Injili

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Injili (Gospel))
Mistari ya kwanza ya Injili ya Mathayo, katika hati ya karne ya 14 A.D. Mojawapo ya hati za kale zaidi za Biblia katika lugha ya Kiajemi

Injili (Kingereza: Gospel na Kiarabu: الإنجيل)‎ Kulingana na mafundisho ya Kiislamu, Injili ambayo kwa Kiingereza ni Gospel: Ni jina la kitabu kitakatifu ‎alichoteremshiwa Nabii Isa (a.s) kutoka kwa Mola wake. Imeelezwa wazi kabisa katika Aya za Qur'an ya ‎kwamba; Injili ni ufunuo utokao kwa Mungu, ambao ndani yake mlikuwa na bishara za wazi kuhusisana ‎na kuja kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na kusisitiza juu ya utume wa Nabii Isa (a.s), huku ‎ikikanusha dhana ya Utatu na Uungu wa Isa (a.s).‎ Kwa mujibu wa maelezo ya Ayatullah Makarem Shirazi, ni kwamba; kitabu kitakatifu cha Isa (a.s) ‎kitokacho mbinguni kimepotea, ila kuna baadhi ya sehemu zilizochanganyika na imani potofu, ambazo ‎zianweza kupatikana katika Injili nyingine mbali mbali.‎

Baadhi ya watafiti wa Kiislamu kama vile Ayatullah Ma'arifat, hawakubaliani na wazo la kwamba Injili ni ‎kitabu kitakatifu alichoteremshiwa Isa (a.s). Ila wao wanaamini kwamba; Kile kilichoteremshwa kwa ‎Nabii Isa (a.s), kilikuwa ni mafundisho na bishara za maelezo ya mdomo kutoka kwa Mola wake, ‎ambazo baadae zilitolewa na kuandikwa mitume wake kisha kukusanywa kwa jina maarufu la Injili.‎

Kwa mujibu wa maoni ya Wakristo, Isa (a.s) hakuwahi kuleta kitabu kinachoitwa Injili. Katika mtazamo ‎wao, Isa (a.s) mwenye ni ufunuo (dhihiriko la ufunuo) wa Mungu na kwamba yeye ni sawa na ujumbe ‎halisi wa Mungu wenyewe, na si kwamba yeye ni mleta wa ujumbe huo. Katika utamaduni na desturi ‎za Kikristo, Injili inahusiana na sehemu fulani tu ya Biblia ya Kikristo, ambayo ndani yake inajumuisha ‎vitabu vinne vya Injili ambavo ni: Injili ya Mathayo, Injili ya Marko, Injili ya Luka, na Injili ya Yohana. ‎Injili nne hizi, ambazo ni vitabu vinne vya mwanzo vya Agano Jipya, viliandikwa na wanafunzi au ‎wanafunzi wa wafuasi (wanafunzi) wa Nabii Isa (a.s) na vinahusiana na maisha na mafundisho ya Nabii ‎Isa (a.s).‎

Bila shaka kuna Injili mbali mbali zilizowahi kuandikwa duniani humu, ila Wakristo, wanakubali na Injili ‎nne tu wanazo ziamini na kuzitambua rasmi kisheria. Injili za Mathayo, Marko, na Luka zinajulikana ‎kama Injili zinazo fanana (Synoptic Gospels), hii ni kwa sababu ya kufanana kwao sana kilugha na ‎kimuktadha. Suala la Uungu wa Yesu (Isa (a.s)), pamoja na madai ya kwamba yeye ni mwana wa ‎Mungu ni itikadi mbili zinazopatikana katika Injili ya Yohana peke yake.‎

Injili ya Barnaba ni moja ya Injili zisizo rasmi ambayo imepata umaarufu miongoni mwa Waislamu, lakini ‎Wakristo wanaiita ni Injili bandia. Injili hii inakanusha Uungu wa Isa na kwamba yeye mwana wa ‎Mungu. Pia Injili hii inakanusha suala la kusulubiwa kwa Nabii Isa (a.s), na inatoa bishara kuhusiana na ‎ujio wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).‎

Baadhi ya changamoto zilizotolewa dhidi ya Injili ni pamoja na: ‎

  • Kutoaminika kwa waandishi wa Injili hiyo, hii ni kutokana na wao kutokuwa na kinga dhidi ya kutenda ‎makosa ua dhambi.‎
  • Uwepo wa migongano, makosa, na imani potofu ndani ya Injili hizo.‎

Kitabu Kitakatifu cha Nabii Isa (a.s)‎

Kulingana na Aya za Qur'ani [1] na Hadithi za Kiislamu, [2] Injili ndio jina la kitabu kitakatifu ‎alichoteremshiwa Nabii Isa (a.s), kitabu ambacho aliteremshiwa kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu (s.w). ‎‎[3] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba kuna Hadithi nyingi mno kuhusiana na kitabu hichi, jambo ‎ambalo laweza mpa mtu uhakika na yakini ya kwamba; kuna uhakika wa kuwepo kwa kitabu kitakatifu ‎kinachoitwa Injili. [4] Kwa mujibu wa maoni ya Ayatullah Makarem Shirazi, mfasiri wa Qur;ani wa ‎Mashehebu ya Shia, ni kwamba; kitabu kitakatifu cha Nabii Isa (a.s) kimepotea, na wanafunzi wa Isa ‎‎(a.s) walinukuu tu baadhi ya sehemu za maandiko ya kitabu hicho katika Injili zao, ambazo ‎zimechanganyika na imani potofu ndani yake. [5]‎

Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti wa elimu ya Qur'ani, akiwemo Muhammad Hadi Ma'arifati, kinyume ‎na imani ya kawaida ya Waislamu kuhusianana na Injili, wao wanaamini kwamba; Injili si kitabu ‎kilichokusanywa kupitia mafunzo aliyo teremshiwa Nabii Isa (a.s) kutoka kwa Mola wake. [6] Kwa ‎maoni ya Ayatullah Ma'arifati, kile alichoteremshiwa Nabii Isa (a.s), kilikuwa ni mafundisho na bishara ‎za maelezo ya mdomo ambayo aliwafundisha watu pamoja na mitume wake wakati wa kipindi cha ‎utume wake. Mitume hao walihifadhi mafundisho hayo na kuyawasilisha kwa vizazi vya baadae hadi ‎yalipokusanywa katika kitabu maarufu kilichoitwa Injili. [7]‎

‎Watafiti hawa wanaona kwamba; Kile kitabu kilicho ashiriwa na Qur'ani kuwa amepewa Nabii Isa (a.s), ‎si kitabu kama vilivyo vitabu vyengine, bali ni aina ya ufunuo na hukumu za kisheria. [8] Wakisisitiza ‎msamamo wao huo, wao wanadai kwamba; Qur'an katika Aya yoyote ile haijawahi kutaja Injili kama ‎kitabu maalumu kwa Nabii Isa (a.s), bali inataja Injili kama ni mkusanyiko wa ufunuo ulioteremshwa ‎kwake. [9] Pia wanasema kuwa Qur'ani ilitumia jina "Injili" ikiarifisha vitabu ambavyo vilijumuisha ‎mafundisho ya lugha ya mdomo yaliyoteremshwa kwa Nabii Isa (a.s). [19]‎ Kwa maoni yao, Injili inajumuisha mafundisho na bishara zilizotolewa kwa lugha ya ya mdomo. ‎Mafundisha ambayo Nabii Isa (a.s) aliwafundisha wafuasi wake, kisha mafundisho hayo baadae yakaja ‎kukusanywa na kuwekwa katika vitabu vinavyojulikana kama Injili. [10]‎

Wasifu wa Injili katika Qur'ani na Hadithi

Neno Injili Katika Aya za Qur'ani, limetumika mara 12 [11] kwa mfumo wa umoja, [12] ambapo ‎imekanushwa uwepo wa Injili nyingi zaidi ya moja. [13] Aya hizi za Qur’ni zinasisistiza ya kwamba; Injili ‎ni wahyi na kuyakinisha wa ukweli wa Taurati. Pia Aya hizo zaeleza ya kwamba; Injili ni shahidi aliye ‎bashiria kuja kwa Nabii Muhammad (s.a.w.w) na kuenea kwa wito wake ulimwenguni. [14] Kulingana ‎na Aya 46 ya Suratu Al-Ma'ida, Injili imebeba ndani yake «uongozi», «nuru», na ni «mawaidha» kwa ‎wacha-Mungu. [15] Pia, katika baadhi ya Aya kama vile Aya 171 ya Surat An-Nisa, imesisitizwa ya ‎kwamba; Isa (a.s) alikuwa mwanadamu na nabii, na kwamba mafundisho ya Utatu na Uungu wa Isa ‎‎(a.s) si miongoni mwa mafundisho sahihi. [16]‎

Kulingana na Hadithi zitokazo kwa Imamu Swadiq (a.s), ni kwamba; Injili iliteremshwa kwa Nabii Isa (a.s) ‎ndani ya usiku wa 12 [17] au 13 wa mwezi wa Ramadhani. [18] Inasemekana kuwa; Injili iliteremshwa ‎mara moja tu yote kwa jumla, yaani haikuwa ikiteremka Aya kwa Aya au Sura baada ya Sura. Kulingana ‎na Hadithi nyingi, Injili pamoja na vitabu vyengine vya mbinguni vipo mikononi mwa Maimamu wa Kishia. ‎‎[19]‎

Injili kwa Mtazamo wa Wanazuoni wa Kiislamu

Wanazuoni wa Kiislamu wamekuwa na mitazamo miwili tofauti kuhusiana na Injili zilizopo:‎

  • Mtazamo wa kwanza unasema kwamba: Sehemu nyingi za Injili ya asili ziliondolewa na waandishi wa ‎baadaye wa Injili na Hadithi za kubuniwa ziliongezwa kitabuni humo. ‎
  • Mtazamo wa pili unasema: Injili ya asili ilitupiliwa mbali na kusahauliwa kabisa, na badala yake, vitabu ‎vingine vikaandikwa na kushika nafasi yake. [20]‎

Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba; Yaliyomo katika Hadithi za Shia kuhusu muqtadha wa Injili ‎yanafanana na yaliyomo katika Injili nne za (Mathayo, Marko, Luka, na Yohana). Jambo ambalo ‎linaonyesha kuwa; Injili zilizopo hivi sasa zinawiana sana na ile Injili iliotajwa na Maimamu (a.s) au ‎masahaba wao, na pia ina mfanano na baadhi ya maandiko ya Injili yalio nukuliwa kutoka kwao. [21] ‎Baadhi ya mambo yafananayo ni: Kupinga suala la kupeleleza watu, kulaumu wenye kujionesha, kuwaepuka ‎waongo, kutanguliza haki za binadamu mbele ya haki za Mungu, kuwajibika (kuhukumiwa) Siku ya ‎Kiyama, pamoja na kuhimiza uvumilivu. [22]‎

Injili kwa Mtazamo wa Wakristo

Katika Ukristo, «Injili ya Mitume» ni nakala ya zamani kabisa ya Injili zilizopo duniani, nayo ni nakala ‎iliyoandikwa kwa lugha ya Kisiria ya kale (Syriac) juu ya ngozi ya samaki. Injili ya Mitume inahifadhiwa ‎katika Maktaba Kuu ya Tabriz nchini Iran. [23] Katika Ukristo Injili inarejelea kila moja ya vitabu vinne ‎vya kwanza vya Agano Jipya [Maelezo 1] ambavyo ni: Mathayo, Marko, [Maelezo 2] ‎Luka, na Yohana. [24] Katika vitabu vya historia ya dini, hasa Ukristo, Injili inarejelea vitabu ‎vilivyoandikwa katika karne za mwanzoni mwa Ukristo kwa ajili ya kurekodi maneno na matendo ya ‎Yesu (a.s). [25]‎

Kwa mtazamo wa Wakristo, Isa (a.s) hakuwahi kuleta kitabu kiitwacho Injili. Kwa mtazamo wao, ‎imani ya kuletwa kwa ufunuo kama vile wanavyo amini Waislamu kuhusiana na Qur'ani na bwana ‎Mtume (s.a.w.w), ni suala lisilo na nafsi yoyote ile katika dini ya Ukristo. Wakristo wanamchukulia Yesu ‎‎(a.s) kama ni kiini cha ufunuo na kwamba yeye mwenyewe ndiye ujumbe wa Mungu, na siyo kwamba ‎yeye ni mleta ufunuo tu, bali yeye ndiye ufunuo halisi. [26]‎ Wakristo wanaamini kwamba; Injili nne zatoa tu wasifu wa maisha na nyeyendo za Isa (a.s) pamoja na ‎kutoa ufafanuzi wa maneno yake (a.s). Hii ni tofauti na Wayahudi ambao wanaamini kuwa Taurati ‎iliteremshwa moja kwa moja kutoka kwa Mungu, kwa maana ya kwamba; kila kilichomo ndani yake ‎kinahisishwa moja kwa moja na Mwenye Ezi Mungu mwenyewe. [27]‎

Wakristo na Injili Nne

Wakristo wanaamini na kukubaliani na Injili nne ambazo ni Mathayo, Marko, Luka, na Yohana, pia ‎wanazihiusabu kuwa ni sahihi; kwani Wakristo wa mwanzo waliziona Injili hizo kuwa maandiko ‎yatkanayo na Mwenye Ezi Mungu. [28] Kwa mujibu wa maelezo ya Thomas Michel, ambaye ni kasisi na ‎mwanatheolojia wa Kikristo (aliyezaliwa 1941), ni kwamba; Wakristo hawaoni aina yoyote ile ‎mgongano kati ya yaliyomo kwenye Injili nne, na wanaziona zote nne kuwa ni zenye kiwango sawa ‎umuhimu na uaminifu. [29] Kwao, kuacha mojawapo ya Injili hizi ni jambo linalo pelekea udhaifu na ‎upungufu wa imani. [30] Katika utangulizi wa Agano Jipya, imeelezwa ya kwamba Wakristo takriban ‎kuanzia mwaka wa 150 BK, walikuwa wakisoma sehemu za Injili nne katika mikutano yao ya Jumapili ‎kanisani, na walikuwa wakiziona kuwa ni maandiko yaliyo rithiwa kutoka kwa Mitume, nao walizipa ‎thamani na mamlaka sawa na vitabu vitakatifu vya mbinguni. [31] Yaani mafundisho yalihisabiwa kuwa ‎ni miongozo ya kisheria kutoka kwa Mungu.‎

Welewa wa Dhana ya Injili

Kiasilia Neno «Injili» lina asili ya Kigiriki likimaanisha habari njema au tangazo au ilani maalumu, [32] ilani ‎ambayo ni bishara njema ya kuja kwa Ufalme wa Mbinguni au kuja kwa Agano Jipya. [33] Hivyo basi ‎kule Injili nne kuwa na ujumbe wa habari njema kuhusu Ufalme wa Mungu au Agano Jipya ndiko ‎kuliko pelekea ziitwe jina la Injili. [34]‎ Imeelezwa kuwa mwanzoni habari njema hii (Injili) ilikuwa ikimaanisha kuja kwa Yesu (a.s) na ‎kulikoshikamana na msamaha na kuja kwa Ufalme wa Mungu. Hata hivyo, katika enzi ya Mitume ‎‎(wanafunzi wa Yesu), ambapo Injili ziliandikwa, Injili na bishara njema hii ilimaanisha tangazo la ‎kudhihiri kwa Mwana wa Mungu na ufufuo wake. [35]‎

