Mkopo:Nabsh al-Qabr, au kufukua kaburi

Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Nabsh Al-Qabr au Kufukua Kaburi (Kiarabu: نبش القبر) ni kitendo cha kuchimbua au kuvunja kaburi kwa kiwango kinachosababisha kuonekana kwa mwili wa marehemu. Ni haramu kisheri kufukua kaburi la Mwislamu kabla ya mwili wake kuharibika. Hii ni kwa mujibu wa fatwa zilizotolewa na wanazuoni wa pande zote mbili, yaani wanazuoni wa Kishia pamoja na Kisunni. Hata hivyo, sheria inaruhusu kitendo hicho katika mazingira maalumu ya dharura, kama vile; iwapo marehemu atakuwa amezikwa katika sehemu isiyo ya heshima inayoendana na mazingira na itikadi za Kiislamu, au penye hatari ya kuharibiwa. Aidha, inaruhusiwa kufukuwa kaburi na kumhamisha maiti fulani, iwapo kutakwa na masuala yanayohusiana na haki za watu wengine (Haqq al-Nas). Kwa mfano, iwapo marehemu atakuwa amezikwa katika ardhi iliyochukuliwa kwa njia isiyo halali, hiyo itatoa fuhalali wa kufukua kaburi na kumhamisha maiti huyo.
Wanazuoni wa upande wa Fiqhi ya Kishia wanaamini kwamba; iwapo aliyefariki dunia atakuwa ametoa wasia maalumu unaowataka watu wake kumzika katika haramu (mava, au jengo lenye kaburi takatifu) ya Maimamu, ila kukatokea jambo lililopelekea kuzikwa eneo jengine, hii huwajibisha kisheria kulifukua kaburi lake na kuuhamisha mwili wake hadi sehemu iliyokusudiwa ndani ya wasia wake. Ila ni kwa sharti ya kwamba; hatua hiyo isiwe ni yenye kupelekea udhalilishaji wa marehemu, wala isije kusababisha madhara mengine yoyote yale ya kimazingira au kijamii. Kuna mifano kadhaa iliyopatikana katika vyanzo vya historia kuhusiana na matukio ya aina kama hayo, likiwemo tukio la kuhamishwa kwa mwili wa Mirza Taqi Khan Amir Kabir, amabye hapo awali alikuwa amezikwa katika mjini wa Kashan na baadaye kuhamishwa na kupelekwa mava ya Karbala.
Tukitupia macho kurasa za vyanzo vya historia ya Uislamu, tutazikuta kurasa hizo zimejaa simulizi za majonzi zinazohusiana na matendo yaliyolenga kubomoa na kuchimbia makaburi ya watu mbali mbali, kwa lengo la kuvunja heshima na utukufu wa makaburi hayo. Miongoni mwa mifano hai ya majaribio hayo, ni zile jitihada za watawala wa Bani Abbasi zilizolenga ufukuaji wa kaburi la Imamu Hussein (a.s) pamoja na Imamu Musa al-Kadhim (a.s). Ama miongoni mwa mifano hai ya zama za karibuni, ni ile hatua ya ufukuaji wa kaburi la Hujr bin Adi lilichimbuliwa katikati ya vuguvugu la kisiasa nchini Syria, tukio lililorikodiwa mnamo tarehe 2 mwezi wa May mwaka 2013.
