Kuzuru Makaburi
Kuzuru Makaburi (Kiarabu: زيارة القبور) Kunamaanisha kutembelea makaburi na kuwepo makaburini hapo kwa ajili ya kuwaheshimu na kuwaenzi waliozikwa makaburini humo. Wanazuoni wa Kiislamu wakifuata Aya za Qur'ani na Hadithi, wamelihisabu suala la kutembelea makaburi -hasa ya Manabii na watu wema- kuwa ni jambo la kisheria. Kuna faida kadhaa zilizo bainishwa na wanazuoni hao katika amali hiyo ya kuzuru makaburi. Hata hivyo, Mawahabi wanakataza vikali amali ya kutembelea makaburi.
Wanazuoni wa Kiislamu -isipokuwa Mawahabi- wote kwa jumla wanakubaliana kuwa ni mustahabu (sunna) kwa wanaume kutembelea makaburi. Ila wanazuoni hao wakhitilafiana kimaoni juu ya hukumu ya wanawake katika kutembelea makaburi hayo. Wanazuoni wengi wa Kiimamiya wamekataa na kusema kuwa; si sunna kwa wanawake kutembelea makaburi, kama ilivyo kwa upande wa wanaume. Pia, ni maarufu kati ya wanazuoni wa upande wa Kisunni kuwa; ni makuruhu kwa wanawake kutenda amali ya kuzuru makaburi.
Dhana ya Kuzuru Makaburi na Nafasi Yake
Kuzuru Makaburi kunamaanisha amali ya kutembelea makaburi na kuwepo karibu na makaburi hayo kwa nia ya kujenga heshima na kuwaenzi waliomo makaburoni humo. Katika istilahi za kidini, pia dhana hii inahusishwa na kutembelea makaburi ya Manabii, Maimamu, pamoja na watu wema. Jambo ambalo hufungamana na ibada maalum zenye ishara na malengo kadhaa, kama vile; kujenga heshima, kuomba msaada (kutawasali) na kupata baraka kutoka kwao. [1] Inasemekana kuwa; kuheshimu makaburi ya marehemu waliomo ndani yake, hasa makaburi watu watukufu na wakuu wa jamii, ni miongoni mwa amali zenye historia refu kabisa kwenye jamii za wanadamu, ambapo tangu zamani za kale, yaonekana kuwa duniani kote watu walikuwa na kawaida ya kuwaheshimu na kuwatembelea maiti wao. [2] Kwa mujibu wa maelezo ya Ja’afar Subhani ni kwamba; Katika utamaduni wa Kiislamu, kutembelea kaburi la Mtume (s.a.w.w), Ahlul-Bait wake (a.s), pamoja na makaburi ya waumini mbali mbali, ni moja ya sehemu muhimu za utamaduni wa Kiislamu. [3]
Dhiyauddin Maqdisi, ambaye ni mwanazuoni na mwanahistoria wa upande wa madhehebu ya Hanbali (aliyefariki mwaka 663 Hijria), ameeleza akisema kuwa; Kwa mujibu wa baadhi ya Riwaya, katika nyakati na maeneo yote duniani, Waislamu walikuwa na kawaida ya kutembelea makaburi na kusoma Qur'ani kwa ajili ya marehemu waliomo makaburini humo. Dhiyauddin Maqdisi anasema kuwa; desturi hii ni desturi yenye sifa ya makubaliano ya kipamoja (ijmau) na hakuna aliyepinga nyenendo hizo. [5] Kutembelea makaburi na kuwazuru waliomo makaburini humo katika siku za Alhamisi na Ijumaa, ni miongoni mwa mila maarufu katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama Iran. Miongoni mwa desturi na amali zifanywazo na baadhi ya watu wakati wa kutembelea makaburi hayo ni; kutia Suratu ya Fatiha pamoja na kusoma Qur'an, kuosha makaburi, kuwasha mishumaa, kuweka maua juu ya makaburi, kugawa sadaka kwa nia ya kumfikishia thawabu marehemu aliyemo kaburini humo. [6]
Uhalali na Athari (Faida) za Kutembelea Makaburi
Wanazuoni wa Kiislamu, wakishikamana na Aya za Qur'an pamoja na Hadithi, wamehalalisha amali ya kutembelea makaburi, hasa ya manabii na watu wema, na wamelishisabu jambo hili kuwa ni miongoni mwa mambo kisheria. Pia wanazuoni hao wametaja faida kadhaa kuhusiana na amali ya kuzuru Makaburi. [7] Miongoni mwa athari zilizotajwa kuhusiana na utembeleaji makaburi ni pamoja na; kukumbuka kifo na kutosahau Akhera,[8] kupata ukuruba wa Mwenye Ezi Mungu,[9] pamoja na kuifanya mioyo iwe laini na tiifu. [10] Pia yasemekana kwamba kwa kutembelea makaburi, mtu anaweza kukumbuka ufupi wa maisha, na kumbukumbu hii inaweza kumfanya ashikamane na maadili mema. Zaidi ya hayo, waliozikwa pia nao hupata manufaa kutoka na dua pamoja na maghufira yaombwayo na wageni watembeleao makaburi hayo. [11]
