Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Tariku al-Salah

Kutoka wikishia

Tariku al-Salah (Kiarabu: تارك الصلاة) ni istilahi ya kitaalamu inayotokana na neno la Kiarabu linalomaanisha mwacha sala. Istilahi hii hutumika kumrejelea yule Muislamu anayeghafilika na utekelezaji wa ibada ya sala kwa makusudi. Katika mafundisho ya Uislamu, sala inachukuliwa kuwa ni nguzo ya pili na muhimu zaidi baada ya kutamka shahada mbili (ushahidi wa upweke wa Mwenye Ezi Mungu pamoja na kukiri utume Mtume Muhammad) (s.a.w.w). Hivyo basi, kwa mujibu wa vielelezo vya sheria za Kiislamu, tendo hili huhisabiwa kama ni moja ya madhambi makubwa , na kwa mujibu vyanzo hivyo, endapo kitendo cha kuacha sala kitaambatanishwa na kukanusha uwajibu wake kisheria, hali hiyo humweka mhusika katika kundi la walioacha dini, yaani wanaoritadi. Aidha, maandiko ya Qur'ani yanabainisha wazi kuwa kosa la kughafilika na sala ni miongoni mwa vikwazo vikuu vinavyoweza kuzuia uwezekano wa kupata shufaa (uombezi) wa Siku ya Kiyama.

Kwa mujibu wa masimulizi yalionukuliwa kutoka kwa bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), kuna athari kadhaa ndani ya maisha binafisi zinazo sababishwa na tendo la kuacha bila ya kuwa na udhuru unaokubalika kisheria (udhr shar'i). Moja ya athari inayoweza kumuathir mwacha sala, ni ile athari ya kutilika kwa matendo yake. Riwaya zinasisitiza kwa; Mwenye Ezi Mungu hubatilisha amali za kila mwenye kuacha aliyeacha kwa makusudi utekelezaji wa sala zake, jambo huondoa thamani ya matendo yake yote ya ibada na hisani alizotekeleza maisahni mwake. Kulingana na Hadith mbali mbali, Shetani hutumia upenyo wa kuachwa wa kuacha sala kama mkakati na msingi mkuu wa kumwongoza mwanadamu katika uasi uliopindukia mipaka. Sala inachukuliwa kuwa ndiyo ngao msingi dhidi ya maovu (tanhaa ani al-fahshaa wa al-munkar). Hivyo basi, kuacha sala huwa ni sawa na kuondoa ngao hiyo, na hivyo kumfanya mhusika kuwa katika hatari kubwa ya kushawishika na vishawishi vinavyopelekea kwenye madhambi makuu (al-kaba'ir), jambo humfanya Mwenye Ezi Mungu kuwa na haki kamili ya kisheria ya kuwaadhibu wale wanaopuuza sala na kuwaweka katika adhabu ya Jahannamu pamoja na kundi la wanafiki (munafiqun). Kutajwa kwao na kuwekwa sambamba na makafiri ni moja ya dilili kuu zinazoashiria uzito na kuwa wa kosa lao la kuacha sala.

Katika historia ya fiqh ya Kiislamu, dhana ya ijmaa (makubaliano ya wanazuoni) huchukua nafasi ya nne katika vyanzo vya sheria za madhehebu ya Shia (baada ya Qur'ani, Sunna, Akili. Kuna maelezo yasemayo kwamba; ndani ya muktadha wa sheria za kifiqhi za madhehebu ya Shia, kuna makubaliano kamili (ijmaa) ya kwamba tendo la kukanusha sala, ni moja ya matendo yanayomtoa mtu katika Uislamu (yanamuingiza mtu uritadi). Hii inatokana na ukweli wa kwamba, sala ni nguzo ya pili ya Uislamu, na wajibu wake umeelezwa bayana ndani ya Qur'ani na Sunna. Pamoja na hayo, sheria za Kiislamu zinatofautisha kati ya mkanushaji sala mwenye welewa kamili juu ya wajibu wa amali hiyo, na yule anayekanusha kunakotokana na shaka ya kielimu (shubhah) husiana na amali hiyo. Iwapo mtu atatoa hoja za kimantiki kwamba kutotimiza wajibu wa sala kulitokana na shubhah (shaka fulani), kama ilivyo kwa aliyeingia katika Uislamu karibuni, hapo hapatokuwa na mwenye haki ya kumhukumu kwa hukumu ya kumtoa katika umma wa Kiislamu.

