Suratu al-A'ala

Kutoka wikishia
Surat al-A’la

Surat al-A’la (Kiarabu: سورة الأعلى) ni sura ya 87 na ni miongoni mwa sura za Qur’an zilizoshushwa Makka (Makki) na ipo katika Juzuu ya 30 ya msahafu. Jina la sura hii yaani al-A’la limechukuliwa kutoka katika Aya yake ya kwanza na maana yake ni “juu kabisa”. Aya za mwanzo za sura hii, zinamtaka Mtume (s.a.w.w) alitakase jina la Mola wake, amtaje na kumsabihi na kisha baadaye zinataja sifa saba za Mwenyezi Mungu. Aidha katika muendelezo wa sura hii Mwenyezi Mungu anazungumzia waumini wanyenyekevu, makafiri waovu na sababu za furaha na huzuni za makundi haya mawili.

Kuhusiana na fadhi la kusoma sura hii, imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ya kwamba: Mwenye kuisoma sura hii Mwenyezi Mungu atampa thawabu za mema kumi kwa kila herufi iliyoshushwa kwa Nabii Ibrahim, Mussa na Muhammad (s.a.w.w). Imekuja katika hadithi pia, Mtume alikuwa akiipenda sana sura hii.

Utambulisho

Hakika amefaulu yule aliyejitakasa (Surat al-A’la:14).
  • Kupewa jina

Surat al-A’la imepewa jina la “al-A’la” kwa mnasaba huu kutokana na kuwa inaanza na kutakasa jina la Mola Mlezi aliye juu kabisa. [1] A’la ina maana ya kitu kilichoko juu kabisa. [2]

  • Mpangilio na mahali iliposhuka

Surat al-A’la ni sura ya 87 [3] na ni miongoni mwa sura za Qur’an zilizoshushwa Makka (Makki) na ipo katika Juzuu ya 30 ya msahafu. Kwa mujibu wa mpangilio wa kushuka, hii ni sura ya nane aliyoshushiwa Mtume (s.a.w.w). Allama Tabatabai, mwandishi wa tafsiri ya al-Mizan anaamini kuwa, Aya 13 za sura hii zimeshuka Makka lakini Aya ya 14 mpaka mwisho kwa sababu zinahusiana na Saumu na mambo yake ya lazima kama Zakat al-Fitr na Sala ya Idi ni mambo ambayo yanaonyesha kwamba, imeshuka Madina, kwani Saumu ilifaradhishwa Madina. Kadhalika anasisitiza kwamba, hadithi ambazo zimeitambua sura hii kwamba, imeshuka Makka, makusudio yake ni hizo hizo Aya 13 za mwanzo. [4]

  • Idadi ya Aya na sifa maalumu

Surat al-A’la ina Aya 19, ina maneno 72, na herufi 296. Sura hii ni miongoni mwa zile sura zinazojulikana kwa jina la Mufassalat (yaani zenye Aya fupi) na ni sura ya mwisho kushuka miongoni mwa sura za Musabbihat (zinazoanza na kumsabihi Mwenyezi Mungu). [5]

Maudhui

Kitabu cha Tafsiri al-Mizan kimeutambua mhimili mkuu wa sura hii kuwa ni tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na kutilia mkazo dhati na nafasi iliyotukuka ya Mwenyezi Mungu na vilevile ahadi za Mwenyezi Mungu kwa Mtume na uthibitisho wake. [6] Kwa mujibu wa mtazamo wa Tafsir Nemooneh, Surat al-A'la imeundwa na sehemu mbili: Sehemu ya kwanza inahusiana na Mtume na inatoa maagizo kwa Mtume ya kumsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kutekeleza ujumbe na risala yake. Kadhalika katika sehemu hii ya kwanza kunatolewa maelezo ya sifa saba za Mwenyezi Mungu. Katika sehemu ya pili Mwenyezi Mungu anazungumzia waumini wanaonyenyekea na makafiri waovu na sababu za furaha na huzuni za makundi haya mawili. [7]

