Aya ya Nafs al-Mutmai’nna
- Kuna tofauti baina ya al-Nafs al-Mutmai’nna na Aya ya al-Nafs al-Mutmai’nna
Aya za al-Nafs al-Mutmai’nna (Kiarabu: آية النفس المطمئنة) ni Aya nne za mwisho katika Surat al-Fajr ambazo ndani yake kumebainishwa sifa maalumu za nafsi iliyotua na kutolewa bishara na habari njema za kuingia peponi kwa mwenye nafsi hiyo.
Wanazuoni wa Kiislamu wanaitambua al-Nafs al-Mutma’inna kuwa ni mwanadamu ambaye katika imani yake kwa Mwenyezi Mungu amefikia katika hatua ya yakini na utulivu na hana muelekeo wa kutenda dhambi. Mwenye kuridhika na mwenye kuridhiwa (Radhia na Mardhia) ni sifa mbili maalumu za hii nafsi: Kuridhika na ujira wa Mwenyezi Mungu au kuridhika na kadha na kadari ya Mwenyezi Mungu na ni mwenye kuridhia kwa radhi za Mwenyezi Mungu ni katika maana ya nafsi iliyotua.
Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, Imam Ali (a.s), Imam Hussein (a.s) na Mashia ni miongoni mwa vielelezo hivyo.
Andiko la Aya na tarjumi yake
Aya za 27-30 za Surat al-Fajr ni Aya inayotambulika au zinazotambulika kwa Aya za al-Nafs al-Mut’mai’nna:
يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ
Ewe nafsi iliyotua!.
ارْجِعِي إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً
Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha.
فَادْخُلِي فِي عِبَادِي
Basi ingia miongoni mwa waja wangu.
وَادْخُلِي جَنَّتِي
'Na ingia katika Pepo yangu.
(Quran: 89: 27-30)
Maana ya al-Nafs al-Mutma’inna
- Makala asili: Al-Nafs al-Mutmai’nna
Al-Nafs al-Mutmainna (nafsi iliyotua) ni hali ya nafsi au ada ya mtu ambayo ndani yake kutokana na kudumu katika kufuata akili katika kujitenga mbali na dhambi, kitendo hiki huwa ni uwezo na ada ya mwanadamu na katika mazingira haya hupatikana hali ya utulivu na uhakika. Katika hali hii nafsi humzuia kuelekea kutenda dhambi. [1] Wanazuoni wa Kiislamu wanasema kuwa, nafsi ina daraja kadhaa: Daraja ya chini zaidi ni al-Nafs al-Ammara ambayo ndani yake mwanadamu hafuati wala kutumia akili (kwa njia sahihi), bali anakuwa ni mwenye kufuata na kuiendea dhambi na ufisadi katika maamuzi na matendo yake. Yaani ni mwenye kuifuata tu nafsi yake kwa kila inachoamrisha na kutaka. Nafsi ya juu zaidi ya hiyo ni nafs lawwamah kwa maana ya nafsi yenye kujialaumu, ambapo katika hali hii mwanadamu ni mwenye kujilaumu kutokana mambo na matendo mabaya ambayo ameyafanya. Ama nafsi ya juu zaidi ya nafsul ammara ni nafs Mut’mainna. Katika hatua na daraja hii ya nafsi, ni kwamba kutokana na mtu kufuata maamuzi ya akili sahihi kwa muda mrefu na kwa daima, hivyo kitendo hiki huwa na athari na mazoea chanya katika nafsi yake na kuipelekea nafsi kufikia hatua na daraja ya utulivu na yakini. [2]
Tafsiri
Wafasiri wanasema kuwa, makusudio ya “al-Nafs al-Mutmai’nna” katika Aya ya 27 ya Surat al-Fajr ni waumini ambao wamefikia yakini na utulivu na ambao hawana shaka na hali ya kusitasita katika imani yao. [3] Allama Tabatabai anasema, nafsi iliyotua (al-Nafs al-Mutmai’nna) ni ile ambayo imefikia utulivu kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, yenye kuridhia radhi za Mwenyezi Mungu na panda shuka za maisha hazina taathira kwake. Mtu wa aina hii ni mkamilifu katika uja na hakengeuki njia nyoofu. [4] Katika tafsiri ya Maj’maa al-Bayan imeelezwa kuwa, nafsi iliyotua ni nafsi ambayo imepata utulivu katika kivuli cha imani na hiyo ni hakika ya imani. [5] Tabrasi anasema katika tafsiri yake ya Majmaa al-Bayan alipokuwa akitoa maana ya Radhia na Mardhiya ya kwamba: Mtu mwenye nafsi iliyotua ni mwenye kuridhia ujira na malipo ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu pia ameiridhia amali na matendo yake. [6] Allama Tabatabai anasema, nafsi iliyotua imepewa sifa ya radhia na mardhiya kutokana na kwamba, kuwa na uhakika na Mwenyezi Mungu kunapelekea nafsi kuridhia kadhwa na kadari. Kwa msingi huo, matukio mabaya hayamkasirishi na hachafuki na kutumbia katika dhambi. Ni kutokana na sababu hii ndio maana “Mardhiyah” maana yake Mwenyezi Mungu amemridhia; kwani Mwenyezi Mungu huingiwa na ghadhabu na mtu, pale mtu huyo anapotoka katika uja na kuabudu. [7]
