu katika eneo lililoko baina ya Makka na Madina na akakariri jambo lilelile. Mtume (s.a.w.w) akamwambia Malaika Jibril, mimi nahofia watu kuliona kuwa ni uongo suala la Ali kuwa mrithi na kiongozi baada yangu na hivyo wasiyakubali maneno yangu. Mara ya mwisho, Malaika wa Wahyi alimshukia Mtume katika eneo la Ghadir Khum na baada ya kukariri amri ya Mwenyezi Mungu alimuahidi kulindwa na wanafiki.

Uwezekano mwingine

Kumetajwa sababu zingine za kushuka Aya hii ambapo Maulamaa wa Kiislamu wakiwemo wa Kishia wamekosoa hayo:

1. Kushuka Makka Aya hii

Baadhi ya Maulamaa wa Ahlu-Sunna wanaamini kuwa, Ayat al-Tabligh (Aya ya Tablighi na kufrikisha ujumbe) ilishuka Makka (mwanzo wa risala ya Mtume) na sababu ya kushuka kwake, ni kuamrishwa Mtume kutangaza na kufikisha ukweli na uhakika wa dini kwa makafiri na washirikina. Kwa mujibu wa hadithi, ili kumlinda Mtume (s.a.w.w) kutokana na hujuma na madhara ya maadui, walinzi waliwekwa kwa ajili yake; hata hivyo, baada ya kuteremka Aya ya Tablighi, aliwaruhusu walinzi kuondoka na akasema kwamba Mwenyezi Mungu atanilinda na watu wabaya, na fauka ya hayo, atachunga na kuhakikisha ukweli wa dini unawafika kwa makafiri na washirikina bila ya woga.[6]

Ukosoaji

Katika kuukosoa mtazamo huu, wafasiri wanakubaliana kwa pamoja yakwamba, Surat al-Maidah iliteremka Madina [7] na kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Abdullah bin Omar, Surat al-Maidah ndiyo Sura ya mwisho kuteremshwa. [8] Kwa hiyo, dhana ya kwamba Aya ya Tabligh iliteremka Makka na pia kwamba Aya hiyo ilisomwa katika sura hiyo, ilikuwa ikisomwa peke yake kwa miaka mingi bila ya kuunganishwa na sura fulani miongoni mwa sura za Qur’an au ilikuwa tu katika hifadhi ya nyaraka sio sahihi. [9]

Mbali na hayo, baadhi ya wataalamu wenye nadharia wamezichukulia riwaya zinazohusu ulindaji roho roho na uhai wa Mtume (s.a.w.w.) huko Makka kuwa ni hadithi za ajabu na hasi. [10]

2. Kuwafikishia ujumbe Ahlul-Kitab

Baadhi ya wameandika kuwa, Aya ya Tablighi ilishuka mjini Madina [11] na lengo la kushuka kwake lilikuwa ni kumpa taklifu na amri Mtume ya kuwafikishia uhakika wa Wahyi Ahlul-Kitabu bila hofu. [12] Abu Hayan anasema, ujumbe ambao Bwana Mtume (s.a.w.w) alitakiwa kuufikisha ilikuwa hukumu ya Rajm (kupigwa mawe) na kisasi ambapo Mayahudi na Wakristo walikuwa wametia mkono na kubadilisha hukumu hizi za Mwenyezi Mungu katika vitabu vya Torati na Injili. [13] Hoja yake ni kwamba, maneno yaliyokuja kabla ya Aya hii yanahusiana na Ahlul-Kitab pia na maudhui ya Aya za Qur’an hazipaswi kuwa ni ngeni kabla na baada yake. [14]

Ukosoaji

Kwa mujibu wa nyaraka na vyanzo vya historia baada ya vita baina ya Waislamu na Mayahudi, vikiwemo Vita vya Bani Quraidha na Khaybar, nguvu na adhama ya Mayahudi iliporomoka na kwa kudhibitiwa kambi zao na kubaidishwa nje ya Madina idadi kadhaa miongoni mwao, ushawishi na satwa yao ikawa imesambaratika. [15] Wakristo nao huko Saudi Arabia hususan katika mji wa Madina hawakuwa na nguvu na makabiliano yao na Waislamu lilikuwa tukio la Mubahala (maapizano) tu [16] ambalo nalo halikufanyika baada ya Wakristo kuingiwa na woga na hofu walipomuona Mtume amekuja katika tukio hilo akiwa pamoja na Ali, Fatma, Hassan na Hussein (a.s).

