Nenda kwa yaliyomo

Suratu al-Falaq

Kutoka wikishia

Surat al-Falaq ni sura ya 113 katika mpangilio wa msahafu na ni katika sura zilizoshuka Makka (Makki). Sura hii ipo katika Juzuu ya 30. Surat al-Falaq ni miongoni mwa sura zinazotambulika kwa jina la Qul Nne (sura zinazoanza na Qul). Kupewa sura hii jina la Falaq yenye maana ya mapambuzuko kumechukuliwa katika Aya ya kwanza. Katika sura hii Mwenyezi Mungu anamuamrisha na kumtaka Mtume Wake ajikinge kwa Mwenyezi Mungu na kila shari, hususan shari ya giza la usiku liingiapo, shari ya wanawake wanaopulizia mafundoni na shari ya mahasidi. Baadhi ya wafasiri wa Qur’an wa Ahlu-Sunna wanasema kwamba, sura hii ilishuka wakati Bwana mmoja Myahudi alipomroga na kumfanyia sihiri Mtume (s.a.w.w) na kwa uchawi huo Mtume akawa ameugua. Baada ya kuja Malaika Jibril na kushushwa Surat al-Falaq na al-Nas, Aya za sura hizo alisomewa Mtume na kupitia kwazo akapona na kuamka kitandani. Baadhi ya Maulamaa wa Kishia wametilia ishkali kauli hii na kusema kuwa, uchawi hauna taathiri yoyote kwa Mtume (s.a.w.w). Sura za al-Falaq na al-Nas zinatambulika pia kwa jina la Mu'awwidhatayn (kinga mbili) kwani husomwa kwa ajili ya kinga. Kuhusiana na fadhila za kusoma Surat al-Falaq kumenukuliwa hadithi kadhaa na miongoni mwazo ni kwamba, kila atakayesoma Surat al-Nas ni sawa na kuwa amesoma vitabu vyote vya Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kadhalika imenukuliwa ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akizitambua sura mbili za al-Falaq na al-Nas kuwa sura pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu.

Utambulisho

Kupewa jina

Sura hii inaitwa al-Falaq, na jina lake limechukuliwa katika Aya ya kwanza ya sura hii. [1] Falaq ina maana ya mapambazuko. [2] Jina jingine la Sura hii ni Mu’awwidha (kujikinga) ambapo limechukuliwa kutokana na neno audh: Kujinga, lililopo katika Aya ya kwanza ya sura hii. [3] Sura mbili za al-Falaq na al-Nas zinaitwa pia kwa jina al-Mu'awwidhatayn. Aidha sura mbili hizi zinatambuliwa pia kwa jina la Mushaqshaqatayn kutokana na kuwa husomwa wakati wa kuhisi hatari. [4]

Mpangilio na mahali iliposhuka

Surat al-Falaq ni miongoni mwa sura za Makki (zilizoshuka Makka) na katika utaratibu wa kushuka inahesabiwa kuwa Sura ya 20 iliyoshushwa kwa Bwana Mtume (s.a.w.w). Katika mpangilio wa sasa wa msahafu, sura hii ni ya 113 [5] na inapatikana katika Juzuu ya 30. Allama Tabatabai, mwandishi wa kitabu cha Tafsir al-Mizan ameitambua sura hii kwamba ni Madani (iliyoshuka Madina) akizingatia hadithi zinazozungumzia kuhusu kushushwa sura hii. [6]

Idadi ya Aya na sifa zake maalumu

Surat al-Falaq ina Aya 5, ina maneno 24 na herufi 73. Kwa upande wa ukubwa, sura hii ni miongoni mwa zile sura zinazojulikana kwa jina la Mufassalat (yaani zenye Aya fupi). Surat al-Falaq ni moja ya sura zinazoanza na neno "Qul" ambazo zinatambulika kama "Qul Nne”. [7]

Maudhui

Katika sura hii Mwenyezi Mungu anamuamrisha na kumtaka Mtume wake ajikinge kwa Mwenyezi Mungu na kila shari, hususan shari ya giza la usiku liingiapo, shari ya wanawake wanaopulizia mafundoni na shari ya mahasidi. Allama Tabatabai anasema katika tafsiri ya al-Mizan kwamba, makusudio ya :

لنَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ

“Yaani wanaopulizia mafundoni” sio wanawake wachawi tu, bali kila mtu ambaye anafanya uchawi na sihiri. [8] Imekuja katika tafsiri ya Nemooneh kwamba: Surat al-Falaq inamfundisha Mtume (s.a.w.w) na Waislamu kujikinga kwa Mwenyezi Mungu na kila shari. [9]

Maudhui ya Surat al-Falaq [10]

Kujikinga kwa Mwenyezi Mungu na shari ya viumbe

Nukta ya kwanza: Aya ya kwanza; kutambulishwa Mwenyezi Mungu kwamba, ndiye ambaye watu wanapaswa kujikinga kwake. Ni lazima kujikinga kwa Mwenyezi Mungu ambaye anaumba vitu ambavyo kimsingi havikuweko.

