Kuoa Dada Wawili kwa Wakati Mmoja
Kuoa Dada Wawili kwa Wakati Mmoja (Kiarabu: الزواج من الشقيقتين) Katika muktadha wa dini ya Kiislamu, haifai dada wawili kuolewa kwa wakati mmoja, ikiwa dada wawili hao wataolewa na mwanaume mmoja katika zama, jambao linachukuliwa kuwa haramu katika dini ya Kiislamu. [1] Mashiko na marejeo ya mafaqihi juu ya uharamu wa jambo ni Aya ya 23 ya surat Al-Nisa, pamoja na Hadithi [2] zinazothibitisha wazi uharamu wa kufunga ndoa ya kudumu au ya muda na dada wawili kwa pamoja na kwa wakati mmoja. [3] Kwa hivyo, endapo mwanamme fulani atampa talaka mkewe au kumaliza kipindi kilichobaki cha mkataba wa ndoa ya muda, pamoja na baada ya kumaliza eda, hapatakuwa na kizuizi zha kisheria au kidini kinachomzuia kuoa dada wa mke wake wa zamani. Hii inaashiria kuwa, licha ya umarufuku wa ndoa ya dada wawili kwa wakati mmoja, ila sheria za Kiislamu zinamruhusu mwanamme kuoa dada wa mke wake wa zamani baada ya kumaliza mchakato wa talaka pamoja na eda. [4]
Muktadha huu unasisitiza kanuni ya kuheshimu mipaka ya dini katika masuala ya ndoa na talaka, na kuonesha jinsi sheria za Kiislamu zinavyozingatia uhusiano wa kisheria na kihisia kati ya wanandoa, huku zikihakikisha kuwa haki za kila upande zinazingatiwa ipasavyo. Katika mtazamo wa wanazuoni wa Kiislamu, hukumu ya uharamu wa kuoa dada wawili kwa wakati mmoja inajumuisha dada wa baba, dada wa mama, pamoja na dada wa kunyonya ziwa moja. [5] Kwa mtazamo wa baadhi ya wanazuoni wa Kishia ni kwamba; ikiwa mtu atafunga ndoa ya muda na dada wawili kwa pamoja, ndoa zote zitachukuliwa kuwa batili. [6] Hii inajumuisha pia hali ya ndoa moja kufanyika kabla ya nyingine; yaani ikiwa mtu atafunga ndoa na dada wa kwanza, ndoa ya dada wa pili itakuwa batili na haitaweza kufungika, isipokuwa baada ya kutimiza masharti yaliotjwa hapo mwanzo. [7] Kwa mujibu wa maoni ya Jawadi Amuli, aliye zaliwa mwaka 1312 Hijiria shamsia, ni kwamba; iwapo mtu atafahamu kuwa tendo hili ni haramu kisha akaendelea kujihusisha nalo, huyo atakuwa amefanya dhambi pamoja na kubatilika kwa ndoa hiyo. [8]
Kulingana na Hadithi za Kishia ni kwamba; kuoa dada wawili kwa wakati mmoja ni haramu, kama ilivyoelezwa na Maimam (a.s) katika Hadithi mbali mbali. Kitabu cha Wasail al-Shi'a kimeorodhesha Hadithi 23 kuhusiana na hukumu ya kufunga ndoa na dada wa mke. [9] Mwandishi wa kitabu kiitwacho Jawahir baada ya kunukuu Hadithi mbili kati ya Hadhithi zinazutoa hukumu ya suala hili, yeye amekiri ya kwamba baadhi ya wakati, Maimamu (a.s) hawakuwa wakitoa matamko ya wazi juu ya uharamu wa tendo hili, kutokana na hali ya taqiyyah (kuficha imani kwa lengo la kulinda dini pamoja na roho zao). [10]
Nassir Makarim Shirazi, mfasiri na mwanafiq’hi wa Kishia, anasisitiza kwamba; sababu ya kuharamishwa kwa kuoa dada wawili kwa wakati mmoja ni kuzuia migogoro na hisia za ushindani kati yao. kwa hiyo kutofanya hivyo ni kudhamini uhusiano mzuri na kudumisha amani kati ya dada hao, na hivyo kuhakikisha mshikamano wa familia baina yao. [11] Katika Aya ya 23 ya surat Al-Nisa, imekataza waziwazi suala la kuoa dada wa mke, sheria za Aya hii hazihusiki na ndoa zilizofafungwa kabla ya kushuka kwa Aya hii. [12] Kwa mujibu wa tafsiri za wanavyuoni kama vile Sheikh Tusi katika Tafsir al-Tibyan na Tabarsi katika Majma' al-Bayan, ni kwamba; kuvuliwa na kutojumuishwa kwa ndoa zilizopita, kunahusiana na ndoa ya Nabii Yakubu (a.s) aliyeoa dada wawili kwa wakati mmoja, ambao ni Raheli na Lia. [13]
Inasemekana kwamba; Kabla ya kuletwa kwa Aya hii, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa wanaume kuoa dada wawili kwa wakati mmoja. Hata hivyo, baada ya kushuka Aya hii, wale waliokuwa na ndoa za namna kama hii walitakiwa kuachana na mmoja wao mara moja ipaswavyo. Ingawa hatua za kisheria hazikuchukuliwa dhidi yao, na watoto walio zaliwa ndani ya ndoa hizo walikubalika kama ni watoto halali. [14]