Nenda kwa yaliyomo

Khaaje Nasiru al-Din al-Tusi

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Khawaja Nasir Dini Tusi)
Khawaja Nasir al-Din al-Tusi

Khawaja Nasir al-Din al-Tusi (597-672 Hijiria) (Kiarabu: الخواجة نصير الدين الطوسي) ni mwanafalsafa na mwanateolojia wa Kishia wa karne ya 7 Hijiria. Khawaja Nasir anatambulika kama mhuishajii wa falsafa na mbunifu wa mtindo wa falsafa katika theolojia ya Kishia. Baadhi ya wanachuoni wa Kishia kama vile Allama Hilli, Ibn Maytham Bahrani na Qutbuddin al-Shirazi walikuwa miongoni mwa wanafunzi wake.

Nasir al-Din al-Tusi ndiye mwandishi wa vitabu na risala nyingi za maadili, mantiki, falsafa, theolojia, hisabati na nujumu. Akhlaq Nasiri, Ausaf al-Ashraf, Asas al-Iqtibas, Sherh al-Isharat, Tajrid al-I'tiqad, Jam'i al-Hisab na kitabu mashuhuri cha Zij-i Ilkhani, Tadhkirat fi ilm al-hay'a katika elimu ya nujumu ni baadhi ya vitabu na athari zake muhimu na maarufu. Pia alijenga na kuasisi kituo cha uchunguzi wa masuala ya nujumu cha Maraghe na maktaba ya Maraghe ambayo ina vitabu zaidi ya 400,000.

Inasemekana kuwa Khawaja Nasir alilazimika kuandamana na baadhi ya watawala wa zama zake; lakini katika kufuatana huko aliweza kuandika na kualifu athari kadhaa; kwa mfano, akiwa pamoja na Hulaku-Khan Mongol, alifanya juhudi kulinda urithi wa Kiislamu uliokuwa katika hatari ya kuangamizwa, na kwa sababu ya hatua zake, baada ya muda mchache Wamongolia walisilimu na kuingia katika Uislamu.

Pia, kuwepo kwake wakati wa kukombolewa Baghdad na Wamongolia kumezingatiwa kuwa ni sababu ya kupungua uporaji na mauaji ya watu na kuokoka wanazuoni wengi kutokana na kifo. Khawaja Nasir al-Din al-Tusi alifariki huko Baghdad na akazikwa katika Haram ya Kadhimein kwa mujibu wa wasia wake. Tarehe 5 Isfand (kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia) ambayo ni siku ya kuzaliwa kwake imesajiliwa kwa jina la Siku ya Mhandisi kwa ajili ya kumkumbuka na kumuenzi alimu na msomi huyu.

Maisha Yake

Muhammad bin Muhammad bin Hasan, anayejulikana kama Khawaja Nasir al-Din Tusi, alizaliwa tarehe 11 Jumadi al-Awwal 597 Hijria mwafaka na 17 Februari 1201 Hijiria huko Tus.[1] Alijifunza Qurani Tukufu, nahw, sarf na masomo mengine ya awali akiwa bado mdogo. Kisha, kwa muongozo wa baba yake, alijifunza utangulizi wa elimu ya hisabati kutoka kwa Kamal al-Din Muhammad. Vile vile alijifunza elimu ya fiq’h na hadithi kutoka kwa baba yake na babu yake, ambao mwenyewe pia walikuwa miongoni mwa wanazuoni wa fiq’h na hadithi wa zama hizo.[2] Mwalimu wake mwingine alikuwa Noor al-Din Ali bin Muhammad Shi'i ambaye ni mjomba wake na ambaye alimfundisha mantiki na falsafa.[3]

Baada ya kifo cha baba yake, Tusi aliondoka katika mji wa Tus na kuelekea Neyshabur, palipokuwa mahali pa kukutana kwa wanachuoni na watafuta elimu wakati huo.[4] Alisoma kitabu cha Isharaat cha Abu Ali Sina katika falsafa kwa Fariduddin Damad na alisoma kitabu chake cha Qanoon katika tiba kwa Qutbuddin Misri[5] na alishiriki katika masomo ya Sirajuddin Qamari, Abu al-Saadat Esfahani na wengineo.[6] Pia alikutana na Farid al-Din Attar katika mji huu.[7] Kadhalika alikuwa mwanafunzi wa Kamal al-Din bin Yunus Mosuli, ambaye alikuwa mahiri na hodari katika elimu nyingi, hasa hisabati. Vilevile alisoma sehemu ya kitabu cha al-Ghuniyah cha Ibn Zuhra kutoka kwa Salim bin Badran Mazni Misri, ambaye alikuwa mmoja wa mafakihi wakubwa wa Shia Imamiya.[8]

