Sheikh Naim Qasim
Naim Qasim Taarifa Binafsi • Kazi: Katibu Mkuu Msaidizi wa Hizbullah nchini Lebanon • Tarehe ya Kuzaliwa: 1953 • Mahali pa Kuzaliwa: Beirut, Lebanon • Nchi ya Ukaazi: Lebanon • Baba: Muhammad Qasim Taarifa za Kisiasa • Kiongozi Mkuu: Sayyid Hassan Nasrallah Taarifa za Kidini na Itikadi • Dini: Uislamu • Madhehebu: Shia • Mwelekeo wa Kifiqhi: Ja’fari Tovuti Rasmi https://naimkassem.com.lb/index.php Uraia: Lebanon
Sheikh Naim Qasim: Sheikh Naim Qasim ni Katibu Mkuu wa nne wa Hizbullahi ya Lebanon na ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho mwanzoni mwa kuchipuka kwake. Pia, anahisabiwa kuwa ni mmoja wa viongozi wakuu wa kisiasa wa jamii ya Kishia nchini Lebanon. Tokea ujanani kwake Naim Qasim, alianza kujishughulisha na shughuli za kisiasa, ambapo alishiriki katika uanzishaji wa harakati za chama cha Amal nchini Lebanon yeye pamoja na Sayyid Musa al-Sadr. Umaarufu wake ulianza kuibuka baada ya kuanzishwa kwa chama cha Muqawama au Upinzani wa Kiislamu nchini Lebanon, ambapo alihudumu kama mwanachama wa Baraza la Ushauri la Hizbullah katika mizunguko (mihula) mitatu. Baadae, alichaguliwa kuwa Mkuu wa Baraza Tendaji la chama hicho. Aidha, alihudumu kama Naibu Katibu Mkuu kwa takriban miaka 33 kabla ya kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu baada ya kuuawa kwa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah mwaka 2024. Pia Sheikh Naim Qasim alikuwa akijishughulisha na kazi kadhaa za kijamii. Miongoni mwa huduma alizotoa katika kazi za jamii ni pamoja na kazi ya uenezi fikra, da'awa, na ualimu. Si ohayo tu, bali pia amechangia katika kuasisi taasisi kadhaa za kitamaduni, pamoja na kushiriki katika hafla zinazohusiana na masuala ya kijamii na kielimu. Pia, kwa hivi sasa, Sheikh Naim Qasim anahudumia kama wakala maalumu wa masuala ya kidini wa Sayyid Ali Khamenei nchini Lebanon. Maisha ya Awali na Masomo Sheikh Naim Qasim alizaliwa katika eneo la Al-Basta Al-Tahta, jijini Beirut, mnamo mwezi wa Februari mwaka 1953 Miladia. [1] Baba yake, ambaye ni Mohamed Naim, alizaliwa katika kijiji cha Kfar Fila, katika eneo la Al-Tuffah, kusini mwa Lebanon. [2] Tangu utotoni mwake, Naim alijishughulisha na kusoma kwa wingi vitabu vya Kiislamu, akijifunza mbinu za kuhutubia na kujiandaa kwa masomo ya kidini tangu mapema. [3] Alipofikia umri wa miaka 18 (mwaka 1971), alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu (Dar al-Mu'allimina wa al-Mu’allimaat) ambacho kilikuwa kikiendesha shughuli zake chini ya Chuo Kikuu cha Lebanon, katika eneo la UNESCO jijini Beirut, ambapo alisoma Kemia kwa lugha ya Kifaransa chuoni humo. [4] Sheikh Naim Qasim alimaliza masomo yake mnamo mwaka 1977, na kupokea shahada ya uzamili (Masters) ya Kemia, na baadaye akafundisha katika shule za sekondari za umma kwa takriban miaka sita. [5] Masomo ya Huaza (Kiseminari) Kwa wakati mmoja, Sheikh Naim Qasim aliweza kufanikisha kusoma masomo yake ya kiseminari ya kiislamu sambamba na masomo yake ya kiakademia. [6] Yeye alijisomea masomo yake ya kidini chini ya miongozo ya wanazuoni kadhaa, ikiwa ni pamoja na: • Sayyid Abbas al-Mousawi • Sheikh Hassan Tarrad • Sayyid Ali al-Amin