Mchakato wa Kuandika na Kuratibu Injili Nne

Kuandika Injili kulianza katikati ya miaka ya 60 BK. Kwanza kabisa ilianza kuandikwa Injili ya Marko, ‎ikifuatiwa na Mathayo na Luka, na mwishoni mwa karne ya kwanza ikaandikwa Injili ya Yohana. [36] ‎Wakristo wanaamini kwamba; Baada ya Yesu (a.s) kupaa mbinguni mnamo mwaka 30 BK, [37] maneno ‎‎(mafunzo) yake matukio yote yanayo husuiana naye yalirithishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo ‎kwa mdomo [38] hadi katikati ya karne ya kwanza BK, ambapo wazo la kuandika masimulizi hayo lilipata ‎nguvu miongoni mwa Wakristo na baadhi yao wakaanza kuandika wasifu na maneno ya Nabii Isa (a.s). ‎‎[39]‎

Uandishi wa Injili ulienda sambamba na juhudi za Paulo za kueneza Ukristo na kuanzisha makanisa ‎mbalimbali. Hii ilisababisha watu wengi kuandika wasifu na matukio yanayohusiana na Yesu (a.s) kwa ‎mitindo na mbinu tofauti, na hivyo kuunda Injili kadhaa. [40] Kwa mujibu wa Thomas Michel, Wakristo ‎wa mwanzo, wakiongozwa au kupewa msaada na Roho Mtakatifu, walichagua Injili nne na vitabu ‎vingine 23 kutoka miongoni mwa maandiko mengi na kuvitambua kama ni vitabu vitakatifu na vilivyo ‎pata muongozo au Ilhamu ya Wahyi kutoka kwa Mungu mwnewe. [41]‎

Kuna mitazamo tofauti kuhusu wakati rasmi wa kurasmishwa au kurasmika kwa Injili Nne. Moja ya ‎maoni ni kwamba mwaka 397 BK katika Mkutano wa Kanisa la Carthage, Injili zote za mwanzo ziliachwa ‎isipokuwa Injili hizi nne tu, na ilipofikia mwanzoni mwa karne ya tano, Injili Nne zikawa rasmi ‎zinazotambulikana kisheria katika Agano Jipya. [42] Wengine wanaamini kuwa; Injili Nne takriban ‎kutoka mwaka 150 BK zilianza kujulikana kama ni kazi za Mitume, na tokea hapo zikwa ndizo Injili zenye ‎mamlaka, ambazo maamrisho na makatazo yake ni sawa na maamrisho ya Mungu Mwenyewe. Na ‎ilipofikia mwaka 170 BK zikapata hadhi ya kazi za kisheria na kuwa ndio Injili rasmi, ingawa hazikutajwa ‎Injili hizo hazikutajwa kwa jina maalumu. [43] Katika utangulizi wa tafsiri ya Agano Jipya, ya Pirooz ‎Sayyaar, imeelezwa kwamba; Mnamo mwanzoni mwa karne ya tatu BK, Injili Nne zilipata hadhi na ‎kuwa ndio Injili rasmi na hakukuwa na mabishano yoyote zaidi juu yake baada ya hapo. [44]‎

Sifa za Injili Nne

Kuna mashaka kuhusiana na waandishi wa Injili Nne hizi, na haijathibitishwa kupitia ithibati yakinifu ya ‎kuwa ni wao ndio waandishi waliandika Injili hizo. [45] Hossein Taufigiy katika kitabu chake «Ashenaaiy ‎ba Adiyane Bozorge» ameandika akisema kwamba; Wakristo wanaamini kuwa Injili Nne ziliandikwa na ‎Mitume au wanafunzi wa Mitume miaka kadhaa baada ya Yesu (a.s) kufariki. [46] Kwa mujibu wa ‎Thomas Michel, Wakristo hawawaoni waandishi wa Agano Jipya kama ni manabii, bali wanaamini ‎kwamba walikuwa tu ni wafuasi wa Yesu (a.s), walioandika vitabu hivyo kwa msukumo wa Ilhamu ya ‎Mungu. [47] Inasemekana kwamba lugha ya awali ya Injili Nne ilikuwa ni lugha ua Kigiriki. [48]‎

Mathayo

Injili ya Mathayo ni kitabu cha kwanza kilichomo katika vitabu vinne vya Agano Jipya. [49] Kwa mujibu ‎wa Thomas Michel, wataalamu (wanazuoni) wa Biblia wanaamini kwamba; Injili ya Mathayo iliandikwa ‎kwa lengo la kuzungumza na kubishana na baadhi ya viongozi wa Kiyahudi. [50] Kuna tofauti za maoni ‎kuhusiana na wakati na mahali pa kuandikwa kwa Injili hii. Baadhi watafiti wanadhani kuwa iliandikwa ‎mnamo mwaka 38 BK, huku wengine wakisema kuwa ni kati ya miaka 50 hadi 60 BK, [51] pia kuna ‎wengine waliodai kuwa iliandikwa mnamo mwaka 70 BK. [52] Pia maoni ya watafiti mbali mbali ‎yanatofautuina kuhusiana na mahali pa kuandikwa kwake kati ya Palestina na Antiokia nchini Siria. [53]‎