Miongoni mwa wanazuoni mbali mbali, kuna kundi maalumu la wanazuoni wanaoshikilia msimamo usemao kwamba; Iwapo mtu ataacha kutekeleza wajibu wa sala kwa sababu tu ya uvivu au kupuuzaji katika utekelezaji wa wajibu wake, huku akiwa bado anakubali na kuamini moyoni mwake kwamba sala ni moja ya amali za lazima kisheria, mtu huyo huingia kwenye kunda na mafasiq (watenda dhambi au mhalifu wa sheria za kidini). Kwa mujibu wa msimamo huu, yoyote yule atakayekuwa na sifa kama hiyo, huchukuliwa hatua za kumrekebisha kulingana na sherira. Hivyo basi yeyote yule anapopuuza sala bila sababu inayokubalika, hata kama atakuwa anakiri kuwa ni wajibu, huyo hustahili kupewa adhabu inayoitwa ta’azir (adhabu yenye kiwango cha kumpa maonyo). Adhabu hii hutolewa na kiongozi wa Kiislamu kwa lengo la kumfunza na kumrudisha kwenye njia sahihi. Pamoja na adhabu hiyo, pia hutapewa amri rasmi ya kuanza kusali tena bila ya kuchelewa. Na ikiwa mtu huyo ataendelea na ukaidi wake, na akaendelea kupuuza sala zinazofuata, na kuiacha hadi kupitia na muda wake (na kugeuka kwa sala ya kulipwa, yaani qadhaa), hapo mtu huyo itabidi kumpa adhabu ya ta’azir (adhabu yenye kiwango cha kumpa maonyo) kwa mara nyengine tena.

Lawama na Makaripio Dhidi ya Kuacha Sala

Katika mfumo wa sheria za Kiislamu, unaojulikana kama Fiqhi, kitendo cha kuacha Sala kwa makusudi (tarku al-ṣalāh) kinaorodheshwa miongoni mwa madhambi makuu (al-kabā'ir).[1] Maandiko ya kidini, hususan yale nayohusiana na Hadithi za Maimamu pamoja na bwana Muhammad (s.a.w.w), yanakwenda mbali zaidi kwa kuwahusisha wale wanaoacha Sala na sifa ya ukafiri.[2] Falsafa ya msingi inayochukuliwa kuhusu kuacha Sala kimakusudi ni kuwa, kitendo hicho ni dhihirisho la kuidharau na kuipuunza (istikhfāf) ibada hiyo msingi. Uchambuzi wa kina wa kauli za Imam Sadiq (a.s) unaonyesha kuwa adhabu ya tendo hili inazidi ile ya madhambi mengine makuu, kama vile unywaji wa pombe. Kwa kuzingatia msingi huu, mwanazuoni wa sheria za Kiislamu wa karne ya kumi na moja Hijria, Hurr al-Amili, anahitimisha uchambuzi wake juu ya kitendo hichi akisema kuwa; kuacha Sala ni kigezo muhimu kinachoweza kutumika katika kumtofautisha Muislamu na asiyekuwa Muislamu, na kwa maelezo yake, mwacha sala ni sawa na kafiri aliyeko nje ya dini.[3]

Ayatollah Nasir Makarim Shirazi, mmoja wa wanazuoni wa Fikhi (Marja' al-taqlid) wa Kishia, anawasilisha hoja yake katika kutofautisha kati ya anayeacha Swala kabisa kabisa (tārik al-ṣalāh), na yule anayeizembea (sāhūn). Kwa mujibu mtazamo wake, hadhi ya tārik al-ṣalāh ni duni zaidi na ni yenye kukabiliwa kubwa zaidi ikilinganishwa na ya yule anayezembea. Hoja yake inajengwa juu ya tafsiri ya Qur'ani, ambayo inatumia istilahi ya "Wayl" kuwaonya wale wanaoswali huku wakiwa wazembe na wasiojali Sala zao. Istilahi ya "Wayl" inabeba maana ya mporomoko, hasara isiyopimika, na kutengwa na rehema ya Kiungu.[4] Shirazi anahitimisha kimantiki kwamba, ikiwa kundi la wazembe (sāhūn) linastahiki onyo kali la kiwango hiki, basi ni dhahiri kuwa kundi la wale wanaoacha Sala kikamilifu (tārik al-ṣalāh), liko katika hali mbaya zaidi na linakabiliwa na athari mbaya zaidi za kiroho na kisheria.[5]