Kuweko katika Ngome za Ismailia

Baada ya Wamongolia kuishambulia kijeshi Iran na kuibuka machafuko hususan katika eneo la Khorasan, Khawaja kwa muda fulani alikuwa akizunguka na katika miji tofauti hadi alipokwenda Qahestan [9] kwa mwaliko wa Nasir al-Din mtawala wa ngome za Ismailiya katika Khorasan. Akiwa huko alitarjumu kwa lugha ya Kifarsi kitabu cha Tahdhib al-Akhlaq watat’hir al-A’raq cha Abu Ali Miskawayh Razi. Aliongezea baadhi ya maudhui kwa jina la Nasir al-Din, Akhlaq Nasiri. [10] Tarehe ya kuandikwa kwa kitabu hiki ilikuwa 630 hadi 632 Hijiria [11] Kadhalika akiwa huko pia aliandika kitabu katika elimu ya maumbo kwa jina la al-Risalat al-Muiniyah, kwa jina la Muin al-Din, mtoto wa Nasir al-Din. [12] Ngome na maboma ya Ismailia, yametambulika kuwa, nguvu pekee mkabala na mashambulio ya Wamongolia. Katika hali ambayo miji ya Khorasan na Neyshabur ilikuwa imeangukia kikamilifu mikononi mwa Wamongolia, ngome hizi zilisimama kidete kwa miaka mingi na hazikusalimu amri kwa Wamongolia. [13]

Alauddin Muhammad, kiongozi wa Ismailia baada ya kupata habari ya kuwepo kwa Khawaja Nasir Tusi pamoja na Nasir al-Din, alimwita Khawaja Nasir na akaenda kwenye kasri ya Maymun Duz akiwa na Nasir al-Din na kiongozi wa Ismailiya alimkaribisha na kumpokea kwa mapokezi maalumu na ya kipekee. Khawaja Nasir al-Din Tusi alikaa naye katika ngome ya Alamut hadi mwana wa Ala al-Din Muhammad, yaani Rukn al-Din alipojisalimisha kwa Wamongolia katika shambulio lao la pili. [14]

Muhuri wa ukumbusho wa Khawaja Nasir al-Din Tusi

Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, kuwepo kwa Khawaja Nasir na kukaa kwake katika ngome za Ismailia haikuwa kwa hiari, bali alilazimishwa kufanya hivyo; [15] hata hivyo, Aqsarai katika Musamara al-Akhbar anaamini kwamba Khawaja Tusi alikuwa na cheo cha Waziri Mkuu kwa Ismailia na alikuwa na daraja na nafasi muhimu kiasi kwamba, alipewa lakabu ya Khawaja Kainat (kiongozi/bwana wa viumbe). [16]

Wale wanaoamini kwamba Khawaja Nasir Tusi alilazimishwa kuwa pamoja na Ismailia na akafungiwa kwenye ngome zao, wanarejea maneno yake ya mwishoni mwa maelezo na sherh ya kitabu cha Isharaat, ambamo anasikitikia hali ya maisha yake katika zama hizo. [17]

Khawaja Nasir al-Din al-Tusi na Hulagu-Khan Mongol

Khwaja Nasir, baada ya shambulio la pili la Wamongolia chini ya amri ya Hulagu-Khan (Hulegu)na kusalimu amri kwa majumba na ngome za Ismailia, alifanikiwa kuingia katika serikali na utawala wa Hulagu-Khan. [18] Kwa mujibu wa Seyyid Mohsen Amin ni kwamba, Khawaja Tusi, bila ya kuwa na uwezo wa kuchagua, alikuwa pamoja na Hulagu na katika hali ambayo hakukuweko na uwezo wa kukabiliana na mashambulio ya wavamizi si kutoka kwa wananchi wala kwa utawala, alijaribu na kufanya juhudi za kulinda turathi za Kiislamu ambazo zilikuwa katika hatari ya kuangamizwa na kwa sababu ya hatua yake hiyo hatimaye baada ya muda fulani Wamongolia walisilimu na kuingia katika dini ya Uislamu. [19] Khawaja Tusi alikuwa pamoja Hulagu Khan katika shambulio lake dhidi ya Baghdad katika mwaka wa 655 Hijria. [20]

