Nenda kwa yaliyomo

Kutawakali

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Tawakkul)

Tawakkul (Kiarabu: التوكل) Istilahi ya tawakkul ina ya sifa moja maalumu ya kimaadili, ambayo huhisabiwa kuwa ndiyo nguzo na msingi mkuu katika maisha ya kiroho. Neno tawakkul linatokana na neno la Kiarabu lenye maana ya kutawakali. Kutawakali humaanisha hali ya kuwepo kwa sifa maridhawa ya kumwachia Mwenye Ezi Mungu mamlaka kamili ya mambo yote na kumtegemea Yeye peke yake kama chanzo cha athari zote katika maisha ya mwanadamu. Qur'an Tukufu imeweka wazi kwamba; tawakkul ni sharti lazimifu lenye kufungamana na imani kamili. Aidha, hadithi za bwana Mtume (s.a.w.w) zimeielezea tawakkul kama ni mojawapo ya nguzo muhimu za imani, zinazomfanya muumini kuwa na uhusiano thabiti na Mwenye Ezi Mungu. Wanazuoni wa maadili, kwa kutumia busara zao za kiakili na kiroho, wameifasiri tawakkul wakisema kwamba: Takkul ni hali thabiti ya mwanadamu, ambayo hubaki imara bila kuyumba, kabla na baada ya kupata au kupoteza mali.

Kiwango cha juu kabisa cha kutawakali ni kile kitendo cha mwanadamu cha kukabidhi mambo yake yote kwa Mwenye zi Mungu, bila kujipa hiari yoyote mbele ya maamuzi ya Mwenye Ezi Mungu, na kuridhika na chochote kile ambacho Mwenye Ezi Mungu amemwandikia. Kiwango cha tawakkul kwa kila mtu kinategemea kiwango chake cha imani na kuamini kwa dhati juu ya upweke wa Mwenye Ezi Mungu.

Kwa mujibu wa wanazuoni wa masuala ya kimaadili, ni kwamba; katika dini ya Kiislamu, tawakkul haina maana ya kujipwetesha, na wala tendo la kutawakkal halipingani na tendo la kufanya kazi kwa bidii huku ukifahamu kwamba; kwamba Mwenye Ezi Mungu ndiye mleta athari wa kila kitendo ukitendacho. Hii ni kwa sababu, vyanzo na visingizio (visababishi) vya nje havina athari za kujitegemea; athari zao zinategemea matakwa ya Mwenye Ezi Mungu na ziko chini ya nguvu za Mwenye Ezi Mungu. Miongoni mwa athari za kutawakali ni: kutosheka na riziki, urahisishwaji wa mambo, na kupata heshima mbele ya watu wengine na kuthaminiwa mbele ya Mwenye Ezi Mungu.

Welewa wa Dhana ya Tawakkul (Kutawakali)

Tawakkul inamaanisha kujidhihirisha kuwa huna uwezo wa kutekeleza jambo fulani, badala yake kumtegemea mwingine juu ya jambo hilo. [1] Kwa mujibu wa maelezo ya Muhammad Mahdi Naraqi katika kitabu chake Jami'u al-Sa'adat, ni kwamba; tawakkul katika utamaduni wa dini ni kutua na kukiri kwamba Mwenye Ezi Mungu pekee ndiye mwenye athari katika utendekaji wa mbambo mbali mbali. Hivyo, mwanadamu apaswa kumtegemea Yeye tu, na yuwatakiwa kukata tamaa kutoka kwa wengine, na kuacha mambo yake yote mikononi mwa Mwenye Ezi Mungu. [2]

Allama Tabataba'i pia naye ameifasiri tawakkul kwa maana ya kumtambua Mwenye Ezi Mungu kwamba ndiye mleta athari pekee katika mambo yote ulimwenguni. [3] Sheikh Sadouq katika kitabu cha Ma'ani al-Akhbar amenukuu Hadithi kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) inayosema kuwa; maana ya tawakkul kule mtu kutambua ya kwamba; viumbe hawawezi kumletea faida wala madhara, na badala yake kujenga matumaini yake kwa Mwenye Ezi Mungu pekee, na kutomwogopa yeyote isipokuwa Yeye, na kufanya kazi kazi na amali zake kwa kumtumaini Mola wake peke Yake. [4]

