Nenda kwa yaliyomo

Sayyid Tijani al-Samawi

Kutoka wikishia
Sayyid Muhammad al-Tijani al-Samawi

Sayyid Muhammad al-Tijani al-Samawi (Kiarabu: السيد محمد التيجاني السماوي) (alizaliwa 1936) msomi na alimu wa Tunisia ambaye aliachana na madhehebu ya Kisuni na kuingia katika madhehebu ya Shia. Awali Tijani alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Maliki. Baada ya kufanya safari nchini Saudi Arabia, alichukua muelekeo wa Uwahabi na akajishughulisha na kueneza imani za Kiwahabi; lakini baada ya safari ya kwenda Najaf na mazungumzo na wanazuoni wa Kishia, aliachana na Uwahabi na kushikamana na madhehebu ya Ahlul-Bayt (Ushia).

Baada ya Tijani Samawi kuwa Mshia, aliandika vitabu kadhaa akitetea madhehebu ya Shia. Miongoni mwa vitabu hivyo ni: "Kisha nikaongoka" ((ثُمَّ اهْتَدَیتُ)) ambapo ndani yake anaelezea mkasa na simulizi yake ya kuwa Shia pamoja na vikao vyake na Maulamaa wa Kishia. Kuwa Shia Tijani Samawi kulikabiliwa na radiamali hasi kutoka kwa Mawahabi. Baadhi yao walitaja athari za Sayyid Tijani Samawi kuwa ni bandia na kwamba, Tijani Samawi ameritadi.

Tijani Samawi anasema, vitabu vya al-Murajaat na al-Nass wal-Ijtihad vya Sharafuddin na vilevile kukutana kwake na Sayyid Muhammad Baqir Sadr, mmoja wa Marajii wa Kishia, ni mambo yaliyokuwa na taathira zaidi ya kufikia uamuzi wa kuachana na Uwahabi na kuingia katika madhehebu ya Shia.

Mazazi na masomo

Muhammad Tijani Samawi alizaliwa mwaka 1936 katika mji wa Gafsa kusini mwa Tunisia. [1] Kwa mujibu wa Tijani Samawi, familia yake asili yake ni Samawah Iraq ambayo ilihajiri na kuelekea kaskazini mwa Afrika katika zama za utawala wa Bani Abbas. [2]

Alikamilisha masomo yake ya awali ya miaka miwili au mitatu katika Chuo Kikuu cha Ez-Zetouna, Tunisia. Baada ya Tunisia kupata uhuru alijiunga na shule za Franco-Arab (Kifaransa-Kiarabu) kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baadaye alianza kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kudumu katika kazi hiyo kwa takribani miaka 17. [3]

Tijani alikwenda Ufaransa kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na alikaa huko kwa zaidi ya miaka minane katika Chuo Kikuu cha Sorbonne na Taasisi ya Elimu ya Juu ya Paris, akifanya utafiti linganishi wa dini, hasa dini za Tawhidi (Mungu mmoja), na kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Sorbonne na shahada ya kwanza ya elimu ya juu ya utafiti katika uwanja huu. Kisha baadaye alikata shauri kusoma taaluma ya falsafa na ubinadamu (philosophy and humanities). Baadaye akasoma taaluma ya historia na madhehebu za Kiislamu katika Chuo Kikuu hicho na kupata shahada ya PhD. Maudhui la tasnifu yake ya udaktari lilikuwa ni fikra za Kiislamu katika Nahj al-Balagha. Alitafsiri Nahj al-Balagha kwa Kifaransa. Baada ya kupata shahada ya udaktari, alifundisha kwa mwaka mmoja katika Chuo Kikuu cha Sorbonne na miaka mitatu katika Taasisi ya Balzac huko Paris. [4]

Akiwa mtoto, Tijani alihifadhi nusu ya Qur’an. Kwa hiyo, alikuwa akishiriki katika Sala ya Tarawehe akiwa Imamu katika mwezi wa Ramadhani. [5] Kulingana naye, jina la Tijani linatokana na kundi la Tariqa la Tijani, ambalo limeenea katika nchi ya Tunisia, Morocco, Algeria, Libya, Sudan. Misri, nk. Kundi hilo linaamini kwamba masheikh na mawalii wote wa Mwenyezi Mungu walipeana elimu wao kwa wao, isipokuwa Sheikh Ahmad Tijani ambaye alipata elimu yake moja kwa moja kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). [6]