Kituo cha kuangalilia Sayari

Baada ya Baghdad kukombolewa na Hulagu-Khan, Khawaja Nasir al-Din Tusi alipendekeza kujengwa kwa kituo cha kutazamia sayari; kwa kuhalalisha hilo kwamba, kulingana na ujuzi alionao katika elimu ya nyota, anaweza kumjulisha Sultani kuhusu matukio yajayo, urefu wa maisha yake na kizazi kwa usaidizi wa kutazama nyota. [21]

Pendekezo hili lilipendwa na Hulagu-Khan na ujenzi wake ulianza mnamo 657 Hijria. [22] Kwa muktadha huo, akawa ameasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maragheh. Kulingana na Seyyid Mohsen Amin, Khawaja Nasir alikifanya kituo cha kuchunguzia sayari cha Maragheh kuwa mahali pa kukusanyia idadi kubwa ya wasomi wa wakati huo, na hivyo kuwaokoa kutokana na kuuawa na pia alifanya jitihada nyingi kukusanya idadi kubwa ya vitabu na kuvihifadhi. [23]

Ujenzi wa kituo cha uchunguzi wa sayari ulidumu hadi mwisho wa maisha ya Khawaja, na zij (jedwali la kale la kuhesabia nujumu) lililopatikana kutoka kwa uchunguzi huu iliitwa Zij Ilkhani. [24]

Maktaba ya Maragheh

Jirani na kituo cha kuangalilia mwenendo wa mwezi, jua na nyota cha Maraghe Khawaja alianzisha maktaba kubwa na yenye thamani kubwa ambamo ndani yake mlikuwa na jumla ya vitabu 400,000 vyenye thamani kubwa. Nasir al-Din alivikusanya vitabu hivyo kutoka katika maeneo mbalimbali kama Baghdad, Sham, Beirut na Algeria.

Vitabu vingi vya kupendeza na muhimu ambavyo viliporwa kutoka Baghdad, Damascus, Mosul na Khorasan vilihamishiwa humo kwa amri ya Hulagu Khan. Khawaja mwenyewe pia aliwatuma watu katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kununua vitabu vya kielimu popote walipovipata na kumpelekea, na popote alipokutana na kitabu chenye manufaa na cha kupendeza, aalikuwa akikinunua. [25]

Kulingana na baadhi ya wanahistoria, karibu vitabu 400,000 vilikusanywa katika maktaba ya Maragheh. [26] Katika maktaba ya Maraghe kulikuweko na aina kwa aina ya vitabu vilivyovyokuwa vimetarjumiwa kwa lugha za Kichina, Kimongolia, sanskrit, Kiashuri, Kiarabu na Kifarsi na vilikuwa viko kwa ajili ya wanaotafuta elimu na wanazuoni wa kituo cha akademia ya kuangalia sayari. Akademia hii kwa hakika kilikuwa kituo cha elimu ambamo ndani yake kulikuwa kukipatikana elimu mbalimbali za zama hizo kama hisabati, nujumu na nyinginezo. [27]

Kuweko katika kukombolewa Baghdad

Ibn Taymiyyah (661 AH-728 Hijria), mmoja wa wanazuoni wa Ahlu-Sunna amedai kwamba, Khalifa wa Baghdad aliuawa kwa amri ya Khawaja Nasir al-Din Tusi; [28] lakini baadhi, wakitumia uchunguzi wa vyanzo vya kabla yake na kutoona habari hizo ndani yake, wameyaona madai hayo kuwa ni uongo na ni tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Khawaja Nasir al-Din al-Tusi. Aidha wamesema kuwa, kuna uwezekana kwamba, vyanzo vilivyokuja baada ya Ibn Taymiyyah viliandika na kuleta habari hizi kwa kumfuata yeye. [29] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba, kuwepo kwa Nasir al-Din Tusi wakati wa kukombolewa Baghdad na Wamongolia kulikuwa sababu ya kupungua uporaji na mauaji ya watu, na kwa msaada wake, wasomi wengi waliokoka kutokana na kifo. [30]