Mapokezi yanayonukuu Hatidhi za bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), yamenukuu Hadithi isemayo kwamba; Kuacha Sala kimakusudi na bila udhuru wa kisheria (udhr shar’i) husababisha kubatilishwa kwa amali za mja. Hii inatafsiriwa kwa maana ya upotevu wa thawabu za matendo mengine yote.[6] Aidha, katika moja ya Riwaya imeelezwa kwamba; Kuacha Sala ni sawa na kumfungulia mlango Shetani, mlango ambao huutumia kwa ajili ya kumwingiza mhusika wake katika bonde la dhambi kuu (kabā'ir).[7] Kulingana na mtazamo wa kisheria, Mwenye Ezi Mungu ana mamlaka kamili juu ya kuwahukumu wanaoacha Sala (tārik al-ṣalāh) na kuwapa adhabu ya moto huku pamoja na kundi la wanafiki (munāfiqūn).[8] Imamu al-Baqir (a.s) anaimarisha uzito wa suala hili kwa kunukuu maneno ya mwisho ya bwana Mtume (s.a.w.w) aliyotoa wakati wa kukaribia kifo chake, akisema: Yeyote anayeidunisha Sala (istikhfāf bi al-ṣalāh) si sehemu ya umma wangu. Kauli ambayo inaweka msisitizo mkubwa juu ya hadhi ya Sala kama kigezo halisi cha Muislamu wa kweli.[9]

Uchambuzi wa Kifiqhi Kuhusu Kategoria za Kuacha Sala

Imeelezewa kwamba; kuna maafikiano ya kifiqhi (ijma') miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu ya kwamba, endapo mtu fulani atakanusha msingi (aṣl) wa Sala na kupinga hukumu yake ya uwajibu (wujūb), huyo atakuwa amepoteza moja kwa moja hadhi yake ya Uislamu,[10] atahisabiwa kuwa ni kafiri na mritadi.[11] Hukumu hii haiwezi kumuingiza yule aliyacha sala kwa msingi wa ya kuwa na shaka (shubha) juu ya msingi huo, kama vile mtu kuwa ni mgeni katika Uislamu (jadīd al-islām) na hivyo kutokuwa na ufahamu kamili kuhusiana na sheria za Kiisalmu.[12] Hata hivyo, iwapo mtu atakiri uwajibu wa Sala kisha akaiacha bila udhuru halali, huyo atastahiki adhabu fulani inayoamuliwa na kiongozi wa Kiislamu ijulikanayo kwa jina la (ta'azīr), jambo ambalo litamsukuma na kumlazimisha ashikanane na Sala zake. Endapo mtu huyo atarudia kosa lake na akaacha Sala zake nyingine kumpita, itabidi kumkabili tena kwa adhabu ya ta'azīr.[13] Kategoria nyengine ya tatu ya mwenye kuacha Sala, inahusiana na yule anayeacha Sala kwa sababu ya uvivu (kasal), bila kukanusha uwajibu wake. Mtu mwenye sifa kama hiyo hukumiwa kwa hukumu ya ufasiki (fisq), yaani huhisabiwa kuwa ni miongoni mwa watenda dhambi, na anayevunja sheria za Mungu kwa uwazi bila ya woga.[14]

