Nenda kwa yaliyomo

Kisomo cha Ndani ya Sala

Kutoka wikishia

Kisomo cha Ndani ya Sala (Kiarabu: قراءة الصلاة) kinahusiana na kusoma baadhi ya Sura za Qur’ani katika Swala. Nalo ni miongoni mwa vifungu vya wajibu wa kiibada ambavyo si miongoni mwa nguzo kuu za Sala. Ingawa kisomo hichi hakiingii moja kwa moja katika nguzo kuu za Sala, ila ni miongoni mwa sharti za lazima zinazotakiwa kufuatwa na kila mwenye kusimamisha Sala. Kulingana na mafundisho ya Kiislamu, mwenye kusali anatakiwa kusoma Surat Al-Faatiha (Hamdu) pamoja na sura nyingine moja kamili katika rakaa ya kwanza, na kufanya tena hivyo hivyo katika yake ya pili, huku akiruhusiwa ima kusoma Surat Al-Faatiha pekee au Tasbihati Al-Arba’a (Subhanallahi, walhamdulillahi, walaa Ilaaha illa Llahu, wallahu Akbar) katika rakaa ya tatu na ya nne. Usahihi wa kutamka kwa lugha ya Kiarabu, kusoma kwa ufasaha, kufuata mpangilio sahihi katika kusoma Sura, na kuendeleza mtiririko bila kukatiza kwa kuweka pengo kubwa kati ya Aya na Aya au kati ya Sura na Sura, ni miongoni mwa mambo ya wajibu katika utekelezaji (usimamishaji) wa sala. Ni haramu kusema Amin baada ya kusoma Surat Al-Faatiha au kusoma sura zenye Aya za sajda baada ya Surat Al-Faatiha. Aidha, kusoma kwa utulivu, na kuelewa maana ya yale yanayosomwa, pamoja na kusoma Suratu al-Qadri katika rakaa ya kwanza na Surat Ikhlas katika rakaa ya pili, ni miongoni mwa sunna za Sala. Hata hivyo, haipendekezwi (makruhu) kurudia na kuripiti Sura moja mara mbili (isipokuwa Suratu AI-khlas) ndani ya rakaa mbili za Sala. Yaani si vizuri mtu kusoma tena Sura ile ile aliyo isoma katika rakaa ya kwanza, ila Surat Al-ikhlas, yaani ikiwa mtu atasoma Surat Al-Ikhlas katika rakaa ya kwanza basi hakuna tatizo kurudia tena Sura hiyo hiyo katika rakaa yake ya pili.

Nafasi na Dhana ya Kisomo katika Sala

Kisomo cha kusoma Qur’ani katika Sala, ni miongoni mwa wajibu muhimu katika ibada ya Sala. [1] Miongoni masharti ya Sala ni kusoma Surat Al-Faatiha (Hamdu) pamoja na Sura moja kamili katika rakaa ya kwanza na ya pili, huku Surat Al-Faatiha (Hamdu) au Tasbiihati Al-Arba’a (Subhanallahi, walhamdulillahi, walaa Ilaaha illa Llahu, wallahu Akbar), zikisomwa katika rakaa ya tatu na ya nne. [2] Kisomo cha Qu’ani katika Sala ni moja ya mambo ya wajibu katika utekelezaji wa sala, ila sio nguzo miongoni mwa nguzo kuu ya Sala. [3] Hii ina maana kuwa iwapo mtu atakosea au kuacha kusoma Sura katika Sala yake bila ya kukusudia, bado Sala yake haitabatilika na itaendelea kuwa ni sahihi. Hata hivyo, endapo kosa hilo litatokea kwa makusudi, bila shaka Sala hiyo itabatilika. [4] Ila moja miongoni mwa nadharia mbali mbali za kifiq’hi, inadai kuwa; kisomo cha Qur’ani katika Sala ni miongoni mwa nguzo kuu za sala, ila nadharia hii haina nguvu wala haikupewa kipau mbele na wanafiq’hi mbali mbali. [5]

