Nenda kwa yaliyomo

Tawhidi katika ngazi ya Matendo

Kutoka wikishia

Tawhidi katika Ngazi ya Matendo (Kiarabu: التَّوحيد الأفعالي) ni imani muhimu yenye maana ya kwamba; kila tukio litokealo ulimwenguni humu, yakiwemo matendo ya viumbe mbali mbali, hutekelezwa na kujiri kupitia idhini, nguvu pamoja na matakwa ya Mwenye Ezi Mungu mwenyewe. Dhana hii inaonesha kuwa Mwenye Ezi Mungu ni chanzo cha kila kitu. Wanazuoni wa Kiislamu wameshimamisha hoja mbali mbali katika kuthibitisha imani hii. Ili kutetea imani ya kwamba; Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, wanazuoni hawa wametumia hoja kadhaa, zikiwemo njia za kiakili pamoja na Aya mbali mbali za Qur'ani.

Kwa mujibu wa itikadi ya Ash’ari, inayojikita katika Tawhidi ya Matendo (upwekeshaji kwenye ngazi ya matendo), ni kwamba; mwanadamu hana hiari yoyote ile katika undendaji wa matendo yake mbali mbali. Kinyume chake, ni itikadi ya Mu'tazila inakubaliana na Tawhidi kwenye ngazi ya Matendo, lakini inakataa itikadi ya kumchukulia Mwenye Ezi Mungu kuwa ndio chanzo cha matendo ya hiari ya mwanadamu, ikihusisha matendo hayo na mwanadamu pekee (yaani wanakataa uwepo wa mkono wa Mungu katika matendo hayo). Kwa upande wa Mashia Imamiyya ni kwamba; wao wanapingana na misimamo yote miwili, ila wao wanasisitiza kwamba: Imani ya Tawhidi katika ngazi ya Matendo haimaanishi kupuuza uhuru wa mwanadamu. Badala yake, wanasema kwamba; matendo ya hiari ya mwanadamu yanahusishwa na pande zote mbili, yaani Mwenye Ezi Mungu pamoja na mwanadamu mwenyewe.

Aidha, imani ya Tawhidi (upwekeshaji Mungu) katika ngazi ya Uumbaji na (upwekeshaji Mungu) Tawhidi katika ngazi ya Upangaji (uendeshaji), ni sehemu mbili asilia za imani ya Tawhidi (upwekeshaji) katika ngazi ya Matendo. Pia kutegemea Mungu kikamilifu na kumwabudu Mwenye Ezi Mungu pekee, ni matokeo ya imani juu ya Upwekeshaji katika Ngazi ya Matendo.

Maana ya Tawhidi (Upwekeshaji) Katika Ngazi ya Matendo

Tawhidi (upwekeshaji) katika ngazi ya Matendo, ni moja ya sehemu muhimu za imani ya Tawhidi (upwekeshaji) katika dini ya Kiislamu, ambayo inajumuisha ndani yake vifungu vinne vya Tawhidi: Tawhidi Katika Ngazi ya Dhati (ذاتی), Tawhidi katika Ngazi ya Sifa (صفاتی), Tawhidi ya Ngazi ya Ibada (عبادی), na Tawhidi ya Ngazi ya Matendo (اَفعالی). [1] Katika mgawanyo wa Tawhidi katika sehemu mbili za; Tawhidi Katika Ngazi ya Nadharia na Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo, Tawhidi ya Matendo inachukuliwa kuwa moja ya matawi ya Tawhidi Katika Ngazi ya Nadharia. Hii inaonyesha kuwa dhana ya Tawhidi ya Matendo inahusiana na welewa wa jinsi Mungu anavyoendesha matendo yatokeayo ulimwengu humu, huku ikisisitiza uhusiano kati ya Mungu na viumbe kupitia Matendo vyao. Katika muktadha huu, Tawhidi ya Matendo inaeleza kwamba kila tendo linalotokea, iwe ni la binadamu au la viumbe wengine, lina asili ya idhini na uthibitisho wa matakwa ya Mwenye Ezi Mungu, kwa hivyo, inasisitiza upweke na uwezo wa Mungu katika uendeshaji wa ulimwengu. [2]

