Suratu al-Nas

Kutoka wikishia
Surat al-Nas

Surat al-Nas (Kiarabu: سورة الناس) ni sura ya 114 (ya mwisho) na ni katika sura za Makki (zilizoshuka Makka) ambayo ipo katika juzuu ya 30 ya Qur'an Tukufu. Surat al-Nas ni miongoni mwa Qul nne (zinazoanza na Qul). Mwenyezi Mungu katika sura hii anamuamrisha Mtume Wake kwamba, ajikinge kwa Mola Mlezi na shari ya wasiwasi wa shetani. Katika baadhi ya tafsiri za Ahlu-Sunna imekuja kwamba, sura hii ilishuka wakati Bwana mmoja Myahudi alipomroga Mtume (s.a.w.w) na kwa uchawi huo Mtume akawa ameugua. Baada ya kuja Malaika Jibril na kushushwa Surat al-Falaq na al-Nas, Aya za sura hizo alisomewa Mtume na kupitia kwazo akapona na kuamka kitandani. Baadhi ya Maulamaa wa Kishia wametilia ishkali kauli hii na kusema kuwa, uchawi hauna taathiri yoyote kwa Mtume (s.a.w.w).

Sura za al-Falaq na al-Nas zinatambulika pia kwa jina la Mu'awwidhatayn (kinga mbili) kwani husomwa kwa ajili ya kinga. Kuhusiana na fadhila za kusoma Surat al-Nas kumenukuliwa hadithi kadhaa na miongoni mwazo ni kwamba, kila atakayesoma Surat al-Nas ni sawa na kuwa amesoma vitabu vyote vya Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kadhalika imenukuliwa ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akizitambua sura mbili za al-Falaq na al-Nas kuwa sura pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu.

Utambulisho

  • Kupewa jina

Sura hii inaitwa Surat al-Nas, ina maana ya "watu" na neno hili limechukuliwa kutoka katika Aya ya kwanza katika sura hii. Surat al-Nas inatambulika pia kwa jina la Mu'awwidha (kinga) na ni kinga kwa Mwenyezi Mungu. Pia, kwa sababu mwanadamu huisoma wakati wa hatari ya kuokolewa, inaitwa Mushaqshaqa. Sura mbili za al-Nas na al-Falaq zinaitwa Mushaqshaqatayn na al-Mu'awwidhatayn.[1]

  • Mpangilio na mahali iliposhuka

Surat al-Nas ni katika sura za Makki (zilizoshuka Makka) na katika utaratibu wa kushuka inahesabiwa kuwa sura ya 21 aliyoshushiwa Bwana Mtume (s.a.w.w). Katika mpangilio wa sasa wa sura kwenye msahafu ni sura ya 114[2] na inapatikana katika juzuu ya 30. Hii ndio sura ya mwisho katika mpangilio wa msahafu. Allama Tabatabai, mwandishi wa kitabu cha Tafsiri al-Mizan, anaichukulia sura hii kama ilivyo Surat al-Falaq kwamba, ni Madani (iliyoshushwa Madina) na kwa kuzingatia hadithi anaamini kwamba, Surat al-Falaq na al-Nas ziliteremshwa pamoja.[3] Javwd Amuli, mfasiri wa Qur'an wa Kishia wa zama hizi anasema kwamba, sura hii inaweza kuwa imeshushwa Makka na inawezekana pia ikawa imeshushwa Madina, kwani haina sifa za Madina kama ambavyo ina sifa za Makka.[4]

  • Idadi ya Aya na sifa zake nyingine maalumu

Surat al-Nas ina Aya 6, maneno 20 na herufi 78. Kwa upande wa ukubwa, sura hii ni miongoni mwa zile sura zinazojulikana kwa jina la Mufassalat (yaani zenye Aya fupi). Surat al-Nas ni moja ya sura zinazoanza na neno "Qul" ambazo zinatambulika kama "Qul nne".[5]

