Ayat al-Khatamiyyah

Kutoka wikishia

Ayat al-Khatamiyah (Aya ya Hitimisho) ni Aya ya 40 katika Surat al-Ahzab na ndio Aya pekee katika Qur'an Tukufu ambayo inamtambulisha Muhammad (saww) kuwa ni Mtume wa mwisho. Kufikia tamati Unabii kwa Utume wa mtukufu Muhammad (saww) ni moja ya dharura na mambo ya lazima ya dini ya Uislamu na ambalo Waislamu wote wanaafikiana juu yake. Mwanzoni mwa Aya Qur'an inakana juu ya Mtume kuwa na mtoto wa kiume wa nasaba na katika mwendelezo wa Aya inaashiriwa kwamba, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii. Baadhi ya wafasiri wanaamini kuhusiana na uhusiano wa mwanzo wa Aya na muendelezo wake kwamba, baada ya kukatwa uhusiano wa kinasaba wa Mtume na watu wengine kunaashiriwa mahusiano yake ya kimaanawi na waumini katika kalibu ya ujumbe (risala ya Utume) na hitimisho la Utume na inawataka inaowahutubu kwamba, wawe na utii kwa Mtume kutokana na nafasi ya Ujumbe wa Utume na uongozi wake. Baadhi ya watu kwa kutegemea tofauti katika maana ya Nabii na Mtume (rasuli), wamesema kwamba Aya hii inahusu tu mwisho wa Unabi, sio mwisho wa utume. Hivyo wanadai kwamba, Qur'an inamtaja Mtume Muhammad kuwa ni hitishimisho la Manabii (Khatam al-Nabiyin), sio Khatam al-Mursalin (hitimisho la Mitume, wajumbe). Kwa hiyo, Mtume ndiye Nabii wa mwisho, si mjumbe wa mwisho, na anaweza kutumwa Mtume mwingine baada yake. Katika kujibu utata huu, wafasiri wamesema kuwa maana ya Nabii inajumuisha Mtume; ina maana kwamba kila mjumbe/Mtume pia ni Nabii. Kwa hiyo, kufikia mwisho wa Unabii maana yake itakuwa pia ni kufikia tamati Ujumbe na risala ya Utume.

Nafasi na umuhimu

Aya ya 40 katika Surat al-Ahbaz inafahamika kwa jina la Ayat Khatamiyyah al-Nub'wah (hitimisho la Unabii) au Ayat al-Khatamiyyah. [2] Aya hii imetambuliwa kuwa hoja ya wazi na bainiifu zaidi kuhusiana na hitimisho la Utume la Mtume Muhammad (saww) [3] na inaashiria moja ya fadhila maalumu za Mtume (saww) ambayo ni huko kuwa kwake kwamba, ni Mtume wa mwisho na hitimisho la Unabii. [4] Suala la kwamba, Mtume (saww) ndiye Mtume wa mwisho na risala yake ndio hitimisho la Unabii ni jambo ambalo Waislamu wanaafikiana [5] na wanalitambua hilo kama dharura miongonii mwa dharura na mambo ya lazima katika dini ya Uislamu. [6] Aya hii imetambuliwa kuwa Aya pekee ndani ya Qur'an ambayo imetaja jina la Muhammad na vilevile lakabu yake ya Khatam al-Nabiyyin. [7]

Andiko la Aya na tarjumi yake

مَا کَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِنْ رِجَالِکُمْ وَلَٰکِنْ رَسُولَ الله وَخَاتَمَ النَّبِیینَ ۗ وَکَانَ الله بِکُلِّ شَیءٍ عَلِیمًا

Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu

Sababu ya kushuka kwake

Katika mlango wa sababu ya kushuka Aya hii imeelezwa kwamba, baada ya Mtume (saww) kumuoa Zaynab bint Jahsh, mke aliyetalikiwa na Zayd bin Haritha (mtoto wa kambo wa Mtume), baadhi ya watu wakiwemo wanafiki [8] walifanya njama za kuonyesha kuwa hatua hiyo ya Mtume haifai, [9] kwani kwa mujibu wa sunna na ada za kijahilia mtoto wa kambo hakuwa tofauti na mtoto wa kuzaa. [10] Mwenyezi Mungu kwa kushusha Aya hiii alionyesha kupinga ada na mazoea haya ya kijahilia [11] na kuonyesha kuwa, kumfanya Zayd kuwa mtoto wake wa kupanga kimsingi kulikuwa kwa ajili tu ya kunyanyua daraja yake [12] na katu hawezi kuwa na nafasi ya mwanawe wa kweli; kama ambavyo pia baba wa kambo au wa kupanga hawezi kuchukua nafasi na daraja ya baba halisi na mzazi. [13] Katika muendelezo wa Aya Mwenyezi Mungu anaashiria aina nyingine ya mahusiano ya Mtume na watu wengine.

