Azaim al-Sujud

Kutoka wikishia

Ayaat al-Sujuud (Kiarabu: آيات السجدة) au Azaim al-Sujuud (Kiarabu: عزائم السجود) inaashiria sura zenye sijda ya wajibu ambazo ni surat Sajda, Fussilat, Najm na Alaq. Sura hizi zina Aya mbazo kama mtu akisikia inasomwa basi ana wajibu wa kusujudu. Sura hizi kadhalika zina hukumu zake maalumu. Ni haramu kwa mtu mwenye janaba au mwanamke mwenye hedhi kusoma sura hizi. Aidha haipaswi kusoma sura hizi katika Swala za wajibu.

Kuna dhikri na dua maalumu zilizonukuliwa kwa ajili ya sijda za wajibu katika Qur'ani. Hata hivyo ili kusujudu sijda ya wajibu haihitajii mtu kuwa na udhu, kufanya ghusli (kwa mwenye janaba na kadhalika) na kuelekea kibla, kama ambavyo sio lazima kusoma dhikri na nyuradi maalumu. Hata hivyo wakati wa kutekeleza sijda ya wajibu ya kusoma au kusikia moja kati ya Aya zenye sijda ya wajibu ni wajibu na lazima kusujudu juu ya kitu ambacho kinajuzu na kusihi kusujudu juu yake.

Kuitwa kwa jina hilo

Azaim au Azaim al-Sujud zinaitwa sura nne za Qur’ani za Sajda, Fussilat, Najm na Alaq ambazo kimsingi ndani yake zina sijda za wajibu. [1] Sura hizi nne zinatambulika pia kwa jina la Sura za Azaim (Sura Zenye Sijda ya Wajibu). Katika baadhi ya vyanzo imetajwa surat al-Luqman kuwa miongoni mwa Sura za Azaim badala ya Fussilat. [2] Azaim ni wingi wa azm ambayo kilugha ina maana ya azma na irada thabiti ya kutenda jambo. [3] Vilevile ina maana ya faradhi ambazo Mwenyezi Mungu ameziwajibisha; [4] na kwa muktadha huo sura zilizotangulia kutajwa ambazo ndani yake kuna Aya za sijda za wajibu zinajulikana kwa jina la Azaim. [5]

Aya zenye sijda

Kwa mujibu wa wanazuoni wa fikihi wa madhehebu ya Kishia, Aya ya 15 ya Surat as-Sajdah, Aya ya 37 katika Surat Fussilat, Aya ya 62 katika Surat al-Najm na Aya ya 19 katika Surat al-Alaq zina sijda ya wajibu. [6] Vilevile kwa mujibu wa Muhammad Hassan Sharif Isfahani mashuhuri kwa lakabu ya Sahib al-Jawahir ni kwamba, kuna Aya 11 katika sura 10 ambapo kuna sijda ya mustahabu. [7] Aya hizo ni ya 206 katika Surat al-Aaraf, ya 15 katika Surat Raad, Aya ya 49-50 za Surat al-Nahl, Aya ya 109 ya Surat al-Israai, Aya ya 58 ya Surat Maryam, Aya za 18 na 77 za Surat al-Hajj, Aya ya 60 ya Surat al-Furqan, Aya ya 26 ya Surat al-Naml, Aya ya 24 katika Surat Swaad, na Aya ya 21 katika Surat al-Inshqaq. [8] Kwa mujibu wa kile kinachonasibishwa na Sheikh Swaduq ni kuwa, kuweko neno “sajda” katika Aya, kunapelekea Aya hiyo kuwa na sijda ya mustahabu. [9]

Mafakihi wa Kishia wakitegemea hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq(a.s) wanaamini kuwa, sijda ni wajibu katika sura nne tu zilizotajwa. [10] Wanazuoni wa fikihi wa madhehebu ya Shafi, Hanbali na Hanafi wa Ahlul-Sunna wao hawajatenganisha baina ya sijda ya mustahabu na wajibu katika Qur’ani hivyo wanaamini kuwa, idadi ya Aya zenye sijda ni 14 huku wanazuoni wa fikihi wa Maliki wao wakisema kwamba, idadi ya Aya zenye sijda ni 11. [11]

Dhikri ya sijda ya wajibu ya Qur’ani

Kumenukuliwa dua na dhirki na maalumu ambazo ni bora kuzisoma wakati wa kutekeleza sijda ya wajibu. [12] Ifuatayo dhikri na dua ambayo imependekezwa kusomwa wakati wa kutekeleza sijda ya wajibu ya kusikia au kusoma Aya ya sijda ya wajibu.