Kuaga Dunia

Khawaja Nasir alifariki dunia tarehe 18 Dhul-Hijjah 672 Hijria alipokuwa Baghdad kwa ajili ya kupanga mambo ya wakfu na wanachuoni. Kwa mujibu wa wasia wake, alizikwa katika Haram ya Kadhimein. [31] Pia alitaka kwamba kusitajwe wala kuashiriwa katika kaburi lake juu sifa zake za kielimu bali juu ya kaburi lake kuandikwe Aya hii: ((وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ ; Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini)). [32] [33]

Madhehebu

Kuna ushahidi mwingi kwamba Khawaja Nasir al-Din Tusi ni Shia Ithnaasharia; kwa mfano, katika vitabu vyake vingi vya kitheolojia, kama vile Tajrid al-I’tiqad, ameashiria Maimamu kumi na wawili na wajibu wa Umaasumu wao. [34]

Vile vile aliandika risala maalum juu ya mada hii, ambapo tunaweza kutaja risala ya "Al-Firqat al-Najiyyah" na " al-Risalat fi Hasr al-Haq Bimaqalat al-Imamiya", na vile vile "Al-Ithna Ashriya" na "al-Risalat Fil Imamah". [35] Pamoja na hayo katika orodha ya kazi za Khawaja Nasir, kuna vitabu na risala zilizonasibishwa kwake ambazo zinaafikiana na mafundisho ya madhehebu ya Ismailia. [36]

Aghalabu ya wanazuoni Shia Ithaasharia wamekana na kupinga kuzihusisha kazi hizi na Khawaja, lakini baadhi ya wahakiki na wasomi wa Kiislamu wa Magharibi wanaamini kwamba, kwa namna fulani Khawaja alibadilisha madhehebu wakati wa kuwepo kwake miongoni mwa Waismailia. [37]

Baadhi wakitegemea athari hizi wanaamini kwamba, baada ya kupata kimbilio katika ngome za Ismailia, alibadili madhehebu kwa muda na kisha akarudi kwenye madhehebu ya Shia Ithnaasharia. [38]

Baadhi ya waandishi pia wanaamini kwamba Khawaja Tusi, akiwa Shia Ithnaasharia, alitumia taqiyyah na ili kuokoa maisha yake, na akiwa katika ngome za Waismailia alijishughulisha na kuandika vitabu na risala zake. [39] Abdallah Ni’mah anaunga mkono dhana hii kwamba, baada tu ya ngome za Waismailia kubomolewa, Khawaja alitangaza kwamba, yeye ni Shia Ithnaasharia. [40]

Nafasi Yake ya Kielimu

Allama Hilli anasema: Shekhe huyu (Khawaja Nasir al-Din al-Tusi) alikuwa mbora kabisa katika zama zake kwenye elimu za kiakili... na ni mtu mwenye tabia njema kabisa ambaye mimi nimewahi kumuona. [41] Khawaja Nasir Tusi amechukuliwa kuwa sawa na Ibn Sina katika elimu; kwa tofauti kwamba Ibn Sina alikuwa amebobea katika tiba na Khawaja Nasir alitabahari katika hisabati.

Baadhi wanaamini kwamba utetezi wa Khawaja Nasir al-Din Tusi kwa Ibn Sina dhidi ya ukosoaji wa Fakhr Razi, katika kitabu cha Sherh Isharaat, ulipelekea kuhuishwa kwa falsafa katika zama hizo. [42] Kadhalika Khawaja anatambulika kama mbunifu wa mbinu ya falsafa katika theolojia ya Shia. [43] Shekhe Murtadha Mutahhari anaamini kwamba, kazi zote za kitheolojia baada ya Khawaja Nasir ziliathiriwa na kitabu chake cha Tajrid al-I’tiqad. [44]

Kwa mujibu wa baadhi ya tafiti za kisasa, Khawaja Nasir Tusi, kwa upande mmoja, alikuwa ni mfafanuzi na mkamilishaji wa wanafalsafa na wasomi waliomtangulia, na kwa upande mwingine, akawa kielelezo cha kuigwa na kufuatwa na wasomi na wanazuoni wa baada yake. [45]

