Fat’wa ya Shaltut ya kujuzisha kufanya ibada kwa mujibu wa fikihi ya Shi'a

Kutoka wikishia

Fat’wa ya Shaltut ya kujuzisha kufanya ibada kulingana na fikihi ya Shi'a ni fat’wa iliyotolewa na Mahmoud Shaltut aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar cha Misri wakati huo akijuzisha Waislamu kufuata fikihi ya Shia. Msukumo wa kutoa fat’wa hii ulibainishwa kuwa ni ubora na umadhubuti wa hoja na dalili za baadhi ya hukumu za kisheria (kifikihi) za Kishia ikilinganishwa na fikihi ya Ahlu-Sunna. Fat’wa hii ilitolewa 17 Rabiul-Awwal 1378 Hijria siku ambayo ilisadifiana na kumbukizi ya kuzaliwa Imam Swadiq (as) na kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa madhehebu ya Shia Imamiya, Shia Zaydiya na madhehebu manne ya Ahlu Sunna. Miongoni mwa yaliyokuwa matokeo ya fat’wa hiyo, ni kuanzishwa kitengo maalumu cha kufundisha Fiq’h al-Muqaranah (Fikihi ya Ulinganishaji) na Fikhi ya Shia katika Chuo Kikuu cha al-Azhar. Kadhalika fat’wa hii ilikuwa na taathira kubwa kwa masalafi ambao walikuwa wakiamini kwamba, Mashia ni makafiri. Fat’wa ya Sheikh Shaltut iliungwa mkono na kupongezwa na baadhi ya Maulamaa wa Ahlu-Sunna kama Muhammad al-Ghazali, Mkuu wa Kundi la Ikhwanul Muslimin na Muhammad al-Fahham. Hata hivyo baadhi ya Maulamaa kama aAbdul-Latif al-Subki na Abul-Wafaa Kiristani waliikosoa fat’wa hii. Yusuf al-Qardhawi mwanazuoni wa Kisuni na mkusanyaji wa baadhi ya vitabu vya Sheikh Shaltut alikuwa akikana kutolewa fat’wa hii.

Kutolewa fat’wa na umuhimu wake

Fat’wa ya Sheikh Shaltut ni jibu la swali la kifat’wa aliloulizwa kuhusu ya kwamba: Je inajuzu Waislamu wote kufuata fikihi ya Shia Imamiya na Zaydiya? [1] Fat’wa hii ilitolewa na Sheikh Mahmoud Shaltu aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar cha Misri wakati huo na mmoja wa waanzilishi wa Dar al-Taqrib Baina al-Madhahib al-Islamiya (Taasisi ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu) ambaye alikuwa fakihi wa Kihanafi. [2] [3]. Fat’wa hii ilitolewa 17 Rabiul-Awwal 1378 Hijria siku ambayo ilisadifiana na kumbukizi ya kuzaliwa Imam Swadiq (as) na kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa madhehebu ya Shia Imamiya, Shia Zaydiya na madhehebu manne ya Ahlu Sunna. [4] Baadhi wanasema kuwa, kutolewa fat’wa hii na Sheikh Shaltut ilikuwa natija ya ufuatiliaji na juhudi za Muhammad Taqi Qumi na Sayyid Boroujerdi na kuasisiwa Dar al-Taqrib. [5] Kabla ya kutolewa fat’wa hii, Masuni hawakuwa wakiamini juu ya kujuzu kufanya ibada kwa mujibu wa fikihi ya Shia. [6] Inaelezwa kuwa, Shaltut alibainisha msukumo wake wa kutoa fat’wa hii kwamba, ni ubora na umadhubuti wa hoja na dalili za baadhi ya hukumu za kisheria (kifikihi) za Kishia ikilinganishwa na fikihi ya Ahlu-Sunna katika masuala kama mirathi na talaka. [7] Miongoni mwa yaliyokuwa matokeo ya fat’wa hiyo, ni kuanzishwa kitengo maalumu cha kufundisha Fiq’h al-Muqaranah (Fikihi ya Ulinganishaji) na Fikhi ya Shia katika Chuo Kikuu cha a;-Azhar nchini Misri. [8] Kadhalika inaelezwa kuwa, fat’wa hii ilikuwa na taathira kubwa kwa masalafi nchini Saudi Arabia ambao walikuwa wakiamini kwamba, Mashia ni makafiri. [9]

