Udhu al-Irtimasi

Kutoka wikishia

Udhu al-Irtimasi au Udhu wa Kuchovya (Kiarabu: الوضوء الارتماسي) Ni mojawapo ya njia za kutia udhu ambapo, baada ya mtu kutia nia, [1] Huingiza uso na kisha mikono yake ndani ya maji kwa nia ya kutia udhu. [2] Pia ni halali kwa mtia udhu kuingiza viungo ndani ya maji, kisha atie nia ya udhu, na kisha avito viungo hivyo nje ya maji. [3] Katika udhu wa al-Irtimasi, baada ya mtu kuingiza uso na mikono yake ndani ya maji, hufuatia tendo la kufuta kichwa na miguu. [4]

Irtimasi ni neno la lugha ya kisheria (kifiqhi) linalomaanisha kuingiza kichwa au viungo vyengine vya mwili ndani ya maji. [5] Suala la mfuatanisho na mpangilio wa udhu katika udhu wa al-Irtimasi ni sawa na udhu wa kawaida. Yaani mwanzo huanzwa uso kisha mkono wa kulia na kisha mkono wa kushoto.

Katika udhu al-Irtimasi, uso na mikono huanzwa kuoshwa kutoka juu kwenda chini; uso huanzwa kuoshwa kutoka kwenye paji la uso chini (mwishoni mwa kidevu), na mikono huingizwa ndani ya maji kuanzia viwikoni. Hata hivyo, ikiwa mtu kwanza atavizamisha viungo vyake kwenye maji kisha akatia nia ya udhu, katika hali hiyo itambidi kuutoa uso wake kuanzi juu ya komo (mwanzo mwa maoteo ya nywele), kisha aitoe mikono kwa kuanzia viiwikoni mwa mikono hiyo. [6]

Kulingana na Fat’wa ya Imamu Khomeini ni kwamba; Katika udhu wa al-Irtimasi, yaruhusiwa mtu kuingiza mikono na uso wake ndani ya maji mara mbili tu: ambapo mara ya kwanza ni wajibu na mara ya pili ni sunna, na zaidi ya hapo haijuzu. [7] Baadhi ya wanazuoni wameruhusu kuosha baadhi ya viungo udhu kwa njia ya Irtimasi na vyengine kwa njia ya udhu wa kawaida (udhu wa tartiibi). [8]

Baadhi ya wanazuoni wameainisha masharti maalumu, ili kuhakikisha kwamba; katika udhu wa irtimasi suala la kufutwa kwa kichwa na miguu kupitia mabaki ya maji ya udhu kunazingatiwa, vinginevyo wudhu wa Irtimasi hautakuwa sahihi. Sharti hizo ni kama ifuatavyo:

  • Imamu Khomeini anaamini kwamba; ili kufutwa kwa kichwa na miguu kutimie kupitia mabaki ya maji ya udhu katika udhu huo wa irtimasi, ni lazima udhu wa Irtimasi ufanyike kwa kuwekwa mikono ndani ya maji, kisha nia ya udhu ifanyike, na kisha mikono iondolewe kutoka kwenye maji hayo. [9]
  • Sayyid Abu al-Qasim al-Khuei na Mirza Jawad Tabrizi, miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, wanaamini kwamba haiwezekani (haijuzu) kuoshwa mkono wa kushoto kwa njia ya Irtimasi.
  • Sayyid Ali al-Sistani, mmoja wa mafaqihi wa Kishia, haioni kuwa na kasoro kufuta kichwa na miguu kupitia mabaki ya maji ya mikono iliyo oshwa kwa njia ya Irtimasi, lakini ameiona kuwa; kufanya hivyo ni kinyume cha tahadhari (ihtiyat). [11]
  • Naser Makarem Shirazi, mmoja wa mafaqihi wa Kishia, anaamini kuwa baada ya mtu kuondoa mikono yake kutoka majini, mtu huyo anapaswa kuwa na nia ya kwamba bado yuko kwenye udhu katika wakati wote ambapo maji hayo yatakuwa bado yanaendelea kutiririka juu ya mikono yake. [12]

Maudhui zinazo fungamana

Vyanzo

  • Bahjat Fūmanī, Muḥammad Taqī. Tawḍīḥ al-masāʾil. Qom: Intishārāt-i Shafaq, 1428 AH.
  • Khāmeneʾī, Sayyid ʿAlī. Ajwabat al-istiftāʾāt. Qom: Markaz-i Nashr-i Āyatollāh Khāmeneʾī, 1420 AH.
  • Khomeinī, Sayyid Rūḥ Allāh. Najāt al-ʿibād. Second edition. Tehran: Muʾassisa-yi Tanẓīm wa Nashr-i Āthār-i Imām Khomeini, 1385 Sh.
  • Khomeiniī, Sayyid Rūḥ Allāh. Tawḍīḥ al-masāʾil. Edited by Muslim Qulipur Gilani. [n.p]: 1426 AH.
  • Khomeiniī, Sayyid Rūḥ Allāh. Tawḍīḥ al-masāʾil (muḥashā). Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn-i Ḥawza-yi ʿIlmiyya, 1424 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tawḍīḥ al-masāʾil. Qom: Madrasat al-Imām ʿAlī b. Abī Ṭālib (a), 1429 AH.
  • Qummī, Abu l-Qāsim. Jāmiʿ l-Shitat fī Ajwabat al-suʾālāt. Tehran: Keyhān, 1413 AH.
  • Shāhrūdī, Sayyid Maḥmūd. Farhang-i fiqh muṭābiq bā madhhab-i Ahl al-Bayt. Qom: Muʾassisat Dāʾirat al-Maʿārif al-Fiqh al-Islāmī, 1426 AH.