Ufasili wa Nabsh-e Qabr Katika Istilahi ya Fani ya Fiqhi
Neno “Nabsh al-Qabr” hufasiliwa kama kitendo cha kulichimbua kaburi kwa namna inayosababisha kudhihirika kwa mwili wa maiti aliyemo ndani yake.[1] Kiima «Nabsh» kinajumuisha maana mbili: ya kwanza ni kufichua hali iliyofichika, na ya pili ni uchimbuaji au uzikuaji wa kitu fula kutoka ardhini.[2] Licha ya maana mbili hizi, pia kulingana na istilahi inayotumiwa na Mafaqihi (Wataalamu wa Sheria za fiqhi), neno Nabsh Qabr kisheria ufumuaji au uchimbuaji wa kaburi kwa kiwango cha kuudhihirika mwili wa maiti aliyemo ndani yake. Hivyo basi, kisheria kitendo cha kuchimbua sehemu ya juu ya kaburi na kusababisha mwili ukuonekano wa maiti aliyemo ndani yake, huhesabiwa kuwa ni kitendo cha Nabsh al-Qabr, hata kama mwili wa maiti huyo haukutolea nje kabisa ya kaburi hilo.[3]
Hukumu ya Kifiqhi Juu ya Kitendo cha Kuchimbua Kaburi

Kulingana na fatwa za Mafaqihi wa madhehebu ya Kishia, kitendo cha kufukua kaburi (Nabsh al-Qabr) la Mwislamu kinahesabiwa kuwa haramu, yaani, kitendo kilichopigwa marufuku kisheria. Hata hivyo, hali hii hubadilika iwapo mwili wa marehemu utakuwa umesharibika kwa kiasi ambacho hata mifupa yake pia imeshageuka udongo, na pia katika hali ambayo kufukuliwa kwake hakutapelekea udhalilishaji au kuvunja heshima ya maiti huyo. Pamoja na kuhalilishwa kwa kitendo hicho kunakotegemea sharti mbili zilizotangulia, ila bado kanuni za fiqhi zinaharamisha moja kwa moja kitendo cha kuchimbua makaburi ya watoto wa Maimamu, mashahidi, pamoja na maulalama (wanazuoni wa dini). Huku hii ni thabiti hata kufariki kwao kushapitia na kipindi cha miaka na miaka.[4]
Kulingana na Hadithi zinazouthamini mwili muumini bila ya kubagua kati ya kipindi cha uhai wake na baada ya kufa kwake, Mafaqihi wamebaini kuwa sababu kuu ya kuharamishwa ufukuaji wa kaburi la Muislamu, ni hatku al- hurmat, yaani, kitendo cha kuvunja heshima ya marehemu aliyetangulia mbele ya haki.[5] Tukiingia kwenye uwanja wa mijadala ya kifiqhi kuhusiana na suala hili, tutamkuta Allamah Hilli alisema kwamba; sababu hasa ya uharamu wa Nabsh al-Qabr inatokana na uwezekano wa kusababisha muthla (kukata au kuvuruga viungo vya mwili wa marehemu).[6] Hata hivyo, kauli hii ilipingwa na kukataliwa na wanazuoni mashuhuri wa sheria za fiqhi, akiwemo Shahid al-Awwal na Muhaqqiq Karaki.[7]
Hata wanazuoni wa Kisunni (Mafaqihi wa Ahlu-Sunna) pia nao ni wenye makubaliano kamili juu ya uharamu wa kuchimbua kaburi (Nabsh al-Qabr), isipokuwa tu pakiwepo dharura maalumu ya kisharia (Daruratu al-Shar‘iyya) itakayoweza kujuzisha kitendo hicho.[8] Mfano wa dharura hiyo ni kuwepo kwa haki za watu wengine (Haqq al-Nas) zilizopuuzwa au kutoeleweka katika mazishi yake ya mwanzo; kama vile; kuwepo kwa mali ya mtu fulani iliozikwa pamoja na mwili wa marehemu huyo. Katika hali kama hii, huwa si haramu kuchimbua kaburi la maiti huyo, kwa ili kurejesha haki hiyo kwa mmiliki wake.[9]
Hali Zinazoruhusu Kuchimbua Kaburi (Nabsh al- Qabr)
Kwa mujibu wa Mafaqihi wa Kishia, kuchimba kaburi kunaruhusiwa tu katika mazingira maalumu:
- Endapo marehemu atakuwa amezikwa katika sehemu ambayo itapelekea heshima yake kudharauliwa au atakuwa yuko katika hatari ya kuathirika (kama vile kufukuliwa na wanyama fulani),[10] au pale sehemu ya mwili wake itapokuwa haikuzikwa pamoja naye, na kwamba watu wake wakataka kuizika sehemu hiyo pamoja naye. [11]
- Endapo kaburi litakuwa lipo katika ardhi iliyotwaliwa kwa dhuluma (ardhu ghasbiyya), au kukiwepo na mali fulani iliyotwaliwa kimabavu ambayo ilizikwa pamoja na marehemu, au mali ya warithi iliyozikwa pamoja naye kimakosa.[11]
- Endapo kutakuwa na haja ya kisheria ya kuufukua mwili wa marehemu fulani ili kuthibitisha haki fulani, au kutekeleza jambo lenye umuhimu wa juu wa kisheria kuliko uharamu wa kufukua kaburi.[12] Mfano wa hilo ni kama vile kumtoa mtoto aliye hai tumboni mwa mama aliyefariki dunia huku akiwa ni mjamzito.[13]
- Kwa mujibu wa baadhi ya baadhi ya mazuoni wakuu wa fani ya fiqhi (Maraji‘al-Taqlid), ni kwamba; iwapo marehemu atakuwa ameusia kuzikwa katika maeneo matukufu ya Maimamu (Haram al-A’imma), kisha akazikwa mahali pengine, basi ni wajibu (lazima) kuchimbua kaburi lake na kuuhamisha mwili wa maiti huyo, mradi tu hatua hiyo isiwe ni yenye kuvunja heshima ya marehemu wala kusababisha madhara fulani.[14]
Ni muhimu kuelewa kwamba; wanazuoni wa fiqhi wa Kishia wana mitazamo inayotofautiana kidogo kuhusiana na masharti mahususi yanayohusiana na ruhusa ya kuchimbua makaburi. Ingawa wote wanakubaliana juu ya msingi wa uharamu wa Nabsh al-Qabr, ila tofauti zao zinajitokeza katika ufasiri wa hali maalum za dharura, namna ya kutathmini heshima ya marehemu, na mipaka ya uhalali wa hatua hiyo kifiqhi.[15]
Matukio ya Kihistoria ya Kufukua Makaburi (Nabsh al-Qabr)
Vyanzo vya kihistoria vinanukuu matukio mbalimbali ya Nabsh al-Qabr (kuchimbuliwa kwa makaburi) yaliyojiri katika nyakati tofauti, ambayo yalitendeka kwa malengo tofauti ya kijamii na kidini. Wakati mwingine, matendo hayo yalilenga kuvunja heshima ya makaburi ya watu mashuhuri, na wakati mwingine yalifanywa kwa nia ya kuhamisha miili ya watu fulani kutoka eneo la kawaida na kwenda katika maeneo matakatifu. Kitendo hichi cha uharibifu wa makaburi, kilipelekea kufichwa kwa baadhi ya makaburi ili kuzuia kitendo cha kuchimbuliwa na kupelekea udhalilishaji wa marehemu aliyemo ndani yake. Mfano wa kihistoria unaojulikana kuhusiana na suala hili, ni kufichwa kwa kaburi la Imamu Ali (a.s), hatua iliyochukuliwa kwa ajili ya kuwazuia Bani Umayya na Khawariji wasiweza kutenda matendo ya udhalilishaji dhidi yake.[16] Matukio mengine ni ya uchimbuaji wa makaburi ni ya watuku wa Kishia ni pamoja na:
- Ufukuaji wa kaburi la Zaid bin Ali mwaka 122 Hijria.[17]
- Jaribio la Ibrahim Dizzaj la kuchimbua kaburi la Imamu Hussein (a.s) kwa amri ya Mutawakkil Abbasi mwaka 236 Hijria.[18]
- Na tukio la kufukuliwa kwa kaburi la Imamu Musa al-Kadhim (a.s) mwaka 433 Hijria.[19]
Kwa mujibu wa maelezo yanayopatikana katika vyanzo vya kihistoria, Abdullah bin Ali al-Abbasi, miongoni mwa watawala wa Damascus walioshika madaraka baada ya kuanguka kwa utawala wa Umawiyya, aliamuru kufukuliwa kwa makaburi kadhaa ya watawala wa ukoo huo, likiwemo kaburi la Mu‘awia bin Abi Sufyan, Yazid bin Mu‘awia, Abd al-Malik bin Marwan na Hisham bin Abdu al-Malik, tukio lililojiri mnamo mwaka 132 Hijria. Baada ya hapo aliamuru mabaki ya miili yao iteketezwe kwa moto.[20]