Maudhui ya Surat al-A'la

Kuwa ya haki risala ya kitawhidi ya Mtume:

  • Maudhui ya kwanza: (Aya ya 1-13) jukumu la Mtume katika kubainisha tawhidi:
  1. Jukumu la Kwanza: (Aya ya 1-5) Kumsabihi Mwenyezi Mungu aliye juu kabisa.
  2. Jukumu la Pili: (Aya ya 6-13) kuwafikishia ujumbe wa tawhidi kwa wanaotafuta haki.
  • Maudhui ya Pili: (Aya ya 14-19) hoja za kuwa haki mwito wa tawhidi wa Mtume (s.a.w.w.):
  1. Hoja ya Kwanza: (Aya ya 14-17) Kuwa watakasifu wanaomuabudu Allah.
  2. Hoja ya Pili: (Aya ya 18-19) Kutoa ushahidi vitabu vya Mitume kuhusu Tawhidi.[8]

Tafsiri

Mtume na kutosahau Qur'an

((سَنُقْرِئُكَ فَلَا تَنسَىٰ ; Tutakusomesha wala hutasahau)). [9]

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anatoa hakikisho kwa Mtume kwamba asiwe na wasiwasi huu ya kwamba, atasahau Aya za Qur'an, bali yule yule aliyemteua yeye na kumfanya Mtume atamfundisha na wala hasahau kile alichofundishwa. Kwa maana kwamba, Mwenye Mungu atamlinda katika hilo na kumfanya asisahau. [10] Allama Tabatabai, ameandika katika tafsiri ya al-Mizan kwamba: "Iqra" inamaanisha kupokea kisomo cha Qarii kwa ajili ya kusahihisha kisomo chake; hata hivyo hii ni maana ya kilugha na ya kiada ya neno na katika Aya hii maana yake ni kwamba, Mwenyezi Mungu amempa Mtume uwezo huo wa kuisoma Qur'an kwa usahihi na vizuri kama ilivyoteremshwa na bila kuacha au kufanya upotoshaji. [11]

Sala ya Idi na Zakat al-Fitr

Imekuja katika tafsiri ya Maj'maa al-Bayan kwamba: Baadhi ya wamesema kuwa, makusudio ya kutakasa na Sala katika Aya za 14 na 15 ni Zakat al-Fitr na Sala ya Idi, lakini yumkini mtu akatia ishkali kwamba, sura hii ni Makki (imeshuka Makka) na katika zama hizo hakukuwa na Zaka wala Sala ya Idi. Katika kujibu hilo imeelezwa kwamba, yuumkini Aya za mwanzo za sura hii zikawa zimeshuka Makka na Aya za mwisho zikiwemo Aya za 14 na 15 zikawa zimeshuka Madina. [12]

Sayyid Hashim Bahrani ameandika katika kitabu chake cha Tafsir al-Burhan chini ya Aya ya 14 ya Surat al-A'la kwamba, imenukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ya kwamba: Swaumu inakamilika kwa kutolewa Zakat al-Fitr, kama ambavyo Sala inakamilika kwa kumsalia Mtume (s.a.w.w). Hivyo basi kila ambaye atafunga Saumu lakini akaacha kwa makusudi kutoa Zakat al-Fitr basi funga siyo yake na mwenye kuswali akaacha kumswalia Mtume (s.a.w.w) basi Sala si yake. Kwani Mwenyezi Mungu ameitanguliza Zakat al-Fitr kwa Sala pale aliposema: "Hakika amekwisha fanikiwa aliye jitakasa. Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akasali". [13]

