Nenda kwa yaliyomo

Aya ya Ahl al-Dhikr

Kutoka wikishia
Aya ya Ahlu-Dhikr
Jina la AyaAya ya Ahlu-Dhikr
Sura HusikaNahl, Anbiyai
Namba ya Aya7 na 43
Juzuu14 na 17
Sababu ya KushukaKupinga Dhana ya Washirikina Kuwa Mitume Lazima Wawe ni Malaika
Mahali pa KushukaMakka
MaudhuiItikadi
Mada YakeKuwauliza Wale Wenye Ujuzi
MengineyoMiongoni Mwa Fadhila za Ahlul-Bayt (a.s)


Aya ya Ahlu-Dhikr (Kiarabu: آية أهلُ‌ الذّكر) (Nahl: 43 na Anbiya: 7) zinataka watu wote hususan washirikina kuwauliza wenye elimu kuhusiana na uhakika wa Utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Aya hii ilishuka wakati washirikina wa Makka walipokana wito wa Mtume (s.a.w.w) na kusema, Mwenyezi anapaswa kuchagua na kuteua Mtume miongoni mwa Malaika.

Kwa mujibu wa mtazamo wa wafasiri makusudio ya Ahl Dhikr katika Aya hizi ni Maulamaa wa Kiyahudi na manasara au wasomi na wajuzi wa habari za kale na wenye ufahamu wa hali ya mambo ya umma na kaumu zilizotangulia na makusudio ya swali ni kuuliza kuhusiana na ishara na alama za Utume ambazo zimo katika vitabu vyao.

Wafasiri wamekuja na hadithi mbalimbali chini ya Aya hizi wakizitumia kama hoja kutoka katika vitabu vya Shia na Ahlu-Sunna wamesema kuwa, mfano wa wazi kabisa wa Ahlu-Dhikr ni Ahlul-Bayt (a.s) ambao ni lazima kuwauliza wao kuhusu hukumu na sheria za dini na tafsiri ya Qur’an.

Katika baadhi ya vitabu vya Usul Aya hii imetumika kwa ajili ya kuthibitisha juu ya kuwa hoja khabar Wahed (hadithi ambayo kutokana na idadi ya wapokezi wake hakuna uhakika kama imetoka kwa Maasumu).

Andiko la Aya na Tarjumi'

﴾وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ إِلاَّ رِجَالاً نُّوحِي إِلَيْهِمْ فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ﴿


Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui.



(Quran: 16: 43).


Sababu ya Kushuka Kwake

Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba wakati Muhammad (s.a.w.w) alipochaguliwa kuwa Mtume, suala hili lilikuwa zito kwao watu wa Makka na wakaukanusha Utume wake. Walisema kwamba Mungu ni mtukufu zaidi ya kuchagua Nabii kutoka miongoni mwa wanadamu. Katika kujibu madai ya washirikina, ikashuka Aya hii na Aya ya pili ya Sura Yunus: (أَكَانَ لِلنَّاسِ عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَى رَجُلٍ مِّنْهُمْ ; Je! Imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia mmoja wao).[1] Kadhalika imeelezwa kwamba, Aya ya al-Dhikr ilishuka kwa ajili ya kujibu madai ya washirikina ambao walikuwa wakisema, kwa nini Mtume wa Allah asiwe anatokana na Malaika. [2]

Maudhui

Tabarsi, katika tafsiri yake ya Majmaal al-Bayan, anazingatia kipande cha mwanzo wa Aya kwamba, kinaashiria nukta hii kwamba, Mungu alimtuma Mtume wake kutoka miongoni mwa watu ili watu waweze kumuona, kuzungumza naye, na kuelewa maneno yake; kwa hiyo, si sahihi kwamba badala ya mwanadamu, malaika amepewa jukumu la kutangaza ujumbe huo akiwa Nabii. [3]