Saahib Al-Jawahar, miongoni mwa wanazuoni wa karne ya 13 Hijria, ameorodhesha na kupambanua tofauti ya maoni zilizopo miongoni mwa wanazuoni kuhusiana na wajibu wa kusoma Sura fulani baada ya Suratu Al-Faatiha (Hamdu) katika Sala. katika maelezo yake anasema kwamba; wanazuoni wa madhehebu ya Kishia wana maoni tofauti kuhusiana na wajibu wa kusoma Suratu fulani baada ya kumaliza Suratu Al-Faatiha (Hamdu) katika Sala. [6] Kulingana na kauli yake, rai maarufu iliyokubaliwa na wengi, ni ile isemayo kwamba; ni wajibu kwa mwenye kusali kusoma Sura moja kamili baada ya kumaliza Suratu Al-Faatiha (Hamdu), [7] isipokuwa pale inapojitokeza dharura fulani katika Sala hiyo, kama vile ufinyu wa muda wa Sala, katika hali ambayo yeye atakuwa hatakuwa na wakati wa kutosha, na kwamba kusoma Sura hiyo kutapelea kumalizika kwa wakati wa Sala. Ila katika Sala za Sunna, mtu naruhusiwa kutosoma Sura baada ya kumaliza Suratu Al-Faatiha (Hamdu). [8] Baadhi ya wanazuoni mashuhuri kama vile Faidh Kashani (aliyefariki mnamo mwaka 1091 Hijria), [9] Muhakik Sabzewari (aliyefariki mwaka 1090 Hijria) [10] na Shubairi Zanjani (aliyezaliwa mnamo mwaka 1306 Hijria ya Shamsia), [11] wanaamini kwamba; ni Mustahabu mtu kusoma Sura nyingine baada ya Surat Al-Faatiha (Hamdu) katika Sala zake.

Mazingatio Lazima (Wajibu) katika Kisomo

Kisomo cha katika Sala ni sharti lenye vipengele maalum ambavyo ni lazima kufuatwa ili kutimiza ibada hii kwa usahihi. Vipengele hivi vinajumuisha mambo yafuatayo:

  • Kusoma kwa Kiarabu Fasaha: Mtu anayesali anatakiwa kusimamisha Sala yake kwa lugha ya Kiarabu na kuhakikisha anatamka herufi zote kwa usahihi, hasa herufi zenye shadda, ili kuwasilisha maana sahihi ya Sala yake.
  • Kufuata Mpangilio na Muwalat ahihi: Ni lazima kuheshimu mpangilio sahihi wa kusoma, ambapo kwanza anatakiwa kutanguliza Suratu Al-Faatiha kabla ya kusomwa Sura nyingine. Pia, lazima kuwepo mwendelezo kati ya Aya za kila Sura bila ya kupoteza mtiririko wa usomaji, wala kujenga pengo kuwbwa baina yake.
  • Kusoma kwa Kudhihirisha Sauti (Kwa Wanaume): Wanaume wanatakiwa kusoma kwa sauti ya kubwa katika rakaa mbili za mwanzo za baadhi ya Sala zao, nazo ni: Sala ya alfajiri, rakaa mbili za mwanzo za Sala ya Magharibi na rakaa mbili za mwanzo za Sala ya Isha.
  • Kusali kwa Sauti ya chini (Kwa Wanaume): Katika rakaa za Sala ya Adhuhuri na Alasiri, pamoja na rakaa ya tatu na ya nne katika Sala ya Magharibi na Isha, wanaume wanatakiwa kusali sala zao bila ya kupaza sauti, kama sehemu ya adabu za Sala na utekelezaji wake sahihi.

Mambo Yanayokatazwa (Haramu) Katika Kisomo cha Swala

Yafuatayo ni baadhi ya mambo haramu yaliyokatazwa katika kisomo cha Sala: [13]

  • Kusema Ameen baada ya kumaliza Surat Al-Faatiha.
  • Kusoma Sura refu ambayo inaweza kusababisha kukiuka muda wa Sala.
  • Kusoma moja ya sura zenye sajda ya lazima, ambazo ni: An-Najm, Fussilat, As-Sajda na Al-Alaq, katika Sala za faradhi.
  • Kusoma zaidi ya sura moja baada ya kumaliza Surat Al-Faatiha. Katika suala hili, kuna pea za fulani zinazohisabiwa kama ni Sura moja, nazo ni; Surat Ad-Duha na Al-Inshirah na Surat Al-Fil na Quraish, Sura hizi husomwa kwa pamoja, kutoka na nadharia isemayo kwaba; kila pea (pair) ya Sura hizi ni sawa na Sura moja. [14]Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa kusoma zaidi ya Sura moja sio haramu, bali ni tendo la makuruhu (halipendezi) tu. [15]

Mambo Yanayopendekezwa Katika Kisomo cha Swala

Yafuatayo ni baadhi ya matendo yanayopendekezwa ili kuboresha kisomo cha Sala na kuimarisha ibada kwa namna iliyo bora zaidi: [16]