Aidha mnamo tarehe 2 mwezi wa May mwaka 2013, kaburi la Hujr bin Adi lilifukuliwa kupitia kundi la wanajihadi waliojiita Jabhat al-Nusra, jambo lililotambuliwa kimataifa kama ni kitendo cha kuvunja heshima ya kidini. Kuhamishwa kwa mwili wa Mirza Taqi Khan Amir Kabir kutoka Kashan kwenda Karbala, ni mfano wa Nabsh al-Qabr uliofanywa kwa lengo la heshima maalumu. Huu ni miongoni mwa mifano ya kumhamisha maiti kwenda katika maeneo matakatifu ya Maimamu au eneo takatifu la wana wema wa Maimamu. Vile vile ile dhana ya kuizika miili katika eneo la muda kama ni amana, tendo linalofanywa kabla ya maziko ya mwisho ya maiti fulani, pia nayo inahusishwa moja kwa moja na dhana ya Nabsh al-Qabr. Mfano hai wa aina hii, ni mwili wa mwanazuoni Sayyid Hadi Khosrowshahi, ambao ulizikwa kwa muda katika mava ya Behesht Ma‘asoumeh (Qom), na baadaye kuhamishwa hadi kwenye maktaba yake binafsi baada ya kipindi cha miaka mitatu.[21] Mfano mwengi hai wa aina hii, ni Dk. Ali Shariati, ambaye mwili wake ulizikwa kwa muda nchi Syria kama amana, ukisubiri kuhamishwa na kwenda kuzikwa nchi Iran.[22]
Rejea
- ↑ Khomeini, Tarjume Tahrir al-Wasilah, 1385 S, juz. 1, uk. 105.
- ↑ Ibn Manzur, Lisan al-Arab, Chini ya Neno «Nabsh».
- ↑ Manafi, «Nabsh qabr», uk. 130-131.
- ↑ Sistani, Sheria za Mazishi, Kipengele cha 630 na 631; Nouri Hamedani, Sheria za Ufukuaji wa Maiti, Kipengele cha 642 na 643; Shubary Zanjani, Sheria za Uchimbaji Maiti, Kipengele cha 733 na 734.
- ↑ Hilli, Tadhkirat al-Fuqaha'i, 1414 AH, juz. 2, uk. 102, Iliyonukuliwa na: Manafi, «Ufukuaji wa Makaburi», uk. 137.
- ↑ Hilli, Tadhkirat al-Fuqaha'i, 1414 AH, juz. 2, uk. 102, Iliyonukuliwa na: Manafi, «Ufukuaji wa Makaburi», uk. 133.
- ↑ Al-Bayan, uk. 80, Iliyonukuliwa na: Manafi, «Ufukuaji wa Makaburi», uk. 135.
- ↑ "Hukumu ya Kufukua Makaburi kwa Mtazamo wa Madhehebu Manne ya Kisunni", Shirika la Habari la Rasa.
- ↑ utakatifu wa kufukua makaburi kutoka kwa mtazamo wa wanasheria wakubwa wa madhehebu ya Kiislamu, "Hifadhidata maalum kwa ajili ya masomo ya Wahhabi
- ↑ Muntaziri, Risale Tawdhih al-Masail, Kipengele cha 676.
- ↑ Muntaziri, Risale Tawdhih al-Masail, Kipengele cha 676.
- ↑ Muntaziri, Risale Tawdhih al-Masail, Kipengele cha 676.
- ↑ Makarim Shirazi, Makala kuhusu Maelezo ya Sheria za Ufukuaji Maiti, Kipengele cha 599.
- ↑ Sistani, Maelezo ya Masuala, Ufukuaji wa Maiti, Kipengele cha 853.
- ↑ Tazama Makarim Shirazi, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala, Sheria za Kufukua Makaburi, Toleo la 599; Sistani, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala, Kufukua Makaburi, Toleo la 853; Wahid Khorasani, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala, Kesi za Ufukuaji, Toleo la 649; Nouri Hamedani, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala, Hukumu kuhusu Ufukuaji, Kipengele 642 na 643; Shubary Zanjani, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala, Hukumu kuhusu Ufukuaji wa Maiti, Kipengele cha 733 na 734.