Kwa mujibu wa maelezo ya Murtadha Mutahhari, ni kwamba; Imani ya Tawhidi katika Ngazi ya Matendo inasisitiza kwamba: mifumo yote ulimwenguni ya sababu na athari (matukio) yanayojiri kupiti sababu hizo, pamoja na kila kitu kitokeacho ulimwenguni humu, ni miongoni mwa matendo ya Mwenye Ezi Mungu. Hii ina maana kwamba hakuna kiumbe chochote kinachoweza kufanya tendo lolote lile kupitia uhuru wake mwenyewe bila idhini ya Mungu; na kila kiumbe katika utendaji wake, hutegemea tendo la Mungu na matakwa Yake katika utekelezaji wa matendo hayo. [3]

Kulingana na imani ya Tawhidi (upwekeshaji) katika Ngazi ya Matendo, ni kwamba; kama ilivyo kwamba Mwenye Ezi Mungu hana mshirika katika Dhati Yake, vivyo hivyo pia hana mshirika katika utendaji wake. Hii ina maana kwamba kila kitu chochote kile kitendwacho na kiumbe fulani hijiri kupitia matendo ya na idhini ya Mungu. [4] Tawhidi katika Ngazi ya Matendo, ni sawa na Tawhidi ya katika Ngazi Dhati na katika Ngazi ya Sifa, ni sehemu ya ngazi za Tawhidi za nadharia, ambayo inahusiana na imani na itikadi ya mwanadamu. Hii ni tofauti na Tawhidi katika Ngazi ya Ibada, ambayo inahusiana na matendo pamoja na ibada ya kumwabudu Mwenye Ezi Mungu. [5]

Katika vyanzo vya kale pamoja na baadhi ya vyanzo vya kisasa vya elimu ya theolojia, hakuna vichwa vya habari vyenye majina ya Tawhidi katika Ngazi ya Matendo (Tawhidu fi Al-Af’aali) au Tawhidi katika Ngazi ya Uumbaji (Tawhidu fi Al-Khaaliqiyya) wala Tawhidi katika Ngazi ya Uendeshaji (Tawhidu Al-Rububiyya). Badala yake, suala hili limejadiliwa chini ya mada mbali mbali zikiwemo; Uumbaji wa Matendo (Kahlqu Al-Af’aali), Muumba wa Ulimwengu (Saani’u Al-Kauni), Mweza (Qaadir), Mtakaji (Muridu) na nyenginezo. Hata hivyo, katika baadhi ya kazi za kisasa za kiteheolojia, Tawhidi katika Ngazi ya Matendo imejadiliwa sambamba na Tawhidi katika Ngazi ya Dhati na Tawhidi katika Ngazi ya Sifa. Katika baadhi ya maandiko, Tawhidi katika Ngazi ya Matendo pia imejumuishwa na kuwekwa sambamba na muktadha wa Tawhidi katika Ngazi ya Uumbaji, Uendeshaji (Rubuubiyya), Utawala (Haakimiyya), na Upangaji wa Sheria. [6]

Aina za Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo

Katika baadhi ya maandiko kuhusiana na elimu ya theolojia (elmu al-kalam), dhana ya Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo imejadiliwa kupitia majina mengine kama vile; Tawhidi Katika Uumbaji (Tawhid fi Al-Khaliiyya) na Tawhidi Katika Uendeshaji (Tawhid fi Al-Rububiyya). [7] Tawhidi Katika Ngazi ya Uumbaji inarejelea ukweli wa kwamba; kila kilichopo katika ulimwenguni ni kiumbe kilichoumbwa na Mwenye Ezi Mungu, [8] na hata vile vilivyotengenezwa au vinavyotokana na viumbe vingine, vyote vinabaki kuwa ni sehemu ya uumbaji wa Mwenye Ezi Mungu. [9] Kwa upande mwingine, Tawhidi Katika Ngazi ya Uendeshaji (Tawhid fi Al-Rububiyya) inaashiria na kusisitiza ya kwamba; Mwenye Ezi Mungu ndiye anayesimamia na kudhibiti mipango yote ya ulimwengu pamoja na viumbe wake. Hii inamaanisha kwamba; Mwenye Ezi Mungu ameweka utaratibu na mfumo maalum ulimwenguni humu, ambao kwa mujibu wake kila mmoja kati ya viumbe wake huweza kutimiza na kufikia kiwango cha malengo yaliyo ainishwa kwa ajili yake. [10]

