Nenda kwa yaliyomo

Suratu al-Insan

Kutoka wikishia
Surat al-Insan

Surat al-Insan au Hal-Ataa’la au Dahr (Kiarabu: سورة الإنسان، أو هل أتى أو الدهر) ni sura ya sabini na sita na ni mojawapo ya sura zilizoteremshwa Madina, ambayo iko katika juzuu ya 29 ndani ya Qurani. Surat Al-Insan inazungumzia kuhusu uumbaji, uongofu wa mwanadamu, sifa za watu wema na baraka na neema ambazo Mwenyezi Mungu amewajaalia viumbe hao. Sura hii pia inaelezea umuhimu wa Qur-ani.

Kwa mujibu wa nadharia za baadhi ya wafasiri na wanazuoni wa Kishia na Masunni, aya ya nane ya sura hii, inayojulikana kama aya ya kulisha maskini, iliteremshwa kwa Ahlul-Bayt (a.s) kwa ajili ya kuonyesha heshima na daraja ya juu waliyonayo watu hao, ambao ni Hadhrat Ali, Fatima Zahra, Hassan, Hussein na mtumishi wao Fidhah. Watu hao walitimiza nadhiri yao ya kufunga saumu siku tatu mfululizo na ingawa walikuwa na njaa, walitoa sadaka chakula chao kwa ajili ya kusaidia masikini, mayatima na mateka.

Miongoni mwa fadhila na malipo yaliyotajwa kwa kuisoma sura hii ni kuwa pamoja na Mtume (s.a.w.w) siku ya kiama.

Majina ya Surat al-Insan

  • Jina

Sura hii inajulikana kwa majina haya maarufu, Insan, Hal-Ataala na Dahr. [1] na inajulikana kwa majina hayo kwa sababu ya maneno hayo matatu yanayoonekana mwanzoni. [2] Sura hii pia inaitwa Abrar (waja wema); kwa sababu neno hili – abrar- linaonekana katika aya ya tano ya sura hiyo,na zaidi ya nusu ya sura hii inaelezera historia ya watu Ahlulbayt hao.[3]

  • Mpangilio na Mahala Ilipoteremshwa

Surat Al-Insaan ni sura ya tisini na nane iliyoteremshwa kwa Mtume (s.a.w.w), na ni sura ya sabini na sita katika mpangilio wa sasa wa msahafu [4] na iko katika juzuu ya 29.[5]

Wafasiri wa Qurani na wanazuoni wamekhitilafiana nadhari ya kuwa sura hii ni ya Makkah au Madina. Kwa mujibu wa nadharia ya mfasiri maarufu wa kishia Nasser Makarim Shirazi, na wafasiri wengi wa Kishia wamekubaliana kinadharia kwamba surah hii yote au baadhi ya aya ambazo zinaelezea matendo mema na cheo walichopewa watu hao itakuwa imeteremshwa Madina. [6] mfasiri maarufu wa wa madhehebu ya Sunni anayejulikana kwa jina la Qurtubi, ni mmoja miongoni mwa wafasiri wa Kisunni katika karne ya saba Qamari, pia amewafiki kuwa sura hii imeteremshwa Madina. Na wanazuoni wengi wa Kisunni walio mashuhuri wamekubaliana kuwa sura hii kuwa ni sura ya Madina. [7] ingawaje, baadhi ya wafasiri wachache wa Kisunni wana nadharia ya kuwa sura hii ni ya Makka [8] na baadhi ya aya za kwanza za sura ni aya za Makka, na kuanzia aya ya nane hadi ya mwisho ni aya za Madina. [9]

  • Idadi ya Aya na Sifa nyinginezo

Surah Insan ina aya 31, maneno 243 na herufi 1089. Kwa upande wa juzuu iko katika juzuu ya ishirini na tisa, na ni mojawapo ya sura ndogo yenye aya fupi, [10] Sura hii ni miongoni mwa sura na aya ambazo zimechongwa katika kaburi la Hadhrat Abbas (a.s).[11]

Maudhui ya Surat Al-Insan

kuhusisna na ufafanuzi wa sura hii, katika kitabu cha tafsiri namune sura hii imegawanya katika mada na maudhui kuu tano:

  • Kwanza: Sura hii inaelezea kuhusu kuumbwa kwa mwanadamu, kutokana na mbegu ya uhai (manii), mwongozo na uhuru wake
  • Pili: Sura hii inaelezea kuihusu ujira na malipo ya watu waliotenda matendo mema ambao ni Ahlul-Bayt (a.s).
  • Tatu: Sura hii inaelezea sifa za watu wema ambazo zinazowafanya wastahiki kupata ujira na thawabu za Mwenyezi Mungu.
  • Nne: Sura hii inaelezea umuhimu wa Qur'an, njia ya kutekeleza maamrisho yake na heka heka za kujiboresha katika kutii amri zake Allah (s.w)
  • Tano: Sura hii inaelezea Ufalme mkuu wa Mwenyezi Mungu.[12]