Allama Tabatabai pia anaizingatia Aya hiyo kwamba, imo katika kubainisha namna ya kutuma Mitume ili washirikina wajue kuwa mwito na ulinganiaji wa kidini ni mwito wa kawaida; kwa tofauti hii kwamba, Mwenyezi Mungu huwatuma wenye mwito huu kwa njia ya wahyi kwa ajili ya kile ambacho ni kheri duniani na akhera, na hakuna nguvu ya ghaibu inayobatilisha hiari na irada ya watu na kuwalazimisha kuukubali mwito wa kidini, na hakuna Nabii aliyedai kwamba kupitia utashi wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu na nguvu ya ghaibu atausambaratisha mfumo unaotawala sasa ulimwenguni. [4] Kwa mtazamo wake kidhahiri ni kuwa, sehemu ya pili ya Aya yaani: (فَسْئَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لا تَعْلَمُونَ ; Basi waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui) Licha ya kuwa mhutubiwa ni Mtume na kaumu yake, lakini inawahutumu watu wote hususan washirikina ya kwamba, kila ambaye hajapata uhakika wa wito wa Unabii na Utume, anapaswa kuuliza wenye elimu. [5] Allama Tabatabai anaamini kuwa, ijapokuwa dhahiri ya Aya ya Ahlu-Dhikr inahutubu watu wote; lakini Mtume na Waumini wanaojua mipango ya Mwenyezi Mungu kuhusu Mitume (ambao wanatoka miongoni mwa watu wa kawaida) na jukumu lao na wala hawana haja ya kuwauliza watu wenye elimu na washirikina ambao si tu kwamba hawauamini Utume na risala ya Mtume wao; bali wanamfanyia dhihaka na kumuita kuwa ni mwendawazimu; natija yake wanabakia wafuasi wa Torati tu (mayahudi) kwa kuzingatia kwamba, wana uadui na Mtume ambao ndio wanaohutubiwa katika Aya hii. [6]

Makarim Shirazi, katika tafsiri yake ya Nemooneh pia, anaizingatia sehemu ya pili ya Aya (kuuliza wenye kujua) kwamba, inatilia mkazo na kuthibitisha ukweli huu kwamba ni wajibu wa Mitume kuwaletea watu wahyi kwa njia za kawaida, si kuwalazimisha watu kwa nguvu isiyo ya kawaida na kuvuruga sheria za kimaumbile na kuwalazimisha watu wakubali wito na kuacha upotofu wote ambapo kama ingekuwa hivyo, kuamini kusingekuwa tena jambo la fahari na ukamilifu. [7]

Ahlu-Dhikr na Mifano Yake

Wafasiri wa Qur’an wamejadili na kufanyia utafiti chini ya Aya hii kuhusiana na makusudio ya Ahl al-Dhikr pamoja na mifano na vigezo vyake. Kwa mujibu wa mtazamo wa wafasiri, kwa kuzingatia muktadha na mlolongo wa Aya hii, inafahamika kuwa, makusudio ya Ahl al-Dhikr ni wasomi na wenye elimu na weledi; wale ambao wana uhusiano na dhikr (Qur'ani, vitabu vya mbinguni n.k.) na katika Aya zilizojadiliwa: Ahl Dhikr ni wanachuoni wa Kiyahudi na Wakristo [8] au wanachuoni wa habari za zamani na wajuzi wa mambo na hali za umma na kaumu zilizopita. [9] Makusudio ya swali nayo ni kuuliza kuhusu alama na ishara za Unabii zilizomo katika vitabu vyao. [10] Hata hivyo, wafasiri wameichukua dhana ya Ahlul-Dhikr kwa ujumla na kutaja mifano mingine kwa ajili yake. Miongoni mwa wafasiri wa Shia na Sunni, kuna mitazamo miwili kuhusu mfano wa Ahl al-Dhikr:

Ahlul-Bayt (a.s)

Wafasiri wa Kishia, wakinukuu hadithi mbalimbali [11] wamewachukulia Ahlul-Bayt (a.s) kama mfano wa wazi wa Ahlu-Dhikr. [12] Katika tafsiri za Ahlu-Sunna pia wakitegemea hadithi mbalimbali ikiwemo ya kutoka kwa Harith ambapo naye amepokea kutoka kwa Imamu Ali (a.s) ni kwamba, makusudio ya Ahlu-Dhikr (wenye elimu) wametambuliwa kuwa ni Muhammad, Ali, Fatima, Hassan na Hussein; wale waliobobea katika elimu na katika tafsiri. [13] Qurtubi na Tabari, miongoni mwa wafasiri wa Kisunni, wananukuu hadithi chini ya Aya ya 7 ya Sura Anbiyyah, ambamo Ali (a.s) alisema wakati wa kuteremka Aya hii kwamba: Sisi ndio Ahl al-Dhikr (wenye elimu). [14]