Tarjumi ya swali la fat’wa ya Shaltut:

Baadhi ya watu wanafikiri kwamba, ili Waislamu waweze kutekeleza ibada na amali zao kwa njia sahihi, ni lazima kufuata moja ya madhehebu manne ya Kisuni ambayo ni maarufu, na baina ya madhehebu hayo, Shia Imamiya na Zaydiya hayapo. Je wewe unakubaliana na nadharia hii kiujumla? Na unaamini kwamba, haijuzu kufuata madhehebu ya Shia Imamiya? [10]

Andiko la Fat’wa

Imekuja katika fat’wa ya Mahmoud Shalut kwamba, kwa mujibu wa itikadi ya baadhi ni kuwa, ili kutekeleza kwa usahihi amali na taklifu za kisheria, inapaswa kurejea na kufuata madhehebu manne ya Kisuni, na madhehebu ya Shia Imamiya na Zaydiya hayapo miongoni mwa madhehebu hayo. Muulizaji alitaka kujua mtazamo wa Sheikh Mahmoud Shalut kuhusiana na kufuata madhehebu kama Shia Imamiya na Zaydiya. Katika kujibu na kufutu hilo, Sheikh Shalult alisema: Uislamu haujawajibisha kufuata madhehebu maalumu na kila Muislamu anaweza kufuata kwa njia sahihi dhehebu lolote miongoni mwa madhehebu kwa njia saihi. Shaltut anasisitiza kuwa, inajuzu kufuata madhehebu ya Shia Ithna’shariya kama ilivyo kwa madhehebu mengine ya Kisuni na Waislamu wanapaswa kujiepusha na taasubi na chuki dhidi ya baadhi ya madhehebu. [11]

Shaltut alimtumia Muhammad Taqi Qumi Katibu Mkuu wa Dar al-Taqrib Baina al-Madhahib al-Islamiya matini na andiko la fat’wa hiyo ili iwekwe katika hifadhi ya kumbukumbu. [12] Ubao wa matini na andiko la fat’wa hii ukiwa na saini ya Shaltul ulikabidhiwa na Muhammad Taqi Qumi kwa Sayyid Hadi Milani na umehifadhiwa katika Taasisi ya Quds Radhawi katika Haram ya Imamu Ridha (a.s). [13]

Tarjumi ya jibu la fat’wa ya Shaltut:

1. Dini ya Uislamu haijamlazimisha yeyote kati wafuasi wake kufuata madhehebu maalumu; bali sisi tunasema kwamba, kila muumini ana haki ya kufuata moja kati ya madhehebu ya Kiislamu ambayo yamenukuliwa kwa usahihi katika vitabu maalumu vya hukumu na sheria vya madhehebu husika vilivyoandikwa, kama ambavyo mtu anayefuata moja kati ya madhehebu haya anaweza kubadilisha madhehebu yake na kufuata madhehebu yoyote ile na hakuna tatizo katika hili.

2. Madhehebu ya Jaafariya ambayo ni mashuhuri kwa jina la Madhehebu ya Shia Ith’naashariya, ni madhehebu ambayo kisheria inajuzu kuyafuata kama ilivyo kwa madhehebu zingine nne za Kisuni na inafaa kwa Waislamu kutambua hili na kujiepusha na chuki, taasubi, kutoa hukumu bila ya hoja na bila ya haki na kuunga mkono madhehebu fulani. Dini ya Mwenyezi Mungu na sheria Zake hazifuati madhehebu na wala sio maalumu kwa madhehebu fulani. Kila ambaye atafikia daraja ya ijtihadi basi ana anuani ya Mujtahidi na amali yake itakubaliwa na Mwenyezi Mungu na inajuzu kwa mtu ambaye hana daraja ya ijtihadi amfuate mujtahidi na akifanyie kazi kile ambacho fakihi wake amekibainisha na katika jambo hili hakuna tofauti baina ya masuala ya kiibada na miamala. [14]

Radiamali

Kufuatia kusambazwa fat’wa ya Shaltut kulitolewa radiamali mbalimbali za kuunga mkono au za kuipinga:

Radiamali za kuunga mkono fat’wa

• Muhammad al-Bahi mmoja wa wakuu wa Jumuiya ya Kukuribisha aliandika makala akiunga mkono hoja za kifikihi za Kishia na hivyo kuunga mkono fat’wa ya Shaltut. [15]

• Muhammad al-Sharqawi aliandika dondoo yenye anuani: Al-Azhar Wal-Madhahib al-Fiq’h al-Islami (al-Azhar na Madhehebu ya Fikihi ya Kiislamu). Aliitambulisha rai na nadharia ya Shaltut kwamba, ni ya kishujaa, ya kujitolea na yenye ukweli. [16]

• Muhammad Taqi Qumi, Katibu Mkuu wa Dar al-Taqrib Baina al-Madhahib, (Taasisi ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu) baada ya kutolewa fat’wa hii, aliandika makala yenye anuani: Qisat al-Taqri (Kisa cha Kukurubisha) [17] ambapo ndani yake alisisitiza juu ya ulazima wa kukurubisha na kadhalika kukurubisha baina ya Shia na Sunni. Makala hii ilichapishwa katika jarida la Risalat al-Islam. [18]

• Muhammad Muhammad al-Madani, Mhariri Mkuu wa Jarida la Risalat al-Islam na Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha al-Azhar, aliandika makala iliyokuwa na anuani ya Rajjah al-Ba'ath fi Kulliyât al-Sharîah ambapo ndani yake alipinga vikali madai dhidi ya Mashia Imamiya na Zaydiya ya kuchupa mipaka kuhusiana na Mitume na Maimamu na kuwaona kuwa ni Miungu na kuyatambua madhehebu hayo kwamba, yana tofauti na makundi mengine ambapo sambamba na kujibu maswali kuhusiana na kufundisha fikihi ya Shia katika Chuo Kikuu cha al-Azhar aliunga mkono fat’wa ya Shaltut. [19]

• Muhammad al-Ghazali aliandika makala yenye anuani: “Ali Awail al-Tariq” katika jarida la al-Azhar na aliitambua fat’wa ya Sheikh Shaltut kuwa ni harakati na hatua kubwa mno. Katika makala hii alimtaja Nader Shah kuwa mtu anayepigia debe umoja na aliyefanikiwa katika kuutambulisha Ushia kama dhehebu la tano rasmi la Kiislamu na akawalaumu kwa kuwapiga vijembe baadhi ya Maulamaa. [20]

Radiamali za kupinga fat’wa

• Sheikh Abdul-Latif al-Subki, Mkuu wa Kamati ya Fat’wa na Sheikh muhimu miongoni mwa wafuasi wa madhehebu ya Hanbali katika al-Azhar aliandika makala yenye lugha kali na kushambulia suala la kutaka kuleta ukuruba baina ya Shia na Sunni na kulitaja hilo kuwa liko mbali na ukweli na linafanyika kwa upande mmoja tu kutoka kwa Ahlul Sunna. [21]

• Yusuf al-Qardhawi, alikana kikamilifu kutolewa fat’wa kama hiyo na Shaltut. Hoja yake ni kutokuweko kwa fat’wa hiyo katika vitabu vya Shaltut. Mkabala wake, Muhammad Hassun ameyatambua madai ya Qardhawi kuwa batili kutokana na hoja mbalimbali kama vile, kutolewa baadaye fat’wa ya Shaltut baada ya kuwa vitabu vyake vilishachapishwa kabla na vilevile matamshi ya wazi ya Mufti wa Misi Ali Gomaa katika kanali ya al-Ekhbariyah. [22]

• Omar Abdallah Ahmad, aliandika makala ambayo ndani yake alinukuu ibara na matamshi ya baadhi ya Maulamaa wa Kisunni katika kupinga mitazamo ya Mashia na hivyo kuipa changamoto fat’wa ya Shaltut. [23]

• Abul-Wafaa Kiristani alimuandikia barua Shaltut na kuuliza maswali na hivyo kumkosoa. Mamhmod Shaltut naye alijibu barua hiyo ambapo sambamba na kujibu maswali hayo alitoa ufafanuzi kuhusiana na fat’wa yake hiyo. [24]