Sa'asa'a bin Sawhan

Kutoka wikishia
Msikiti wa Sa'asa'a huko Kufa

Sa'asa'a bin Sawhan (Kiarabu: صَعْصَعة بن صَوحان) alikuwa mmoja wa masahaba wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ambaye alishiriki katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawan. Sa'sa'a bin Sawhan alikuwa na ujuzi na kipaji cha kuhutubu na kuongea na alitumia ujuzi huo kumtetea Imam Ali (a.s) na kumkosoa Mu'awiyah bin Abi Sufyan. Imam Ali (a.s) amemtambulisha Sasa'a kama mmoja wa masahaba wake wakubwa. Imam Swadiq (a.s) pia alimchukulia kuwa ni miongoni mwa watu wachache waliomtambua Imam Ali (a.s) kwa jinsi alivyostahiki. Msikiti wa Sa'asa'a huko Kufa unanasibishwa na yeye.


Nasaba

Sa'asa'a bin Sawhan alitokana na kabila na familia ya Abdul-Qais [1]. Bwana huyu alizaliwa karibu na Qatif na baada ya muda fulani aliishi katika mji wa Kufa, Iraq [2]. Ni kutokana na sababu hiyo pia aliitwa "Kufi" (mtu wa Kufa). [3] Lakabu ya Sa'asa'a ni "Aba Talha" [4]. Ndugu zake Zayd na Sayhan walikuwa miongoni mwa Mashia wa Amirul-Muminina Ali bin Abi Talib (a.s). [5]

Katika zama makhalifa

Sa'asa'a alisilimu wakati wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), lakini hakubahatika kumuona Mtume. [6] Wakati wa Omar bin Khattab, Khalifa wa pili, Abu Musa Ash'ari alipeleka mali kwa Khalifa. Khalifa akaigawanya mali ile na kiwango fulani kikabakia. Aliuliza maoni ya Waislamu kuhusu mali iliyobakia. Sa'asa'a alisema: "Shauriana na watu katika masuala ambayo Mwenyezi Mungu hajasema chochote kuyahusu katika Qur’an. Lakini yale ambayo Mwenyezi Mungu ametoa hukumu yake basi, fanya kama ilivyo.” [7]

Sa'asa'a alikuwa mmoja wa wapinzani wa Khalifa wa tatu huko Kufa. Khalifa alimpeleka uhamishoni Syria pamoja na watu kadhaa akiwemo kaka yake Zayd bin Sawhan na Malik Ashtar [8] Vyanzo vya kihistoria vimeripoti mazungumzo muhimu kati yake na Othman ambayo yanamkosoa khalifa huyo wa tatu. [9] Imam Swadiq (as) amenukuliwa akisema:

“Hapakuwa na mtu yeyote pamoja na Imam Ali (a.s.) ambaye alimfahamu jinsi anavyostahiki, isipokuwa Sa'asa'a na masahaba zake.” [10]

Swahaba wa Imam Ali (as)

Kwa mujibu wa Sheikh Mufid, Sa'sa'a alikuwa mmoja wa masahaba wakubwa wa Imam Ali (as). [11] Kadhalika Ibn Qutaybah al-Dinawari, msomi na mwanazuoni wa karne ya 3 Hijria amelitaja jina la Sa'asa'a katika orodha ya kundi la watu mashuhuri katika Mashia. [12] Kwa mujibu wa riwaya ya Masoudi katika kitabu cha Moruj al-Dhahab, Imam Ali (a.s.) alimtambulisha Sa'asa'a kuwa miongoni mwa shakhsia wakubwa wa Kiarabu na mmoja wa wakuu wa Masahaba wake [13].Kwa mujibu wa riwaya ya Kulayni, Imam Ali (a.s) alimfanya shahidi wa wosia wake. [14]

Sa'asa'a alishiriki katika kusindikiza jeneza la Imam Ali (a.s) na baada ya kuzikwa, alifika kwenye kaburi lake na huku akimimina udongo juu ya kichwa chake na kulia, alitamka maneno ambayo, sambamba na kueleza fadhila za Imam Ali (a.s), kutoka kwa Mwenyezi Mungu, alimuomba Allah amfanye yeye kuwa mmoja wa marafiki wa Imam Ali (a.s.) na amsaidie kuendeleza njia yake. [15]

Sa'asa'a alimchukulia Imam Ali (a.s.) kuwa mpambaji wa ukhalifa na aliamini kwamba aliupa thamani na nafasi ukhalifa na kwamba hitajio la ukhalifa kwa Imam Ali (a.s.) ni kubwa kuliko hitajio lake kwa ukhalifa. [16]