Kitabu hichi kinamtambulisha Nabi Isa (a.s) kama ni mkamilishaji wa dini ya Kiyahudi, mwalimu mkuu, ‎Musa mpya na mwenye sheria ya Agano Jipya. [54] Yaliyomo katika Injili hii yanajumuisha mambo ‎yafuatayo:‎

  1. Nasaba ya Yesu (Nabii Isa (a.s))
  2. Jinsi ya kuzaliwa kwake
  3. Majaribu aliyoyapitia mikononi mwa Shetani
  4. Amri za kimaadili kwa watu na wanafunzi wake
  5. Miujiza ya Yesu
  6. Kuchaguliwa kwa mitume kumi na mbili
  7. Kudhihirika kwa Musa (a.s) na Eliya mbele yake
  8. Njama za kumuua Yesu
  9. Kufufuka kwake kutoka kaburini [55]‎

Mwandishi wa Injili ya Mathayo, alikuwa ni mmoja wa mitume wa Yesu (Nabii (a.s)) ambaye ‎inasemekana kabla ya kumuamini Yesu (a.s), alikuwa mtoza ushuru na mkusanya kodi. [56] Hapo ‎zamani, Injili ya Mathayo ilidhaniwa kuwa ndiyo Injili ya kwanza na ya zamani zaidi, Ila watafiti wa leo ‎wanaamini kwamba Injili ya Marko ndiyo ya zamani zaidi kuliko Injili nyengine zote. [57]‎

Marko

Injili ya Marko inachukuliwa kuwa ndiyo Injili fupi na ya zamani zaidi. [58] Mwandishi wake, Marko, ‎hakuwa miongoni mwa mitume wa Yesu (Nabii (a.s)); bali alikuwa ni mfuasi na mwanafunzi wa mtume ‎Petro. [59] [Maelezo 3] Yeye Alikusanya Injili yake karibu na mwaka 60, [60] 61, [61] au 70 BK, [62] ‎akiwa Italia au Roma. [63] Injili hii inasisitiza sana ubinadamu (sio Ungu) wa Yesu (a.s) pamoja na ‎mateso aliyoyapitia. [64]‎ Injili ya Marko imegawika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza inahusina na utambulisho wa Yesu ‎Yesu na ufalme wake, na sehemu ya pili inahusiana na kifo chake. [65] Marko ‎anazingatia zaidi matendo ya Yesu na kutoa taarifa kuhusiana na jinsi alivyo kabiliana na ‎Pepo (Shetani) kuwatoa kutoka kwa wagonjwa wa akili, kusamehe wadhambi, na kufanya miujiza. [66] ‎Injili hii inamtambulisha Yesu kuanzia wakati alipobatizwa na Yohana Mbatizaji (Baptist au ‎Nabii Yahya Mwana wa Nabii Zakaria) na kuanza kwa Utume wake, bila kuzungumzia nasaba na ‎kuzaliwa kwake. [67] Sentensi ya kwanza ya Injili ya Marko inasema: «Mwanzo wa bishara (Injili) ya ‎Yesu Kristo, Mwana wa Mungu». [68]‎

Luka

Injili ya Luka, ambayo inachukuliwa kuwa ndiyo Injili refu zaidi, [69] iliandikwa kati ya miaka 70 na 90 BK ‎ikilenga wapagani [70] huko Roma. [71] Sifa maalum ya Injili hii ni kwamba; Inatoa maelezo kamili juu ya ‎kuzaliwa na utoto wa Yesu. [72] Pia inaelezea kuzaliwa kwa Yohana (Nabii Yahya a.s), ‎miujiza kadhaa ya Yesu, kuwapa mitume nguvu za kipekee, kuteua watu sabini (mbali ‎na mitume) kwa ajili ya kuhubiri, kusulubiwa kwake pamoja na kufufuka kwake kutoka kaburini. [73] ‎Katika Injili hii, mitume wanamwita na kumtambua Yesu kama ni «Mungu» [74] na pia ‎inamtaja Yesu kama mtu mkamilifu. [75]‎

Luka alikuwa mwanafunzi na mfuasi wa Paulo Mtume mwenye asili isiyo ya Kiyahudi, hivyo hakuwa ‎miongoni mwa mitume wa Yesu. [76] Luka ni mwandishi pekee wa Agano Jipya ambaye ‎hakuwa Myahudi. [77]‎