Ali Rabbani Golpaygani ameashiria baadhi ya Aya zinazothibitisha Tawhidi ya Mwenye Ezi Mungu katika Uumbaji. Miongoni mwa Aya zilizo tajwa na mwanazuoni huyu, ni Aya ya 16 ya Surat Ar-Ra’d, Aya ya 62 ya Surat Az-Zumar, pamoja na Aya ya 62 ya Surat Ghafir. Kwa mujibu wa maelezo ya Aya hizi, Mwenye Ezi Mungu ndiye muumbaji wa kila kitu «خالقُ کلِّ شی».[11] Kwa upande wa Tawhidi Katika Ngazi ya Uendeshaji (Tawhid fi Al-Rububiyya), Aya muhimu zinazothibitisha jambo hili ni pamoja na Aya ya 54 ya Surat Al-A’raf inayosema: (أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ‌ ; Tambueni ya kwamba uumbaji na uendeshaji ni wa Mwenye Ezi Mungu pekee). Vilevile Aya ya 50 ya Surat Ta-Ha inasema: (رَ‌بُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ; Mola wetu ni yule aliyeumba kila kitu na kisha akaiongoza). [12] Aya mbili hizi za mwisho zinaeleza kwa uwazi kabisa dhana ya Tawhidi Katika Ngazi ya Uumbaji pamoja na Tawhidi Katika Ngazi ya Uendeshaji. [13]

Hoja za Kiakili Kuhusiana na Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo

Wanafalsafa wa Kiislamu wametoa hoja mbalimbali katika kuthibitisha Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo. Kwanza kabisa, wameanza kwa kutoa ufafanuzi usemao kwamba; kila kiumbe ulimwenguni humu, ima ni kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, ni matokeo ya uumbaji wa Mwenye Ezi Mungu. Pili, chanzo cha kupatikana kwa kitu kifulani, kinachukuliwa kuwa ndio msingi wa uhalisia wa kuwepo kwa kitu hicho. Kwa hivyo, Mwenye Ezi Mungu ndiye chanzo na muumbaji wa viumbe vyote vilivyomo ndani ya ulimwengu wa matokeo (ulimwengu wa uwepo). [14]

Muhammad Taqi Misbah Yazdi, akifuata fikra za Sadr al-Muta’allihin na misingi ya falsafa za Hikmatu Al-Muta'aliya (Hekima za Ngazi za Juu), ambazo ni fikra za Mulla Sadra, anatoa hoja thabiti zaidi katika kujenga hoja za kifalsafa. Akielezea suala hili anasema kwamba; Hakuna hata Sababu moja mingoni mwa mwa visababishaji vya matokeo mbali mbali yenye uhuru binafsi katika utendaji wake. Kwa maana nyingine, kila kisababishi ni chenye kumtegemea Mwenye Ezi Mungu kwa kila hatua miongoni mwa hatua zake. Kwa hivyo, haiwezekani kiumbe chochote kile kuwa na uwezo kutekeleza tendo lolote lile kwa uhuru kamili, bila kutegemea nguvu ya Mwenye Ezi Mungu. Hii ina maana ya kwamba;  uumbaji ni kazi ya Mwenye Ezi Mungu peke yake. [15]

Ushahidi wa Qur'ani Kuhusiana na Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo

Ili kuthibitisha Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo, wanazuoni wa Kiislamu wametaja Aya na Riwaya kadhaa, kama ushahidi katika kuonesha kuwa; Mwenye Ezi Mungu ndiye mwenye Mamlaka pekee katika sekta ya uumbaji. Murtadha Mutahari, akitoa ufafanuzi ba maelezo kuhusiana na Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo, ameitaja Aya ya 111 ya Surat Al-Isra kama ni ushahidi wa hajo zake. [16] Katika Aya hiyo Mwenye Ezi Mungu anasema: Wa qul alhamdu lillahi alladhi lam yattakhidh waladan wa lam yakun lahu sharikun fil mulk wa lam yakun lahu waliyyun minadh dhull «وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِ‌يكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ» (Na sema: Sifa njema zote ni za Mwenye Ezi Mungu ambaye hakujichagulia mwana, wala hana mshirika katika ufalme wake, wala hana rafiki kwa sababu ya udhaifu fulani). Aya hii inaonesha wazi kwamba Mwenye Ezi Mungu hana mshirika wala msaidizi katika kuutawala ulimwengu. Vilevile, kulingana na imani ya Motahari; Kauli ya: «Kigezo:Arsbic» (Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu), ni moja ya dalili ya wazi inayothibitisha Tawhidi (upweke wa Mungu) Katika Ngazi ya Matendo. [17]

