Nenda kwa yaliyomo

Nabii Harun

Kutoka wikishia
Dhabahu linalohusishwa na Nabii Harun juu ya mlima Hori magharibi mwa Jordan

Nabii Harun (Kiarabu: النبي هارون) ni miongoni mwa Mitume wa Mwenyezi Mungu, kaka, mrithi na aliyekuwa pamoja na Nabii Mussa (a.s) ambapo katika Qur’an Nabii Mussa ananukuliwa akieleza na kubainisha ufasaha wa ndugu yake huyu katika kuzungumza. Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w), nafasi ya Imam Ali (a.s) kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) imefananishwa na ile ya Harun kwa Mussa. Hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo vya Kishia na Kisuni na inatambulika kwa jina la Hadithi ya Manzila (daraja).

Wakati Nabii Mussa alipoenda katika Mlima Sinai kwa ajili ya kuchukua mbao zilizokuwa na sheria na amri, Harun alichukua nafasi ya Mussa. Katika kipindi hiki mtu aliyejulikana kwa jina la Samiri alimtengeneza ndama wa dhahabu na akaanza kuwalingania watu wamuabudu ndama huyo. Hivyo basi Harun alikuwa mahali pa Mussa wakati Bani Israil walipoanza kuabudu ndama. Licha ya jitihada zake, hakuweza kuwazuia kufanya hivyo. Hata hivyo kitabu cha Torati kimenasibisha utengenezaji huo wa ndama na Harun. Yaani kinasema, Harun ndiye aliyemtengeneza ndama huyo.

Harun aliaga dunia huko Tur Sina akiwa na umri wa miaka 123. Kaburi lililo juu ya mlima Hor wa magharibi mwa Jordan linasemekana kuwa la Harun. Ndio maana Mlima Petra pia unajulikana kama Jabal Harun (Mlima wa Harun).

Familia

Harun (a.s) alikuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu na alikuwa ndugu (kaka mkubwa) yake Nabii Mussa (a.s). Baba yake alikuwa Imran na mama yake alikuwa Yokebedi. [1] Harun alikuwa mkubwa kuliko Mussa lakini aliteuliwa na kupatiwa Utume baada ya ndugu yake. Nasaba yake inarejea na kufika kwa Safiyya binti wa Huyayy bin Akhtab mmoja wa wake za Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliyetokana na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir. [2]

Utume

Mayahudi, Wakristo, [3] na Waislamu [4] wanaamini Utume wa Harun. Kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), Utume uliendelea kupitia kizazi chache [5] na Mitume akiwemo Iliyas wanahesabiwa kuwa, miongoni mwa wajukuu zake. [6]

Kwa mujibu wa aya za Qur’an Tukufu, wakati Nabii Mussa (a.s) alipoteuliwa na Mwenyezi Mungu na kuwa Mtume, alimuomba Allah amfanye nduguye Harun kuwa waziri na mtu atakayefuatana naye, kwani yeye ni mbora katika ufasaha na uzungumzaji. [7] Kadhalika katika Aya za Qur’an kumebainishwa kuwa pamoja na bega kwa bega Nabii Mussa na Harun wakati wa kumlingania Firaun Mungu mmoja. [8] Imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) akitoa wasifu wa hali ya Mussa na Harun (a.s). [9]

Katika Qur’an Utume wa Harun umeashiriwa. [11] Katika Surat al-Saffat Mussa na Harun wametambulishwa kuwa washirika katika kunufaika na kitabu cha Mwenyezi Mungu, kuwaongoza kwenye njia nyoofu na kutenda wema na hisani. [12]

Katika riwaya na hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) inayomnukuu Mtume (s.a.w.w), inasemekana kwamba wakati Mtume (s.a.w.w) alipokwenda katika safari ya Mi'raj na alipofika mbingu ya tano, alimuona mtu shupavu na mwenye nguvu na mwenye macho makubwa akiwa amezungukwa na kundi la Umma wake. Mtume alishangazwa na wingi wa idadi yao na akamuuliza Jibril, mtu huyu ni nani? Jibril alimwambia kwamba, huyu ni Harun mwana wa Imran. Kisha Mtume akamsalimia na kumuombea msamaha, naye pia akamsalimia Mtume na kumuombea msamaha. [13]

Mrithi wa Mussa na kisa cha ndama wa Samiri

Makala asili: Ndama wa Samiri

Wakati Nabii Mussa alipokwenda katika Mlima Sinai kwa ajili ya kuchukua mbao zilizokuwa na sheria na amri, alimuweka Harun nafasi yake. [14] Katika kipindi hiki mtu aliyejulikana kwa jina la Samiri alimtengeneza ndama wa dhahabu [15] na akaanza kuwalingania watu wa kaumu ya Mussa wamuabudu ndama huyo. [16] Licha ya jitihada zake, hakuweza kuwazuia kufanya hivyo. [17] Baada ya Mussa kurejea alizungumza na Harun kwa ukali sana na kumhoji kwa nini hakuwazuia jambo hilo. [18] Jambo hili linaashiria katika Aya ya 150 ya Surat A’araf: Na aliporudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika na kuhuzunika, alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na akamkamata kichwa ndugu yake akimvutia kwake. (Harun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu. Kwa muktadha huo, Mussa akamuombea msamaha kaka yake kwa Mwenyezi Mungu. [19]