Yohana

Injili ya Yohana inachukuliwa kuwa kitabu cha mwisho cha maisha na mafundisho ya Yesu (Nabii Isa ‎‎(a.s)), ambayo ndani yake inasisitiza juu ya ubinadamu wa juu wa Yesu. [78] Yohana ‎alikuwa ni mmoja wa mitume kumi na mbili wa Yesu. [79] Kuna tofauti za maoni ‎kuhusiana na mwaka wa kuandikwa kwa Injili hii. [80] Kuna mitazamo tofauti kuhisana na hili, nayo ni; ‎Mtazamo wa jadi ambao unazingatia na kuamini kuwa mwishoni mwa karne ya kwanza BK, ambapo ni ‎mwanzoni mwa mwaka 85 BK na kuendelea, kuwa ni ndiyo mwaka wa kuandikwa kwake. [81] ‎Wengine wanaamini kwamba Injili hii iliandikwa kati ya mwaka wa 50 na 70 BK. Pia kuna wano amini ‎kuwa mwaka 65 BK ndiyo mwaka hasa wa kuandikwa kwae. [82] Katika Injili hii; maneno na mafunzo ‎ya Yesu yamepewa kipau mbele zaidi, kuliko maisha yake. Pia maneno ya Yesu katika Injili yametolewa kwa njia ya hotuba refu zaidi zinazojumuisha mawazo magumu na ya ‎siri ndani yake. [83] Mwandishi anasema kuwa lengo la kuandika Injili hii ni kwa kutumia kauli isemayo: ‎‎«Maandiko haya yameandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na ‎kwa imani hiyo muweze kuwa na uzima kwa jina lake». [84]‎

Katika Injili ya Yohana, Yesu ametambulishwa kama ni Mwana wa Mungu [85], Kalima ‎‎(Neno) [86], na yule aliye wa tangu na tangu na wa milele [87]. Pia Katika baadhi ya matukio [88], Yesu ‎anaonekana kupewa cheo cha Mungu ndani ya Injili hii. [89] Vile vile imenukuliwa ya kwamba; Hii ndiyo ‎Injili pekee inayo zungumzia Faraklit wa muahidiwa (ambaye maana yake ni Mfariji), na imesemwa ‎kwamba yeye atakuja baada ya Yesu ambaye atafundisha kila kitu na kuongoza ‎ulimwengu huu. [90]‎

Katika tafsiri ya «Pirooz Siaar» kwenye utangulizi wa Injili ya Yohana katika kitabu cha Agano Jipya, ‎imeeleza kwamba; Kuna shaka mbali mbali kuhusiana na mwandishi wa Injili ya Yohana, hii ni kutokana ‎na uwepo wa migongano na utata iliomo ndani yake. Inawezekana kwamba baadhi ya maudhui zake ‎ziliongezwa na wanafunzi wa Yohana baada ya kifo chake. Pia, inawezekana kuwa Injili hii iliandikwa na ‎kuendelezwa katika hatua mbalimbali. Kwa mujibu wa mwandishi wa utangulizi huo, jina la mtu wa ‎mwaisho aliyeandika na kuhariri Injili hii halijulikani. [91]‎

Injili Zinazo Fanana (Synoptic Gospels)

‎ Injili tatu za Mathayo, Marko na Luka zinaitwa Injili zinazo fanana (Synoptic Gospels), hii kwa sababu ‎ya kufanana na kuendana kwao katika lugha na kimuktadha. [92] Kwa hiyo Injili hizi inatafautiana na ‎Injili ya Yohana. Vipengele vinavyo tofautisha Injili ya Yohana na Injili hizo tatu, vimeelezwa kama ‎ifuatavyo:‎

  • Inajumuisha miujiza ambayo haipo katika Injili nyingine, miongoni mwake ni kama vile; muujiza ‎wa kubadilisha maji kuwa divai huko Kana pamoja na kufufuka kwa mtu aitwaye Lazaro.‎
  • Ina hotuba refu kuliko Injli nyengine. ‎
  • Ina Christolojia (Christology) maalum (tafiti kuhusiana na uhakika wa Yesu na nafasi yake) inayo ‎inasisitiza Uungu wa Yesu (Nabii Isa ‎‎(a.s)). [93] ‎Injili zinazo fanana (Synoptic Gospels), zinachukuliwa kuwa ziliathiriwa na fasihi ya Kiyahudi, wakati ‎Injili ya Yohana inachukuliwa kuwa iliathiriwa na falsafa ya Kigiriki. [94]‎

Injili Zisizo Rasmi

Mbali na Injili nne, pia kuna Injili na vitabu vyengine visivyo rasmi, vinavyo julikana kama «Apokrifa» au ‎vitabu bandia vya Agano Jipya ambavyo kanisa halivitambui. [95] Injili ya Waebrania, Injili ya Wamisri, ‎Injili ya Petro, Injili ya Tomo, Injili ya Filipo, na Injili ya Utoto ni miongoni mwa Injili hizo zisizo rasmi [96].‎

Injili ya Barnaba

Injili ya Barnaba ni miongoni mwa Injili zisizo rasmi ambazo zimevutia sana hisia za Waislamu; hata ‎hivyo, Wakristo wanaiona Injili hii kuwa ya bandia. [97] Inasemekana kwamba; Injili hii ilitambuliwa ‎kuwa isiyo rasmi pamoja na Injili nyengine mia tatu katika Baraza la Nikea (baraza la kwanza la ‎ulimwengu la kanisa) mwaka mnamo mwaka 325 BK. [ 98] Baada ya hapo, mapapa waliitangaza kuwa ni ‎miongoni mwa vitabu vilivyopigwa marufuku. [99]‎ Sababu za marufuku na kutotambulika kwa Injili hii zimetajwa kuwa ni kule kutokubaliana kwa ‎maudhui zake na imani rasmi za kanisa. Pia, ndani yake kuna maandiko yenye upinzani na mtume Paulo ‎na imani zake. [100]‎