Ukafiri wa Mwenye Kuacha Sala

Kwa mujibu wa baadhi ya Riwaya, kitendo cha kuacha sala kinaonekana kuhusishwa moja kwa moja na hali ya ukafiri. Bwana Mtume (s.a.w.w) ananukuliwa katika mapokezi akimweka mwacha Sala kwa makusudi katika kundi la makafiri.[15] Kwa kutegemea msingi huu wa kimapokezi, Imamu Kadhim (a.s), katika muktadha wa kuorodhesha madhambi makuu (al-Kaba'ir), ameonekana kujumuisha kosa la kuacha Sala kwa kukusudia ndani ya orodha hiyo, huku akihisabu kila ukiukaji wa wajibu wa Mwenye Ezi Mungu kama ni sehemu ya orodha hiyo.[16] {Maelezo | وَ تَرْكُ الصَّلَاةِ مُتَعَمِّداً أَوْ شَيْئاً مِمَّا فَرَضَ اللهُ لِأَنَّ رَسُولَ اللهِ ص قَالَ مَنْ تَرَكَ الصَّلَاةَ مُتَعَمِّداً فَقَدْ بَرِئَ مِنْ ذِمَّةِ اللهِ وَ ذِمَّةِ رَسُولِ اللهِ} Mtume (s.a.w.w) amenukuliwa akisisitiza kwamba; Sala ndiyo kigezo msingi kinachotofautisha baina ya utumishi kwa Mwenye Ezi Mungu (ubudiyyah) na ukafiri (kufr).[17] Hivyo, kuacha Sala kunaonekana si tu kama dhambi, bali kama ni hatua ya kuvuka mipaka ya imani na kuingia katika hali ya ukafiri. Mtazamo huu unaimarishwa zaidi na kauli inayohusishwa na Imamu Sadiq (a.s), ambaye pia anamfafanua anayeacha sala kama kafiri, jambo linaloipa dhana hii uzito wa kipekee katika sheria za Kiislamu.[18]

Kwa mujibu wa ufafanuzi wa mwanahadithi wa Kishia wa karne ya kumi na moja Hijria, Muhammad Baqir Majlisi, dhana ya imani ina vipimo viwili: itikadi ya ndani (i'tiqad al-qalb) na uthibitisho wa kimatendo (al-'amal). Akiendelea na ufafanuzi wake huu anaeleza ya kwamba; imani haiwezi kuwa ya moyoni pekee; bali ni lazima iandamane na utekelezaji wa wajibu za kisheria (wajibat), pamoja na kujiepusha na yaliyoharamishwa (muharramat). Kutokana na msingi huu wa kitheolojia, Majlisi anahitimisha ya kwamba; hilo ndilo lililopelekea baadhi ya riwaya kumtaja mtu anayeacha Sala kimakusudi (Tarik as-Salat) kwa sifa ya ukafiri.[19] Hii ni kwa sababu kitendo cha kuacha nguzo muhimu kama Sala kinachukuliwa kuwa ni ushahidi dhahiri wa mapungufu katika uthibitisho wa kimatendo wa imani. Pia katika muktadha wa sheria za Kiislamu (fiqh), Allamah al-Hilli, ambaye ni mwanafiqhi mashuhuri wa Kishia wa karne ya saba na nane Hijria, anadai kuwepo kwa ijmai (makubaliano ya wanazuoni) juu ya hukumu ya kuritadi (uasi wa imani) kwa watu wa aina hii. Kulingana na dai lake hilo, hukumu ya wenye kuacha Sala huwa ni adhabu ya kifo (qatl).[20]

Kuna tofauti za kimtazamo miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu kuhusiana na hadhi ya mtu anayeamini kuwa Sala ni wajibu kisha akaiacha kwa makusudi.[21] Baadhi ya wanazuoni wametoa mapendekezo ya adhabu za hatua kwa hatua. Kwa mujibu wa mtazamo huu, mtu anayeacha Sala kwa mara ya kwanza anapaswa kupewa adhabu ya ta’azir inayotolewa na kiongozi wa kiislamu. Ikiwa ataendelea na kosa hili na kulirudia kwa mara ya tatu au ya nne,[22] baadhi yao wametoa hukumu ya kifo.[23] Hata hivyo, kuna mitazamo ya kisasa inayotofautiana na msimamo huu. Kwa mfano, Sayyid Ali Sistani, mmoja wa viongozi wakuu wa kidini wa Kishia, anaamini kwamba kitendo cha kuacha Sala peke yake hakitoshi kumfanya mtu kuwa kafiri na kutoka nje ya Uislamu, ingawa anasisitiza kwamba; kitendo hicho ni miongoni mwa madhambi makubwa.[24] Vilevile, Mirza Jawad Tabrizi, mwanazuoni mwingine mashuhuri wa Kishia, ametoa ufafanuzi kuhusu hadhi ya usafi wa mtu huyo, akisema kwamba mtu anayeacha Sala hachukuliwi kuwa ni najisi, na hivyo Waislamu wengine wanaweza kuendelea kushirikiana naye katika masuala ya kijamii.[25]