Wanazuoni wengi wa Kiislamu pamoja na wanazuoni wa Kiislamu wa Kimagharibi wamemsifu. [46] Kauli mbalimbali zilizotolewa kuhusiana na Khawaja Tusi zinaonyesha nafasi na daraja yake ya kielimu. Baadhi yaa kauli hizo ni: Sultan al-Muhaqqiqin, [47] Fakhru al-Hukamaa, Muayyid al-Fudhalaa, Nasir al-Millah wal Din. [48], Muhaqqoq Mudaqqiq Tusi na Hakim Adhim Qudousi na [49] Afdhwal al-Mutaakhirin wa Akmal al-Mutaqaddimin. [50]

Tarehe 5 Isfand (kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia) ambayo ni siku ya kuzaliwa kwake imesajiliwa kwa jina la Siku ya Mhandisi kwa ajili ya kumkumbuka na kumuenzi alimu na msomi huyu na kila mwaka hufanyika hafla mbalimbali kwa mnasaba wa siku hii. [51]

Wanafunzi

Baadhi ya wanafunzi wa Khawaja Nasir al-Din al-Tusi ni:

  1. Allama Hilli, fakihi na mwanateolojia mkubwa wa Kishia (aliaga dunia 726 Hijria), alisoma falsafa kwa Khawaja Tusi [52] na aliandika sherh na ufafanuzi wa kitabu cha Khawaja cha Tajrid al-I’tiqad kinachojuliakana kwa jina la Kashf al-Murad. Kitabu hiki ndicho mashuhuri zaidi miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kutoa sherh na ufafanuzi wa kitabu cha Tajrid al-I’tiqad. [53]
  2. Ibn Maytham Bahrani, mwandishi wa kitabu cha Misbah al-Salikin (ufafanuzi wa Nahaj al-Balagha), mwanafalsafa, mwanateolojia, mwanahisabati na fakihi ambaye katika faslafa alikuwa mwanafunzi wa Khawaja Nasir lakini katika fiq’h alikuwa mwalimu wake. [5]]
  3. Qutb al-Din al-Shirazi (aliaga dunia 710 Hijria), wakati Khawaja alipokwenda Qazvin akiwa na Hulagu Khan alikuwa pamoja na Khawaja kisha akaambatana pamoja naye Maragheh na akawa mwanafunzi wa Khawaja katika elimu ya jiometri (maumbo), hisabati, falsafa na tiba. Khawaja alikuwa akimuita kwa jina la Qutb Falak al-Wujud. [55]
  4. Seyyid Rukn al-Din (Hassan bin Muhammad bin Sharfshah Alawi), alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Khawaja na amefafanua baadhi ya athari za mwalimu wake. [56]
  5. Kamal al-Din Abdul-Razaq Sheybani Baghdadi (664-723) mashuhuri kwa jina la Ibn al-Fuwati, ni mmoja wa waaandishi wa historia wa karne ya 7 Hijria na vitabu vya “Mu’jam al-Adaab” na “Al-Hawadith al-Jami’ah” ni miongoni mwa athari zake. [57]
  6. Imad al-Din Harbawi maarufui kwa jina la Ibn al-Khawwam (643-728 Hijria) alikuwa mahiri mno katika zama zake katika taaluma za hesabu na tiba. [58]

Vitabu Vyake

Makala asili: Orodha ya vitabu cya Khawaja Nasir al-Din al-Tusi

Majimui ya vitabu na athari za kielimu za Khawaja Nasir al-Din al-Tusi (aliaga dunia 672 Hijria) imetambuliwa kuwa ni zaidi ya 184. Khawaja ameandika vitabu katika nyanja mbalimbali kama hisabati, jiometri, theolojia, falsafa, irfan, mantiki, fiq’h, tiba, Ulum Ghariba na Tafsir ya Qur’an. Akthari ya athari zake ameziandika kwa lugha ya Kiarabu. Katika utangulizi wa kitabu cha Sherh Isharaat, anaelezea taabu, mashaka na ghamu alizokumbana nazo wakati wa kuandika vitabu. [60] Baadhi ya vitabu vyake ni:

Rejea

  1. Niʿma, ʿAbd Allāh, Falāsifat al-Shīʿa, 1987, uk. 535
  2. Amin, al-Ismāʿīlīyyun wa l-Mughul wa Nasīr al-Dīn al-Tūsī, 2005, uk. 16-20
  3. Amin, al-Ismāʿīlīyyun wa l-Mughul wa Nasīr al-Dīn al-Tūsī, 2005, uk. 20
  4. Amīn, Aʿyān al-Shīʿa, 1986, juz. 9, uk. 415
  5. Naṣīr al-Dīn al-Ṭūsī, Tansūkhnama-yi Īlkhānī, 1363 Sh, uk. 15
  6. Amīn, Aʿyān al-Shīʿa, 1986, juz. 9, uk. 415
  7. Amīn, Aʿyān al-Shīʿa, 1986, juz. 9, uk. 415
  8. Naṣīr al-Dīn al-Ṭūsī, Tansūkhnama-yi Īlkhānī, 1363 Sh, uk. 16

Vyanzo

  • Amīn, Ḥasan al-. Al-Ismāʿīlīyyūn wa l-Mughul wa Nasīr al-Dīn al-Tūsī. Qom, Muʾassisat Dāʾirat al-Maʿārif al-Fiqh al-Islāmī, 2005.
  • Amīn, al-Sayyid Muḥsin al-. Aʿyān al-Shīʿa. Ed. Ḥasan al-Amīn. Beirut, Dār al-Taʿāruf, 1986.
  • Aqsarāʾī, Maḥmūd b. Maḥmūd al-. Musāmarat al-akhbār. Tehran, Asāṭīr, 1362 Sh.
  • ʿAzīzī, Faḍāʾil wa sīra-yi chāhārdah maʿsūm dar athār-i ustād ʿAllāma Ḥasanzāda-yi Āmulī, 1381Sh, p. 402
  • Farhāt, Hānī. Andīshahā-yi falsafī wa kalāmī-yi Khwāja Naṣīr al-Dīn-i Ṭūsī. Translated by Ghulāmriḍā Jamshīdnijhād. Tehran, Markaz-i Pazhūhishī-yi Mīrāth-i Maktūb, 1389 Sh.
  • Ibn Kathīr, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Ed. ʿAbd Allāh b. ʿAbd al-Muḥsin al-Turkī. Egypt, Hijr li-l-ṭibāʿat wa l-Nashr wa l-Tawzīʿ wa l-Iʿlān, 1997.
  • Khwānsārī, Muḥammad Bāqir. Rawḍāt al-jannāt. Qom, Dihāqānī (Ismāʿīlīyān), 1390 AH.
  • Kutubī, Muḥammad b. Shākir. Fawāt al-wafayāt. Ed. Iḥsān ʿAbbās. Beirut, 1974.
  • Mudarrisī Raḍawī, Muḥamamd Taqī. Aḥwāl wa āthār-i Khwāja Naṣīr al-Dīn. Tehran, Bunyād-i Farhang-i Irān, 1354 Sh.
  • Naṣīr al-Dīn al-Ṭūsī, Muḥammad b. Muḥamamd. Tansūkhnama-yi Īlkhānī. Ed. Muḥammad Taqī Mudarris Raḍawī. Tehran, Iṭṭilāʿāt, 1363 Sh.
  • Niʿma, ʿAbd Allāh. Falāsifat al-Shīʿa ḥayātuhum wa ārāʾuhum. Beirut, Dār al-Fikr al-Lubnānī, 1987.
  • Amīn, Sayyid Ḥasan. "Khwāja Naṣīr al-Dīn-i Ṭūsī wa naqsh-i ū dar gustarish-i Tashayyuʿ wa ḥifẓ-i āthār-i Islāmī". Translated by Mahdī Zandīya. Journal of Shīʿashināsī, no. 5, spring 1383 Sh.
  • Naṣīr al-Dīn al-Ṭūsī, Muḥammad b. Muḥamamd. Tajrīd al-iʿtiqād. Ed. Muḥammad Jawād Ḥusaynī Jalālī. Tehran, Maktab al-Iʿlām al-Islāmī, 1407 AH.
  • Zaydān, Jurjī. Tārīkh al-tamaddun al-Islāmī. Egypt, 1914.