Sura hii inaelezea baraka na neema za mbinguni, mfasiri wa Kisunni Alusi amenukuu akisema: Kuwa sura hii imeteremshwa kwa heshima na fadhila za watu watano wa familia ya Mtume, ambaye Fatima (a.s) ni miongoni mwa wanawake wa mbinguni (Hur al-Ayn) kwa sababu hiyo basi,hakuna jina lililotajwa kwa heshima yake. [13] mfasiri wa madhehebu ya kishia Allameh Tabataba'i pia alisema katika kitabu chake cha Al-Mizan kwamba katika Sura Al-Insan hakukutajwa Hoor Al-Ain kama moja ya neema muhimu zaidi za mbinguni, na kutokana na hili inaweza kuthibitishwa kwamba miongoni mwa Abrari waliotajwa katika Aya za sura hii ni wanawake. [14]

Aya Mashuhuri

Aya maarufu ya sura hii ni aya It’-aam (Aya ya kulisha) «وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا» (آیه ۸) Na huwalisha chakula maskini na yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakipenda

Tabia na Sifa za Watu Wema

Katika Surat Al- Insan (aya 7-11), zimeelezwa sifa tano za watu wema (Abrar)ambazo ni hizi zifuatazo: 1. Wanatimiza nadhiri 2. Wanaiogopa Siku ambayo shari na adhabu yake itaenea. 3. Ingawa wanahitaji chakula chao lakini wanawapa masikini, mayatima na wafungwa. 4. Wanafanya hivi kwa ajili ya ridhaa za Mwenyeezi Mungu na hawatarajii malipo au shukrani kutoka kwa mtu yeyote. 5. Wanamuogopa na wanamhofu Mola wao mlezi na siku ya kiza, tabu na kutisha (yaani Siku ya Kiyama).[16] Aya ya nane ya Sura Insaan (pamoja na aya za kabla na baada yake) inajulikana kama aya ya kulisha. [17] Kwa mujibu wa nadharia ya Ayatullah Makarem Shirazi, na wanavyuoni wengine wa Kishia wanakubali kwamba aya hii pamoja na aya nyingine (aya kumi na nane za sura hii au zote) zimeteremshwa kuhusu saumu ya Sayyidna Ali (a.s.), Fatima (s.a.), Hasnain (a.s.) na Fidhah.[18] Imepokewa kwamba watu hawa, ingawa walikuwa na njaa, walitoa chakula chao kufuatia maombi ya masikini, mayatima na mateka. [19] Kuna riwaya nyingi zinazoelezea hadhi hii ya ukoo. [20] Ayatullah Makarem Shirazi akirejelea riwaya ya Ibn Abbas kuhusu adhama na fadhila ya Ahl al-Bayt (PBUH) kutoka kwa wapokezi 34 wa Kisunni ambao Allameh Amini alisimulia katika Kitab al-Ghadir. [21] Alichukulia simulizi hii kuwa maarufu miongoni mwa wafuasi wa madhehebu ya Sunni[22]

Chanzo cha uteremshwaji wa aya ya 7-8 na ufafanuzi wake

Imepokewa kwa Abdallah bi Abbas akisema: Walipatwa na maradhi Hassan ana Hussein (a.s) ikawa babu yao Mtume Muhammad (s.a.w.) anakwenda kuwaona, Sayyidna Ali (a.s) akashauriwa aweke nadhiri kwa ajili ya watoto wake, akasema Sayyidna Ali ikiwa watapoa basi atafunga tatu kwa kumshukuru Mwenyeezi Mungu, bibi Fatma bint Rasuli naye akasema hivyo hivyo, na mtumishi wao Fidha akasema ikiwa watapona mabwana zangu basi nitafunga siku tatu kumshukuru Mwenyeezi Mungu kwa kuwaponya, muda mfupi Mwenyeezi Mungu akawapoza na nyumbani mwao hakuna chakula, Sayyidna Ali akatoka nje kwenda kutafuta rizki na akarudi na pishi tatu za ngano, bibi Fatma akachukuwa pishi moja akaiandaa kwa ajili ya chakula chao, Saayyidna Ali alipomaliza kuswali pamoja na Mtume akaingia nyumbani kikaandaliwa chakula, mara maskini akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Amani juu yenu enyi watu wa nyumba ya Muhammad, mimi masikini katika watoto wa kiislamu nipeni chakula Mwenyeezi Mungu atakupeni chakula cha peponi. Sayyidna Ali akamsikia, akaamrisha apewe chakula chote kilichokuwa kimeandaliwa hapo, siku hiyo wakakaa kutwa kucha hawana walichokula isipokuwa maji.

