Al-Nafs Al-Ammara (Kiarabu: النفس الأمارة) Nafsi yenye kuamrisha ; ni hali ya kinafsi ambayo inavuta na kumshawishi mtu kufanya mambo, maovu, mabaya na madhambi. Istilahi hii imechukuliwa kutoka katika aya ya 53 ya Surat Yusuf. Maana ya matamanio ya nafsi ni ileile nafsi ya kuamrisha. Hali kadhalika kinachokusudiwa katika jihadi ya nafsi au jihadi kubwa ambayo imebainishwa katika riwaya, ni kupambana na nafsi yenye kuamrisha.

Al-Nafs Al-Ammara (yenye kuamrisha) ni mkabala wa na Al-Nafs Al-Lawwamah, (yenye kujilaumu) na Al-Nafs Al-Mut’mainnah, (yenye utulivu na kutulia). Nafsi yenye kuamrisha maovu inajulikana kwamba ni daraja ya chini zaidi ya nafsi. Daraja ya juu ya hapo ni nafsi yenye kujilaumu (nafs lawwama), nayo ni nafsi ambayo inamfanya mwanadamu ajilaumu mwenyewe kutokana na makosa na dhambi zake alizofanya. Ama nafsi ya juu zaidi ya nafsi ya kujilaumu, ni nafsi yenye kutulia (nafs mut’mainnah) ambapo kwa kuwa na hali hiyo ya kinafsi mwanadamu anakuwa katika hali ya utulivu na yakini.

Utambuzi wa maana

Al-Nafs Al-Ammara au nafsi yenye kuamrisha, inakusudiwa kuwa ni nafsi yenye kuamrisha sana mambo maovu; nayo ni hali ya kinafsi ambayo ndani yake mwanadamu hawezi kufuata wala kutumia akili (kwa njia sahihi), bali anakuwa ni mwenye kufuata na kuiendea dhambi na ufisadi katika maamuzi na matendo yake[1]. Yaani ni mwenye kuifuata tu nafsi yake kwa kila inachoamrisha na kutaka. Istilahi inapatikana katika Aya isemayo: ((إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَ‌ةٌ بِالسُّوءِ ; Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana (mambo) mabaya))[2]. Hivyo basi kama tulivyoashiria istilahi hiyo imechukuliwa kutoka katika Aya hiyo tukufu.[3]. Nafs Ammara inajulikana kuwa ndio yale matamanio na hawaa za nafsi.[4]

Nafs Ammara, nafsi ya daraja ya chini zaidi

Baadhi wanaona kuwa, nafsi ina daraja tofauti tofauti na wanaihesabu na kuiweka Nafs Ammar (nafsi yenye kuamrisha maovu) katika daraja ya chini zaidi ya nafsi. Wanasema kwamba; Nafsi ina daraja kadhaa; ambapo daraja ya chini zaidi ni nafs ammara (yenye kuamrisha mabaya), ambapo katika hali ya nafsi hiyo, mwanadamu hawezi kutumia wala kufuata maamrisho na maamuzi ya akili salama. Nafsi ya juu zaidi ya hiyo ni nafs lawwamah kwa maana ya nafsi yenye kujialaumu, ambapo katika hali hiyo mwanadamu ni mwenye kujilaumu kutokana mambo na matendo mabaya ambayo ameyafanya. Ama nafsi ya juu zaidi ya nafsul ammara ni nafs Mut’mainnah[5]. Katika hatua na daraja hii ya nafsi, ni kwamba kutokana na mtu kufuata maamuzi ya akili sahihi kwa muda mrefu na kwa daima, hivyo kitendo hiki huwa na athari na mazoea chanya katika nafsi yake na kuipelekea nafsi kufikia hatua na daraja ya utulivu na yakini[6].

Kutopingana nafsi tofauti na utambulisho mmoja wa mwanadamu

Maulamaa wa dini tukufu ya kiislamu wanasema kwamba, mwanadamu ana nafsi (ambayo ni yeye mwenyewe yaani mmoja) na mtu kuwa na nafsi moja haipingani na suala la uwepo wa nafs Ammara, nafs lawwama wala nafs Mut’mainnah ambazo zina maana ya nafsi yenye kuamrisha maovu, nafsi yenye kujilaumu kutokana na makosa yake na nafsi yenye utulivu na yakini. Wanazuoni wa Kiislamu wanaamini kwamba, istilahi hizi (za aina za nafsi) ni hali, hatua na daraja mbali mbali ambazo zinaonyesha nafsi na kuitambulisha hali zake[7]. Yaani ni kwamba; wakati ambapo nafsi inapotoa amri ya (mtu) kufanya mambo mabaya au matendo maovu, tunasema kwamba hiyo ni nafs ammara yenye kuamrisha maovu. Wakati ambapo nafsi (ya mtu) yenyewe inajilaumu kutokana na makosa yake, nafsi hiyo tunaiita kwa jina la nafs Lawwama au nafsi yenye kujuta kutokana na makosa yake[8].