Kwa mtazamo wa Muhammad Taqi Misbah Yazdi; Aya ya 22 ya Suratu Al-Anbiya, ni msingi muhimu wa kuthibitisha Tawhidi ya Ufalme wa Matendo. Aya hii imekuja kwa ibara isemayo: ‎لو کَانَ فِیهِمَا آلِهَةٌ إلاَّ اللّٰهُ لَفَسَدَتَا (Kama ingekuwa kwenye mbingu na ardhi kuna Miungu zaidi ya Mungu Mmoja, basi mbingu na ardhi zingeharibika). Kwa mujibu wa maoni ya Misbah Yazdi, Aya hii imekuja kuthibitisha kwamba ulimwengu una Mungu mmoja tu. [18]

Misbah Yazdi anaelezea hoja ya kiakili iliyotumika katika Aya hii kwa kama ifuatavyo:

  1. Kama suala la uumbaji lingelikuwa limetawaliwa na sababu (Muumba) zaidi ya moja, basi kamwe isingewezekana vimbe vilivyomo ndani ya ulimwengu huu kufuata muundo wenye mfumo mmoja wa kimaumbile, kwani kiasilia, kila kiumbe hufungamana na chanzo chake binafsi, na wala hakikubali kuchukua athari (mfumo) kutoka kwenye chanzo chengine.
  2. Kiuhalisi ulimwengu unaonyesha kuwa unafuata mpangilio mmoja thabiti, na kuna uhusiano maalum kati ya wahusika wote waliomo ulimwenguni.
  3. Kwa hiyo, bila shaka ulimwengu huu una chanzo kimoja tu cha msingi, nacho ni yule Muumba pekee na mmoja tu. [19]

Natija Mbili za Imani Juu ya Tawhidi ya Katika Ngazi ya Matendo

Kuna aina mbali mbali za natija zilizo orodheshwa katika baadhi ya kazi andishi za fani theolojia ya Kiislamu, kuhusiana na imani juu ya Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo. Miongoni mwazo ni kutegemea Mungu pekee (kutawakali). Kwa mujibu wa maoni ya Muhammad Taqi Misbah Yazdi, mtu anayekubaliana na imani ya Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo hutambua na kuamini kwamba, hakuna kiumbe anayestahili kuabudiwa ila Mwenye Ezi Mungu. Hii inatokana na ukweli wa kwamba; ni Mungu pekee aliye Muumba na Mlezi wa mwanadamu, na hivyo ni Yeye pekee ndiye anayestahiki ibada na kutegemewa kikamilifu. [20]

Zaidi ya hayo, kwa mujibu wake, ni kwamba; Kwa kuwa iamni ya Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo inaonesha kwamba: ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye kutenda na kuathiri ulimwenguni humu kwa uhuru kamili, na bila kutegemea kiumbe kingine. Hivyo basi, yeye pekee ndiye anayepaswa kutegemewa katika kila jambo. [21] Muhammad Taqi Misbah Yazdi anabainisha kwamba; Aya isemayo: اِیّاکَ نَعبُدُ وَ اِیّاکَ نَستَعین (Ni Wewe pekee tunaye kuabudu, na ni Wewe pekee tunaye kuomba msaada), imekuja kufafanua imani hii muhimu ya Tawhidi ya Katika Ngazi ya Matendo. [22]

Uhusiano kati ya Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo na Hiyari ya Mwanadamu