Katika moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) imesimuliwa ya kwamba, Imamu Sadiq alisema kuwaambia watu akisema; “Tembeleeni makaburi ya waumini; kwani wao wanapenda kuwa karibu na nanyi, kwani wao hupata khofu pale wanapokuwa mbali nanyi”. [12] Pia katika moja ya Hadithi nyingine, iliyosimuliwa kutoka kwake, ni kwamba Yeye (a.s) aliwaambia watu akisema; “Watembeleeni wafu wenu kwani wao hufurahia ziara zenu, na yeyote anayekwenda kwenye makaburi ya wazazi wake, baada ya kuwaombea, amalizie kwa kuomba haja zake”. [13]
Hoja na Ithibati Juu ya Uhalali wa Kutembelea Makaburi
Wanazuoni wa Kiislamu wamehalalisha kuzuru makaburi, hasa kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja makaburi ya waumini, na wamelihisabu kuwa ni jambo la kisheria, na wakalitolea ushahidi kwa kutumia ithibati zifuatazo:
- Qur'ani: Aya ya 84 ya Surat al-Tawba inazungumzia kuzuia na kumkataka bwana Mtume (s.a.w.w) asimsalie maiti yeyote yule miongoni mwa maiti wa wanafiki, na wala asisimama kando ya makaburi yao kwa ajili ya kuwaombea dua. [14] Wafasiri wa Qur’ani wanasema kuwa; katazo hili ni kwa ajili ya kunaonesha uhalali wa kusimama kando ya kaburi na kusoma dua, na kuihisabu amali hiyo kuwa ni ibada halali; laa si hivyo! Basi Mwenye Ezi Mungu asingekataza kuwafanyia hivyo wanafiki tu, bali alijumuisha makaburi ya kila mfu. [15]
- Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w): Kutembelea makaburi kulikuwa halali na ni jambo la kawaida tangu mwanzoni wa Uislamu. Ibn Shabba katika kitabu chake "Tareekh al-Madina al-Munawwara" anaripoti akisema kwamba; Pale bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akirudi kutoka kwenye ukombozi wa mji wa Makka na kulekea Madina, alitembelea kaburi la mama yake (bibi Amina) na kusema: "Hili ni kaburi la mama yangu, nilimwomba Mwenye Ezi Mungu ruhusa ya kumtembelea Nay akanirihusu kufanya hivyo." [16] Pia inasemekana kuwa alitembelea makaburi ya mashahidi wa vita vya Uhud [17] pamoja na makaburi ya waumini wengine yalioko ndani ya mava ya Baqi. [18]
- Desturi na nyenendo za Maimamu Maasumina (a.s): Katika vyanzo vya kihistoria, kuna ripoti kadhaa zinazohusiana na Maimamu kutembelea makaburi. [19] Kwa mfano, imeelezwa ya kuwa; Bibi Fatima (a.s) alikuwa na kawaida ya kutembelea kaburi la Hamza bin Abdul-muttalib kila Ijumaa, akiswali na kumlilia kaburini kwake. [20] Pia imeripotiwa na Imamu Baqir (a.s) ya kwamba; Ilikuwa ni kawaida ya Imamu Hussein (a.s), kila usiku wa Ijumaa kwenda kutembelea kaburi la Imamu Hassan (a.s). [21] Katika moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Ridha (a.s) imesimuliwa ya kwamba; Imamu Sajjad (a.s) alikuwa na kawaida ya kutembelea kaburi la Imamu Ali (a.s), akasimama kando ya kaburi hilo, akilia na kutoa salamu zake za kiheshima na mapenzi kwa Imamu Ali (a.s). [22] Vilevile, katika vyanzo vya Hadithi za Kishia, kuna Hadithi kadhaa zinazozungumzia faida na mapendekezo ya kutembelea kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), Maimamu wa Kishia (a.s), pamoja na makaburi ya waumini wa kawaida. [23]