Katika kitabu kiitwacho Akhlaq Dar Qur’an, ukweli wa tawakkul umetafsiriwa kuwa ni "kuweka imani ya dhati moyoni juu ya Mwenye Ezi Mungu katika kila hatua ya maisha na kuacha kutegemea vitu vingine kinyume na Mwenye Ezi Mungu." Hii haimaanishi kuwa tunatakiwa kuachana na matumizi ya sababu za kimaisha, juhudi za kimwili, au mipango ya kiakili; badala yake, inasisitiza kwamba vitendo vyote vinapaswa kufanywa huku tukitambua kwamba uwezo wa kweli na nguvu zote zinatoka kwa Mwenye Ezi Mungu tu. [5]

Uhusiano wa Tawakkul na Tafwidh, Rida na Taslim

Tawakkul ina uhusiano wa karibu sana na tafwidh, na uhusiano huu unaweza kufahamika baada kuingia katika tafiti za kidini. Kulaini, katika kitabu chake maarufu Al-Kafi, amekusanya Hadithi za mada ya tafwidh na tawakkul kwenye mlango moja alioita «Bab al-Tafwidh ila Allah wa al-Tawakkul alaihi» (Mlango wa Kuyaweka Mambo mikononi mwa Mwenye Ezi Mungu na Kumtegemea Yeye).[6] Katika utafiti wake Abdulrazzaq Kashani, mwanafalsafa maarufu wa Shia aliyeishi mnamo mwaka wa 735 H., akiielezea tawakkul amesema kuwa; tawakkul ni tawi la tafwidh. [7] Imamu Khomeini katika maelezo yake fafanuzi juu ya “Arba'in Hadith” (Hadithi Arubaini), akifafnua tofauti zilizopo kati ya tawakkuli na tafwidh anasema; “Kuna tofauti muhimu kati ya tawakkul na tafwidh”. Imam Khomeini anaeleza ya kwamba; “Katika tafwidh, mtu hujikuta akiwa hana uwezo wowote ambapo huamini kwamba, Mwenye Ezi Mungu pekee ndiye mwenye nguvu na athari katika mambo yote. Hii ina maana kwamba mtu anajisalimisha kikamilifu mbele ya matakwa ya Mungu bila kujihusisha na juhudi binafsi. Kwa upande mwingine, katika tawakkul, mtu anamchagua Mwenye Ezi Mungu kama wakili wake, akimpa jukumu la kumchagulia lenye kheri na manufaa katika maisha yake. Hii inaonyesha kwamba ingawa mtu anategemea msaada wa Mwenye Ezi Mungu, ila bado anachukua hatua na juhudi za kufanikisha malengo yake, huku akitegemea msaada wa Mwenye Ezi Mungu katika juhudi hizo. [8]

Tofauti hizi zinaonyesha jinsi imani ya Kiislamu inavyotoa mwongozo kuhusu ushirikiano kati ya juhudi za kibinadamu na utegemezi wa Mwenye Ezi Mungu katika maisha yake ya kila siku. Tawakkul ina uhusiano wa karibu na sifa nyingine za kimaadili kama vile ridha (kuridhika) na taslim (kujisalimisha). Kwa mujibu wa maoni ya wanairfani (wazamifu wa bahari ya mapenzi ya Mungu) wa Kiislamu, ni kwamba; daraja za ridha na taslim ziko juu zaidi kuliko daraja ya tawakkul. Katika daraja ya tawakkul, mtu humchagua Mwenye Ezi Mungu kama wakili wake, lakini bado anaweza kuwa na uhusiano na mambo ya kidunia katika kufankisha mahitajio yake. [9] Hata hivyo, katika viwango vya ridha [10] na taslim, [11] mtu hukubali na kuridhika na kila kitu ambacho Mwenye Ezi Mungu amemkadiria, hata kama hakiendani na matarajio ya moyo wake au ni kinyume na kile anacho kitarajia.