Mfungamano wa mwanzo na mwisho wa Aya

Mwanzoni mwa Aya, uhusiano wa kibaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na watu wote umekataliwa, na katika muendelerzo wa Aya, ujumbe wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Utume wa Mtume Muhammad (saww) umetajwa na kuashiriwa. [15] Baadhi wakiwa na lengo la kuyahusisha madhumuni na makusudio wamesema, licha ya kuwa, uhusiano wa kinasaba wa Mtume na wengine umekatwa, lakini kunathibitishwa uhusiano wake wa kimaanawi na umma wake katika kalibu ya ujumbe (risala) na mwisho wa Utume. [16] Katika ibara inayoshabihiana na hiyo, Mtume (saww) ametajwa kuwa ni baba wa waumini wote wa kila dini; kwa sababu yeye ni Mtume wa mwisho na mrithi wa Manabii wote. [17] Katika suala hili, mapenzi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kwa watu wake kwa kuzingatia kwamba hakutakuwa Mtume tena, [18] ni kama baba ambaye mtoto wake hana mwingine ila baba huyu tu. [19] Baadhi ya watu wanaamini kwamba, kutajwa risala na ujumbe wa Mtume na hitimisho lake la Mitume baada ya kukataliwa mtoto kwa ajili yake ni kwa minajili ya kuwafanya wasikilizaji waelewe kwamba kumtii Mtume wa Mwenyezi Mungu si kwa sababu ya uhusiano wa baba, bali ni kwa sababu ya nafasi ya Utume na ni uongozi wake [20]

Utambuzi wa maana ya Khatam

Baadhi ya wasomaji wa visomo saba walisoma neno "خاتم" kwa kasr yaani Khatim badala ya Khatam, [21] baadhi ya wengine kama Asim [22] na wasomaji wengine [23] walisoma kwa fat’h yaani Khatam. Khatam kwa fat’h ina maana kwamba, Mtume Muhammad (saww) ndiye Mtume wa mwisho [24] na Khatim yaani kwa kasr ina maana kwamba, yeye ni mwenye kuhitimisha mlolongo wa Unabii. [25] Baadhi wanaamini kwamba, kusoma neno hili kwa fat’h au kasr hakuna tofauti sana na kuna maana moja. [26] Baadhi ya wafasiri wanaamini kwamba, Khatam maana yake ni kitu ambacho kinafikia tamati kupitia kwake na ni sawa na kupiga muhuri, ambapo kupitia muhuri huu nyumba, chombo au barua hulindwa kutokana na mabadiliko yoyote ya baadaye. [27] Kwa upande mwingine, kwa kuwa moja ya zana na nyenzo za kugongea muhuri ilikuwa pete ambapo muhuri wa kila mtu ulikuwa ukichongwa juu yake ni kutokana na sababu hiyo ndio maana khatam inajulikana pia kwa maana ya pete [28] na pete za mapambo ambazo hazina mchoro wa muhuri nazo zinafahamika pia kwa jina la khatam. [29] Ni kwa kuzingatia hayo, ndio maana baadhi wamefikiri kwamba kutajwa Mtume wa Uislamu (saww) kwa wasifu wa mwisho wa Mitume sio mwisho wa utume na makusudio ya Aya ni kudhihirisha msimamo wake kuwa ni pambo la Mitume. Tafsiri hii imekataliwa na baadhi ya wafasiri kutokana na uhusiano kati ya maneno khatam na pete. [30]


Hitimisho la Utume na risala

Makala asili: al-Khatamiya

Baadhi ya wakati kumekuwa kukizungumziwa na kutiliwa shaka kuhusu madhumuni na maana inayopatikana katika Aya hii [31] na hata asili ya al-Khatamiyyah (hitimisho) [32]. Baadhi wanasema kuwa, wamesema kwamba Aya hii inahusu tu mwisho wa Unabii, sio mwisho wa utume. Hivyo wanadai kwamba, Qur'an inamtaja Mtume Muhammad kuwa ni hitimisho la Manabii (Khatam al-Nabiyin), sio Khatam al-Mursalin (hitimisho la Mitume, wajumbe). Kwa hiyo, Mtume ndiye Nabii wa mwisho, si mjumbe wa mwisho, na anaweza kutumwa Mtume mwingine baada yake. [33] Katika kujibu utata huu, wafasiri wamesema kuwa maana ya Nabii inajumuisha Mtume [34]; ina maana kwamba kila mjumbe/Mtume pia ni Nabii. Kwa hiyo, kufikia mwisho wa Unabii maana yake itakuiwa pia ni kufikia tamati Ujumbe na risala ya Utume. [35] Hata hivyo kuna maana zingine ambazo zimetajwa. [36]


Kukinzana Aya na watoto wa Mtume na nafasi ya Hassanayn (as)

Ingawa Aya ya al-Khatamiyyah imeeleza wazi na bayana kabisa kwamba, haijamchukulia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kama baba wa yeyote kati ya wanaume waliozungumziwa, uwepo wa watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) kama vile Qasim, Abdullah na Ibrahim na Imam Hassan na Imamu Husein (as) ambao walikuwa wakijitambua kuwa ni watoto wa Mtume (saww), ni moja ya changamoto za Aya hii. [37] Katika kujibu baadhi ya watu wamesema kuwa neno “Rijal” ambalo maana yake ni wanaume lililotumika katika Aya hiyo, halijumuishi watoto waliokufa utotoni. [38] Aidha Hassan na Hussein wakati wa kushuka Aya hii hawakuwa wamefikia kipindi cha kubaleghe na hivyo walikuwa ni watoto. [39] Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu anasema katika Aya hiyo kwamba, Mtume wake si baba wa mwanaume yeyote kati ya wanaume waliopo na wa sasa miongoni mwenu. [40]