- Desturi na matendo ya Masahaba na Tabiina (waliofuatia baada yao): Kuna ripoti kadhaa za Masahaba na Tabiina za kutembelea makaburi katika vyanzo mbali mbali vya kihistoria na Hadithi, ikionesha kwamba; Masahaba na wafuasi wao, hawakulihisabu jambo hili kuwa ni miongoni mambo maovu yaendayo kinyume na sheria za dini. [24]
- Ijmaa (mawafikiano) ya Wanazuoni: Uhalali wa kutembelea kaburi la Mtume (s.a.w.w) na makaburi ya waumini na watu wema ni jambo lenye makubaliano (ijmaa) ya wanazuoni wa Kiislamu. [25] Qadhi ‘Iyadhu (aliyefariki mnamo mwaka 544 Hijria), ambaye ni mwanazuoni na faqihi wa Madhehebu ya Maliki, amesema katika kitabu chake kiitwacho "Al-Shifa bi Ta'arifi Huquq al-Mustafa" ya kwamba; ni Miongoni mwa nyenendo na desturi za Waislamu zenye faida, ambazo Waislamu wote wamekubaliana nazo, ni amali ya kutembelea kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w). [26]
- Desturi na nyenendo za Waislamu: Kutembelea makaburi ya waumini na kuwaombea waliozikwa makaburini humo, ilikuwa ni moja ya desturi za Waislamu tangu zama za bwana Mtume (s.a.w.w). [27] Abu Bakar Kashani, faqihi wa kutoka upande wa Kisunni wa karne ya sita Hijiria, kwa kutilia maanani Hadithi hii ya bwana Mtume (s.a.w.w), isemayo; (نَهَيْتُكُمْ عَنْ زِيَارَةِ الْقُبورِ فَزُوروهَا ; Nilikukatazeni kutembelea makaburi, lakini sasa tembeleeni), [28] amesema kwamba; Baada ya bwana Mtume (s.a.w.w) kuruhusu kutembelea makaburi, Waislamu walilihisabu jambao hilo kuwa ni halali, na wamekuwa wakifanya hivyo tangu wakati huo hadi leo. [29]
Adabu za Kutembelea Makaburi
Wanazuoni wa Kiislamu, kwa kuzingatia Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumu (a.s), wameorodhesha adabu na matendo kadhaa yanayopendekezwa wakati wa kuzuru makaburi, baadhi ya yake ni kama ifuatavyo:
- Kwenda kutembelea makaburi siku ya Alhamisi, hasa wakati wa jioni. [31]
- Kuweka mkono juu ya kaburi na kuelekea Kibla. [32]
- Kusoma Suratu al-Qadri mara saba. [33]
- Kusoma Ayatu al-Kursi na Sura al-Ikhlas mara tatu. [34]
- Kusoma Suratu al-Fatiha na Sura za al-Mu'awwidhatain (Qul a’udhu birabbi al-Nnasi na qul audhu birabi al Falaq). [35]
- Kumwaga na kunyunyiza maji juu ya kaburi. [36]
- Kuomba dua na kumwombea rehema na maghufira aliyezikwa kaburini humo. [37]
Hukumu ya Kutembelea Makaburi kwa Upande wa Wanawake
Hakuna khitilafu wala tofauti yoyote ile kati ya wanazuoni wa Kiislamu kuhusiana na uhalali na kupendekezwa amali ya kutembelea makaburi kwa upande wa wanaume, ila kwa upande wa wanawake, wanazuoni wamekhitilafiana juu ya kuwepo ruhusa na uhalali wa kisheria unaowaruhusu wanawake kwenda kuzuru makaburi. Maoni ya wanazuoni wa Kiislamu kuhusiana na ruhusa hiyo ni kwama ifuatavyo:
- Msimamo wa madhehebu ya Shia Imamiyyah: Wanazuoni wa madhehebu ya Shia Imamiyyah wamehalalisha na kupendekeza wanawake kwenda kuzuru makaburi. Sahibu Hadha'iq, ambaye ni faqihi na mwanhadithi wa Kishia, amedai kuwepo kwa makubaliano ya wanazuoni kuhusiana na jambo hili. [38] Hata hivyo, Muhaqqiq al-Hilli katika kitabu chake al-Mu'utabar, na Allama al-Hilli katika chake Muntaha al-Mataalib wamesema kwamba; jambo hili ni miongoni mwa mambo yanayo chukiza (makruhu). [39] Shahid al-Awwal katika kitabu chake Dhikra al-Shia alikubaliana na msimamo wa Muhaqqiq al-Hilli akisema kuwa; Yawezekana kwamba, kule kutoa hukumu ya makruh kwa wanawake kutembelea makaburi, ni kwa sababu ya jambo hili kuweza kuwa na mgongano na amri ya wanawake kujisitiri, ambapo hukuhi itapelekea kuepukana na wanaume wasio maharimu. Hata hivyo, iwapo hakutakuwepo na mgongano baina ya mbambo mawili hayo, basi si halali tu, bali amali hiyo linapendekezwa kwa wanawake kama ilivyo kwa upande wa wanaume. [40]