Uzito wa Dhambi ya Kuacha Sala Ikilinganishwa na Dhambi Nyingine

Kwa mujibu wa riwaya mbili zilizopokewa katika kitabu cha Al-Kafi na Irshad al-Qulub; dhambi ya kuacha Sala inamehisabiwa kuwa na uzito mkubwa zaidi hata kupindukia dhambi za kuchoma Msahafu na kufanya kosa zina (uzinifu). Riwaya hizi zinamweka mwacha sala katika kategoria ya ukafiri wa kumkana Mwenye Ezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w).[26] Ufafanuzi wa kitheolojia na kifiqhi kuhusu mantiki ya uzito huu umetolewa na wanazuoni mbali mbali akiwemo Sheikh Saduq, katika kitabu chake Ilal al-Shara'i (Sababu za Kuwepo kwa Sheria), pamoja na mwandishi wa kitabu kiitwacho La'ali al-Akhbar (bwana Muhammadnabi bin Ahmad Tuisikani). Wanazuoni hawa wanaeleza kwamba; chanzo cha uzito wa dhambi hii ni hali ya kisaikolojia na kiroho aliyonayo mtendaji wa dhambi hiyo. Kwani Mtu anayeacha Sala huwa hafanyi hivyo kwa kuongozwa na msukumo wa kihisia (kimatamanio) wa kutafuta ladha fulani inayopatikana ndani ya kitendo hicho cha haramu, bali hufanya hivyo kutokana na dharau (istikhfaf) ya kuidharau ibada yenyewe. Hii ni tofauti na dhambi nyingine ambazo mara nyingi husababishwa na kushindwa kwa mtu mbele ya matamanio ya nafsi (ghalabat al-shahwah) au kutafuta anasa iliyokatazwa kisheria. Kwa hiyo, kuacha Sala kunatafsiriwa si kama kufanya dhambi kutokana na udhaifu wa mja, bali kama uasi wa kimakusudi na dharau mbele ya mamlaka ya Mungu.[27]

Rejea

  1. Tayyib, Atyab al-Bayan, 1999 AH, juz. 14, uk. 168.
  2. Tayyib, Atyab al-Bayan, 1999 AH, juz. 14, uk. 168.
  3. Hurr Amili, Wasail al-Shiah, Beirut, juz. 3, uk. 28.
  4. Taleqani, Partawi az Quran, 1983 AH, juz. 4, uk. 273.
  5. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1995 AH, juz. 27, uk. 361.
  6. Majlisi, Bihar al-Anwar, 1982 AH, juz. 79, uk. 202.
  7. Majlisi, Bihar al-Anwar, 1982 AH, juz. 79, uk. 202.
  8. Sheikh Saduq, Uyun Akhbar al-Ridha, 1958 AH, juz. 2, uk. 31.
  9. Kulayni, al-Kafi, 1986AH, juz. 3, uk. 269.
  10. «حکم تارک الصلاه», Tovuti ya Muflihun.
  11. Sheikh Tusi, al-Khilaf, 1986 AH, juz. 5, uk. 359.
  12. Shahid Awwal, al-Durus, 1996 AH, juz. 1, uk. 144.
  13. Sheikh Tusi, al-Khilaf, 1986 AH, juz. 1, uk. 689.
  14. Sheikh Tusi, al-Khilaf, 1986 AH, juz. 5, uk. 359.
  15. Ibn Abi Jumhur, Awali al-Laali, 1984 AH, juz. 2, uk. 224.
  16. Kulayni, al-Kafi, 1986 AH, juz. 2, uk. 287.
  17. Shuayri, Jami al-Akhbar, Najaf, uk. 74.
  18. Kulayni, al-Kafi, 1986 AH, juz. 2, uk. 279.
  19. Majlisi, Bihar al-Anwar, 1982 AH, juz. 66, uk. 127.
  20. Hilli, Tadhkirat al-Fuqaha, 1993 AH, juz. 2, uk. 391.
  21. «حکم تارک الصلاه», Tovuti ya Muflihun.
  22. Shahid Awwal, al-Durus, 1996 AH, juz. 1, uk. 144.
  23. Sheikh Tusi, al-Khilaf, 1986 AH, juz. 1, uk. 689.
  24. «پرسش و پاسخ، تارک نماز», Tovuti rasmi ya Ayatullah Sistani.
  25. Tabrizi, Istiftaat Jadid, bila tarehe, juz. 2, uk. 115.
  26. Kulayni, al-Kafi, 1986 AH, juz. 2, uk. 287; Daylami, Irshad al-Qulub ila al-Sawab, juz. 1, uk. 190.
  27. شیخ صدوق، علل الشرائع، ج۲، ص۳۳۹، «لئالی الاخبار، ص۱۲۹۷»، کتابخانه دیجیتال مرکز آموزش الکترونیکی دانشگاه قرآن و حدیث.