Kushiriki katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawan

Sa'asa'a alishiriki katika vita wakati wa utawala wa Imam Ali (a.s). Katika vita vya Jamal, kaka yake Sayhan alikuwa mshika bendera wa kabila la Abdul-Qais. Baada ya kufa shahidi Sayhan, kaka yake mwingine Zayd alikuwa mshika bendera, na baada ya kufa shahidi Zayd, Sa'asa'a mwenyewe alichukua bendera. [17]

Katika vita vya Siffin Sa'asa'a alikuwa kamanda wa kabila la Abdul-Qais. [18] Kabla ya kuanza vita, jeshi la Muawiya lilikuwa limedhibiti maji na halikuwa likiruhusu jeshi la Imam Ali (a.s) kuyafikia maji hayo. Imam Ali (a.s) alimtuma Sa'sa'a kwa ajili ya mazungumzo na Muawiya bin Abi Sufyan.[19]

Kabla ya kuanza kwa vita vya Nahrwan pia, Imam Ali (a.s) alimtuma Sa'sa'a kwa Makhawarij kwa ajili ya kufanya mazungumzo nao na kuwanasihi. [20] Katika mazungumzo haya, alisisitiza juu ya kumfuata Imam Ali (a.s). Nukuu ya mazungumzo ya Sa'asa'a na Makhawarij inapatikana katika kitabu Al-Ikhtasas kilichoandikwa na Sheikh Mufid. [21]

Kumpinga Mu'awiya

Kwa mujibu wa al-Kashshi katika kitabu cha Maraf al-Rijal, wakati wa sulhu kati ya Imam Hassan (a.s) na Mu'awiya, Sa'asa'a alikuwa mmoja wa wale ambao Imam Hassan (a.s) aliwapatia amani kwa Mu'awiya. [22] Baada ya sulhu ya Imam Hassan (a.s), Mu'awiya alimuona Sa'asa'a huko Kufa na akamwambia:

Naapa kwa Mungu, sikutaka uwe katika amani yangu. Katika jibu lake, Sa'asa'a alisema: Naapa kwa Mungu, sikupenda kukuita kwa jina hili pia; kisha akamsalimia Mu'awiya kwa cheo cha Khalifa. Mu’awiya akasema, “Kama kweli wewe ni mkweli (katika kunitambua mimi kama khalifa), nenda kwenye mimbari na umlaani Ali (a.s).” Sa'asa'a alikwenda kwenye mimbari na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu, alisema maneno yaliyokuwa ya pande mbili: Enyi watu, ninatoka kwa mtu (Mu’awiya) ambaye ameniamuru nimlaani Ali (a.s). Basi mlaanini (mwenyewe) na alikusudia kumlaani Mu'awiya. [23]

Ibn A'tham Kufi anasimulia kwamba siku moja, Mu'awiya aliwaambia wazee wa Kufa: Mtazamo wenu ni upi, licha ya ujinga wenu nimekusameheni katika hali ambayo mlistahiki adhabu? Mwenyezi Mungu amrehemu Abu Sufyan, ambaye alikuwa ni mtu mvumilivu na mwenye subira, na lau watu wote wangekuwa katika kiizazi chake, wote wangekuwa na subira. Sa'sa’a akasema: Wallahi, ewe Mu’awiya, watu hawa ni watoto wa watu bora kuliko Abu Sufyan, na watu wapumbavu na wajinga kutoka katika kizazi cha Abu Sufyan ni zaidi ya wenye subira wao. [24]

Umahiri katika kuhutubu

Sa'asa'a alikuwa na ustadi na umahiri katika kuongea na kutoa hotuba. Vyanzo vya kihistoria na hadithi vimemtambulisha kuwa ni mtu fasaha na na aliyekuwa amebobea katika balagha. [25]Imam Ali (a.s) amemtaja Sa'asa'a kuwa ni "Al-Khatib al-Shahshah" (khatibu mahiri). [26] Kadhalika Mu'awiya na Mughira bin Shu'ba wamezungumzia balagha na ufasaha wake. Mu'awiya anamtaja Sa'sa'a kuwa mtu mwenye ulimi mkali. [27]

Al-Kashshi anasema: Sa'asa'a alikuwa akitumia umahiri wake kwa ajili ya kumtambulisha na kumtetea Imam Ali bin Abi Talib (a.s). [28]

Kuaga dunia

Msikiti na kaburi linalohusishwa na Sa'asa'a huko Bahrain

Inaaminika kwamba Sa'sa'a aliaga dunia katika mji wa Kufa katika zama za ukhalifa wa Mu'awiya. [29] Hata hivyo imeelezwa katika baadhi ya vyanzo kwamba, Mughira alimhamishia Sa'sa'a kwa amri ya Muawiya katika kisiwa kimoja huko Bahrain na alifia huko takribani mwaka 70 Hijria. [30]