- Msimamo wa Ahlu-Sunna: Kulingana na maelezo ya Taqi al-Din al-Subki katika kitabu chake Shifa-u al-Siqaami na kitabu «Al-Mawsu'ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaitiyyah», ni kwamba; msimamo mashuhuri kati ya wanazuoni wa Ahlu-Sunna, ni makruhu kwa wanawake kuzuru makaburi. [41] Hata hivyo Baadhi yao wanao sema kwamba jambo hilii ni jambao linalopendekezwa kwa wanawake kama ilivyo kwa upande wa wanaume. [42]
- Msimamo wa Mawahabi: Muhammad bin Abdul Wahhab na wafuasi wake wajulikanao kwa jina la Mawahabi, wameharamisha wanawake kuzuru makaburi. Uamuzi huo umeegemea kwenye Hadithi isemayo: (لَعَنَ اللَّهُ زَوَّارَاتِ الْقُبُورِ ; Laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya wanawake wanaozuru makaburi). [43] Hii ndiyo Hadithi iliyotegemewa na Mawahabi kwatika kuwaharamishia wanawake amali ya kuzuru makaburi. [44] Baadhi yao wamesema kuwa neno "laana" katika Hadithi linaashiria kuwa ni haramu na hata wakasema kuwa; ni dhambi kubwa kwa wanawake kuzuru makaburi. [45] Hata hivyo, msimamo huu umekosolewa na wanazuoni wa Kiislamu. Wengine kama vile Tirmidhi na Hakim al-Nishaburi, kutoka kwa wanahadithi wa Ahlu-Sunna, wamesema kuwa; Hadithi hii ilihusiana na wakati ambapo bwana Mtume (s.a.w.w) alikuwa amekataza kuzuru makaburi; ila baadae hukumu hii ilifutwa wanawake nao wakaruhusiwa kuzuru makaburi. [46] Pia kuna wengine waliosema kuwa; Hadithi hii inahusiana na hali ambapo kutembelea makaburi kutasababisha kutendeka kwa dhambi au jambo fulani la haramu. [47] Wengine kama vile Qurtubi (aliyefariki mnamo mwaka 671 Hijria), ambaye ni faqihi na mfasiri wa upande wa madhehebu ya Maliki, wamesema kuwa neno زَوَّارَات «Zawwaaraat» lililoko katika Hadithi hiyo, wingi wa utendaji wa wa amili hiyo kwa mfumo wa kufurutu ada, na linawahusu wanawake wanaotembelea makaburi mara kwa mara, kwa hiyo laana iliyo tangazwa katika Hadithi hiyo, haimhusu kila mwanamke. [48] Kulingana na fatwa iliyotolewa na Dar al-Iftaa' ya Misri «دار الإفتاء مصر», ni kwamba; kutembelea makaburi ni jambo linalopendekezwa kwa watu wote, wake kwa wanaume, na hukumu ya Hadithi iliyo tajwa katika mjadala huu, inahusiana na hali ambapo kuzuru makaburi huko kutapelekea kuhuisha vilio, huzuni na maombolezo makaburini humo. [49]
Upinzani wa Ibn Taimiyyah na Mawahabi Dhidi ya Amali ya Kuzuru Makaburi
Ibn Taymiyyah na Mawahabi, kwa kutumia Hadithi ya Shaddu al-Rihal (شَدُّ الرِحال), wameharamisha safari ya kusafiri kwa ajili ya kuzuru makaburi, hata kama litakuwa ni kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), na wakalihisabu jambo hilo kuwa ni la bid'a na la kishirikina. [50] Kwa mujibu wa mtazamo wao, kulingana na Hadithi hii, ni halali tu kusafiri kwa ajili ya kutembelea misikiti mitatu mitakatifu, nayo ni; Masjid al-Haram, Masjid al-Aqsa, na Masjid al-Nabawi. [51]
Wanazuoni wa Kiislamu wamekosoa vikali msimamo huu. Wanazuoni wengi wa Ahlu-Sunna kama vile Nawawi,[52] Ibn Hajar al-Asqalani,[53] Ghazali,[54] Mulla Ali Qari Hanafi,[55] Shamsu al-Din al-Dhahabi,[56] Jassas,[57] Ibn Abidina faqihi wa Kihanafi,[58] Zaraqani faqihi wa Kimaliki,[59] Ibn Qudamah faqihi wa Kihanbali[60] na wengi wengineo, wanaamini kuwa; Hadithi ya Shaddu al-Rihal iliyo rejelewa na Ibn Taymiyyah kwa ajili ya kupinga amali ya kuzuru makaburi, hasa kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), haikuja kwa ajili ya kuzuia na kuharamisha ziara hizo,[61] bali ni kwa ajili ya inabainisha ubora wa misikiti hiyo mitatu mitukufu.