Makala kuu: Hiyari ya Mwanadamu

Ingawa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu yanakubaliana na msingi wa Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo, ila wanatofautiana kuhusiana na athari zake juu ya hiyari na uhuru wa mwanadamu. [23] Ash'ariyah wanasema kwamba; Kwa kuwa hakuna msababishaji mwingine isipokuwa Mwenye Ezi Mungu pekee, basi mwanadamu hawezi kuwa ni msababishaji halisi wa vitendo vyake; kwa mtazamo wao, vitendo vya mwanadamu si vitendo vyake mwenyewe bali ni vitendo ya Mungu. [24] Kwa upande mwingine, Mu'tazilah wanasisitiza imani isemayo kwamba; Mwenye Ezi Mungu amewapa wanadamu hiyari na uhuru kamili juu ya matendo yao, hivyo wanadamu wana uwezo wa kutenda matendo yao kwa uhuru kamili. Kwa hiyo vitendo vyao si vitendo vilivyo umbwa na Mwenye Ezi Mungu, bali ni matendo yao wenyewe. [25]

Wafuasi wa madhehebu ya Shia Imamiyyah wamechukua msimamo wa kati na kati juu ya suala hili. Wao wanasema kwamba; Ingawa mwanadamu ana hiyari ya kutekeleza vitendo vyake mwenyewe, ila yeye hana uhuru kamili juu ya ukamilishaji wa matendo yake, hii ni kwa kuwa Mwenye Ezi Mungu ndiye msababishaji msingi wa kila kitendekacho. [26] Kwa mtazamo wa wanatheolojia wa Kishia, msimamo wa Ash'ariyyah unapingana na majukumu ya kimaadili aliyowekewa mwanadamu kutoka kwa Mungu wake, pia imani yao inakwenda kinyume na suala la malipo ya thawabu na adhabu za Akhera. [27] Ukiachana na mtazamo wa Ash'ariyyah, pia mtazamo wa Mu'tazilah nao unakosolewa kwa kudhoofisha Tawhidi Katika Ngazi ya Uumbaji pamoja na mamlaka ya Mungu juu ya kila kitu. [28] Kwa mtazamo wa Kishia, Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo haipingani na hiyari ya mwanadamu, hii ni kutokana na kwamba; vitendo vya mwanadamu vinafanyika ndani ya matakwa na mpangilio wa vitendo vya Mungu mwenyewe. Hivyo basi, vitendo vya mwanadamu vinaweza kutambuliwa kama ni vitendo vya Mwenye Ezi Mungu, huku pia vikihusishwa na mwanadamu mwenyewe kwa wakati mmoja. [29]

Bibliografia

Kuna vitabu kadhaa vilichapishwa kuhusiana na muqtadha wa Tawhid Katika Ngazi ya Matendo (Tawhidi Af’ali), na miongoni mwa hivyo ni:

  • «Tawhidi Af’ali az Negahe Mazahibu wa Firaqe Islami» (Tawhid Katika Ngazi ya Matendo Kulingana na Maoni ya Madhehebu na Makundi ya Kiislamu), kilichoandikwa na Hassan Torkashwand. Kitabu hichi kinafafanua maana halisi ya Tawhid Katika Ngazi ya Matendo (Tawhidu Af’ali), na kutoa muhtasari na tathmini ya mitazamo ya madhehebu na makundi ya Kiislamu, huku kikitoa uchambuzi wa mtazamo wa Uwahabi juu ya mada hii. [30]
  • «Tawhidi Af’ali dar Aasare As-Sadiqain (a.s)» Tawhidi Katika Ngazi ya Matento Kutoka Katika Vyanzo vya As-Sadiqain (yaani Imamu Baaqir na Imamu Sadiq) (a.s). Kilichoandikwa na Mahdi Erteghaei akishirikiana na Mahdi Safaei-Asl. Waandishi wameigawanya milango ya kitabu hichi katika sura nne: hatua za Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo, uhusiano wa Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo na suala la sababu na visababishaji vya matukio, hiari ya mwanadamu na matukio ya mabalaa, na natija juu ya imani ya Tawhidi Katika Ngazi ya Matendo. Wamefanya hivyo wakitegemea mafundisho yatokayo kwa Imamu Baqir (a.s) na Imamu Swadiq (a.s). [31]
  • «Tawhidi Af’ali dar Sahife Sajjadiyya» (Tawhid Katika Ngazi Matendo Kutoka Katika Kitabu cha Sahifa Sajjadiyya), kilichoandikwa na Mahdi Safai-Asl. Kitabu hichi kinafafanua masuala ya Tawhid Katika Ngazi Matendo na aina zake kwa mujibu wa kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. [33]

Maudhui Zinazo Fungamana

Rejea

Vyanzo