Kwa mujibu wa Aya za Qur’an Tukufu, kuabudu ndama Bani Israel ilikuwa kazi ya Samiri [20] na Harun alipambana na hilo; [21] hata hivyo kitabu cha Torati ambacho ni kitabu kitakatifu kwa Mayahudi, kimemnasibisha na Harun ulinganiaji na uabudu ndama. [22]

Kushabihishwa nafasi ya Imam Ali (a.s) na Harun (a.s)

Makala asili: Hadithi ya Manzila

Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) daraja na nafasi ya Imam Ali (a.s) kwa Mtume (s.a.w.w) imefananishwa na nafasi na daraja ya Haruna kwa Mussa. [24]. Hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo vya Kishia [25] na Kisuni, [26] na inatambuliwa kwa jina la Hadithi ya Manzila. Kwa mujibu wa hadithi hii, Mtume (s.a.w.w) alimhutubu Imam Ali (a.s) akisema: Wewe kwangu daraja yako ni mithili ya Harun kwa Mussa; kwa tofauti hii kwamba, baada yangu hakuna Mtume tena. [27]

Kuaga dunia na lilipo kaburi lake

Kaburi linahusishwa na Nabii Haroun katika kijiji cha Catherine huko Jordan

Ahmad bin Abi Ya’qubi [28] anasema, Nabii Harun aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 123 baadhi ya nukuu zinaonyesha kuwa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 128, katika zama za Nabii Mussa (a.s), kwa mujibu wa nukuu ya Ibn Masuud [29], Nabii Harun aliaga dunia akiwa na uumri wa miaka 126. Katika kitabu cha al Bidiu wal Tarikh [30] inaelezwa kuwa, aliaga dunia akiwa na miaka 128 ikiwa ni miaka mitatu kabla ya kufariki dunia Nabii Mussa (a.s) Kadhalika baadhi ya nukuu nyingine ikiwemo hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ni kwamba, wakati Nabii Harun anaaga dunia alikuwa na umri wa miaka 133. [31]

Kwa mujibu wa hadithi, Mussa alimchukua Harun na kumpeleka katika Mlima Sinai na huko Malaika wa mauti akachukua roho ya Harun. [32] Nabii Mussa alirejea kwa Bani Israeil na kuwapa habari ya kifo cha Harun. Bani Israel walimkadhibisha Mussa na kusema: Wewe ndiye uliyemuua. Mwenyezi Mungu akatoa amri kwa Malaika walete jeneza la Harun hewani na walipomuona Harun wakafahamu kwamba, ameaga dunia. [33] Kwa mujibu wa ripoti ya Ya'aqubi ni kwamba, mtoto wa Harun yaani Eleazar alikuwa pamoja na Nabii Mussa wakati wa kifo cha baba yake. [34]

Katika eneo la magharibi mwa Jordan juu ya mlima Hor kuna kaburi ambalo linasemekana kuwa ni la Nabii Harun. [35] Mlima huu ni mashuhuri pia kwa majina ya kama Mlima Petra na Jabal Harun (Mlima wa Harun). [36] Ujenzi wa kaburi hili unarejea nyuma katika karne ya 8 Hijiria. [37]. Kadhalika kuna kaburi jingine katika kijiji cha utalii cha St. Catherine huko Jordan (moja ya maeneo ya pwani ya Ghuba ya Aqaba) ambalo liko juu ya muinuko mdogo ambalo linanasibishwa na Nabii Haruna (a.s). [38]

Vyanzo

  • Bukhārī, Muḥammad b. Ismāʿīl al-. Ṣaḥīḥ al-Bukhārī. Beirut: Dār al-Fikr, 1401 AH.
  • Ibn ʿAbd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Al-Istīʿāb fī maʿrifat al-aṣḥāb. Edited by ʿAlī Muḥammad al-Bajāwī. Beirut: Dār al-Jīl, 1412 AH.
  • Ibn Manẓūr, Muḥammad b. Mukarram. Mūkhtasar tārīkh Dimashq. Edited by Ruḥiyat al-Nuḥas and Riyādh ʿAbd al-Ḥamīd Murād and Muḥammad Muṭīʿ. Damascus: Dār al-Fikr, 1402 AH-1989.
  • James Hawkes. Qāmus kitāb-i muqaddas. Tehran: Intishārāt-i Asāṭir, 1377 Sh.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1403 AH.
  • Muslim Nayshābūrī. Ṣaḥīḥ Muslim. Beirut: Dār al-Jīl/Dār al-Āfāq al-Jadīda, [n.d].
  • Mashāyikh, Fāṭima. Qiṣaṣ al-anbīyāʾ. Tehran: Intishārāt-i Farḥān, 1381 Sh.
  • Shaykhī, Ḥamīd Riḍā. Payāmbar az nigāh-i Qurʾān wa Ahl al-Bayt. 3rd edition. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1386 Sh.
  • Rāmīn-nizhād, Rāmīn. Mazār-i haḍrat-i Hārūn. Accessed 2021/08/08.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī Jāmiʿa-yi Mudarrisīn-i Ḥawza-yi ʿIlmīyya-yi Qom, 1417 AH.
  • Maqām al-Nabi Hārun (a); Jordan Heritage. Accessed 2021/08/08.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].