Idadi ya Manabii na vitabu vya mbinguni

Aya za mwishoni mwa Surat al-A'la zinaonyesha kuwa, watukufu Nabii Ibrahim na Mussa (a.s) nao walikuwa na vitabu vya mbinguni (walivyoteremshiwa na Mwenyezi Mungu). Kumenukuuliwa hadithi kutoka kwa Abu Dharr ya kwamba amesema: Siku moja nilimuuliza Mtume, hivi Manabii wa Mwenyezi Mungu ni wangap? Akasema: 124,000. … Kisha Mtume akasema: Ewe Abu Dharr Manabii Wanne walikuwa Waarabu: Hud, Swaleh, Shuaib na Mtume wako. Nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu alishusha vitabu vingapi? Akasema: 104. Vitabu 10 alishushiwa Nabii Adam, Nabii Shuaib alishushiwa vitabu 50, Akhnoukh ambaye ni Nabii Idris alishusshiwa vitabu 30 na yeye alikuwa mtu wa kwanza kuandika kwa kalamu, Ibrahim alishushiwa vitabuu 10 na Torati ilishushwa kwa Nabii Mussa, Injili kwa Nabii Issa, Zaburi kwa Nabii Daud na Furqan (Qur'an) ilishushwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). [14]

Aya mashuhuri

  • ((إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ وَمَا يَخْفَىٰ ; Hakika Yeye anayajua yaliyo dhaahiri na yaliyo fichikana)) (Aya ya 7)

Imekuja katika tafsiri ya Aya hii kwamba, mambo ya dhahiri na yaliyo jificha hayana tofauti kwa Mwenyezi Mungu, kwa maana kwamba, ni kitu kimoja, kwani kila kilichoko, kiwe kinaonekana dhahir shahir au kimefichikana kimeumbwa na Yeye. [16] Mulla Sadra ameandika: Aya hii inatahibitisha elimu ya Mwenyezi Mungu na inamuweka mbali Muumba na ujahili na mapungufu. [17]

Fadhila na sifa maalumu

Makala asili: Fadhila za sura

Kuhusiana na fadhila za kusoma sura hii, imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ya kwamba: Mwenye kuisoma sura hii Mwenyezi Mungu atampa thawabu za mema kumi kwa kila herufi iliyoshushwa kwa Mtume Ibrahim, Mussa na Muhammad (s.a.w.w). Imenukuliwa hadithi pia kutoka kwa Amirul-Muumina (a.s) kwamba, Mtume alikuwa akiipenda sana sura hii. [18] Kadhalika imenukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) kwamba: Mwenye kusoma Surat al-A'la katika faradhi (Sala za wajibu) au katika Sala za Nafila (Sunna), siku ya Kiyama ataambiwa, kwa matakwa ya Allah ingia peponi kupitia mlango wowote kati ya mipango ya peponi. [19]

Vyanzo

  • Baḥrānī, Sayyid Hāshim b. Sulaymān. Al-Burhān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Bunyād-i Biʿthat, 1416 AH.
  • Faḍl Allāh, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Min waḥy al-Qurʾān. Second edition. Beirut: Dār al-Milāk li-l-Ṭibāʿa wa l-Nashr, 1419 AH.
  • Khurramshāhī, Bahāʾ al-Dīn. Dānishnāma-yi Qurʾān wa Qurʾān pazhūhī. Tehran: Dūstān-Nāhīd, 1377 Sh.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Barguzīda-yi tafsīr-i nimūna. Edited by Aḥmad ʿAlī Bābāyī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1382 Sh.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1366 Sh.
  • Maʿrifat, Muḥammad Hādī. Āmūzish-i ʿulūm-i Qurʾān. [n.p]: Markaz Chāp wa Nashr-i Sāzmān-i Tablīghāt, 1371 Sh.
  • Mullā Ṣadrā, Muḥammad b. Ibrāhīm. Tafsīr al-Qurʾān. Edited by Muḥammad Khājūy. Second edition. Qom: Intishārāt-i Bīdār, 1366 Sh.
  • Ṭabāṭabāyī, Mūhammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Second edition. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1974.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Hāshim Rasūlī & Yazdī Ṭabāṭabāyī. Third edition. Tehran: Intishārāt-i Nāṣir Khusru, 1372 Sh.