Sijida ya Kisomo
- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Sijida ya kisomo (Kiarabu: سجدة التلاوة) ni sijida ambayo huwa wajibu au mustahabu wakati wa kusoma au kusikia Aya ya Qur'ani ambayo ina sijida. [1] Kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi wa Kishia, Aya ya 15 ya Surat Sajdah, Aya ya 37 Surat Fussilat, Aya ya 62 Surat al-Najm na Aya ya 19 Surat al-Alaq ni Aya zilizo na sijida ya wajibu. [2] Kadhalika kwa mujibu wa Sahib al-Jawahir Aya 11 katika Qur'an zina sijida ya mustahabu. [3] Aya hizo ni: Aya ya 206 Surat al-A'raf, Aya ya 15 Surat Ra'ad, 49-50 za Surat al-Nahl, Aya ya 109 Surat al-Israa, Aya ya 58 Surat Maryam, 18 na 77 katika Surat al-Hajj, Aya ya 60 Surat al-Furqan, Aya ya 26 Surat al-Naml, Aya aya 24 Surat Swaad na Aya ya 21 Surat al-Inshqaq. [4] Kwa mujibu wa kile kilichonasibishwa na Sheikh Saduq ni kuwa, kuweko neno "Sijda" katika Aya kunapelekea Aya hiyo kuwa na sijida ya mustahabu. Kwa maana kwamba, mtu asomapo au asikiapo Aya hiyo ikisomwa anapaswa kusujudu. [5]
!Dua au dhikri ifuatayo imependekezwa kusomwa wakati wa sijida ya kisomo:
﴾لا اِلهَ اِلَّا اللهُ حَقًّا حَقًّا، لا اِلهَ اِلَّا اللهُ ایماناً وَ تَصْدیقاً، لا اِلهَ اِلَّا اللهُ عُبُودِیةً وَرِقّاً، سَجَدْتُ لَک یا رَبِّ تَعَبَّداً وَرِقّاً، لا مُسْتَنْکفاً وَ لا مُسْتَکبِراً، بَلْ اَنَا عَبْدٌ ذَلیلٌ ضَعیفٌ خائفٌ مُسْتَجیرٌ﴿
[6]
Sijida ya kisomo na hukumu zake hujadiliwa na kuzungumziwa katika milango ya tohara [7] na Sala [8] katika vitabu vya fikihi. Baadhi ya hukumu zake ni:
- Sijida ya wajibu ya Qur'an, wajibu wake ni wa mara moja na hapo kwa hapo; kwa maana kwamba, mtu anaposoma au kusikia Aya yenye sijida miongoni mwa Sura za Azaim (zenye sijida ya wajibu) kusujudu huwa wajibu hapo hapo, mara moja na bila kuchelewa. [9]
- Katika kusujudu sijida ya kisomo sio lazima kuwa na udhu, kuoga (kwa mwenye janaba na mfano wake), kuelekea kibla na kusoma dhikri maalumu. Lakini ni lazima kuweka paji la uso juu ya kitu ambacho inajuzu kusujudu juu yake. [10] Pamoja na hayo, kuna dhikri maalumu zilizonukuliwa kwa ajili ya kusoma katika sijida ya kisomo. [11]
- Endapo mwenye janaba au hedhi watasikia Aya za sijida basi ni wajibu kwao kusujudu. [12] Hata hivyo kwa mujibu wa fat'wa ya mafakihi ni haramu kwa mwenye janaba [13] na hedhi [14] kusoma Azaim al-Sujud (sura zenye sijida ya wajibu).
- Endapo mtu akiwa katiika Sala akasoma moja ya sura hizi kwa kusahau ikiwa atakumbuka kabla ya kufikia Aya ya sijda au akafahamu hili akiwa katikati ya sura, anapaswa kuiacha sura hiyo na kusoma sura nyingine (isiyokuwa na sijda ya wajibu); na ikiwa atakumbuka hilo baada ya kupita katika Aya yenye sijda au baada ya kuwa ameshasoma zaidi ya nusu ya sura kuna hitilafu za kimitazamo baina ya Marajii kuhusiana na namna ya kutekeleza sijda hiyo na jinsi ya kuendelea na Sala yake. [15] Kwa mujibu wa fat'wa ya Imamu Khomeini (r.a) ni kwamba, katika hali hii anapaswa kutekeleza sijda kwa ishara na kutosheka na kusoma sura yenye sijda. [16] [22] Kadhalika kwa mujibu wa fatuwa ya Ayatullah Sayyid Ali Sistani na Sayyid Moussa Shubairi Zanjani ni kuwa, kama hatoleta sijda ya wajibu Sala yake ni sahihi ingawa anakuwa ametenda dhambi. [17] Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi wa Kishia ni kwamba, kusoma kwa makusudi sura zenye sijida ya wajibu katika Sala za wajibu, kunapelekea Sala kubatilika. [18]