Hivyo basi, kwa kuzingatia nguvu aliyokuwa nayo Mtume na Waislamu katika miaka ya mwishoni mwa umri wa mbora huyo wa viumbe, hakukuwa na sababu ya Mtume kuwa na hofu na Mayahudi au Manasara hata hilo liwe sababu ya woga katika kutangaza na kuwafikishia ujumbe na risala ya dini. Fauka ya hayo, kwa upande wa maudhui, Aya ya Tablighi, maudhui yake si ngeni na Aya za kabla na baada yake, kwani Aya za kabla na baada yake zinawalaumu Mayahudi na Manasara ambao walikuwa wakidhani kwamba kwa kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu, zama za mamlaka ya Uislamu zitapita na kwa mara nyingine tena msingi wa ushawishi wao na utawala wao utarejea. Hata hivyo Aya ya tablighi ambayo inazungumzia kuainishwa kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada ya Mtume (s.a.w.w) imebatilisha dhana na taswira yao hiyo na jambo hili lina mafungamano na Aya ya al-Ikmal (kukamishwa dini) ambayo ilishuka baada ya kutangazwa Wilaya na uongozi wa Imamu Ali (a.s). [17]

3. Ukumbusho kwa Mtume

Ibrahim bin Muhammad Hamui Juweyni, mmoja wa wasomi na wataalamu wa elimu ya hadithi na mmoja wa Masufi aliyeishi katika karne ya 7 na ya 8 Hijiria anasema kuwa, kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kushuka kwa Aya ya Tablighi ilikuwa ni ukumbusho kwa Mtume (s.a.w.w). Katika hadithi hii, Mtume alipokuwa katika safari yake ya Miraj alisikia sauti na mwito akiwa katika mbingu ya saba ambao ulikuwa ukisema, Ali (a.s) ni Aya (alama na ishara) ya Mwenyezi Mungu na rafiki wa waumini, hivyo mtambulishe kwa watu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) baada ya kurejea katika safari ya Miraj, alisahau mwito na sauti ile na hivyo Aya ya Tablighi ilishuka kumbukumbusha hilo. [18]

Nukta muhimu

Umuhimu wa jukumu hili

Aya hii inaonyesha umuhimu na unyeti mkubwa wa ujumbe unaotakiwa; kwa sababu ni wazi kwamba ikiwa ujumbe huo hautafikishwa, utume wa Bwana utakuwa haujatekelezwa, na ni kana kwamba ujumbe una thamani sawa na ujumbe wa Unabii na Utume. Haiwezi kudhaniwa kuwa ujumbe ulikuwa katika uwanja wa imani, kama vile Tawhidi, Utume, na Ufufuo, au suala la kifiqhi, kama vile sheria za Sala, Saumu na Hija, kwa sababu Surah al-Maida ilikuwa ni miongoni mwa surah za mwisho zilizoteremshwa, na ukweli huu uliteremshwa kwa Mtume na kufikishwa kwa watu kabla ya hapo. Inawezekana kusema kwamba, mwishoni mwa uhai wa Mtume (s.a.w.w) ilikuwa imefika zamu ya kutangaza jambo ambalo, pamoja na kuwa muhimu na jipya kwa watu, lilizingatiwa kuwa ni kamilisho la asili ya Utume na hilo halikuwa jingine isipokuwa ni mpango wa uongozi wa Umma wa Kiislamu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). Kimsingi ni kuwa, kile ambacho Bwana Mtume alipewa jukumu la kukifikisha kilikuwa na umuhimu ambapo kama asingelifanya hilo, sheria na hukumu zingine pamoja na amri na maagizo ya dini yasingekuwa na maana na athari yoyote. Ingekuwa kama vile mwili usio na roho, na jambo hilo ndio ule uongozi na Wilaya ya Ali kwa Umma wa Kiislamu ambao ilikuwa ni lazima kwa idhini ya Mwenyezi Mungu aainishwe na kuteuliwa Imamu ambaye atailinda dini, atakuwa msimamizi wa mambo ya Waislamu na mbunifu wa mambo katika jamii na hadithi za Kisuni na Kishia zimethibitisha hili na Aya ya 67 ya Surat al-Maidah imeshuka kuhusiana na Wilaya na uongozi wa Imamu Ali (as). [1]