Katika kitabu cha Basair al-Darraj, kuna riwaya 28 katika mlango wenye anuani isemayo: فی ائمة آل محمد انهم اهل الذکر الذین امر الله بسؤالهم; Maimamu wa familia ya Muhammad ni wale ambao ni wenye elimu ambao Mwenyezi Mungu ameameamrisha waulizwe wao; Imenukuliwa katika mlango huo kwamba, makusudui ya Ahlu-Dhikr ni Ahl-Bayt (a.s). [15] Miongoni mwazo ni hadithi ya 11 ya mlango huu ambayo imenukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ambapo alisema katika kufasiri Aya hii ya kwamba, makusudio ya Dhikr ni Muhammad (s.a.w.w) na sisi Maimamu ni familia yake na ni sisi ambao tunapaswa kuulizwa. [16] Katika kitabu cha Kafi Sheikh Kulayni pia ameileta katika kitabu chake hicho hadithi isemayo: ان اهل الذکر الذین امر الله الخلق بسؤالهم هم الائمه ; Hakika Ahlu-Dhikr ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha kuulizwa ni Ahlul-Bayt. [17] Allama Majlisi pia katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar katika mlango wa: Hakika Ahlu-Bayt ndio Ahl Dhikr” ananukuu hadithi ambayo inaeleza kwamba, makusudio ya Ahlu-Dhikr ni Maimamu wa Shia. [18]

Kwa mujibu wa Makarim Shirazi, kukubali suala la kwamba Ahlul-Bayt ni mfano wa wazi kabisa wa Ahlu-Dhikr hakupingani na kuteremshwa kwa Aya hii kuhusu wanavyuoni wa Kitabu; kwa sababu suala hili limerudiwa mara nyingi katika hadithi za ufafanuzi wa Qur'an na kuna mifano maalumu ambayo haiwekei mipaka maana pana ya Aya. [20]

Wanazuoni

Kulingana na baadhi ya watafiti, mara nyingi kulingana na muktadha wa Aya hiyo, watu Ahlu-Dhikr imeelezwa na kutolewa maana kuwa ni watu wa kitabu au watu wa elimu (wasomi). [21] Maana ya Ahl Dhikr inajumuisha wale wote ambao wana ujuzi na ufahamu zaidi. Aya hii inachukuliwa kuwa ni muongozo wa moja ya kanuni za kiakili na kanuni za jumla za kiakili, ambayo inazungumzia ulazima wa mjinga kumrejelea mwanachuoni katika kila nyanja na fani, na kwa ajili hiyo, ni wazi kwamba, utaratibu huu ni sio amri ya ibada, na sio amri ya Kimola. [22]

Wafasiri wa Ahlu Sunna wametoa maana 15 kuhusu Ahlu-Dhikr [23] ambapo makusudio yake ni makundi matatu: Ahlul-Kitab kwa sura aam na jumla zaidi (kila kitabu ghairi ya Torati na Injili) au kwa sura khaas na maalumu zaidi (kwa mfano Ahl torati), Ahl Qur’an [24] na Ulamaa wa Ahlul Bayt. [25]

Matumizi ya Kifikihi; Hoja ya Khabar Wahid

Katika usul Fiq’h baadhi wakiwa na lengo la kuifanya khabar wahed (hadithi ambayo kutokana na idadi ya wapokezi wake hakuna uhakika kama imetoka kwa Maasumu) kuwa hoja huitumia Aya hii ya Ahl Dhikr; kwa ujengeaji hoja huu kwamba, wakati katika Aya kuuliza wanaojua na wenye elimu kunahesabiwa kuwa ni jambo la wajibu, basi ni wajibu pia kusikiliza maneno yao; kinyume na hivyo wajibu wa kuuliza utafutwa na kuondolewa. [26] Hata hivyo kuna waliokosoa ujengeaji huu. Miongoni mwao ni Sheikh Murtadha Ansari ambaye amesema, kwa mujibu wa hadithi makusudio ya Ahlu-Dhikr ni Maimamu na sio wapokezi wa hadithi zao. [27]

Rejea

Vyanzo