Injili ya Barnaba inatofautiana na Injili nne rasmi katika nyanja kadhaa ndani yake, miongoni mwazo ni ‎kama ifuatavyo:‎

  • Inakataa Uungu na kupinga kwamba Yesu si mwana wa Mungu. [101]‎
  • Katika Injili ya Barnaba, mara kadhaa, kupitia maneno ya Yesu (a.s), zimenukuwa habari zisemazo ‎kuwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni Masihi. [102]‎
  • Kulingana na Injili hii, badala ya Yesu (Nabii Isa (a.s)), mmoja wa mitume wa Yesu aliye kuwa ‎akifanana naye sana aliye julikana kwa jina Yuda Iskarioti, alisulubiwa msalabani. [103]‎

Pia, ndani ya Injili ya Barnaba mna mafunzo yenye migongano na yale yaliyomo ndani ya Qur'ani pamoja ‎na imani za Waislamu kwa jumla. Miongoni mwa migongano hiyo ni pamoja na kwamba, kwa mujibu ‎wa Injili hii, wanadamu ni watoto wa Mungu nao ni wenye dhambi asilia. Vile vile Injli hii inasema ‎kwamba manabii nao ni wenye kutenda dhambi isipokuwa Yesu (a.s) tu peke yake. Mitume ‎kama vile Ibrahim, Haruni na Ayubu (a.s) wanatuhumiwa na dhambi na kuwa na upendo wa kishirikina ‎Injilini humo. [104]‎

Watafiti wa Kikristo wanaamini kuwa; Injili hii imeandikwa katika kipindi tofauti na zama za Nabii ‎Isa (a.s) na katika eneo tofauti na Palestina. [105] Thomas Michel ambaye ni Mchungaji Mkristo, ‎ameeleza akisema kuwa; Wataalamu kwa kuzingatia ushahidi wa kihistoria na wa kilugha, waeweza ‎kufikia natija ya kwamba, Injili hii imeandikwa mwishoni mwa karne ya kumi na sita. [106] Kwa upande ‎mwingine, baadhi ya watafiti wa Kiislamu wanaamini kuwa Injili hii ndiyo Injili asili. [107]‎

Kuna maoni tofauti kuhusiana na mwandishi hasa wa injili hii. Wengine wanachukulia Barnaba kama ‎jina la mmoja wa wahubiri wa Kikristo anayeitwa Yusufu ambaye alikuwa ni mzaliwa wa Kupro (Cyprus) ‎atokaye katika familia ya Kiyahudi na ukoo wa Lawi, ambaye mwana wa nabii Yakobo (Yakubu). [108] ‎Kwa juhudi zake nyingi kijana huyu katika kuhubiri Ukristo, alipewa jina la Barnaba, likimaanisha ‎mhubiri mwenye nguvu. [109] Barnaba alikuwa ni mtu mwenye kuaminika mbele ya mitume [110] na ‎kwa mujibu wa Agano Jipya, alikuwa ni mtu mwema na mwenye imani. [111] Kinyume chake, baadhi ‎ya wanatheolojia wa Kikristo wanadai kwamba mwandishi wa Injili hii alikuwa ni Mspaniola na ni ‎Mkristo wa karne ya kumi na sita ambaye alikuja kusilimu baadae. [112]‎

Ukosoaji na Vikwazo Dhidi ya Injili

Wakosoaji wa Injili nne na Agano Jipya kwa ujumla wamewasilisha ukosoaji kadhaa, ikiwemo:‎

  • Ukosefu wa Uaminifu Juu ya Waandishi:‎ Wakosoaji wamesema kuwa; Kwa mujibu wa Wakristo wote duniani ni kwamba, waandishi wa Injili ‎hawakuwa manabii na wala hawakuwa na kinga dhidi ya makosa na utendaji dhambi; badala yake, ‎walikuwa ni wanadamu wa kawaida waliomwamini bwana Yesu (Nabii Isa ‎‎(a.s)). Katika Injili, kuna ‎maneno ya wazi yanayo sema kuwa, baadhi ya mitume na wanafunzi wa Yesu ‎walionyesha kutoamini, kukamusha Yesu na maneno yake, na kuto elewana baina yao. Kwa hivyo, ‎haiwezekani kutegemea vitabu hivi kama chanzo kikuu cha mafundisho ya Yesu. [113] ‎Thomas Michel, mtaalamu wa theolojia ya Kikristo, ameonesha wazi kuwa Wakristo wengi ‎hawakubaliani na utukufu wa lafudhi (maneno) ya maandiko ya Injili, yaani haamini kuwa maneno yake ‎yanatoka kwa Mungu moja kwa moja. Wakristo wote wanaamini kuwa; ni kweli ujumbe halisi unatoka ‎kwa Mungu; lakini muundo wake unatoka kwa wanadamu ambao kama wanadamu wengine, wako ‎katika hatari ya kukosea. Kwa hivyo, huenda mwandishi wa kibinadamu wa vitabu na ujumbe huu ‎akaingiza maoni yake mitelezo na makosa katika vitabu hivyo. [114]‎
  • Mikanganyo na Migongano ya Injili:‎ Baadhi ya migongano na kutokubaliana kwa ibara za Injili mbali mbali, imekuwa ndiyo sababu ya ‎kuzikataa na kuzihisabu kuwa hazina uaminifu kamili ndani yake. [115] Kwa mfano, kuna mikanganyo ‎mikubwa kati ya Injili za Mathayo, Luka na Marko kuhusiana na nasaba ya Yesu. Katika ‎Injili za Mathayo [16] na Luka, [117] Yesu ametambulishwa kuwa ni wa kizazi cha Daudi, ‎lakini katika Marko, [118] inasemekana kuwa Daudi alikuwa akimuona Yesu kama ‎ni Mungu wake. Kwa hiyo, inawezekanaje Yesu, awe ni mtoto wa Daudi? ‎Mikanganyo mingine iliyotajwa ni pamoja na; jinsi Yesu alivyokamatwa, alama ya ‎mwanafunzi msaliti (Yuda Iskariote), na tukio la kufufuka kwa Yesu kutoka kaburini ‎kwake. [119]‎
  • Makosa na Ngano za Paukwa Pakawa za Injili:‎ Mafundisho ya Utatu, mafundisho ya fidia amabayo kwa mujibu wake Yesu alijitoa ‎kafara ili kuwaokoa wanadamu na kuwasamehe dhambi zao, pamoja na kusamehewa kwa dhambi ‎kupitia makasisi wa kanisa, ni miongoni mwa imani za kihistoria zilizotajwa katika Injili. [120] Pia kuna ‎Makosa kadhaa yanayo husishwa na Injili. [121]‎

