Fouad Ali Shukr
Fouad Ali Shukr (1961–2024) (Kiarabu: فؤاد علي شكر), maarufu kwa jina la Haj Mohsin au Sayyid Mohsin Shukr, alikuwa ni mmoja wa makamanda wakuu wa kijeshi wa Hizbullah ya Lebanon na mshauri wa karibu wa Sayyid Hassan Nasrallah. Fouad alifariki dunia mnamo tarehe 30 Julai 2024 (sawa na tarehe 9 Murdad 1403 S, kwa kalenda ya Kiajemi), kifo chake kilijiri kufuatia shambulio la anga lililofanywa na vikosi vya Israel katika jengo lililoko eneo la Dhahiya mjini Beirut. Fouad alikuwa na jukumu muhimu katika kuunda na kuongoza vikundi vya awali vya upinzani nchini Lebanon dhidi ya uvamizi wa Israel. Vyombo vya habari vya Israel vilimfafanua kama msimamizi wa mradi wa makombora ya Hizbullah.
Kifo cha Fouad Shukr kiliibua hisia kali katika maeneo mbalimbali duniani. Viongozi wa kisiasa na kidini walilaani vikali mno kitendo hicho, huku Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrallah, akiapa kulipiza kisasi kwa mauaji hayo.
Nafasi Yake
Fouad Shukr, anayejulikana kama Haj Mohsin au Mohsin Shukr, alikuwa ni mmoja wa makamanda wakuu wa kijeshi wa kikundi cha Hizbullah ya Lebanon, na ni mshauri wa karibu wa kijeshi wa Sayyid Hassan Nasrullah, aliye kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah. Shukr alikuwa na mchango mkubwa katika mipango ya operesheni mbali mbali dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. [1] Vyombo vya habari vya Israel vimemwelezea Fouad Shukr kama ni mtu wa pili kwa umuhimu ndani ya kikundi cha Hizbullah, na alifahamika kama ni msimamizi halisi wa mradi wa makombora yanayoongozwa kupitia vikosi vya Hizbullah. Viongozi wa Marekani walimuelezea pia kama ni mbunifu mkuu wa operesheni ya Hizbullah ya mwaka 1983 mjini Beirut, iliyopelekea wanajeshi 241 wa Marekani walipoteza maisha yao. [2]
Wasifu wa Maisha
Fouad Shukr alizaliwa mnamo tarehe 25 Aprili mwaka 1961 katika kijiji cha Nabi Sheeth, kilichoko eneo la Baalbak, Lebanon. [3] Katika miaka ya 1980, Fouad Shukr alichukua jukumu muhimu katika kuunda vikundi vya awali vya upinzani dhidi ya uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Mnamo mwaka 1982 Fouad Shukr alijeruhiwa akiwa mstari wa mbele katika mapambano hayo dhidi ya Wazayuni. Aidha, kati ya mwaka 1992 hadi 1995, aliratibu vikosi vya kijeshi vya Lebanon kwa ajili ya kupelekwa Bosnia na Herzegovina, akilenga kulinda Waislamu dhidi ya mashambulizi ya Waserbia wakati wa vita vya Balkan. [4]
Kulingana na maelezo kutoka kwa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Fouad Shukr alikuwa ni mmoja wa waanzilishi muhimu wa harakati za upinzani za nchini Lebanon. [5] Tangu kuanzishwa kwa Baraza la Jihadi la Upinzani wa Kiislamu, yeye alihudumu kama ni mjumbe wa baraza hilo na kusimamia operesheni za kijeshi za kutoa msaada dhidi ya jeshi la maadui katika uwanja wa vita huko Lebanon, hasa baada ya kuanza kwa Operesheni ya Tofaan al-Aqsa. [6]
Fouad Shukr alikuwa na uhusiano wa kwa karibu mno na Imad Mughniyeh, kamanda maarufu wa Hizbullah, aliyeuawa kwa njama mjini Damascus mnamo mwaka 2008. [7] Mnamo mwaka 2017, Marekani ilitangaza zawadi ya dola milioni tano kwa yeyote atakayetoa taarifa za kumkamata Fouad Shukr, [8] na ilipofikia mwaka 2019 Fouad Shukr alikabiliwa na vikwazo kutoka nchini Marekani. Aidha, Jeshi la Israel pia lilitangaza zawadi ya dola milioni tano kwa taarifa yoyote itakayosaidia kukamatwa kwake. [9]
Kuuawa kwa Fouad Shukr
Fouad Shukr aliuawa mnamo tarehe 30 Julai 2024 (sawa na tarehe 9 Mordad 1403, kwa kalenda ya Kiajemi), kupitia shambulio la anga lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya jengo la makazi lililoko katika eneo la Dhahiya, mjini Beirut. [10] Jeshi la Israel lilidai kuwa shambulio hilo lilikuwa ni jibu la shambulio lililofanywa na Hizbullah katika eneo la Majdal Shams, ambapo walidai kuwa Fouad Shukr ndiye aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo. Hata hivyo, Hizbullah ilikanusha kuhusika na shambulio hilo. [11] Kwa mujibu wa maelezo ya harakati za upinzani za Lebanon, shambulio dhidi ya Majdal Shams lilitokana ama na hitilafu za mifumo ya ulinzi ya Israel au lilikuwa ni njama iliyopangwa na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kuibua mfarakano kati ya Druziy (Druze) na upinzani wa Lebanon, huku ikilenga kupotosha umma juu ya vitendo vyao vya uhalifu huko Gaza. [13]
Hizbullah imeeleza kuwa mauaji ya Fouad Shukr, yalitokana na msaada wake kwa watu wa Gaza dhidi ya uvamizi wa Israel. Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, alitoa kauli thabiti na kula kiapo ya kwamba watalipiza kisasi tokana na mauaji hayo yaliyo fanya na vikosi vya Israel. [14]
Majibu kwa Mauaji ya Fouad Shukr
Harakati za mazishi ya Fouad Shukr zilifanyika mnamo tarehe 11 Agosti mwaka 2024, zikiongozwa kwa heshima rasmi na hotuba kutoka kwa Sayyid Hassan Nasrullah. [15] Viongozi mbalimbali wa kisiasa na kidini walikosoa na kutoa salamu zao za rambirambi kuhusiana na tukio hilo. Miongoni mwa viongozi waliotoa salamu za rambambi kwa kujiri tukio hilo, ni pamoja na: Bashir Hussein Najafi, mmoja wa mafaqihi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf; [16] Sayyid Hashim Husseini Bushihri, kiongozi wa Jumuiya ya Jaamiatu Al-Mudarrisina ya Qom; [17] Hussein Salami, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu; [18] Abdul-Malik al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen; [19] pamoja na viongozi wa Hamas na Mabrigedia wa Izz al-Din al-Qassam; [20] na Muhammad Baqir Qalibaf, Rais wa Baraza la Ushirikiano la Kiislamu (Majlis Shuraye Islami). [21]
Ili kujibu mauaji ya Fouad Shukr, mnamo tarehe 25 Agosti 2024, Hizbullah ya Lebanon ilifyatua zaidi ya makombora 300 dhidi ya vituo vya kijeshi vilivyopo katika maeneo yanayo tawaliwa kimabavu na utawala wa Kizayuni. [22]