Vyanzo

  • Ibn Abi Jumhur, Muhammad bin Zayn al-Din, Awali al-Laali al-Aziziyya fi al-Ahadith al-Diniyya, Tahqiq na tas-hih Mujtaba Iraqi, Qum, Dar Sayyid al-Shuhada, 1984.
  • "Porsesh wa Pasokh, Tarik Namaz", Tovuti rasmi ya Ayatullah Sistani, tarehe ya kutembelewa: 24 Septemba 2022.
  • Tabrizi, Jawad, Istiftaat Jadid, Qum, Ofisi ya Ayatullah Tabrizi, Chapa ya kwanza, Bila tarehe.
  • Hurr Amili, Muhammad bin Hasan, Wasail al-Shia ila Tahsil Masail al-Sharia, Tahqiq Abdulrahim Rabbani Shirazi, Beirut, Dar Ihya al-Turath al-Arabi, bila tarehe.
  • "Hukm Tarik al-Salah", Tovuti ya Muflihun, Tarehe ya kutembelewa: 24 Septemba 2022.
  • Hilli, Hasan bin Yusuf, Tadhkirat al-Fuqaha, Qum, Muassasat Aal al-Bayt Alayhim al-Salam, Chapa ya kwanza, 1993.
  • Daylami, Hasan bin Muhammad, Irshad al-Qulub ila al-Sawab, Qum, al-Sharif al-Radi, Chapa ya kwanza, 1991.
  • Shuayri, Muhammad bin Muhammad, Jami al-Akhbar, Najaf, Matbaat Haydariyya, Chapa ya kwanza, bila tarehe.
  • Shahid Awwal, Muhammad bin Makki, al-Durus al-Shariyya fi Fiqh al-Imamiyya, Ofisi ya Machapisho ya Kiislamu, Qum, Chapa ya pili, 1996.
  • Sheikh Saduq, Muhammad bin Ali, Ilal al-Sharai, Qum, Kitabforushi Dawari, Chapa ya kwanza, 2006.
  • Sheikh Saduq, Muhammad bin Ali, Uyun Akhbar al-Rida (a.s.), Tahqiq na tas-hih Mahdi Lajwardi, Tehran, Nashr Jahan, Chapa ya kwanza, 1958.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin Hasan, al-Khilaf, tahqiq na tas-hih Ali Khurasani, Sayyid Jawad Shahristani, Mahdi Taha Najaf na Mujtaba Iraqi, Qum, Ofisi ya Machapisho ya Kiislamu, Chapa ya kwanza, 1986.
  • Taleqani, Sayyid Mahmud, Partawi az Quran, Tehran, Shirkat Sahami Intishar, Chapa ya nne, 1983.
  • Tayyib, Sayyid Abdulhusayn, Atyab al-Bayan fi Tafsir al-Quran, Tehran, Intisharat Islam, Chapa ya pili, 1999.
  • Kulayni, Muhammad bin Yaqub, al-Kafi, Tahqiq na tas-hih Ali Akbar Ghaffari na Muhammad Akhundi, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyya, Chapa ya nne, 1986.
  • "Laali al-Akhbar, uk. 1297", Maktaba ya Kidijitali ya Kituo cha Mafunzo ya Kielektroniki cha Chuo Kikuu cha Quran na Hadith, Tarehe ya kutembelewa: 25 Oktoba 2022.
  • Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar, Beirut, Dar Ihya al-Turath al-Arabi, Chapa ya pili, 1982.
  • Makarim Shirazi, Nasir, Tafsir Nemuneh, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyya, Chapa ya kwanza, 1995.