Suratu al-Kafirun

Kutoka wikishia

Surat al-Kafirun ni Sura ya 109 katika mpangilio wa msahafu. Sura hii ni katika sura zilizoshuka Makka na ipo katika juzuu ya 30 ya Qura’n tukufu. Sababu ya kuitwa sura hii kwa jina la Kafirun ni kutokana na kuzungumzia kwake makafiri. Mwenyezi Mungu katika Sura hii anamuagiza na kumpa amri Mtume (saww) atangaze wazi kujibari na kujiweka mbali na kuabudu masanamu na awaambie kwamba, hawezi kufuata dini yao na kwamba, katu hatakubaliana nao na wala hatofanya nao mapatano. Inaelezwa kwamba, sura hii ilishuka wakati kundi la makafiri lilipopendekeza kwamba, muda fulani makafiri wawe katika dini ya Mtume (saww) na Mtume naye kipindi fulani awe mfuasi wa dini yao na hivyo aabudu masanamu. Kwa maana kwamba, wapokezane kila mmoja kufuata dini ya mwenzake. Kumenukuliwa hadithi na riwaya mbalimbali kuhusiana na fadhila za kusoma sura hii kwamba, endapo mtu atasoma sura hii kabla ya kulala, basi huwa ni kinga na kama itasomwa katika Sala za wajibu, hupelekea msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye kuisoma, kwa baba, mama na wanawe.

Utambulisho

Kupewa jina

Sura hii inaitwa al-Kafirun; kwa sababu imeshuka kuhusiana na makafiri na inaanza kwa kuwahutubu makafiri. Kumebainishwa pia majina mengine kuhusiana na sura hii ambapo miongoni mwa majina hayo: Ibada na Jahd. Kuitwa sura hii kwa jina la ibada sababu yake ni kwamba, neno ibada na mnyambuliko wake yametumika sana katika sura hii na Jahd ni kwa maana ya kukataa na kukana, na hili limetumika kutokana na kuwa, Surat al-Kafirun inazungumzia watu ambao wanaikana dini ya Mwenyezi Mungu. [1]

Mpangilio na mahali iliposhuka

Surat al-Kafirun ni katika sura za Makki (zilizoshuka Makka) na katika mpangilio wa kushuka ni sura ya 18 iliyoshushwa kwa Mtume Muhammad (saww). Katika mpangilio wa sasa kwenye msahafu sura hii ni ya 109. [2] na ipo katika juzuu ya 30 ya Qur’ani Tukufu. Mwandishi wa Tafsir al-Mizan anasema, kuna hitilafu kuhusiana na kwamba, sura hii ni Makki au Madani (imeshuka Makka au Madina) lakini anaamini kwamba, kwa mujibu wa siyaq na na nidhamu inayotawala kwake ni dhahiri kwamba, sura hii imeshuka Makka. [3]

Idadi ya Aya zake na sifa nyingine maalumu

Surat al-Kafirun ina Aya 6, maneno 27 na herufi 99. Sura hii ni miongoni mwa sura fupi za Qur’ani na ni katika sura zinazojulikana kama mufassalat (sura zenye Aya fupi). Surat al-Kafirun ni moja kati ya sura nne ambazo zinaanza na Qul (sema). [4]

Maudhui

Mwenyezi Mungu katika Sura hii ya al-Kafirun anamtaka na kumuagiza Mtume wake atangaze kujibari na kujiweka mbali na ibada ya masanamu na atangaze hilo wazi na aeleze kwamba, makafiri nao hawako tayari kuikubali dini yake; hivyo basi si dini ya Muhammad ambayo wao wataifuata na kuifanya kuwa dira yao ya maisha na wala dini yao ya kuabudu masanamanu haiwezi kumvuta Muhammad na kumfanya aifuate; kwa msingi huo makafiri wanapaswa kukata tamaa na kusahau kabisa kwamba, Mtume atafanya mapatano nao. [5]


Maudhui ya Surat al-Kafirun [6]

Kuweko tofauti baina ya sheria zilizoletwa na Mtume na itikadi makafiri

Utangulizi: Aya ya 1; jukumu la Mtume kwa ajili ya kujibari na kujitenga na makafiri.

Maudhui ya kwanza: Aya ya 2-5; tofauti ya muabudiwa wa Mtume na makafiri.

Nukta ya kwanza: Aya ya 2-3; hakuna wakati ambao muabudiwa wa Mtume na makafiri atakuwa mmoja.

Nukta ya pili: Aya ya 4-5: Huko nyuma pia hakuna wakati ambao muabudiwa wa Mtume na makafiri alikuwa mmoja.


Maudhui ya Pili: Aya ya 6; kuweko tofauti baina ya sheria zilizoletwa na Mtume na itikadi makafiri

Nukta ya kwanza: Makafiri wanafuata itikadi na dini ambayo wameianzisha wao wenyewe.