Wasiwasi wa Mtume wa kufikisha ujumbe husika

Kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, Mtume (s.a.w.w) alikuwa na wasiwasi kuhusiana na kufikisha ujumbe huo. Hata hivyo Mwenyezi Mungu Mungu akamuahidi kwa kumwambia: Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Kwa kauli hiyo, Mwenyezi Mungu akawa amemuondolea wasiwasi Bwana Mtume. Wasiwasi wa Mtume haikuwa ni hofu na woga wa roho yake. Kama alikuwa na wasiwasi basi hofu na wasiwasi wake ulitokana na ni kuwa, asije akauawa kabla ya kufikisha ujumbe aliotakiwa kuufikisha au alikuwa na wasiwasi huu kwamba, watu (wanafiki) watamkadhibisha, watamtuhumu na hivyo kuzuia taathira ya tablighi ya dini ya Mwenyezi Mungu. [20] Kutokana na kutoshushwa Aya kuhusiana na washirikina, makureshi na Ahlul-Kitab, inafahamika kuwa, makusudio ya “watu” katika Aya ya Tablighi ni wanafiki katika jamii ya Kiislamu. [21] Mtume (s.a.w.w) katika kumtangaza na kumtambulisha Amirul-Muuminina (a.s) kama mrithi wake na kiongozi wa Waislamu baada yake alikuwa na wasiwasi na hofu ya upinzani na kufanyika ukwamishaji mambo kutokana na kuwa:

  • Wanafiki walikuwa na tamaa ya urithi wa Mtume kama mkuu wa jamii na waliona kufikiwa kwa neema za kidunia kuko katika kudhibiti urithi na uongozi baada ya Mtume huyo, na Imamu Ali (as) kuwa mrithi na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume, kungezifanya ndoto na matumaini yao yaote mbawa. [22]
  • Imamu Ali (a.s) alikuwa akitambulisha kama mtu mwenye misimamo thabiti na isiyotetereka. [23]
  • Waislamu wapya ambao ndugu na jamaa zao waliuawa zaidi na Ali katika vita, walikuwa na chuki na hasama na Ali (a.s) katika nyoyo zao. [24]
  • Wakati Mtume (s.a.w.w) anaaga dunia Ali alikuwa na umri wa miaka 33 na kukubaliwa kama kiongozi katika jamii ambayo umri na utu uzima kilikuwa kigezo muhimu cha kushika uongozi na nyadhifa, halikuwa jambo jepesi. [25] Jambo hili lilionekana wazi katika vita vya Tabuk ambapo Mtume (s.a.w.w) alimteua Ali (a.s) kushika nafasi yake mjini Madina au mwishoni mwa umri wake pale alipomteua Usama bin Zayd kuwa kamanda wa jeshi. [26]