Maudhui

Mwenyezi Mungu katika sura hii anamuamrisha Mtume Wake kwamba, ajikinge kwa Mola Mlezi na Khannas (shari ya wasiwasi wa shetani)[6] Maudhui na yale yaliyozungumziwa katika sura hii yanafanana na yale yaliyomo katika Surat al-Falaq, Sura zote mbili zinazungumzia kujikinga kwa Mwenyezi Mungu na shari kwa tofauti hii kwamba, katika Surat al-Falaq imezungumziwa kwa mapana zaidi yaani aina mbalimbali za shari; lakini katika sura hii ya al-Nas imezingatiwa zaidi suala la wasiwasi wa asiyeonekana (wasiwasi wa shetani, khannas).[7]

Maudhui ya Surat al-Nas

Kujikinga kwa Mwenyezi Mungu na shari ya wasiwasi wa shetani

Nuta ya kwanza: Aya ya 1-3; sababu za kujinga kwa Mwenyezi Mungu

Sababu ya kwanza: Aya ya 1; Mwenyezi Mungu ni mlezi wa wanadamu.

Sababu ya pili: Aya ya 2; Mwenyezi Mungu ni Mfalme wa wanaadamu.

Sababu ya tatu: Aya ya 3; Mwenyezi Mungu ni muabudiwa wa watu.


Nukta ya pili: Aya ya 4-6; sifa za wenye kutia wasiwasi

Sifa ya kwanza: Aya ya 4; wenye kutia wasiwasi daima ni wenye kuvizia na kuweka mtego.

Sifa ya pili: Aya ya 5; wenye kutia wasiwasi wanafanya hili katika vifua vya watu.

Sifa ya tatu: Aya ya 6; wenye kutia wasiwasi wako katika makund mawili, majini na watu.

Sababu ya kushuka

Kuhusiana na sababu ya kushuka sura hii, kuna hadithi zilizonukuliwa katika vyanzo vya Ahlu-Sunna ambazo Maulamaa wa Kishia wamezikataa.[8] Imekuja katika kitabu cha al-Durr al-Manthur, moja ya vitabu vya tafsiri vya Kisuni ya kwamba, Bwana mmoja Myahudi alimroga Mtume. Jibril akaja kwa Mtume akiwa na Mu'awwidhatayn (Surat al-Falaq na al-Nas) na kusema: Bwana mmoja Myahudi amekuroga na uchawi wake uko katika kisima fulani. Mtume (saww) akamtuma Ali bin Abi Talib(a.s) ili akalete uchawi huo; kisha akatoa amri ya kufunguliwa mafundo yake na asome moja ya Aya za Mu'awwidhatayn kwa kila fundo atakalofungua. Baada ya mafundo yote kufunguliwa na sura hizi mbili zikawa zimeisha, Mtume (s.a.w.w) akapata uzima wake wa kiafya.[9]

Allama Muhammad Hussein Tabatabai ameandika katika tafsiri al-Mizan ya kwamba, hakuna hoja kwamba Mtume (s.a.w.w) anaweza kustahimili uchawi na uchawi usiweze kusababisha maradhi katika mwili wake; bali Aya za Qur’an zinaonyesha kuwa moyo na nafsi, na akili na fikra za Mtume (s.a.w.w) ziko salama kutokana na uchawi na athari na upenyaji wa mashetani.[10]

Fadhila na sifa maalumu

Makala asili" Fadhila za sura

Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba yeyote anayesoma Surat al-Nas na al-Falaq, ni kana kwamba amesoma vitabu vyote vya Mitume wa Mwenyezi Mungu.[11] Imam Baqir (a.s) pia ameeleza kwamba yeyote anayesoma Mu’awwidhatayn (Surat al-Nas na al-Falaq) na Ikhlas katika swala ya witr, ataambiwa ewe mja wa Mungu, bishara njema kwako Mungu amekubali swala yako imetakabaliwa.[12]