Nukta ya pili: Aya ya 6; Mtume anafuata dini na sharia ya Mwenyezi Mungu.

Sababu ya kushuka

Wafasiri wa Qur’ani (akiwemo Tabari, Tusi, Zamakhshari, Tabarsi na Abul-Futuh) ameandika kuhusiana na sababu ya kushuka sura hii ya kwamba, kundi la watu miongoni mwa wakubwa wa Qureshi ambao walikuwa viongozi wa ukafiri na upotofu wakiwemo Walid bin Mughira, Aas bin Wail, Umayya bin Khalf, Aswad bin Abd al-Muttalib na Harith bin Qays walikwenda kwa Mtume na kutoa pendekezo la mapatano baina ya pande mbili yaani baina yao na Mtume. Na Walikuwa wakisema, kipindi fulani wewe Mtume (kwa mfano mwaka mmoja) uwe katika dini yetu na uabudu tunachokiabudu na uabudu waungu wetu na masanamu yetu na kipindi fulani (mwaka mmoja mwingine) sisi tujiunge na dini yako na tumuabudu Mungu wako. Mtume (saww) alipinga vikali kabisa pendekezo hilo na ndipo ikashuka sura hii. [7]

Aya ya sita na ufahamu usio sahihi kwayo

Kuhusiana na tafsiri ya Aya ya 6 katika Surat al-Kafirun inayosema:

“Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu”, Allama Tabatabai anasema: Yumkini hapa ikawapitikia watu akilini na katika fikra zao ya kwamba, watu wana hiari na uhuru kamili katika kuchagua dini. Kwa maana kwamba, wamepewa uhuru wa kuchagua dini waitakayo; kwa maana kwamba, mtu anaweza kuichagua shirki au ikampitia mtu kwamba, Aya hii inataka kumuamrisha Mtume kwamba, asishughulishwe na dini ya makafiri kwa maana kwamba, awaache kama walivyo na asishughulishwe nao; hata hivyo uwelewa huu sio sahihi; bali Aya inataka kusema, Mtume katu hawezi kujiunga na kuelekea katika dini yao na wao pia hakuna wakati ambao wataitikia mwito wa haki. [8] Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai katika muendelezo anaandika: Baadhi ya wafasiri ili kuondoa ufahamu huu usio sahihi wamesema kuwa, neno dini lililokuja katika Sura hii maana yake ni ujira na malipo; yaani ujira na malipo yangu ni ya kwangu na malipo yenu ni kwa ajili yenu. [9]

Fadhila zake

Makala asili: fadhila za sura

Kuhusiana na fadhila za kusoma sura hii inaelezwa kwamba, Bwana mmoja alimwambia Bwana Mtume ya kwamba, nifundishe kitu ambacho nitakisema wakati wa kulala. Mtume akamwambia, kila unapotaka kulala, soma Surat al-Kafurun na kisha ulale, kwani hii ni kinga ya shirki. [10] Kadhalika Imam Sadiq (as) amenukuliwa akisema kuwa, thawabu za kusoma sura hii ni sawa na kusoma robo ya Qur’an yote. Kila ambaye atasoma Surat al-Kafirun na Ikhlas katika Sala zake za wajibu, Mwenyezi Mungu humsamehe yeye, baba, mama na watoto wake pia. [11] Aidha amesema: Katika rakaa mbili za Sala ya Alfajiri soma sura yoyote uitakayo, lakini mimi napenda kusoma Surat Ikhlas (Qul-huwallah) na Surat al-Kafirun. [12] Aidha imeusiwa kusoma Surat al-Kafirun katika nafila ya Magharibi. [13] Imekuja katika hadithi mbalimbali ya kwamba, sura hii ina baadhi ya sifa maalumu kama vile: Shetani kuwa mbali na mtu anayesoma sura hii, [14], kujibiwa dua kama mtu ataisoma mara 10 wakati wa kuchomoza jua, [15] au kumuona Mtume usingizini, soma mara 100 usiku wa kumkia Ijumaa. [16]


Hukumu ya Kifiq’h

Kwa mujibu wa fat’wa za mafuqaha wa Kishia, kama mtu anayeswali baada ya kusoma Surat al-Fatiha, akawa ameanza kusoma Surat al-Kafirun au Qul-Huwallah, hawezi kukatisha na kusoma sura nyingine; lakini katika sura nyingine kama mtu hajafika nusu ya sura anaweza kuikatisha na kusoma sura nyingine. [17]

Surat al-Kafirun na tarjuma yake

بسم الله الرحمن الرحيم

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ

لا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ

وَلا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُد

وَلا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ

وَلا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ

لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِين


Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Sema: Enyi makafiri!

Siabudu mnacho kiabudu

Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu

Wala sitaabudu mnacho abudu

Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu.

Nyinyi mna dini yenu, nami nina dini yangu