Nafasi na Umuhimu wa Tawakkul

Neno «tawakkul» na maneno yake yanayohusiana nalo yametajwa mara 70 katika Qur'ani Tukufu. [12] Katika Aya kdhaa za Qur'an Imani inaonekana kujadiliwa sambamba na tawakkul, [13] na mara kadhaa tawakkul imetambuwa kama ni sifa lazimufu inayofungaman na kulazimiana na Imani. [14] Kwa mfano, katika Sura ya 8, Aya ya 2 (Al-Anfal), waumini wametambulishwa kuwa ni wale wanaomtegemea Mwenye Ezi Mungu peke Yake. Aidha, katika Aya nyingi, kumekuja mafuzo na mwongozo usemao: «وَ عَلی اللّهِ فَلْیتَوَکَلِ المُؤمنون ; Basi waumini wawe ni wenye kutawakali kwa Mwenye Ezi Mungu Mungu». [15] Kulingana na aya za Qur'an, Mwenyezi Mungu anawapenda wale wanaomtegemea, [16] na kwa yeyote anayemtegemea Mwenyezi Mungu, Yeye humtosheleza katika kila hali. [17] Sehemu ya Aya zinazozungumzia tawakkul (kama vile Aya ya 49 na 61 ya Surat Al-Anfal na Aya ya 51 ya Surat At-Tawba), zimekuja zikizungumzia masuala ya jihad na vita dhidi ya makafiri, au amani na kuanzisha mahusiano ya kisiasa na wao, na pia zimekuja zikielezea mtazamo na nyenendo za wanafiki. [18]

Tawakkul, kama inavyoelezwa katika Qur'ani, ina nafasi ya kipekee katika maisha ya waumini na ni ishara ya imani thabiti kwa Mwenye Ezi Mungu, huku ikiwasukuma waumini kuendelea na juhudi zao zote kwa kuamini kwamba matokeo ya mwisho yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hii inazidi kuonyesha umuhimu wa tawakkul katika maamuzi kibinafsi na ya kisiasa, ikiwa ni msingi muhimu ujengao msimamo thabiti katika hali zote za maisha ya Muislamu.

Pia tawakkul ina nafasi maalum katika ulimwengu wa Hadithi, nali ni suala lililothaminiwa na ukihimzwa katika maisha ya kila waumini. [19] Kwa mujibu wa Hadithi kutoka kwa Imamu Ali (a.s), tawakkul, pamoja na tafwidh (kuacha mambo mikononi mwa Mungu), rida (kuridhika na maamuzi ya Mwenyezi Mungu), na taslim (kujisalimisha kwa amri za Mungu), ni miongoni mwa nguzo nne za muhimu za imani. [20] Aidha, katika moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), tawakkul inatajwa kama ni sehemu ya yakini. [21] Katika hadithi maarufu ya Imamu Sadiq (a.s) inayojulikana kama «جنود عقل و جهل» Hadithi ya Majeshi ya Akili na Ujinga, tawakkul imearifishwa kua ni miongoni mwa majeshi ya akili na ni kinyume cha tamaa. [22]

Wanazuoni wa maadili ya Kiislamu wanaona tawakkul kama mojawapo ya hatua muhimu katika safari ya muumini ya kukuza maadili yake ya kiroho, [23] na ni mojawapo ya sifa za kimaadili ambazo zinaimarisha uhusiano wa muumini na Muumba wake. Kwa mujibu wa mafundisho haya, tawakkul sio tu ni tabia njema, bali pia ni ishara ya imani thabiti na katika kumwamini Mwenye Ezi Mungu. [24]

Daraja na Viwango vya Tawakkul

Katika maandiko ya vyanzo vya kimaadili na kisufi, tawakkul imeorodheshwa na kuanishwa katika daraja tatu, zinazo tofautiana kwa mujibu wa nguvu na udhaifu wake. [25]