Kadhalika imenukuliwa ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akizitambulisha sura mbili za al-Falaq na al-Nas kuwa sura pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu.[13] Ama kuhusiana na sifa maalumu za sura hii imenukuliwa ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akisoma sura mbili za al-Nas na al-Falaq na kuwakinga Imam Hassan (a.s) na Imam Hussein (a.s).[14] Imekuja katika nukuu nyingine kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ya kwamba, kila ambaye atasoma sura za Tawhid, al-Nas, na al-Falaq kila usiku mara 10 basi ni mithili ya mtu aliyesoma Qur'an yote na huondoka katika madhambi yake na kuwa kama siku aliyozaliwa na mama yake, na kama atakufa katika mchana au usiku wa siku hiyo, basi atakuwa amekufa shahidi.[15]

بِسْمِ اللهِ الرَّحْمنِ الرَّحِیم: قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ﴿1﴾ مَلِكِ النَّاسِ﴿2﴾ إِلٰهِ النَّاسِ﴿3﴾ مِنْ شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ﴿4﴾ الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ﴿5﴾ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ﴿6﴾

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu, Sema: Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanadamu. Mfalme wa wanadamu, Mungu wa wanadamu, na shari ya wasiwasi wa Shetani al-Khannas, Anayetia wasiwasi katika vifua vya watu, Kutokana na majini na wanadamu.



(Quran: 114:1-6)


Rejea

  1. Khurramshāhī, Dānishnāma-yi Qurʾān, juz. 2, uk. 1271-1272.
  2. Maʿrifat, Āmūzish-i ʿulūm-i Qurʾān, juz. 2, uk. 166.
  3. Tabatabai, Al-Mizan, 1394 H, juz. 20, uk. 395.
  4. http://javadi.esra.ir/-/%D8%AA%D9%81%D8%B3%DB%8C%D8%B1-%D8%B3%D9%88%D8%B1%D9%87-%D9%86%D8%A7%D8%B3-1399-01-29
  5. Khurramshāhī, Dānishnāma-yi Qurʾān, juz. 2, uk. 1271-1272.
  6. Ṭabāṭabāyī, al-Mīzān, juz. 20, uk. 395.
  7. Makārim Shīrāzī, Barguzīda-yi tafsīr-i nimūna, juz. 5, uk. 538-632.
  8. Ṭabāṭabāyī, al-Mīzān, juz. 20, uk. 394.
  9. Suyūṭī, al-Durr al-manthūr, juz. 6, uk. 417.
  10. Ṭabāṭabāyī, al-Mīzān, juz. 20, uk. 394.
  11. Ṭabrisī, Majmaʿ al-bayān, juz. 10, uk. 491.
  12. Ṭabrisī, Majmaʿ al-bayān, juz. 10, uk. 491.
  13. Majlisī, Biḥār al-anwār, juz. 92, uk. 368.
  14. Khurramshāhī, Dānishnāma-yi Qurʾān, juz. 2, uk. 1271-1272.
  15. Kafʿamī, al-Balad al-amīn, uk. 33.

Vyanzo

  • Khurramshāhī, Bahāʾ al-Dīn. Dānishnāma-yi Qurʾān wa Qurʾān pazhūhī. Tehran: Dūstān-Nāhīd, 1377 Sh.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1403 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Barguzīda-yi tafsīr-i nimūna. Edited by Aḥmad ʿAlī Bābāyī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1382 Sh.
  • Maʿrifat, Muḥammad Hādī. Āmūzish-i ʿulūm-i Qurʾān. [n.p]: Markaz Chāp wa Nashr-i Sāzmān-i Tablīghāt, 1371 Sh.
  • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Al-Durr al-manthūr fī tafsīr al-maʾthūr. Qom: Kitābkhāna-yi Āyatollāh Marʿashī al-Najafī, 1404 AH.
  • Ṭabāṭabāyī, Mūhammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Second edition. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1974.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Hāshim Rasūlī. Tehran: al-Maktaba al-'Ilmīyya, [n.d].