Nenda kwa yaliyomo

Khatam al-Nabiyyin (Lakabu)

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na lakabu ya Khatam al-Nabiyyin. Ili kufahamu kuhusiana na maisha na shakhsia ya Bwana Mtume (s.a.w.w) angalia makala ya Muhammad (s.a.w.w).

Khatam al-Nabiyyin au Khatam al-Anbiya (Kiarabu: خاتَم الأنبياء أو خاتَم النبيين) (mwisho wa Manabii ni moja ya lakabu za Mtume Muhammad bin Abdillah (s.a.w.w) ambayo inabainisha hitimisho la Utume. Kwa maana kwamba, baada yake hakuna Mtume atakayeletwa na kutumwa na Mwenyezi Mungu. [1] Ibara ya Khatam al-Nabiyyin imekuja katika Aya ya 40 ya Surat al-Ahzab ambayo ni mashuhuri kwa jina la Aya ya Khatamiyat (Aya ya hitimisho). Moja ya sababu za Waislamu kuamini hitimisho la Utume na kufikia tamati mlolongo wa kutumwa Mitume ni ibara hii ya Qur'ani. [2]

Ibara hizi mbili zimenukuliwa na kutumika katika vyanzo vya hadithi na kuna ibara zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu (a.s) kama katikka dua ya 17 ya Sahifat al-Sajjadiyyah, baadhi ya hotuba za Imamu Ali (a.s) katika Vita vya Siffin, [3] katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Ali (a.s) katika kitabu cha Qurb al-Asnad, [4] na katika hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Usul al-Kafi.[5]

Kundi la Mabahai ambalo lilidai kudhihiri na kuja dini mpya katika karne ya 12, kuna wakati lilisema Khatam ina maana ya kito cha pete [6] ambapo hiyo inaonyesha daraja maalumu ya Mtume (s.a.w.w) na kumtaja Muhammad kuwa ni pambo la Mitume na sio kwa maana ya hitimisho. [7] Baadhi pia wamesema; Qur'ani imetumia neno Khatam al-Nabiyyin na sio Khatam al-Mursalin. Kwa msingi huo, Mtume Muhammad ni Nabii wa mwisho na sio Rasuli (mjumbe) wa mwisho na yumkini baada yake akatumwa mjumbe mwingine. [8]

Wanazuoni wa Kiislamu katika kujibu wamesema, Khatam katika asili ina maana ya mhitimishaji na pete imeitwa Khatam kutokana na kuwa, huko nyuma pete ilikuwa ikitumia kupigia mhuri barua. Kwa msingi huo, kutumia lafudhi au neno «khatam» kwa maana «pambo» ni kinyume na maana ambayo inafahamika na akili katika Aya husika. [9] Kadhalika kama ilivyokuja katika Tafsir Nemooneh ni kuwa, daraja ya risalah (ujumbe) ni ya juu zaidi ya Unabii na mtu ambaye anafikia daraja ya risalah akthari yao walikuwa Manabii. Natija yake ni kuwa, wakati Unabii unapofikia mwisho, katika hatua ya awali risalat au utume nao unapaswa kuwa umefikia tamati. [10]

Nchini Iran na katika mataifa mengine ya Kiislamu, baadhi ya misikiti, shule, vyuo vya kielimu (Hawza), Vyuo Vikuu na kadhalika vimepewa jina la Khatam al-Nabiyyin au Khatam al-Anbiya. [10] Kadhalika ibara zilizochukuliwa kutoka katika lakabu hii kama «Asalaam alaa Khatam al-Nabiyyin» imechongwa na kuandikwa juu ya pete.

Rejea

Vyanzo