  • Daraja ya Kwanza: Katika hatua hii, muumini hua na imani kwa Mwenye Ezi Mungu kama anavyomwamini wakili wake wa kisheria. [26] Hii ni imani inayo mfanya mtu kumtegemea Mwenye Ezi Mungu kama wakili wake wa kimahakama, ambapo anamwomba Mungu kwa matumaini na matarajio kamili. Mulla Muhammad Mahdi Naraqi anaihisabu daraja hili kuwa ni daraja ya kiwango cha chini zaidi katika tawakkul. [27]
  • Daraja ya Pili: Hapa, hali ya mtu anaye mtegemea Mwenye Ezi Mungu inafanana na hali ya mtoto mchanga kwa mama yake, ambapo mtoto hana tegemeo jingine wala hifadhi isipokuwa kwa mama yake tu. Tofauti kati ya daraja hii na daraja ya kwanza ni kwamba; hapa muumini anamtegemea Mwenye Ezi Mungu peke Yake, bila kujielewa kuwa kuwa yeye yupo katika hali ya kutawakali. [28] Wanazuoni wa maadili wanakubali kwamba; kufikia kiwango hichi cha juu cha tawakkul ni sifa za watu maalumu ambao wamebarikiwa na imani thabiti, na ambao wamejitolea kwa ajili kuufikia ukuruba wa Mola wao.[29]
  • Daraja ya Tatu: Kwa mujibu wa wanazuoni wa maadili, katika daraja hii, mwenye kutawakali hujiona kama maiti mikononi mwa mkosha maiti, ambapo yeye kiuhalisia huwa hana uwezo wa kufanya chochote na hujisabilia kikamilifu mbele ya maamuzi na matakwa ya Mwenye Ezi Mungu. [30] Tofauti na daraja ya pili, ambapo mwenye kutawakali alikuwa akimwomba Mola wakw, katika daraja hii mwenye kutawakali aweza kuachana na maombi na kutaka msaada, hii ni kwa kuwa yeye ana imani kamili juu ya jicho la huruma la Mwenye Ezi Mungu. [31] Naraqi anaihisabu daraja hii kuwa ndiyo daraja ya juu zaidi katika tawakkul, na anaieleza kuwa ni ngazi nadra sana kufikiwa. Kwa mtazamo wake, ni kwamba; hii ndiyo tawakkul aliyo shikamana nayo Nabii Ibrahim pale alipokuwa akirushwa kwenye moto. [32] [Maelezo 1]

Kwa mujibu wa maelezo ya Naraqi katika kitabu chake Jami'u al-Sa'adat, ni kwamba; tawakkul za watu hutofautiana na hutegemea kiwango cha yakini na imani zao katika kumwamini Mwenye Ezi Mungu. Kadiri imani ya mtu inavyokuwa thabiti, ndivyo tawakkul yake inavyokuwa na daraja ya juu zaidi. [33]

Njia za Kufikia Daraja ya Tawakkul

Kwa mujibu wa Muhammad Mahdi Naraqi, njia ya kufikia kiwango cha juu cha tawakkul ni kule mtu kuboresha na kuimarisha imani ya juu ya upwekeshaji wa Mwenye Ezi Mungu. Mtu anapaswa kukihisabu kila kitu kuwa ni matokeo ya kitendo miongoni mwa matendo ya Mwenye Ezi Mungu, na kuto muhisabu mwengine au kitu chengine kuwa na aina ya athari fulani katika matokea mbali mbali. [34] Hii inamaanisha kwamba mtu anahitaji kuwa na mtazamo wa kina kuhusiana na jinsi Menye Ezi Mungu anavyo endesha mambo yote ya maisha, bila kujali athari za nje zilizo dhahiri mbele ya fikra zetu. Naraqi pia anashauri kwamba mtu ajiingize katika tafakuri kuhusiana na uumbaji wa Mwenye Ezi MUngu, na kuelewa kwa kina juu Aya za Qurani zinazohusiana na tawakkul. Aidha, kusoma historia ya watu waliopita ambao walimtawakkal Mwenye Ezi Mungu. Hilo linaweza kutasaidia katika kuimarisha na kuboresha hali hii ya imani. [35]