Katika mji wa Askar huko Bahrain, kuna kaburi linalohusishwa na Sa'sa'a, ambapo kuna Msikiti wa Sa'asa'a bin Sawhan. [35] Pia, karibu na Msikiti wa Sahla huko Kufa, Iraq, kuna msikiti uitwao Sa'sa'a ambao unanasibishwa naye. [31]

Monografia

Kitabu "Zayd va Sa'asa'a va Pesaran Sawhan" kilichoandikwa na Kamran Mohammad Hosseini, kilichapishwa mwaka 1395 Hijria Shamsia kikiwa na kuurasa 136. Kitabu hiki kinazungumzia maisha na utendaji wa Sa's'aa bin Sawhan na nduguye Zayd bin Sawhan. [32]


Vyanzo

  • Aḥmadī Mīyānajī, ʿAlī. Makātīb al-aʾimma. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1426 AH.
  • Dhahabī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Tārīkh al-Islām wa wafayāt al-mashāhīr wa l-aʿlām. Edited by Bashār ʿAwād Maʿrūf. [n.p]. Dār al-Gharb al-Islāmī, 2003 AH.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Muḥammad. Usd al-ghāba fī maʿrifat al-ṣaḥāba. Beirut: Dār al-Fikr, 1409 AH-1989.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH-1965.
  • Ibn Aʿtham al-Kūfī, Aḥmad b. Aʿtham. Kitāb al-Futūḥ. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Aḍwaʾ, 1411 AH-1991.
  • Ibn Khaldūn, ʿAbd al-Raḥmān b. Muḥammad. Dīwan al-mubtadaʾ wa l-khabar fi tārīkh al-ʿarab wa al-barbar wa man ʿātharahum min dhawi al-shaʾn al-ʾakbar. Edited by Khalīl al-Shaḥāda. 2nd edition. Beirut: Dār al-Fikr, 1408 AH.
  • Ibn Dāwūd al-Ḥillī, Ḥasan b. 'Alī. Kitāb al-rijāl. Tehran: Dānishgāh-i Tehrān, 1342 Sh.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad b. Manīʿ al-Ḥāshimī al-Baṣrī. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1418 AH.
  • Ibn Abd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Al-Istīʿāb fī maʿrifat al-aṣḥāb. Edited by ʿAlī Muḥammad al-Bajāwī. Beirut: Dār al-Jīl, 1412 AH-1992.
  • Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allāh b. Muslim . Al-Maʿārif. Edited by Tharwat ʿAkkāsha. Cairo: Al-Hayʾa al-Misrīyya al-Āmma li l-Kitāb. 1992 CE.
  • Ibn al-Mashhadī, Muḥammad. Al-Mazār al-kabīr. Edited by Jawād Qayyūmī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1419 AH.
  • Kashshī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Ikhtīyār maʿrifat al-rijāl. Edited by Muḥammad Rajāʾī. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1363 Sh.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Ikhtiṣāṣ. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī and Maḥmūd Muḥarramī Zarandī. Qom: al-Muʾtamar al-ʿĀlamī li-Alfīyat al-Sheikh al-Mufīd, 1413 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Jumal wa al-nuṣra li sayyid al-ʿitra fī ḥarb al-Baṣra. Edited by ʿAlī Mīrsharīfī. Qom: Kungira-yi Shaykh Mufīd, 1413 AH.
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Murūj al-dhahab wa maʿadin al-jawhar. Edited by Asʿad Dāghir. Qom: Dār al-Hijra, 1409 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Naṣr b. Muzāhim Minqarī. Waqʿat Ṣiffīn. Edited by ʿAbd al-Salām Muḥammad Hārūn. Qom: Maktabat Ayatullāh al-Marʿashī al-Najafī, 1404 AH.
  • Sayyied Raḍī, Muḥammad Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣaliḥ. Qom: Hijrat, 1414 AH.
  • Shahīd al-Awwal, Muḥammad b. Makkī. Al-Mazār fī kayfīyyat zīyārāt al-Nabī wa al-aʾimma. Qom: Muʾassisa Imām Mahdī, 1410 AH.
  • Thaqafī al-Kūfī, Ibrāhim b. Muḥammad. Al-Ghārāt. Edited by Mīr Jalāl al-Dīn Armawī. Tehran: Intishārāt-i Anjuman-i Āthār-i Millī, 1395 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].
  • Zamakhsharī, Maḥmūd b. ʿUmar al-. Al-Fāʾiq fī gharīb al-ḥadīth. Edited by Ibrāhīm Shams al-Dīn. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1417 AH.
  • Ziriklī, Khayr al-Dīn al-. Al-Aʿlām. 8th edition. Beirut: Dār al-ʿIlm li-l-Malāyyīn, 1989.