Siku ya pili bibi Fatma akachukuwa pishi moja nyengine kuandaa chakula cha mkate Saayyidna Ali alipomaliza kuswali pamoja na Mtume akaingia nyumbani kikaandaliwa chakula, mara yatima akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Amani juu yenu enyi watu wa nyumba ya Muhammad, mimi yatima katika watoto wa kiislamu wa Muhajiriyna baba yangu ameuliwa vitani naomba chakula Mwenyeezi Mungu atakupeni chakula cha peponi. Siku ya tatu bibi Fatma akachukuwa pishi iliyobakia katika zile pishi tatu alizozileta mumewe, akaiandaa chakula cha mkate Saayyidna Ali alipomaliza kuswali pamoja na Mtume akaingia nyumbani kikaandaliwa chakula, mara mfungwa akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Amani juu yenu enyi watu wa nyumba ya Muhammad, mimi mfungwa (mateka) wameniteka na kunifunga na kuninyima chakula naomba chakula Mwenyeezi Mungu atakupeni chakula cha peponi.

Wakampa chakula chote, wakashinda siku tatu usiku kucha na mchana kutwa hawana chakula ila maji tu, ndipo Mtume Muhammad (s.a.w) alipokwenda akaikuta hali hiyo, Mwenyeezi Mungu akamteremshia Mtume wake aya 7-8 ya sura hii al-Insaan.

Kinywaji cha Mvinyo Kilicho Safi na Tohara

وَسَقَاهُمْ رَبُّهُمْ شَرَابًا طَهُورًا


Na Mola wao Mlezi huwanywesha mvinyo safi!.



(Surat al-Insan: 21)

Mwandishi wa kitabu cha Al-Mizan anaelezea mvinyo uluiotajwa katika aya hii ni wenye utakaso usio na aina ya uchafu au ovu wowote, miongoni mwa uovu ni kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu Mtukufu, sifa za watu wema waliotajwa katika sura hii inaonyesha wazi kuwa hakuna pazia baina yao na Mwenyeezi Mungu. kama alivyoeelezwa katika Aya ya 10 ya Sura Yunus: watukufu hao maombi yao ya mwisho ni kumhimidi na kumtakasa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, Allameh Tabataba'i katika kitabu chake cha Al-Mizan anaamini kwamba Mwenyeezi Mungu aliwatakasa watu wema hao katika Aya"Wasaqaahum Rabbuhum sharaaba taahura.

Ayat Al- Ahkaam

Aya ya saba ya Suratul Al-Insan imeorodheshwa kuwa ni miongoni mwa aya za al-Ahkam. [24] Kuhusiana na aya hii inayosema kwamba kuweka nadhiri ni miongoni mwa sifa za watu wema, [25] inasemekana kwamba inajuzu na hata ni wajibu kuweka nadhiri.[26]

Sifa na Fadhila za Surat Al-Insan

Imenukuliwa Katika Hadithi mbali mbali kuwa sura hii ina fadhila nyingi kwa watakaoisoma, miongoni mwa fadhila hizo ni: Ujira wa kupewa pepo, kukaa pamoja na Mtume (s.a.w) siku ya kiama, nakadhalika . Imeelezwa pia kwamba Imam Ridha (a.s) alikuwa akiisoma Sura Al-Hamd na Surah Al-Insan katika rakaa ya kwanza katika swala ya asubuhi siku ya Jumatatu na Alhamisi, na katika rakaa ya pili baada ya Al-Hamd, alisoma Sura Ghaashiyyah na akasema kwamba yeyote atakayefanya hivi, Mwenyezi Mungu atamlinda na shari katika siku mbili hizi.[29]

Baadhi ya sifa pia zimetajwa kwa ajili ya kusoma sura hii, kama vile mtu akiendelea kuisoma Sura al-Insan, ikiwa roho yake ni dhaifu, atakuwa na nguvu za kiroho. [30] Kusoma sura hii ni muhimu kwa kuimarisha akili na kuepukana na wasiwasi.[31] Mbali ya kuwa sura hii imetafsiriwa katika vitabu vya tafsiri, bali pia kuna vitabu mbali mbali vilivyoitafsiri sura hii kwa undani kabisa na kuandika kwa kina maudhui yake.