  • Kusoma kwa Utaratibu na kwa Kuzingatia Maana: Inapendekezwa kusoma Sura na tasbihi kwa utulivu na umakini, huku mtu akifahamu na kuelewa maana ya maneno anayoyasema ili kuleta unyenyekevu wa kweli katika ibada yake.
  • Kuanza kwa Ibra ya Kutafuta Kinga ya Mwenye Ezi Mungu: Inapendekezwa kusema kwa sauti ya chini «A’udhu billahi minash-Shaytanir-rajim» kabla ya kuanza kusoma Suratu Al-Faatiha katika rakaa ya kwanza, hii ni kwa nia ya kutafuta kinga dhidi ya ushawishi wa Shetani.
  • Kusoma «Bismillahir-Rahmanir-Rahim» kwa Sauti ya Juu: Inapendekezwa kwa wanaume kupaza sauti wakati wa kusoma "Bismillahir-Rahmanir-Rahim» kabla ya kuanza kusoma Suratu Al-Faatiha na Sura nyingine katika Sala za Adhuhuri na Alasiri.
  • Kusema «Alhamdulillahi Rabbil-‘Alamin» Baada ya Suratu Al-faatiha: Inapendekezwa kusema Alhamdulillahi Rabbil-‘Alamin Baada ya kumaliza kusoma Suratu Al-Faatiha, ili kuonyesha shukrani na kumtukuza Mwenye Ezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
  • Kusema «Kadhalika Allahu Rabbi» baada ya Suratu AI-khlas: Inapendekezwa kusema Kadha lika Allahu Rabbi, baada ya kumaliza Suratu al-Ikhlas (Surat Al-Tawhid), kwa maana ya kuthibitisha ukuu na uweza wa Mwenye Ezi Mungu.
  • Kusema «Astaghfirullaha Rabbi wa atubu ilaih» baada ya Tasbihi Nne: Inapendekezwa kusema mtu kusema Astaghfirullaha Rabbi wa atubu ilaih, Baada ya kumaliza kusoma tasbihi nne katika rakaa ya tatu na ya nne ambazo ni; “Subhanallahi, walhamdulillahi, walaa Ilaaha illa Llahu, wallahu Akbar”, zenye maana ya kuomba msamaha na kurejea kwa Mwenye Ezi Mungu.
  • Kusoma Sura Maalumu katika Rakaa ya Kwanza na Pili: Inapendekezwa kusoma Suratu al-Qadri (Innaa Anzalnaahu), katika rakaa ya kwanza na Surat Al-Ikhlas katika rakaa ya pili ya kila Sala, kwa lengo la kuongeza mafanikio ya ibada hiyo.

Mambo Yanayochukiza (Makruhu) Katika Kisomo cha Ndani ya Swala

Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayohisabiwa kuwa ni makuruhu (yanayochukiza) katika kisomo cha ndani ya Sala, ingawa hayabatilishi Sala, ila mambo haya yanaweza kupunguza thamani na unyenyekevu katika ibada hii:

  • Kutosoma Suratu Al-Ikhlas: Ni makruhu mtu kuacha kusoma Suratu Al-Ikhlas katika Sala zote za siku nzima, kwani Sura hii ina umuhimu maalum katika kuimarisha imani ya Tawhid (upweshaji wa Mwenye Ezi Mungu).
  • Kusoma Al-Ikhlas kwa Pumzi Moja: Ni jambo linalochukiza mtu kusoma Suratu Al-Ikhlas kwa pumzi moja, bila kupumua kwenye kila kituo cha Aya zake. Na ni vyema mtu kusoma Sura hii kwa utulivu na mapumziko ili kuheshimu Aya zake zenye maana nzito katika masuala ya imani.
  • Kurudia Sura Moja katika Rakaa Mbili: Inachukiza mtu kurudia Sura moja katika rakaa mbili za Sala za sala moja, isipokuwa Sura ya Al-Ikhlas ambayo hakuna umarufuku wala ubaya wowote ule katika kurudia kwake. Hii ni kwa sababu ya uzito wa maneno yake yaliobeba na maana nzito ndani yake.
  • Kuacha Sura na Kuanzisha Sura Nyingine: Inachukiza mtu kusoma Sura fulani kisha kuacha Sura hiyo na badala yake kuanzisha Sura nyengine, kabla ya kukamilika kwa nusu ya Sura ya kwanza, [18] isipokuwa Surat Al-Ikhlas na Al-Kafirun, ambazo ni marufuku mtu kuachana nazo na kuanzisha Sura nyengine baada ya kuzianzisha Sura hizo. [19]

Haya ni miongoni mwa mambo yanayochukiza, lakini hayaathiri uhalali wa Sala. Ila yameorodheshwa ili kusaidia wenye kuswali kuimarisha ubora wa kisomo na kuepuka makosa yanayoweza kupunguza thamani ya ibada hii muhimu.

Rejea

Vyanzo