Shughuli Zake za Kitamaduni na Kijamii Naim Qasim ni miongoni mwa waliochangia kuanzishwa kwa "Umoja wa Wanafunzi wa Kiislamu wa Lebanon", kazi ambayo aliifanya akiwa pamoja na vijana wengine we misimamo ya kiimani. Kazi ilitendeka kwa lengo la kueneza mawazo ya Kiislamu katika vyuo vikuu na mashuleni, wakati alipokuwa katika masomo yake ya chuo kikuu mwanzoni mwa miaka ya 1970. [8] Pia alikuwa ni mmoja wa walioshiriki wa Harakati za Mahrumina (Harakati za Utetezi wa Wanyonge), pale zilipoanzishwa na Imam Musa al-Sadr manmo mwaka 1974, ambazo baadae zilikuja kujulikana kwa jina la Afwaju Al-Muqawama Al-Lubnaniyya (Amal). [9] Naim Qasim alikuwa ni miongoni mwa waliohudhuria mikutano ya kwanza ya kuanzishwa kwa harakati hizo, ambapo alipewa jukumu la kushika nafasi ya Naibu Msimamizi Mkuu wa Utamaduni katika Harakati za Amal, na baadaye akawa Msimamizi wa Itikadi na Utamaduni. [10] Baada ya mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Naim Qasim aliamua kujiuzulu na kutengana na Kikundi cha Harakati za Amal. Alifanya hivyo ili kujiendeleza na masomo yake ya kiseminari pamoja na shughuli zake za kidini, ikiwa ni pamoja na; kufundisha, kutoa mihadhara misikiti pamoja na maeneo mengine ya ibada (hussainiyat) huko Beirut na maeneo ya kusini mwa jiji hilo. [11] Mchango Wake Katika Kuelimisha Jamii Sheikh Naim ni miongoni mwa waliosaidia kuanzishwa kwa Taasisi ya Elimu ya Kidini ya Kiislamu mnamo mwaka 1977, [12] yenye malengo kufundisha dini ya Kiislamu katika skuli za umma na binafsi. Lengo ambalo lilikamilika kwa kusambaza walimu katika kila shule mbali mbali kwa ajili ya kufundishe somo la dini mara moja au mara mbili kwa wiki. Baada ya kuasisiwa kwa taasisi hiyo, Sheikh Naim alibaki kuwa kiongozi wa chama hicho hadi kufikia mwaka 1990. [13] Ushirikiano Wake Katika Runinga na Redio Sheikh Naim Qasim alikuwa na kawaida ya kutoa mihadhara kupitia vipindi vya runinga vinavyolenga utamaduni, malezi, na maadili. Vipindi hivi vilirushwa mara kwa mara kupitia vyombo mbali mbali vya habari kama vile; Chanel ya Sirat, [14] Idhaa ya Al-Manar, [15] Redio Nur, Redio Huda, Redio Albashair, pamoja na kadhalika. [16]
Ushiriki wa Kimataifa Pia Sheikh alionekana kushiriki mikutano kadha ya kimataifa nchini Iran, ikiwa ni pamoja na; mikuto iliyokuwa ikiandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Ahlulbayt (a.s), [17] mikutano ya Baraza la Kuleta Upatano kati ya Madhehebu ya Kiislamu, [18] Mikutano ya Umoja wa Kiislamu, [19] na Mikutano ya Siku ya Al-Quds Duniani. [20] Kuteuliwa Kwake Kama Wakala Maalumu wa Ayatullahi Khamenei Mnamo Mwaka 1446 Hijria (2024 Miladia), Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sayyid Ali Khamenei, alimteua Sheikh Naim Qasim (Katibu Mkuu wa Hezbollah) kuwa kushika nafasi ya uwakala, hivyo akawa ni wakala wake makhususi wa mambo ya kisheria nchini Lebanon. [21] Shughuli za