Kuchagua madhehebu ya Shia

Tijan alipo onana na kiongozi na Marjii wa Kishia, Sayyid Muhammad Baqir Sadr

Tijani alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Maliki. [7] Mnamo mwaka wa 1964, alishiriki kongamano huko Makka kuhusiana na Waarabu Waislamu, na katika safari hii, kifikra na kiitikadi alielekea upande wa imani ya Uwahabi, na baada ya hapo alijishughulisha na kueneza imani zao. [8]

Katika safari yake ya Beirut, Lebanon, Tijani alikutana na mmoja wa maprofesa wa Kishia wa Chuo Kikuu cha Baghdad, aliyeitwa Mun’im na katika mazungumzo naye, aliwashutumu Mashia kwa ukafiri na ushirikina. Lakini Mun’im alimwalika Iraq ili akaujue Ushia.[9] Tijani alikubali mwaliko wa Mun’im na katika safari yake ya kwenda Iraq, alizuru Haram ya Imamu Ali (a.s), haramu ya Kadhimein na kaburi la Sheikh Abdul Qadir Gilani, kama ambavyo alikutana pia na baadhi ya wanazuoni wa Kishia. [11] Kukutana kwake na Ayatullah Khui na Sayyid Muhammad Baqir miongoni mwa Marajii wa Kishia ilikuwa sababu ya yeye kurekebisha baadhi ya itikadi zake kuhusiana na Mashia. [11]

Amezungumzia kuhusu athari za wanazuoni wa Kishia, hasa Seyyid Muhammad Baqir Sadr, juu yake, na katika kitabu chake “Kisha nikaongoka” kama ambavyo ameripoti maswali yaliyoulizwa na majibu ya Ayatullah Sadr.[12]

Baada ya mikutano hiyo, alianza kufanya utafiti ili kupata ukweli. Kuhusiana na hilo, yeye mwenyewe anasema: “Nilifunga mapatano na nafsi yangu, kuchukua na kuzifanya hoja na nyaraka zisizo na shaka hadithi sahihi zinazokubaliwa na Mashia na Sunni, na kuziacha kando hadithi zinazoaminiwa na madhehebu moja tu. [13] Tijani alijipinda kusoma na kufanya utafiti kuhusiana na itikadi za Shia na imani zao. Vitabu muhimu vilivyomshawishi na kumuathiri katika suala hili vilikuwa ni vitabu vya al-Murajaat na al-Nass Wal-Ijtihad vilivyoandikwa na Seyyid Abdul-Hussein Sharafuddin.[14]

Vitabu vyake

Baada ya kuwa Shia, Tijani aliandika vitabu vinavyothibitisha usahihi wa mashehebu ya Shia na kwamba Mashia wako katika haki na kupinga maoni ya Masunni. Baadhi ya hivyo ni: "Kisha nikaongoka" (ثُمَّ اهْتَدَیتُ), Ahl al-Bayt ni Ufunguo wa Matatizo, Ili Niwe Pamoja na Wakweli, Waulize Wanaofahamu, Njia ya Kuokoka, na Safari na kumbukumbu. [15]

Katika kitabu chake cha “Kisha Nikaongoza” amesimulia jinsi alivyobadilisha madhehebu yake na kuwa Shia. Katika kitabu hiki sambamba na kuelezea historia ya maisha yake, mikasa na safari yake huko Iraq, amezungumzia pia mazungumzo yake na wanazuoni na Maulamaa wa Kishia. Katika kitabu hiki, Tijani Samawi anatumia hadithi za Ahlu-Sunna kutetea madhehebu ya Shia. Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha 14 ikiwemo lugha ya Kiswahili na kina anuani: “Kisha Nikaongoka”. Miongoni mwa lugha ambazo kitabu hiki kimetarjumiwa ni Kifarsi pia na kimechapishwa mara kadhaa nchini Iran.

Kitabu cha dondoo za fikra, ni muktasari wa vitabu sita vya Sayyid Tijani al-Samawi ambapo kazi hii imefanywa na Hussein Ghaffari Saravi. [16]

Radiamali

Katika mahojiano, Tijani alisema baada ya kujiunga na madhehebu ya Shia, alikabiliwa na jibu kali na hasi la Mawahabi na Wasaudi. Kulingana naye, awali walikanusha kuwepo kwa mtu aitwaye Tijani ambaye amekuwa Shia. Kisha wakadai kwamba, kitabu cha Thumma Ihtadaitu (Kisha Nikaongoka) ni kazi ya Israel. Baadhi yao pia walisema kwamba yeye si Shia wala Sunni; bali ameritadi. [17]