- ↑ Maqadasi, Bazpashuhi Tarikh Wiladat wa Shahadat Maasuman (a.s), 1391 S, uk. 239.
- ↑ Tabari, Tarikh al-Tabari, 1967, juz. 7, uk. 187.
- ↑ Tusi, Amali, 1414 AH, uk. 326.
- ↑ Ibn Athir, Al-Kamil Fi al-Tarikh, 1965, juz. 9, uk. 577.
- ↑ Ibn Athir, Al-Kamil Fi al-Tarikh, 1965, juz. 5, uk. 430; Abu al-Fida, Tarikh abi al-Fida, 1997, juz. 1, uk. 294.
- ↑ Mwili wa Ayatollah Khosrowshahi ulihamishiwa mahali pa wosia wake baada ya miaka mitatu, Shirika la Habari la IKNA.
- ↑ «Ihsan Shariati: Mwili wa baba yangu ulihifadhiwa na kuzikwa kwa muda nchini Syria», Tovuti ya Khabar Online.
Vyanzo
- «Ihsan Shariati: Mwili wa baba yangu ulihifadhiwa na kuzikwa kwa muda nchini Syria», Tovuti ya Khabar Online, Tarehe ya Kuchapishwa: Juni 20, 2018, Tarehe ya Ukaguzi: Mei 10, 2023.
- «Kuchunguza utakatifu wa kufukua makaburi kutoka kwa mtazamo wa wanasheria wakubwa wa madhehebu ya Kiislamu»,Hifadhidata Maalum ya Masomo ya Wahhabi. Tarehe ya Kuchapishwa: Septemba 1, 2014, Tarehe ya Ukaguzi: Mei 10, 2023.
- Mwili wa Ayatollah Khosrowshahi ulihamishiwa mahali pa wosia wake baada ya miaka mitatu, Shirika la Habari la IKNA, Tarehe ya Kuchapishwa: 09 Esfand 1401 AH.
- Abu al-Fida, Ismail ibn Ali, Historia ya Abu al-Fida, juz. 1, Beirut, Dar al-Kutub al-Ilmiyah, 1997 BK / 1417 AH.
- Ibn Athir, Ali ibn Muhammad, Al-Kamil Fi al-Tarikh, juz. 5, Beirut, Dar al-Sad, 1385 AH/1965 AD.
- Ibn Manzur, Muhammad Jamal al-Din, Lisan al-Arab, juz. 6, Beirut, Dar al-Sadr, Chapa ya Tatu, 1994 AD.
- Hilli, Hassan ibn Yusuf, Tadhkirat al-Fuqaha'i, Qom, Ahlul-Bayt, 1414 AH.
- «Hukumu ya Kufukua Makaburi kwa Mtazamo wa Madhehebu Manne ya Kisunni», Shirika la Habari la Rasa. Tarehe ya Kuchapishwa: Septemba 5, 2017, Tarehe ya Ukaguzi: Mei 7, 2017.
- Khomeini, Sayyid Ruhullah, Tarjume Tahrir al-Wasilah, Iliyotafsiriwa na Taasisi ya Ukusanyaji na Uchapishaji wa Kazi za Imam Khomeini (RA), Toleo la Kwanza, 2006.
- Khormouji, Muhammad Jafar, Haqaiq al-Akhbar Nasiri, Tehran, Machapisho ya Kitabu cha Wafanya Ziara, 1965.
- Sistani, Sayyid Ali, Sistani, Sayyid Ali, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala, Sheria za Kufukua Makaburi, Tovuti ya Ofisi ya Ayatullah Sistani, Iliyokaguliwa: 10 Mei 1402.
- Shubary Zanjani, Sayyid Musa, Makala kuhusu Maelezo ya Masuala na Ayatullah Shubairy Zanjani, Tovuti ya Ofisi ya Ayatullah Shubary Zanjani, Iliyokaguliwa: 10 Mei 1402.
- Tabari, Muhammad ibn Jarir, Historia ya Tabari, juz. 7, Beirut, Rawa'i' al-Turath al-Arabi, 1387 AH/1967 AD.
- Tusi, Muhammad bin Hassan, Al-Amali, Qom, Dar al-Thaqafa, 1414 AH.