Nukta ya pili: aya ya 2-5; Shari ambazo ni lazima kujikinga kwa Mwenyezi Mungu kwazo.


Kundi la kwanza: Aya ya 2-3; shari za kimaumbile

Mfano wa kwanza: Aya ya 2; viumbe vyote ambavyo vinamdhuru mwanadamu.


Mfano wa pili: Aya ya 3; giza la usiku

Kundi la pili: Aya ya 4; shari za kibinadamu

Mfano wa kwanza: Aya ya 4; watu wenye shari na wanawake wanaopulizia mafundoni

Mfano wa pili: Aya ya 5; mahasidi na wenye hila.


Sababu ya kushuka

Kuhusiana na sababu ya kushuka sura hii, kuna hadithi zilizonukuliwa katika vyanzo vya Ahlu-Sunna ambazo Maulamaa wa Kishia wamezikataa. [11]

Imekuja katika kitabu cha al-Durr al-Manthur, moja ya vitabu vya tafsiri vya Kisuni ya kwamba, Bwana mmoja Myahudi alimroga Mtume. Malaika wa Wahyi Jibril akaja kwa Mtume akiwa na Mu'awwidhatayn (Surat al-Falaq na al-Nas) na kusema: Bwana mmoja Myahudi amekuroga na uchawi wake uko katika kisima fulani. Mtume (saww) akamtuma Ali bin Abi Talib (a.s) ili akalete uchawi huo; kisha akatoa amri ya kufunguliwa mafundo yake na asome moja ya Aya za Mu'awwidhatayn kwa kila fundo atakalofungua. Baada ya mafundo yote kufunguliwa na sura hizi mbili zikawa zimeisha, Mtume (s.a.w.w) akapata uzima wake wa kiafya. [12]

Allama Muhammad Hussein Tabatabai ameandika katika tafsiri al-Mizan ya kwamba, hakuna hoja kwamba Mtume (s.a.w.w) anaweza kustahimili uchawi na uchawi usiweze kusababisha maradhi katika mwili wake; bali Aya za Qur’an zinaonyesha kuwa moyo na nafsi, na akili na fikra za Mtume (s.a.w.w) ziko salama kutokana na uchawi na athari na upenyaji wa mashetani. [13]

Mitazamo ya wafasiri kuhusu sihiri na uchawi

Sayyid Radhii (aliyeaga dunia 406 Hijria) ameandika kuhusiana na tafsiri ya Aya ya 4 ya Surat al-Falaq (Na shari ya wanaopulizia mafundoni) kwamba: Aya hii ni istiara [14] na makusudio yake ni kujikinga kwa Mwenyezi Mungu na shari ya wanawake ambao husambaratisha maamuzi makuu ya wanaume (ambapo kutokana na ugumu wake hilo limeshabihishwa na mafundo) na hudhoofisha uwezo wao (wa wanaume) kwa hila na vitimbi vyao. [15] Baadhi ya wafasiri wa Qur’an wa Ahlu-Sunna [16] wamekataa uchawi na kijicho. [17] Hii ni katika hali ambayo, Allama Tabatabai anaandika: Aya hii (Aya ya 102 ya Surat al-Baqara) inaonyesha kuwa, Qur’ani imesadikisha kuwa ukweli suala la sihiri na uchawi. [18]

Fadhila na sifa maalumu

Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba yeyote anayesoma Sura mbili za al-Nas na al-Falaq, ni kana kwamba amesoma vitabu vyote vya Mitume wa Mwenyezi Mungu. [19] Imam Baqir (a.s) pia ameeleza kwamba yeyote anayesoma Mu’awwidhatayn (Surat al-Nas na al-Falaq) na Ikhlas katika Swala ya witr, ataambiwa ewe mja wa Mungu, bishara njema kwako Mungu amekubali swala yako imetakabaliwa. [20] Kadhalika imenukuliwa ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akizitambua sura mbili za al-Falaq na al-Nas kuwa sura pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu. [21] Imekuja katika nukuu nyingine kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ya kwamba, kila ambaye atasoma sura za Tawhid, al-Nas, na al-Falaq kila usiku mara 10 basi ni mithili ya mtu aliyesoma Qur'an yote na huondoka katika madhambi yake na kuwa kama siku aliyozaliwa na mama yake, na kama atakufa katika mchana au usiku wa siku hiyo, basi atakuwa amekufa shahidi. [22]

Ama kuhusiana na sifa maalumu za sura hii imenukuliwa ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akisoma sura mbili za al-Nas na al-Falaq na kuwakinga Imam Hassan (a.s) na Imam Hussein (a.s). [23].

Surat al-Falaq na tarjuma yake

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّ‌حْمَـٰنِ الرَّ‌حِيمِ

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ

مِن شَرِّ مَا خَلَقَ

وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ

وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ

وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ


Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko.

Na shari ya alivyoviumba.

Na shari ya giza la usiku liingiapo.

Na shari ya wanaopulizia mafundoni.

Na shari ya hasidi anapohusudu.