Bibliografia Kuhusu Injili‎

Vitabu vingi vimeandikwa kwa lugha ya Kifarsi na Kiarabu kuhusu Injili. Baadhi ya vitabu hivyo ni:‎

  • Al-Taudhihu fi Bayani Maa Huwa al-Injil wa Man Huwa al-Masihu: Kilichoandikwa na Muhammad Hussein Kashif al-Ghita (Aliye zaliwa mwaka 1256 na kufariki ‎‎1333 Shamsia), ambaye ni mmoja wa marajii (mujitahid) wa kidini huko Najaf. Mwandishi katika kitabu ‎hichi, ameelezea misingi ya Injili na imani za Ukristo kwa kutumia rejea kutoka kwenye Biblia yenyewe. ‎Kitabu hiki kimetafsiriwa kwa Kifarsi na Sayyid Hadi Khosrowshahi kwa jina la “Pazuhesh Dar Baariye ‎Injil wa Masiih na kuchapishwa na Bustan Book Publishing.‎
  • Injil Yohanna fi al-Mizan: Kitabu hichi ni cha Kiarabu kilichoandikwa na ‎Muhammad Ali Zahran, ambacho kinachambua maudhui, historia na mwandishi wa Injili ya Yohana. ‎Kitabu hichi kimetolewa na Dar al-Arqam Publishing.‎
  • Seir Taarikhi Injil Barnaba: Kilichoandikwa na Hussein Taufiqi. Kitabu hichi ni ‎kitabu kidogo kinacho husiana na historia ya Injili ya Barnaba na muhtasari wa maudhui yake pamoja na ‎majibu kwa baadhi ya maswali kuhusu Injili hiyo. Kimechapishwa na Shirika la Dar al-Haq mwaka 1361 ‎Shamsia. [122]‎
  • Tathawwur al-Injil; al-Masih Ibnullah Am Malikun min Nasali Dawud? Dirasatun Naqdiyah wa ‎Turjamah Jadidah li Aqdami al-Anajil Taksyifu Mafahim Mutsairah. Asili ya kitabu hichi ni kwa lugha ya Kiingereza kilicho andikwa na Enoch Powell, kisha kutafsiriwa kwa ‎Kiarabu na Ahmad Ibbash. Kwa mara ya kwanza kitabu hichi kilichapishwa na Dar Qutaiba huko Beirut.‎

Masuala Yanayo Husiana

Maelezo

  1. Agano Jipya ni mkusanyo wa vitabu 27 vinavyokubaliwa na ‎Wakristo wote na kugawanywa katika sehemu nne kuu: Injili, Matendo ya Mitume, Barua za Mitume, ‎na Ufunuo. Agano Jipya linakabiliana na Agano la Kale. Agano la Kale ni vitabu vitakatifu vya ‎Wayahudi ambavyo Wakristo pia wanaviheshimu. (Taufiqi, «Ashenayee ba Adyane Bozorg», 1389 S, ‎uk. 168-170).
  2. Marko pia huandikwa kwa kutumia vokali ‎ya «A» kama (Márqus) huku wakati mwengine ikionekana kutumiwa vokali ya «U» kama (Múrqus).
  3. Petro anachukuliwa kuwa ni mtume na mfuasi mkuu wa Yesu (a.s). Jina lake ‎halisi lilikuwa ni Shimon, lakini Yesu (a.s) alimpa jina la Petro, ambalo linamaanisha "mwamba", na ‎akamteua kuwa ndio msingi wa kanisa na jamii ya Kikristo. (Toufighi, «Ashenaaaiy ba Adyane ‎Bozorg», 1389 S, uk. 148).

Rejea

Vyanzo