لاَ إِلَهَ إِلاَّ اَللَّهُ حَقّاً حَقّاً لاَ إِلَهَ إِلاَّ اَللَّهُ إِيمَاناً وَ تَصْدِيقاً لاَ إِلَهَ إِلاَّ اَللَّهُ عُبُودِيَّةً وَ رِقّاً سَجَدْتُ لَكَ يَا رَبِّ تَعَبُّداً وَ رِقّاً لاَ مُسْتَنْكِفاً وَ لاَ مُسْتَكْبِراً بَلْ أَنَا عَبْدٌ ذَلِيلٌ خَائِفٌ مُسْتَجِيرٌ


Hukumu zake

Sura za Azaim au sura zenye sijda za wajibu na hukumu zinazohusiana nazo zimebainishwa katika milango ya tohara [13] na Swala [14] kwenye vitabu vya fikihi. Kwa mtazamo wa wanazuoni wa fikihi sura hizi zina hukumu zake kama:

  • Ni haramu kwa mtu mwenye janaba [15] na mwanamke mwenye hedhi [16] kusoma sura hizi. Wanazuoni wa elimu ya fikihi wamehitalifiana kuhusiana na je kusoma Aya zenye sijda ndio haramu au kusoma sura yote kamili.[17] Allama Hilli amesema, ni haramu kwa mtu mwenye janaba na mwanamke mwenye hedhi kusoma hata herufi moja ya Aya hizi za sijda. [18]. Hata hivyo, mwenye janaba au hedhi akisikia moja ya Aya zenye sijda ya wajibu inasomwa ni wajibu kwake kusujudu. [19]
  • Kwa mujibu wa fatuwa za mafakihi wa Kishia ni kwamba, kusoma kwa makusudi sura zenye sijda ya wajibu katika Swala za wajibu, kunapelekea Swala kubatilika. [20] Endapo mtu atasoma katika Swala moja ya sura hizi kwa kusahau ikiwa atakumbuka kabla ya kufikia Aya ya sijda au akafahamu hili akiwa katikati ya sura, anapaswa kuiacha sura hiyo na kusoma sura nyingine (isiyokuwa na sijda ya wajibu); na ikiwa atakumbuka hilo baada ya kupita katika Aya yenye sijda au baada ya kuwa ameshasoma zaidi ya nusu ya sura kuna hitilafui za kimitazamo baina ya Marajii kuhusiana na namna ya kutekeleza sijda hiyo na jinsi ya kuendelea na Swala yake. [21] Kwa mujibu wa fatuwa ya Imamu Khomeini (r.a) ni kwamba, katika hali hii anapaswa kutekeleza sijda kwa ishara na kutosheka na kusoma sura yenye sijda. [22] Kadhalika kwa mujibu wa fatuwa ya Ayatullah Sayyied Ali Sistani na Sayyied Moussa Shubairi Zanjani ni kuwa, kama hatoleta sijda ya wajibu Swala yake ni sahihi ingawa anakuwa ametenda dhambi. [23]
  • Kusujudu sijda ya wajibu ya Qur’an wajibu wake ni wa haraka na hapo hapo; kwa msingi huo kwa kusoma na kusikia Aya miongoni mwa Aya katika sura za Azaim (zenye sijda ya wajibu), hapo hapo huwa wajibu kusujudu sijda ya wajibu. [24]
  • Katika kusujudu sijda ya wajibu ya Qur’an, sio wajibu kuwa na udhu, kuoga josho (kwa mwenye janaba na kadhalika), kuelekea kibla na kusoma dua na dhikri maalumu. Hata hivyo ni wajibu kuweka paji la uso na kusujudu juu ya kitu ambacho inasihi kusujudu juu yake kama turba na kadhalika. [25]. Pamoja na hayo kumenukuliwa dhikri na dua maalumu ambazo ni bora kuzisoma wakati wa kutekeleza sijda ya wajibu. [26]