Kupaka wanja

Kutoka wikishia


Kupaka wanja (Kiarabu: الاكتحال) ni katika mambo ya mustahabu na sunna za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu wa madhehebu ya Shia ambapo waliwausia watu wengine kulitekeleza hilo. Katika hadithi kumeelezwa faida za kimaada na kimaanawi za kupaka wanja kama vile kuzuia na kutibu baadhi ya maradhi ya macho na kusaidia kufanya ibada na kukesha usiku kwa ajili ya ibada.

Katika sheria za fikihi kumetajwa hukumu za kupaka wanja. Baadhi ya mafaqihi hawakuchukulia kupaka wanja kuwa ni mapambo yaliyoharamishwa ya wanawake mbele ya wananaume wasio maharimu. Ni makuruhu kwa aliyefunga Saumu kupaka wanja endapo harufu na ladha yake itafika kooni. Pia, wengine wanaona kuwa ni kikwazo kwa maji ya udhu kufika mwilini. Mafakihi wamechukulia kupaka wanja kuwa ni miongoni mwa mambo ya haramu (yaliyokatazwa) kwa aliyevaa ihramu.

Utambuzi wa maana na nafasi yake

Kifaa cha kupakia wanja kilichotengenezwa kwa mawe katika karne ya 4 hadi karne ya 6 Hijiria, kinacho nasibishwa na Iran na Asia ya kati.

Kupaka wanja macho ambako katika Fiqhi kunafahamika kama Iktihal [1] ni katika njia za kujipamba [2] na pia ni katika mambo ya mustahabu ambapo wanaume na wanawake wameusia kutekeleza sunna hii. [3]

Katika vyanzo vya Kiislamu, kupaka wanja kunatajwa kuwa ni miongoni mwa sunna na mwenendo wa Mtume [4] na Maimamu (a.s) wameusia hili [5] na hilo limetambuliwa kuwa ni dalili ya imani [6] na wakawahimiza masahaba wao kupaka wanja. [7] Baadhi ya vitabu vya hadithi vimeweka mlango maalumu wa hadithi zinazohusiana na maudhui ya kupaka wanja. [8]

Iktihal katika lugha ya Kiarabu maana yake ni kuweka kitu juu ya jicho [9] au kila kitu chenye faida kwa ajili ya kutibu ambacho huwekwa juu ya jicho. [10]

Hukumu za kifiq’h za wanja

Maudhui ya kupaka wanja imezungumziwa katika milango mbalimbali ya fiq’h:

Katika hukumu za mavazi

Baadhi ya mafaqihi hawaoni kama kupaka wanja kuwa ni katika mapambo yaliyoharamishwa ya wanawake mbele ya wananaume wasio maharimu wao. [11] Kadhalika baadhi ya wahakiki wameona suala la kupaka wanja kuwa ni mfano wa:((إِلّا ما ظَهَرَ مِنْها ; isipo kuwa unao dhihirika)), katika aya isemayo:[13] [12] ((وَ لا یبْدِینَ زِینَتَهُنَّ إِلّا ما ظَهَرَ مِنْها ; wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika)). Katika tafsiri ya Aya iliyotangulia kuna hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) [14] na Imamu Muhammad Baqir (a.s) [15] ambapo kupaka wanja kunatambulishwa kuwa ni katika mapambo ya dhahiri ambayo ni mubaha kwa wanawake.

Katika Ihramu

Kuna tofauti ya maoni na mitazamo kuhusu kama ni haramu au makuruhu kutumia wanja mweusi mtu akiwa amevaa ihramu.[16] Baadhi ya mafaqihi wameona kuwa ni haramu kwa wanaume na wanawake [17] kutumia wanja mweusi wakiwa katika hali ya ihramu, [18] hata kama si kwa ajili ya kujipamba.[19] Hata hivyo kama mtu atalazimika kutumia wanja katika Ihram haitakuwa haramu. [20].

Baadhi ya watu wamedai juu ya kuwa maarufu na kuweko makubaliano kwa ajili ya kuwa haramu kupaka wanja wakati wa Ihram, [21] ingawa Sheikh Tusi aliona kuwa ni miongoni mwa mambo ya makuruhu (machukizo) ya Ihram.[22] Katika baadhi ya vitabu vya hadithi kama vile Wasail al-Shia [23] na Mustadrak al-Wasail [24], kumetengwa mlango maalumu wa hadithi zinazozungumzia kuwa haramu kupaka wanja katika hali ya Ihram.

Baadhi ya mafaqihi wanaamini kwamba, kupaka wanja ukiwa katika Ihram hakuna adhabu ya kafara, lakini kama wanja huo utakuwa na harufu nzuri, kwa mujibu kauli yenye nguvu jambo hilo litakuwa na kafara. [25]

Katika Sala na Saumu

Baadhi ya wanazuoni mtazamo wao ni kuwa, inaruhusiwa kupaka wanja mtu akiwa katika hali ya kufunga Saumu na wengine wameliona jambo hili kuwa ni katika mambo yanayobatilisha Saumu; [26] lakini baadhi ya mafaqihi wanaamini kwamba, kupaka wanja wakati mtu amefunga Saumu ni jambo la makuruhu (kuchukiza) ikiwa ladha yake au harufu itafika kooni. [27]

Wanja umetambuliwa kuwa mojawapo ya vikwazo vya maji ya udhu kufika mwilini. [28]

Faida

Katika hadithi za Kiislamu, kumeashiriwa faida za wanja kwa macho [29] na katika baadhi ya hadithi inapendekezwa kupaka wanja kwa ajili ya kinga [30] na kutibu baadhi ya magonjwa ya macho. [31] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) inaelezwa kuwa, kupaka wanja usiku kuna faida kwa mwili na mchana ni mapambo. [32] Faida zingine za kupaka wanja zilizoelezwa katika hadithi ni, kusaidia kukua kwa kope, ukali na uimara wa macho, [33] kuondolewa kwa vumbi machoni, [34] kusaidia kukesha usiku, [35] kusujudu kwa muda mrefu, [36] na mng'ao na nuru kwa muonekano na sura ya mtu. [37]

Katika baadhi ya hadithi, kumetolewa tahadhari kuhusiana na aina ya wanja, [38] kiwango cha kutumia [39] na wakati wa kutumia [40] na kuna dua maalumu iliyoashiriwa ambayo husomwa wakati wa kupaka wanja. [41].