Qaida ya Nafyu al‑Sabil
Qaida (Kaida) ya Nafyu al‑Sabil: ni kaida maalumu ya kifiqhi inayothibitisha kutokuwepo kwa hukumu yoyote ile ya kisheria katika dini ya Kiislamu, inayojuzisha au kuhalalisha tasallut (udhibiti/utawala) wa kafiri juu ya Mwislamu. Kaida hii hutajwa kama ni mojawapo ya kaida zenye umuhimu wa hali ya juu zaidi, yenye matumizi mapana zaidi na yenye uzito mkubwa zaidi miongoni mwa zile ahkām thanawiyya (hukumu mbadala) zinazotolewa kulingana na mazingira tofauti. Kaida hii ni kaida ya mbele zaidi inayoshika hatamu kwa kuzitangulia na kuzipiku hukumu zote zile za awali (zilizokuja kulingana na misingi ya awali ya sheria). Hivyo basi, iwapo hukumu fulani ya awali itakinzana na kaida hii, papo hapo hukumu hiyo hubatilika kisheria na kukaa kando bila ya upinzani.
Baadhi ya mafaqihi wamepanua zaidi wigo wa kaida hii, wao wanaamini kuwa; Kaida hii yatakiwa kutawala katika nyanja zote za mahusiano, yawe ya mtu binafsi au ya kijamii kati ya Waislamu na wasio Waislamu. Wakirejelea na kutegemea ya kaida hii, mafaqihi hawa wametoa fatwa ya ubatili wa ndoa kati ya mwanamke Kiislamu na mwanamme wa kafiri, kwa kuwa jambo huanzisha sabil (njia ya udhibiti) wa kafiri juu ya Mwislamu. Dalili ya msingi ya Qur’ani kuhusiana na kaida hii, ni ile Aya iitwayo “Aya ya Nafyu al‑Sabīl”.
Pia wanazuoni huithibitisha kaida hii kupitia Hadithi isemayo: “Uislamu ni wa juu, na wala hakuna chenye hadhi ya kukaa juu yake.
Ufafanuzi Wake na Nafasi Yake Katika Kifiqhi na Kisheria za Jamii
Nafyu al‑Sabil ni kanuni ya kifiqhi, kwa maana kwamba; Mwenyezi Mungu hatungi wala haruhusu hukumu yoyote itakayochochea au kusababisha wasioamini kupata udhibiti juu ya waumini. [1] Kwa maneno mengine, katika dini ya Kiislamu, hakuna hukumu yoyote ile inayoweza kusababisha kafiri kuwa na udhibiti juu ya Mwislamu. [2]
Mafaqihi wameitumia qaida hii katika milango mbalimbali ya fani fiqhi. Kwa mfano Sheikh Ansa akitegemea qaida hiyo, ametoa hukumu ya kukataza, tendo la Mwislamu kumuuza mtumwa wa Kiislamu kwa asiyekuwa Muislamu. Kwa mtazamo wake, kulingana na muktadha wa kaida husika, muamala huo hauwezi kukubalika kisheria. [3] Kwa mujibu wa maelezo ya Amid Zanjani, kanuni hii ni miongoni mwa kanuni muhimu mno zinazotambulika katika nyanja za kifiqhi, na hasa katika fiqhi ya kiuchumi na fiqhi ya kisiasa. Kaida hii hufanya kazi zake ndani ya mahusiano yote ya wanadamu, yawe ni mahusiano binafsi au ya kijamii kati ya Waislamu na wasio Waislamu. [4] Pia, Sheikh Ansari akielezea kaida hii, ameandika kuwa; kanuni hii ina kipaumbele juu ya kanuni nyengine nyingi za kifiqhi. [5]
Kwa mujibu wa Ibara ya 153 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran: “Ni marufuku kufunga mkataba wa aina yoyote ule, ambao ungeanzisha au kusababisha tasallut (udhibiti) wa kigeni juu ya rasilimali asilia na uchumi wa taifa, utamaduni, majeshi, pamoja na nyanja nyingine za utawala wa nchi. [6]
Vielelezo
- Makala Asili: Aya ya Nafyu al‑Sabil na Hadithi ya al‑I‘itila