Kwa mujibu wa tafsiri Nemooneh neno “raadhiya” linaonyesha kuwa, wenye nafsi hii wanaona kutimia kwa ahadi zote za Mwenyezi Mungu na wameridhika nazo. Hii inaonyesha daraja ya kuridhia na kujisalimisha kikamilifu; daraja ambayo kupitia kwayo kila kitu kinapitia katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mardhiyah nayo ina maana kwamba, wenye nafsi hii wameridhiwa na Mwenyezi Mungu. [8]
Baadhi wamesema, kuhutubiwa nafsi na kuambiwa “Rejea kwa Mola wako Mlezi” hii ni kuhusiana na Siku ya Kiyama wakati waumini watakapotaka kuingia peponi. Kuna baadhi pia wanaamini kwamba, nafsi huambiwa maneno haya wakati wa kuaga dunia. [9] Allama Tabatabai amekubaliana na nadharia ya pili. [10] Kadhalika kwa mtazamo wake ni kwamba, Aya inayosema, “Basi ingia miongoni mwa waja wangu”, inaonyesha kuwa, nafsi iliyotua imefikia katika daraja kamili ya uja na kuabudu; yaani daraja ambayo ndani yake haitaki kitu isipokuwa ambacho kinatakiwa na Mwenyezi Mungu. [11] Kwa mujibu wa Allama Tabatabi ni kwamba, Aya ya ya 30 katika Surat al-Fajr inayosema: “Na ingia katika Pepo yangu”, kumetumika ukarimu maalumu; kwani ni Aya pekee ya Qur’an ambayo Mwenyezi Mungu ameinasibisha pepo kwamba, ni yake. [12]
Imam Ruhullah Khomeini anamtambua mwanadamu kwamba ni kiumbe ambaye katika dhati yake ni mwenye kutafuta nguvu mutlaki, ukamilifu mutlaki na elimu mutlaki, na kwa kuwa nguvu mutlaki haipatikani kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ukweli wa mambo ni kuwa anataka haki kwa fitra na maumbile yake na yeye mwenyewe hafahamu kwamba, bila ya kuunganika na bahari ya ukamilifu mutlaki, hawezi kupata utulivu. “Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!”. Kwa mtazamo wake ni kuwa, nafsi hufikia utulivu pale inapofikia katika ukamilifu mutlaki, Ukamilifu mutlaki ni pale anapokuwa na itikadi kwamba, awepo Mwenyezi Mungu tu na asiyekuwa yeye asiwepo. Katika hali hii nafsi hii haizingatia cheo, uongozi wala ufalme bali humzingatia Allah Mola Muumba na utajo huwa ni maalumu kwa Allah pekee. [13]
Tafsiri kwa mujibu wa hadithi kuhusu al-Nafs al-Mutma’inna
Katika vitabu vya tafsiri kwa mujibu wa hadithi na vitabu vingine vya hadithi, kumebainishwa mifano na vielelezo vya nafsi iliyotua. Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) katika Tafsir Furat al-Kufi [14], na Shawahid al-Tanzil, [15], Imam Ali (a.s) ametajwa kuwa mfano na kielelezo cha al-Nafs al-Mutma’inna. Kwa mujibu wa kitabu cha Tafsir al-Qumi, Imam Swadiq (a.s) amesema, makusudio ya nafsi iliyotua ni Imam Hussein (a.s). [16] Imekuja pia katika kitabu cha hadithi cha Bihar al-Anwar cha Allama Majlisi ya kwamba, Surat al-Fajr ni Sura ya Imam Hussein; kwani Hussein alikuwa na nafsi iliyotua. Katika hadithi hii, maswahaba wa Imam Hussein pia wametambulishwa kwamba, wameridhia na wameridhiwa; kwani Siku ya Kiyama watakuwa ni wenye kumridhia Mwenyezi Mungu na Allah atakuwa ni Mwenye kuwadhiria. [17]
Katika kitabu cha al-Kafi kilichoandiokwa na Sheikh Kulayni, imenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ambapo amefasiri Aya ya al-Nafs al-Mutmai’nna au Aya za al-Nafs al-Mutmai’nna (Aya za nafsi iliyotua) namna hii: Ewe nafsi ambaye umepata utulivu na yakini kwa Muhammad na Ahlul-Bayt (a.s), rejea kwa Mola wako katika hali ambayo, umeridhika na Wilaya (uongozi) ya Ahlul-Bayt (a.s) na utakuwa ni mwenye kuridhia na ujira wa Mwenyezi Mungu. Basi ingia katika orodha ya waja wangu yaani Muhammad na watu wa nyumba yake na ingia peponi.” [18]
Rejea
Vyanzo
- Furāt al-Kūfī, Abu l-Qāsim Furāt b. Ibrāhīm. Tafsīr Furāt al-Kūfī. Tehran: Sāzmān-i Chāp wa Intishārāt-i Wizārat-i Irshād-i Islāmī, 1410 AH.
- Ḥaskānī, ʿUbayd Allāh b. ʿAbd Allāh al-.Shawāhid al-tanzīl li-qawāʿid al-tafḍīl. Edited by Muḥammad Bāqir Maḥmūdī. Tehran: Majmaʿ Iḥyāʾ al-Thiqāfat al-Islāmī, 1411 AH.
- Imām Khomeinī, Sayyid Rūḥollāh. Ṣaḥīfa-yi nūr. Tehran: Markaz-i Nashr-i Āthār-i Imām Khomeinī, 1378 Sh.
- Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
- Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
- Misbāḥ Yazdī, Muḥammad Taqī. Āʾyīn-i parwāz. 9th edition. Qom: Intishārāt-i Muʾassisa-yi Āmūzishī wa Pazhūhishī-yi Imām Khomeiniī, 1399 Sh.
- Muṭahharī, Murtaḍā. Majmūʿa-yi āthār. Qom: Intishārāt-i Ṣadrā, 1389 Sh.
- Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Ṭayyib Mūsawī Jazāʾrī. Qom: Dār al-Kitāb, 1404 AH.
- Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
- Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Maʿrifa, 1406 AH.