Kisiasa Hapo mwanzo Sheikh Naim alikuwa ni Mkuu wa Baraza Wabunge katika chama cha Hezbollah, ambalo linalosimamia masuala maalumu, ikiwa ni pamoja na; kuchunguza Kikundi cha "Wafadhili wa Muqawama" (كتلة الوفاء للمقاومة), kufuatilia kazi za wabunge pamoja na harakati zao za kisiasa. [22] Pia, Sheikh Naim alikuwa ni Mkuu wa Halmashauri ya Ufuatiliaji wa Serikali, inayoshughulikia masuala matatu muhimu ambayo ni: • Kuchunguza mifumo, nyenendo na maamuzi ya wizara mbalimbali. • Ufuatiliaji wa mambo yanayohusiana na mawaziri wa Hezbollah katika utekelezaji wa wajibu wao serikalini. [23] • Kufuatilia masuala ya manispaa na vyama vya wafanyikazi. [24] Kwa zaidi ya miaka 30, Sheikh Naim aliongoza Uratibu wa Uchaguzi wa Bunge wa Hezbollah, kuanzia uchaguzi wa kwanza wa bunge wa mwaka 1992 hadi alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho. [25] Ushiriki wa Kikanda Ama kwa upande wa masuala ya kikanda, Sheikh Naim alikuwa ni mmoja wa mwanachama wa kamati ya Kiarabu ya watu wanaounga mkono Intifada ya Palestine (اللجنة الشعبية العربية لمساندة الانتفاضة), [26] ambayo ililenga kuunganisha juhudi za wanajamii katika nyanja mbalimbali kama vile; nyanja za kielimu, kijamii, na kisiasa kwa ajili ya kuunga mkono haki za Wapalestina. [27]
Kuteuliwa Kwake Kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah Hapo awali (wakati wa kuanzishwa kwa chama cha Hizbullahi), Sheikh Qasim alikuwa ni mwanachama wa Baraza la Shura la Hizbullah kwa muda wa mihula mitatu. Akiwa katika nafasi hiyo, aliongoza shughuli za kielimu na tafiti maalumu huko Beirut. [28] Baadae, alikuja kuteuliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji, [29] kisha baadae akawa Mwenyekiti wa Baraza hilo. [30] Pia aliwahi kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah katika enzi ya Bwana Abbas al-Musawi (Katibu Mkuu wa pili wa Hizbullah) mwaka 1991. [31] Sheikh Naim alibaki katika nafasi hiyo hadi baada ya kifo cha Bwana Abbas na akaendelea nayo hadi kuingia madarakani kwa Bwana Hassan Nasrallah (Katibu Mkuu wa tatu) mwaka 1992. Bado yeye aliendelea kushika nafasi hiyo hadi mwaka 2024, alipouawa Bwana Hassan Nasrallah kupitia shambulio la Israel, lililojiri katika makao makuu ya Hizbullah huko Subiani ya Kusini mjini Beirut. [32] Baada ya tukio hili, mnamo tarehe 29 Oktoba mwaka 2024, Baraza la Shura la Hizbullah limmteua Sheikh Qasim kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullahi. [32] Uhusiano kati ya Bwana Hassan Nasrallah na Sheikh Qasim ulidumu kwa zaidi ya miaka 35, wakifanya kazi kwa pamoja katika Baraza la Shura, ambapo wakuwa wakionana mara kwa mara kupitia mikutano ya baraza hilo, huku wakiwa na ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana na mageuzi ya kisiasa. [33] Uhusiano Wake na Imam Khomeini na Wila ya Faqih Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Sheikh Naim Qasim alishawishika mno na haiba na uongozi wa Imam Khomeini (r.a). Jambo lilipelekea kushiriki katika kamati za Kiislamu zilizounga mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shughuli za kamati hizi ilikuwa ni kusambaza habari, maandamano, na kufanya mihadhara katika kuunga mkono mapinduzi hayo. [34] Mara zote Sheikh Qasim alikuwa mstari wa mbele katika mikutano iliyofanyika kati ya kamati za Kiislamu na vyama vya mbali mbali vya Kiislamu kama vile; mikutano ya Chama cha Da'wa tawi la Lebanon, mkutano ya wasomi wa Bonde la Bekaa, na mkutano wa Chama cha Harakati za Amal mwaka 1982. Mikutano hii ilikuwa na umuhumu mno, ambayo pia lichangia kuanzishwa kwa Hizbullah. [35] Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, ni miongoni mwa wanaamini na wenye itakadi mno juu ya kuwepo kwa nguvu za Utawala wa Kifiqhi (Wilayatu Al-Fafaqiih), na uongozi wa Sayyid Ali Khamenei baada ya Imamu Khomeini. Sheikh Qasim alikuwa mapenzi kwa Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran, hatimae akaandika kitabu kuhusiana na Imam Khomeini kiitwacho “Al-Imamu Al-khomeini Baina Al-Asala wa Al-Tajdiid” (Imamu Khomeini: Kati ya Uhalisia na Mageuzi". Pia baadae aliandika kitabu maalumu kwa kuhusiana na Sayyid Khamenei, kiitwacho “Al-Waliyyu Al-Mujaddid” (Kiongozi Mleta Mageuzi). [36] Mnamo mwaka 2014, wakati wa safari yake kwenda Iran kushiriki katika kongamano la "Wanazuoni wa Kiislamu Kuunga Mkono Mapambano ya Palestina, Sheikh Qasim aliandamana na ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu kumtembelea Sayyid Khamenei alipokuwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. [37] Kwa upande wake, Sayyid Khamenei alimpokea Sheikh Naim Qasim katika makazi yake huko Tehran, ili kuskiliza kutoka kwake maendeleo ya hivi karibuni kuhusiana na vita vya Tufani al-Aqsa pamoja na vita kwa ajili ya kutoa msaada kwa Ukanda wa Gaza. [38] Kazi za Uandishi
Sheikh Naim Qasim anajulikana kama ni mtu mwenye upeo juu wa kiutamaduni, na mwenye ufahamu wa kipekee wa kidini na kisiasa. Hili limeonekana katika kazi zake nyingi za uandishi, ambazo ni zaidi ya vitabu ishirini. [39] Sheikh Qasim ameonekana kuandika vitabu vyake katika nyanja mbalimbali kama vile; dini, maadili, siasa, mwanamke, na jamii. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri zaidi ni: [40]
• Kitabu kiitwacho "Hizbullah"; ambacho kinaelezea malengo, historia, na mtazamo wa kisiasa wa chama cha Hizbullahi katika nyanja mbalimbali. • Kitabu chenye jina la "Imam Khomeini: Kati ya Uhalisi na Mageuzi"; ambacho kinazungumzia mtazamo wa mageuzi Imamu Khomeini (r.a). • Kitabu kiitwacho "Kiongozi Mleta Mageuzi"; ambacho kinaeleza mabadiliko ya kilimwengu na umuhimu wake katika kuwasilisha mtazamo wa Uislamu ulimwenguni kupitia uzoefu wa; Sayyid Khamenei, maelekezo yake, na uongozi wake katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. • Mfululizo wa tafsiri ya kitabu cha Imamu Zein Al-Abidina (a.s), kiitwacho “Risalatu Al-Huquuq”, ambayo kinajumuisha sehemu saba ndani yake: o Haki za Viungo vya Mwili. o Haki za Wazazi na Mtoto. o Haki za Vitendo. o Haki za Mume na Mke. o Haki za Mwalimu na Mwanafunzi. o Haki Tatu. o Haki za Watu. [41]