Kupambana na al-nafs al-ammara

Makala asili: Jihadi ya Nafsi

Katika hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) inabainisha kwamba: Vita vya kijeshi vinajulikana kwa jina la jihadi ndogo na mapambano dhidi ya nafsi yamepewa jina la jihadi kubwa[9]. Allama Tabatabai anaamini kwamba mapambano na nafsi ambayo yemetajwa katika riwaya ni mapambano na nafs ammara (yenye kuamrisha maovu)[10]. Hali kadhalika Allama Muhammad Baqir Majlisi kwa kutumia hadithi isemayo kwamba adui wako mkubwa zaidi ni nafsi yako! Naye anaamini kwamba, nafsi inayokusudiwa ni nafsi yenye kuamrisha maovu[11]. ‘’ Adui mkubwa zaidi ‘’ wa mwanadamu ni nafs ammara yaani nafsi yenye kuamrisha (maovu).[12] Shahidi Muratadha Mutahhari pia kwa kutegemea hadithi isemayo: المُجاهِد مَن جاهَدَ نَفْسَه; Mwenye kufanya jihadi ni yule mwenye kupambana na nafsi yake[13], ameandika kwamba; makusudio ya jihadi ya nafsi ni kupambana na nafs ammara yenye kuamrisha maovu[14].

Rejea

  1. Mishbah Yazdi, Ayne Parvaz, 1399 S, uk. 27
  2. Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, 1403 H, juz. 67, uk. 37
  3. Surat Yusuf: aya 53
  4. Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, juz. 67, uk. 36; Mutahhari, Majmu'i-e Athar, 1389 S, juz. 23, uk. 592
  5. Mishabah Yazdi, Ayne Parvaz, uk. 26-27; Mutahhari, Majmu'i-e Athar, juz. 3, uk. 595-596
  6. Mishbah Yazdi, Ayne Parvaz, uk. 27
  7. Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, juz. 67, uk. 36-37; Mutahhari, Majmu'i-e Athar, juz. 3, uk. 595; Mishbah Yazdi, Akhlaq va Efrane Islami, uk. 8
  8. Mishbah Yazdi, Akhlaq va Erfane Islami, uk. 8
  9. Tazama: Kulaini, al-Kafi, 1407 H, juz. 5, uk. 12
  10. Allamah Tabatabai, al-Mizan, 1417 H, juz. 14, uk. 411
  11. Majmu'atu Warram, 1410 H, juz. 1, uk. 59
  12. Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, juz. 67, uk. 36-37
  13. Sayyied Radhi, al-Majazat al-Nabawiyyah, 1422 H, uk. 194
  14. Mutahhari, Majmu'i-e Athar, juz. 23, uk. 592

Vyanzo

  • Kulaini, Muhammad bin Yaqub. Al-Kafi. Peneliti dan editor Ali Akbar Ghaffari dan Muhammad Akhundi. Teheran: Dar al-Kutub al-Islamiyah, cet. IV, 1407 H.
  • Al-Majlisi, Muhammad Baqir. Bihar al-Anwar li Durar Akhbar Aimmah al-Athhar. Beirut: Dar Ihya' al-Turats al-Arabi, vet. II, 1403 H.
  • Mishbah Yazdi, Muhammad Taqi. Ayne Parvaz, ringkasan Jawad Muhditsi. Qom: Penerbit Muassasah Amuzeshi va Pazuheshi Imam Khomaini, cet. VIIII, 1399 HS.
  • Muthahhari, Murtadha. Majmu'i-e Atsar. Teheran: Penerbit Shadra, 1389 HS.
  • Sayyied Radhi, Muhammad bin Hassan. Al-Majazat al-Nabawiyyah. Peneliti/editor Mahadi khushmand. Qom: Dar al-Hadits, cet. I, 1422 H.
  • Tabatabai, Sayyied Muhammad Hussein. Al-Mizan fi Tafsir al-Quran. Qom: Kantor Penerbit Islami, cet. V, 1417 H.
  • Warram bin Ibn Piras, Mas'ud bin Isa. Majmu'atu Warram. Qom: Perputakaan Faqih, cet. I, 1410 H.