Samaki mwenye magamba

Kutoka wikishia
Samaki mwenye magamba

Samaki Wenye Magamba (Kiarabu: الأسماك ذوات الفلس) ni samaki ambawo ni halali kuliwa. Katika fikihi ya Kishia, samaki kuwa na magamba ni kigezo cha kuwa kwake halali. Baadhi ya wanazuoni wa fikihi wanaitambua hukumu hii kuwa ni mahususi na maalumu kwa Waislamu wa Shia Imamiyyah. Katika hadithi na riwaya za Kiislamu kumeashiriwa samaki halali na haramu kuliwa kwa msingi wa hukumu hii.

Mafakihi wanasema kuwa, ni batili na haramu kuuza na kununua samaki wasio na magamba kwa ajili ya kula. Kwa mujibu wa fat’wa yao, kama sehemu ya mwili wa samaki ndio itakayokuwa na magamba hilo linatosha kumfanya samaki huyo kuwa halali kuliwa. Kuna hitilafu za kimitazamo baina ya wanazuoni kuhusiana na samaki wenye magamba madogo ambayo hayawezi kuonekana na macho ya kawaida (isipokuwa kwa kutumia chombo kama darubini).

Utambulisho

Samaki mwenye magamba ni samaki ambaye ana magamba nje ya mwili. [1] Katika fikihi ya Kiislamu, samaki ambao wana magamba maudhui yao imekuja katika milango ya kuwinda, kuchinja, vyakula na vinywaji. [2] Samaki kuwa na magamba ni kigezo cha kuwa kwake halali. [3] Katika vyanzo vya riwaya vya Kishia kuna hadithi zilizokusanywa kuhusiana na hukumu ya samaki wenye magamba. [4].

Hukumu ya Kifiqhi

Wanazuoni na mafakihi wa Shia Imamiyyah wanasema kuwa, ni halali kula samaki mwenye magamba na kwamba, samaki asiye na magamba ni haramu kumla. [5] Makusudio ya samaki asiye na magamba ni samaki ambaye kiasili hana magamba. [6] Kwa msingi huo, samaki ambao wana magamba au ambao magamba yao yameondoka hawajumuishi na hukumu hii. [7]

Kuhusiana na sababu ya kuharamishwa kula samaki wasio na magamba imeelekezwa kuwa, kimsingi ni walaji wala mizoga na nyama zao zimechafuliwa kutokana na kuwa hawana magamba. [8]

Hukumu ya Mayai ya Samaki

Kwa mujibu wa fat’wa na wanazuoni na mafakihi waliowengi, hukumu ya kula mayai ya samaki (roe) inafuata hukumu ya samaki mwenyewe. Kwa msingi huo kama samaki fulani atakuwa ni halali kuliwa basi mayai yake pia yatakuwa halali kuliwa. [9] Baadhi wamekuja na ufumbuzi mwengine; ambapo,miongoni mwake ni kuwa, kama mayai ya samaki yatakuwa magumu ni halali kuyala na kama yatakuwa malaini basi ni haramu kuyala. [10] Hata hivyo baadhi wamesema kuwa, ufumbuzi huu ni pale ambapo nyama ya samaki husika haifahamiki kuwa ni halali au ni haramu. [11]

Uhalali wa Samaki Mwenye Magamba ni Hukumu Mahususi ya Mashia

Baadhi ya mafakihi wa Kishia kama Sheikh Tusi na Sayyid Murtadha, wametambua kwamba, kuwa halali samaki mwenye magamba na kuwa haramu wanyama wengine wa baharini ni miongoni mwa hukumu maalumu na mahususi kwa Waislamu wa Shia Imamiyyah. [12] Baadhi ya wengine wameashiria kuwa mutawatir (upokewa kwa wingi) hadithi zinazohusiana na maudhui hii [13] na hilo kuwa mashuhuri baina ya masahaba, [14] na kudai kwamba, hilo ni jambo ambalo wanazuoni wamefikia kauli moja (ijmaa), [15] na kulitambua hilo kama moja ya sifa maalumu za madhehebu ya Shia Imamiya. [16]

Mafakihi wasio wa Shia Imamiya hawatambui kama uhalali wa samaki ni mahususi kwa samaki mwenye magamba. Abu Hanifa mtazamo wake ni kuwa, samaki wote ni halali. Kadhalika Imamu Shafi’i na Malik bin Anas wao wamesema kuwa, wanyama wote wa baharini ni halali kuliwa. [17] Kwa msingi huo, kundi fulani la mafakihi, linasema kwamba, kuwa halali samaki mwenye magamba ni maafikiano (ijmaa) ya Waislamu na kuharamishwa kula samaki asiye na magamba na wanyama wa baharini ambao hawahesabiwi kuwa ni samaki ni maafikiano (ijmaa) ya Waislamu wa Shia Imamiya. [18]