Dalili kuu zinazotajwa na kutegemewa kama ni vielelezo vya Qaida (kaida) ya nafyu al‑sabil, ni ile Aya ya Nafyu al‑Sabīl, pamoja na hadith inayothibitisha uluwwu (ubora) wa Uislamu, ambazo ndizo msingi wa istidlāl wa mafaqihi juu ya kaida hii. [7] Aidha, kuthibitisha kwake pia kumetegemezwa juu ya misingi ya ijmaa pamoja na misingi ya akili ya kimantiki, kama vyanzo na vielelezo vya ushahidi wa kifiqhi. [8]
Katika “Aya ya Nafy Sabīl” Mwenye Ezi Mungu anasema: «لَنْ يَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا» (Katu Mwenyezi Mungu hatoweka aina yoyote ya njia [ya utawala au udhibiti] kwa makafiri juu ya Waumini). [9] Imedaiwa kuwa; kwa kuwa mara kadhaa katika kihistoria, makafiri wameonekana kuwashinda waumini, jambao ambalo pia limethibitishwa na kutajwa ndani ya Qur’ani, hivyo basi Aya hii haiwezi kuwa na maana ya kwamba; makafiri hawajawahi kuzipiku nguvu za waumini. Kwa hiyo maana ya Aya hii ni kwamba; katika dini yetu hakuna hukumu yoyote ile inayoruhusu au kuhalalisha makafiri kupata mamlaka juu ya Waislamu. [10]
Miongoni mwa Riwaya maarufu za Sheikh Saduq kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), ni ile Riwaya ijulikanayo kiumaarufu kwa jina la “Hadithi Al-I’itila”, Hadithi hii imekuja ikisema; “الْإِسْلَامُ يَعْلُو وَ لَا يُعْلَىٰ عَلَيْهِ وَ الْكُفَّارُ بِمَنْزِلَةِ الْمَوْتَى لَا يَحْجُبُونَ وَ لَا يَرِثُونَ.” Tafsiri ya kauli hii ni kuwa; (Uislamu una sifa ya kuvipidukia vitu vyote, na wala hakuna kitu chochote kile chenye haki ya kukaa juu yake, na hali ya makafiri ni swa na hali ya maiti katika katika sheria za mirathi, hawawezi kuwa ni cha urithi wa mtu fulani, wala wao hawana haki ya kupata mirathi. [11]
Kwa mujibu wa ufafanuzi wa Ayatullahi Fadhel Lankarani, riwaya hii—kwa kuzingatia maneno yake ya mwisho (“makafiri ni kama wafu …”)—haijaja kutangaza kwamba; katu kufru au makafiri hawatapata nguvu na uwezo wa kuupindukia Uislamu, bali imekuja kubainisha kuwa, hakuna hukumu yoyote ile ya sharia iliyowekwa itakayowafanya makafiri kuwa ubora au fulani dhini ya Waislamu; yaani, sheria zote baina ya Waislamu na makafiri zimeainishwa kwa ajili ya kudhamini maslahi ya Waislamu. [12]
Kaida ya Nafyu al‑Sabil Kama Hukumu Mbadala (Hukmu Thanawiyya)
Qaida (kaida) ya Nafyu al‑Sabil ni miongoni mwa hukumu mbadala (hukmu thanawiyya), [13] nayo ina mamlaka (ina hukuma) juu ya hukumu msingi za awali (ahkamu al‑awwaliyya); hivyo, kila hukmu ya awali inayogongana na qaida ya Nafyu al‑Sabil, hubatilishwa na nafasi yake hutawaliwa na kaida (qaida) ya ya Nafyu al‑Sabil. [14] Miongo mwa mifano ya kisheria kuhusiana na kaida hii ni kwamba: kwa mujibu wa kaida ya uhalali wa biashara (halaliyyat al-mu'amalat), itakuwa ni halali kwa mfanya biashara kumuuzaji wa mtumwa Mwislamu na kuuzia kafiri. Hata hivyo, kwa kuwa tendo hili la kibiashara hupelekea udhibiti wa kafiri dhidi ya Mwislamu, hii inapelekea kubatilishwa kwa biashara hiyo kupitia misingi ya kaida ya Nafyu Sabil. Kadhalika, ndoa ya mwanamke Mwislamu ya kuolewa mwanamume kafiri. Ingawe ndoa kama ndoa, ni jambo lisilo na dosari ndani yake, ila ndoa hiyo hubatilika chini ya kaida hii, hii ni kupitia kigezo cha kwamba; jambo hilo linasababisha udhibiti wa mume kafiri juu ya mke Mwislamu. [15]
Matumizi ya Kifiqhi na Kisiasa