Kwa mtazamo wa Naraqi, dalili kuu ya kuonesha kuwa mtu ana tawakkul, ni kipato au kupoteza kipato, ambapo mwenye sifa ya tawakkul huwa hataharuki wala kubadilika hali yaka katika hali zote mbili. [36]

Matokeo ya Tawakkul

Qur'ani na hadithi zinaelezwa kwa kina na uwazi kabisa juu ya athari na matokeo ya tawakkul (kutawakali). Kwa mfano, aya ya 3 ya Surat At-Talaq inaeleza wazi kwamba mtu anayemtegemea Mungu kwa dhati, Mwenye Ezi Mungu atamtosheleza na kumsaidia. Pia, kuna Hadithi nyingi zinazo elezea athari hii ya tawakkul, ambazo zinathibitisha suala hili kwa kurejelea Aya hiyo. [37] Katika moja ya Hadithi Imam Ali (a.s) anasema; "Yeyote anayemtegemea Mwenye Ezi Mungu kwa moyo mmoja, basi matatizo yake tamrahisikia, na tapata sababu za kutatua matatizo yake". [38] Hii inaonyesha jinsi tawakkul inavyoweza kuleta nafuu na mabadiliko chanya katika maisha ya mtu fulani, huku ikitufundisha kuwa imani thabiti juu ya Mwenye Ezi Mungu inaweza kutatua matatizo na kuleta faraja kwa waumini.

Wanazuoni wa maadili, wakirejea Aya isemayo: «وَ مَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَإِنَّ اللَّهَ عَزيزٌ حَكيمٌ؛ ; Na mwenye kumtegemea Allah (kutawakkal kwa Allah), basi bila shaka Allah ni Mwenye nguvu na Mwenye hekima», [39] wanaamini kwamba; mtu mwenye kumtawakkal Mwenye Ezi Mungu hatapitia hali ya kudhalilishwa mbele ya wengine. [40] Aidha, kwa mujibu wa moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), yeyote anayependa kuwa na nguvu zaidi juu ya wa watu wengine, anapaswa kutawakkal kwa Mwenye Ezi Mungu. [41]

Uhusiano kati ya Tawakkul na Juhudi za Kazi

Kulingana na nukuu za Ghazali na Muhammad Mahdi Naraqi, ni kwamba; baadhi ya watu wanaiona tawakali kama ni mtindo wa kukunja mikono na kuacha kufanya kazi kwa juhudi. [42] Hata hivyo, Faidhu Kashani amelifuta wazo hili kwa kusema kwamba; katika dini ya Kiislamu, tawakkul haipingani na suala la watu kujitahidi katika utendaji wao wa kazi mbali mbali. [43]

Katika kitabu cha tafsiri ya Qur’ani kiitwacho Tafsir al-Namune, imeelezwa kwamba; kuamini juu ya visaidizi na visababisha vya nje vihisiwavyo na wanadamu, hakupingani na upwekeshaji Mungu katika ngazi ya vitendo; kwa visaidizi na sababu dhahiri, hazina uwezo wa kujitegemea katika utendaji wake, bali athari hizo ziko ndani ya uwezo na matakwa ya Mwenye Ezi Mungu. [44] Hadithi pia zinashauri watu kutumia visaidizi na visababishi dhahiri asilia sambamba na kutawakali. Kwa mfano, imepokewa kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), akisema kwamba: "Kwanza mfunge ngamia wako kisha tawakali".[45]

Maelezo

  1. Katika tukio ambalo Ibrahimu alitupwa kwenye moto, Malaika Jibrilu alikuja kwa ajili ya kumsaidia akimuuliza, "Je, unahitaji msaada wowote?" Ibrahimu akajibu, "Lakini kwako sina sihitaji kitu". (Naraqi, Jama'u al-Sa'adat, 1383 Q, juz. 3, uk. 223-224).

Rejea

Vyanzo