Vigezo vya Kiriwaya

Baadhi ya mafakihi kwa kuzingatia hadithi na riwaya mbalimbali, wameashiria baadhi ya majina ya samaki ambao ni halali na ambao ni haramu kuliwa [19] na kukusanya hukumu za Maulamaa kuhusiaba na hili. [20]

Kobe, chura na kaa ni miongoni mwa wanyama wa baharini ambao kutokana na kutokuwa kwao ni samaki na kutokuwa na magamba katika hadithi wametajwa kuwa ni haramu kuliwa. [21] Samoni (samaki mkubwa mwenye nyama nyekundu), samaki wadogo wenye magamba laini, panzi wa buluu au uduvi na kamba ni miongoni mwa aina ya samaki ambao wametambuliwa kuwa ni halali kuwala. [22]

Mafakihi kama Sheikh Tusi, [23] Muhaqqiq Hilli [24] na Kaidari mwandishi wa kitabu cha Isbah al-Shiah [25] wakitegemea hadithi, wameona kuwa ni makuruhu (haipendezi) kula nyama ya baadhi ya wanyama wa baharini kama mkunga ambaye ni samaki mwenye umbo la nyoka (anguilloidei) ingawa kuna wengine wanaona kuwa ni haramu kuliwa kutokanma na kuwa hahesabiwi kuwa ni samaki au kutokana na kuwa hawamtambui kuwa ana magamba. [26] Kundi hili la wanazuoni limezijaalia kuwa ni katika taqiyyah hadithi ambazo zinaashiria kuwa makuruhu. [27] Aidha kuna hitilafu pia baina ya wanazuoni kuhusiana na vigezo vya baadhi ya samaki walioashiriwa katika riwaya. [28]

Kiwango na Kigezo cha Magamba

Kwa mujibu fat’wa ya baadhi ya Mamujitahidi, hakuna ulazima mwili wa samaki uwe na magamba sehemu zote bali inatosha tu samaki awe na magamba katika baadhi ya sehemu ya mwili wake na hivyo kuwa halali. [29] Kuainisha kwamba, mwili wa samaki una magamba au la ni jambo linalorejea kwa mtu mwenyewe [30] au watu wenye ujuzi na ubobezi katika mambo ya samaki ambao wanaweza kubainisha kwamba, samaki huyu ana magamba au hana. [31]

Baadhi wanaamini kwamba, kama mtu ataingiwa na shaka kwamba, samaki huyu ana magamba au la, anapaswa kujaalia kwamba, hana na hivyo ni haramu kumla; [32] isipokuwa kama samaki huyo atakuwa anauzwa katika soko la Waislamu [33] au atokee mtu muadilifu na kutoa ushahidi kwamba, samaki huyu ana magamba. [34] Kwa msingi huo, kama mtu ataingiwa na shaka na samaki wanaouzwa katika soko lisilo la Waislamu, anapaswa kujipeusha kula samaki hao. [35]

Kuna hitilafu za kimitazamo baina ya wanazuoni kuhusiana na samaki wenye magamba madogo ambayo hayawezi kuonekana na macho ya kawaida (isipokuwa kwa kutumia darubini). Kwa kuzingatia hayo samaki kama beluga, [36] papa [37] na samaki mwenye mayai (roe) [38] ni miongoni mwa samaki ambao mafakihi wameulizwa kuhusiana na uhalali wao.

Baadhi ya Marajii wanaamini kuwa, magamba ya samaki yanapaswa kuonekana kwa jicho pasi na kutumia chombo (kama darubini na kadhalika) na katika ada na mazoea ya jamii yawe yanafahamika kuwa ni magamba. [39] Ayatullah Tabrizi anaamini kuwa, haijatbithi kuwa na magamba samaki wa caviar ( samaki mwenye mayai). [40] Baadhi ya marajii wengine kama Ayatullah Bahjat anaamini kuwa, inatosheleza pia kuona magamba kwa kutumia darubini. [41] Ayatullah Makarim Shirazi katika kujibu swali aliloulizwa kuhusiana na uhalali wa papa amesema kuwa, mtazamo wa ada na mazoea [42] au usadikishaji wa wenye ujuzi na utaalamu katika hilo [43] ni jambo linalotosheleza kuwa halali samaki.

Kuna kundi la wahakiki ambalo linaamini kwamba, kuruhusiwa kula samaki (kuwa halali) ni samaki kuwa na magamba iwe magamba hayo yanaokana kwa jicho la kawaida au kwa kutumia chombo na wenzo kama darubini na kadhalika. [44]