Kaida ya Nafyu al‑Sabil imekuwa na matumizi mengi katika fiqhi, huku mafaqihi wengi wakitoa fatwa zao kadhaa kwa mujibu wake. [16] Miongoni mwa fatwa zilizotolewa kwa mujibu wa kaida hii, ni ile fatwa na hukumu ya kifiqhi isemayo kwamba; Kwa kuwa haijuzu kwa asiye Mwislamu kumiliki mtumwa wa Kiislamu, hivyo basi ni haramu kumuuzaji au kumtoa zawadi mtumwa wa Kiislamu kwa asiye Mwislamu. Pia fatwa za wanazuoni zinasema kwamba; Kisheria, asiyekuwa Mwislamu hawezi kuwa ni mlezi wa mtoto wa Kiislamu. [17]
Baadhi ya wanazuoni na watafiti mbali mbali ya mambo ya kishiria, wakirejea kanuni hii, wamesema kwamba; Ni kwa Waislamu kufunga na kuziba njia zote zile zinazoweza kupelekea ushawishi na udhibi wa makafiri juu ya jamii za Kiislamu, iwe ni katika nyanja za kisiasa, kijeshi, kiuchumi au kitamaduni. Kanuni hii ina sura mbili, chanya na hasi: upande wa sura hasi unaangazia kukanusha utawala na udhibiti wa wageni juu ya hatima na mustakabali wa kisiasa na kijamii wa Waislamu; ama upande wa sura chanya unaielekeza jamii ya Kiislamu kwenye wajibu wao kidini wa kulinda uhuru wa kisiasa na kuondoa misingi ya utegemezi juu ya wengine. [18]
Mifano Hai ya Hukumu Zilizotolewa kwa Mujibu wa Kaida Hii
Kuna viongozi kadhaa wa kidini na mafaqihi wa Kishia waliotumia kaida ya Nafyu al‑Sabīl na kutoa fatwa maalumu kulingana na hali mbalimbali, ili kuondoa udhibiti wa makafiri juu ya Waislamu, miongoni mwazo ni:
- Fatwa ya kuharamisha tumbaku: Mirza Shirazi, mmoja wa marjaa (faqihi mkuu) wa Kishia akirejelea kaida hii, aliamua kutoa fatwa ya kuharamisha tumbaku, kama mwitikio na radiamali dhidi tendo la kampuni ya Uingereza kumili au kumilikishwa haki kamili na ya kipekee ya biashara ya tumbaku nchini Iran. Fatwa hiyo ilisababisha mwamko uliopelekea maandamano makubwa ya umma, na hatimaye kufutwa kwa mkataba huo mnamo mwaka 1309 Hijiria. [19]
- Upinzani dhidi ya Kapitulesheni: Imamu Khomeini, kiongozi wa kwanza wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa kutegemea kanuni hiyo hiyo ya Nafyu al‑Sabil, alipinga katakata kupitishwa kwa Kapitulesheni (mswada uliotoa kinga ya kisheria kwa raia wa Kimarekani, wakiwemo washauri wao wa kijeshi, nchini Iran), mswada uliopitishwa mnamo mwaka 1343 Shamsia katika Bunge la Iran. Akisimama kwa ajili ya kupinga mswada huo, alitangaza msimamo wake kupitia Aya ya Nafyu al‑Sabīl isemayo:
(وَلَنْ يَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا): (Na Mwenyezi Mungu kamwe hatojaalia makafiri kuwa na njia ya kuwatawala (kuwadhibiti) Waumini). [20]
Monografia (Kitabu Maalum)
Kitabu Qaida ya Nafy al‑Sabīl: Ni monografia iliandikwa kwa lugha ya Kifarsi, kazi iliyofanya Fatime Ghafarnia. Kazi hii inatathmini uwezo na ufanisi wa kaida hii hiyo ya kifiqhi na namna ya utumikaji wake kama nyezo maalumu katika nyanja mbali mbali, zikiwemo nyanja za kifiqhi, Sheria ya Kiraia, Katiba, pamoja na nyanja zinazoambatana na masuala ya utamaduni, uchumi na sera za nje za Iran. Monografia hii imechapishwa na Taasisi ya Hajar Publications, taasisi inayofungamana na Kituo cha Usimamizi cha Hawza ya Kielimu ya Wanawake, mwaka 1391 Shamsia. Kitabu hichi kilichapishwa ikiwa na kurasa 247. [21]