Maneno ya mwisho katika Aya

Maneno ya mwisho katika aya ya Tablighi (Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri), yana uhusiano na madhumuni na yanaonyesha kuwa, makusudio ya watu katika Aya hii ni makafiri wasioambilika ambao wanafanya njama za kuzuia tablighi na kufikishwa ujumbe na risala ya Bwana Mtume (s.a.w.w) kuhusiana na Wilaya na uongozi wa Imamu Ali (as). Allama Muhammad Hussein Tabatabai mwandishi wa tafsiri ya al-Mizan anasema: Maneno haya ya: (Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri) yaliyoko mwishoni mwa Aya ya 67 ya Surat al-Maidah, kwa hakika yanafasiri sentesi ya kabla yake ya : (Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu), kwa maana kwamba, kulindwa Mtume na mafundisho ya Uislamu kunako hatari, vitisho na hujuma ya wanafiki kuko kwa namna hii kwamba, Mwenyezi Mungu hatoruhusu makafiri, madhalimu na mafasiki ambao wote wanautakia mabaya Uislamu, Mtume na Waislamu wawe na taathira kwa tablighi na risala ya Mtume. Hata kama maadui hao wanaweza kufikia malengo yao batili kwa muda na katika zama na sehemu fulani, lakini hilo haliwezi kuwa jambo la daima na la milele. [27]

Rejea

Vyanzo

  • Qurʾān.
  • Abū Ḥayyān, Muḥammad b. Yūsuf. Tafsīr al-baḥr al-muḥiṭ. Beirut: [n.p], 1983.
  • Abū l-Futūḥ al-Rāzī, Ḥusayn b. ʿAlī. Rawḍ al-Jinān wa rawḥ al-Janān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Abū l-Ḥasan al-Shaʿrānī & ʿAlī Akbar al-Ghaffārī. Tehran: [n.p], 1382-1387 Sh.
  • ʿAyyāshī, Muḥammad b. Masʿūd al-. Tafsīr al-ʿAyyāshī. Edited by Hāshim Rasūlī Maḥallātī. Tehran: al-Maktaba al-ʿIlmīyya al-Islāmīyya, 1363 Sh.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Mafātiḥ al-ghayb (al-Tafsīr al-kabīr). Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Ibn ʿĀshūr, Muḥammad Ṭāhir. Tafsīr al-taḥrīr wa l-tanwīr. Tunis: [n.p], 1984.
  • Ibn ʿAṭīyya, ʿAbd al-Ḥaq b. Ghālib. Al-Muḥarrar al-wajīz fī tafsīr al-kitāb al-ʿazīz. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Salām ʿAbd al-Shāfī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1422 AH.
  • Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʾīl b. ʿUmar. Tafsīr al-Qurʾān al-ʿaẓīm. Khalīl al-Mis. Beirut: Dār al-Qalam, [n.d].
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1412 AH.
  • Qurṭubī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Al-Jāmiʿ li-aḥkām al-Qurʾān. Beirut: Beirut: [n.p], 1965.
  • Suyūṭī, Jalāl al-Dīn al-. Al-Durr al-manthūr fī l-tafsīr bi-l-maʾthūr. Beirut: Dār al-Fikr, 1414 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʿ al-bayān. Edited by ʿAbd Allāh b. ʿAbd al-Muḥsin al-Turkī. [n.p]: Dār al-Hijr li-l-Ṭibāʿa wa l-Nashr, 1422 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārikh al-Ṭabarī (Tārīkh al-umam wa l-mulūk). Edited by Muḥammad Abū l-Faḍl Ibrāhīm. Beirut: Rawāʾiʿ al-Turāth al-ʿArabī, 1387 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Iʿlām al-warā bi-aʿlām al-hudā. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt li-Iḥyāʾ al-Turāth, 1417 AH.
  • Thaʿālabī, ʿAbd al-Raḥmān b. Aḥmad al-. Jawāhir al-ḥisān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Abū Muḥammad al-Ghamārī al-Idrīsī al-Ḥasanī. Beirut: [n.p], 1416 AH.
  • Tirmidhī, Muḥammad b. ʿĪsā al-. Al-Jāmiʿ al-ṣaḥīḥ. Shākir Aḥmad Muḥammad. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1408 AH.