Usul al-Kafi

Kutoka wikishia

Isichanganwe na kufahamika kimakosa na al-Kafi (kitabu).

Usul ala-Kafi ni anuani ya sehemu ya kwanza ya sehemu tatu za kitabu cha hadithi cha al-Kafi. Sehemu hii ni makhsusi kuhusiana na hadithi zilizopokewa kuhusiana na itikadi za Waislamu wa Kishia na maisha ya Maimamu wa Kishia na kumekusanywa humo baadhi ya hadithi zinazohusiana na miamala ma mienendo ya mtu binafsi Mwislamu. Usul al-Kafi, ni moja ya vyanzo muhimu sana vya itikadi za Waislamu wa Kishia ambapo kimechapishwa na kusambazwa mara chungu nzima kikiwa kando na chenye kujitegemea mbali na kitabu cha al-Kafi kama ambavyo kimetrajumiwa kwa lugha nyingine na kuandikwa vitabu vinavyotoa sherhe na ufafanuzi wa Usul al-Kafi.

Mwandishi

Makala kuu: Muhammad bin Ya’qub al-Kulayni

Abu Ja'far Muhammad bin Ya'qub bin Is'haq al-Kulayni al-Razi mashuhuri kwa “Thiqatul al-Islam al-Kulayni (aliaga dunia 329 Hijria), ni mmoja wa wasomi na wanazuoni wakubwa wa elimu ya hadithi na mwandishi wa kitabu cha al-Kafi moja ya vitabu vya hadithi vyenye itibari kubwa kwa Mashia na ni moja kati ya vitabu vinne (Kutub al-Ar’baa) vya hadithi vya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Yeye alizaliwa katika zama za Ghaiba ndogo ya Imamu Mahdi (atfs) na alikutana na baadhi ya wapokezi wa hadithi waliosikia hadithi moja kwa moja kutoka kwa Imamu Hassan al-Askary (as) au Imamu al-Hadi (as). Inaelezwa kuwa Shekhe al-Kulayni alikuwa na umakini mno katika kunukuu hadithi. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Ibn Qulawayh, Muhammad bin Ali Majilawayh al-Qummi na Ahmad bin Muhammad al-Razi.

Utambulisho wa kitabu

Usul ala-Kafi ni anuani ya sehemu ya kwanza kati ya sehemu tatu za kitabu cha hadithi cha al-Kafi. Sehemu hii ni makhsusi kuhusiana na hadithi zilizopokewa kuhusiana na itikadi za Waislamu wa Kishia na maisha ya Maimamu wa Kishia na kumekusanywa humo baadhi ya hadithi zinazohusiana na miamala ma mienendo ya mtu binafsi ya Mwislamu (hadithi 3,758). Katika sehemu nyingine mbili za kitabu, mwandishi amejihusisha na hadithi za maudhui za kifiq’hi na mawaidha na nasaha za kimaadili (kiakhlaq). [1] Kwa kuzingatia kwamba, kitabu cha al-Kafi ndicho pekee kilichojihusisha na hadithi za kiitikadi miongoni mwa Kutub al-Ar’baa (vitabu vinne vya hadithi vya Mashia), sehemu ya kitabu hiki daima imekuwa ikizingatiwa na Waislamu wa Kishia na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana imechapishwa kama kitabu kinachojitegemea. Maulamaa wa Kishia wameandika vitabu mbalimbali vya kufafanua Usul al-Kafi kama ambavyo sehemu hii ya kitabu cha al-Kafi imetarjumiwa kwa lugha ya Kifarasi na kuchapishwa. Milango ya Usul al-Kafi

Usul al-Kafi kinaundwa na sehemu kuu nane jumla ambapo Shekhe al-Kulayni ametambulisha kila sehemu miongoni mwa sehemu hizi kwa anuani ya kitabu. Anuani hizo jumla ni:

• Kitab al-Aql Wal-Jahl.

• Kitab Fadh al-Ilm, kinajumuisha milango 22.

• Kitab al-Tawhid, kina milango 35.

• Kitab al-Hujjah, kina milango 130, na ndani yake kuna hadithi kuhusiana na udharura wa Imamu, majina ya Maimamu wa Kishia, sifa zao, sira na mwenendo wao na hoja za kuthibitisha Uimamu wao.

• Kitab al-Iman Wal-Kufr, kinajumuisha milango 209.

• Kitab al-Duaa, kinaundwa na milango 60.

• Kitab Fadhl al-Qur’an, kina jumla ya milango 14.

• Kitab al-Ish’rah, kina milango 29.

Kitabu cha kwanza cha Usul al-Kafi ni Kitab al-Aql Wal-Jahl na hadithi ya kwanza ya kitabu hiki imenukuliwa kutoka kwa Imamu Muhammad Baqir (as) kuhusiana na nafasi na daraja ya akili katika uumbaji na kigezo chake kwa ajili ya taklifu za Mwenyezi Mungu, adhabu na ujira. [2] Kitabu cha mwisho cha Usul al-Kafi ni Kitab al-Ish’rah na mlango wake wa mwisho ni mlango wa kukataza kuchoma karatasi yenye maandishi na hadithi ya mwisho ni kutoka kwa Imamu Kadhim (as) kuhusiana na kile ambacho kimeandikwa jina la Mwenyezi Mungu nyuma yake amesema: Kioshe kwa maji. [3]

Sherhe

Waliotoa sherhe na ufafanuzi wa al-Kafi wamegawanyika makundi mawili; kundi la kwanza ni lile ambalo limetoa sherhe na ufafanuzi wa kitabu chote cha al-Kafi ikiwemo sehemu yake ya Usul al-Kafi. Ama kundi la pili lenyewe limejihusisha tu na kutoa sherhe na ufafanuzi wa Usul al-Kafi. Vitabu mashuhuri viliavyoandikwa kutoa sherhe na ufafanuzi wa Usul al-Kafi ni:

• Dirakhshan partu'i az usul al-Kafi kilichoandikwa na Sayyid Muhammad al-Husayni al-Hamadani kwa lugha ya Kifarsi kikiwa na juzuu 6.

• Sharh Usul al-Kafi, mwandishi: Sadr al-Din Muhammad al-Shirazi anayejulikana pia kwa jina la Mulla Sadra. Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu na kina juzuu tatu.

• Sharh al-Kafi, kilichoandikwa na Mulla Salih Mazandarani kwa lugha ya Kiarabu na kina juzuu 12.

• Al-Dhari'a ila hafidh al-Shari'a, mwandishi: Muhammad bin Muhammad Mu'min Gilani, kina juzuu mbili.

• Al-Hashiya 'ala usul al-Kafi mwandishi: Muhammad Amin al-Astarabadi.

• Al-Hashiya 'ala usul al-Kafi mwandishi: Sayyid Ahmad b. Zayn al-'Abidin al-'Alawi al-'Amili.

• Al-Hashiya 'ala usul al-Kafi mwandishi: Sayyid Badr al-Din bin Ahmad al-Husayni al-'Amili.

Mbali na vitabu hivyo, kuna vitabu vingine vilivyoandikwa kutoa udfafanuzi wa Usul al-Kafi ambavyo havikukamilika.

Tarjumi za Kifarsi

• Tarjumi ya Muhammad Baqir Kameraei, kilichosambazwa na al-Maktabat al-Islamiyah Tehran kikiwa na juzuu 4.

• Tarjumi ya Muhammad Baqir Kameraei, kilichochapishwa na taasisi ya uchapishaji ya Us’wa kikiwa na juzuu 6.

• Tarjumi ya Seyyid Jawad Mustafawi.