Tajrid al-I'tiqad (Kitabu)

Kutoka wikishia

Tajrid al-I'tiqad au Tajrid al-Kalam ni kitabu chenye maudhui ya elimu ya teolojia (aqaid). Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu na Khawaja Nasir al-Din al-Tusi (aliyeaga dunia 672 H). Kitabu hiki kinabainisha na kuthibitisha itikadi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithna'asharia kwa mbinu na utendaji wa kifalsafa. Baadhi ya maudhui zilizotajwa katika kitabu hiki mbali na kuthibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu na sifa Zake ni: Kuwa jumuishi kwa walimwengu wote risala na Utume wa Mtukufu Muhammad (s.a.w.w), Qur'ani kuwa ni muujiza, kutokuweko mtu mwingine anayestahiki ukhalifa na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume ghairi ya Imam Ali (a.s), kuwa kwake mbora zaidi ya wengine, Maimamu kuwa ni Maasumu (watu wasiotenda dhambi) na kwamba, mwanadamuu atafufuliwa Siku ya Kiyama kiroho na kimwili (roho ikiwa na mwili wake). Tajrid al-I'itiqad ni moja ya athari na vitabu vyenye thamani kubwa katika uga wa imani na itikadi za madhehebu ya Shia na kinahersabiwa kuwa ni katika matini mukhtasari zaidi za teolojia ya Shia; na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kumeandikwa athari na vitabu vingi vikitoa sherhe na ufafanuzi au kukikosoa kitabu hiki. Katika utambuzi wa kitabu cha Tajrid al-I'tiqad kwa akali kumeandikwa vitabu 231 vinavyosherehesha na kufafanua kitabu hiki kutoka kwa wasomi na Maulamaa wa Kisuni na Kishia katika uga huu; miongoni mwavyo ni Kashf al-Murad kilichoandikwa na Allama Hilli na Tasdid al-Qawaid kilichoandikwa na Abdul-Rahman Isfahani. Shahidi Murtadha Mutahhari anaamini kuwa, katika kitabu hiki Khawaja Nasir al-Din al-Tusi aliitoa teolojia katika nafasi ya elimu ya majadiliano na kuikurubisha na elimu ya hoja.

Mwandishi

Makala asili: Khawaja Nasir al-Din al-Tusi

Nasir al-Din Muhammad ibn Muhammad al-Tusi mashuhuri zaidi kwa jina la Khawajah Nasir al-Din al-Tusi ni mwanafalsafa na mwanahisabati mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa Tous Iran mwaka 597 na kuaga dunia Baghdad, Iraq 672 H. Katika kipindi cha utawala wa Hulaguu Khan Mongol, aliasisi kituo cha uchunguzi wa masuala ya nujumu cha Maraghe mwaka 660 Hijria. [1] Kuna takribani athari 200 za vitabu, sherhe na makala zingine katika maudhui tofauti zilizoandikwa na Nasir al-Din Tusi zikiwemo za elimu za kiakili kama falsafa na teolojia, akhlaq na elimu nyingine kama jiometri, hisabati, fizikia, fikihi, tafsiri, historia, mashairi, tiba na kadhalika. [2] Hata hivyo vitabu kama tajrid al-I'tiqad, tajrid dar mantiki, Fusul Nasiriyah, Ausaf al-Ashraf, Qawaid ala-Aqaid ni baadhi ya vitabu vyake muhimu zaidi. [3]

Mambo Jumla na Yaliyomo

Tajrid al-I'tiqad au kama ilivyokuja katika baadhi ya nakala kwa jina la Tajrid al-Aqaid, [4] au kama alivyotaja Agha Bozorg Tehrani katika kitabu chake cha al-Dhariah kwamba, ni Tajrid al-Kalam, [5] kimeandikwa na Khawaja Nasir al-Din al-Tusi [6] na kwa mujibu wa rai na mtazamo mashuhuri, kitabu hicho kilifikia tamati kuandikwa mwaka 660 Hijria. [7] Kitabu hiki ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu, kimechanganya na kujumuisha falsafa ya Kiislamu na teolojia ya Kishia ambapo masuala ya teolojia yamebainishwa humo kwa mbinu na utendaji wa kifalsafa. [8] Kuanzia karne ya 7 Hijria, kitabu cha Tajrid al-I'tiqad kilikuwa dira na muongozo wa maandiko, athari na vitabu vya teolojia (itikadi) vya Waislamu wa madhehebu ya Kishia na Kisuni. [9] Kitabu hiki kimeandikwa katika na faslu (milango) sita. Miongoni mwa faslu zake muhhimu zaidi:

1. Mambo jumla.

2. Kuthibitisha uwepo wa Muumba na sifa Zake.

3. Utume: Katika mlango huu kuna vipengee kumi kama, kutumwa Mitume, ulazima wa mab'ath, sifa za Mitume, miujiza, karama zao, kubaathiwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Qur'ani kuwa ni muujiza, na kadhalika.

4. Uimamu: Hapa kuna mada 12 zikiwemo maudhui kama ulazima wa Imam kuteuliwa, Umaasumu, Imam kuwa mbora zaidi kuliko wengine, Uimamu wa Imam Ali, kutokuwa na ustahiki mtu mwingine kuchukua ukhalifa na kuwa kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume (s.a.w.w) ghairi ya Imam Ali (a.s), Maimamu 12 na kadhalika.

5. Ufufuo, hapa kuna faslu 11 ambapo miongoni mwazo ni uwezekano wa kuumbwa ulimwengu mwingine, ufufuo (wa kimwili), thawabu na adhabu, msamaha wa Mwenyezi Mungu, shifaa, tawba na kadhalika. Katika faslu ya kwanza kunazungumziwa uwepo na kutokuweko (ujud wa adam).

Nafasi ya Kitabu cha Tajrid al-I’tiqad

Tajrid al-I’tiqad ni moja ya vitabu muhimu mno vya teolojia (itikadi) ya Kishia na kinatambuliwa kuwa kitabu cha kipekee. [10] Licha ya udogo wa kitabu hiki, lakini akthari ya Maulamaa wa madhehebu ya Kishia na wa madhehebu zingine, wameandika vitabu wakikifafanua na kukitolea maelezo na wamesema kuhusiana na kukubali au kupinga hoja na nadharia za Khawaja Nassir al-Din Tousi. [11] Agha Bozorg Tehrani mmoja wa watambuzi mahiri na watajika wa vitabu ambaye ni Mshia, amekitambua kitabu cha Tajrid al-I’tiqad kwamba, moja ya athari za Kishia zenye thamani mno. [12]

Kwa mujibu wa Ali Sadrai ni kuwa, kwa akali kuna vitabu 231vilivyoandikwa kufafanua kitabu cha Tajrid al-I’tiqad. [13] Wahakiki wanaamini kuwa, katika kitabu hiki Khawaja Nasir al-Din al-Tusi kwa kujumuisha falsafa ya Mashaiyya (Peripatetic school of philosophy iliyoasisiwa na Aristotle) na teolojia ya Kishia ameweza kukurubisha elimu za falsafa na teolojia baina ya wanafikra wa Kishia. [14]

Nakala Zilizopo

Kuna nakala nyingi zilizochapishwa za kitabu cha Tajrid al-I’tiqad; miongoni mwa nakala hizo ni ile iliyoandikwa 669 Hijria na ambayo inapatikana katika maktaba ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) mjini Tehran. [15] Nakala iliyochapishwa ya Tajrid al’tiqad ilisambazwa kwa mara ya kwanza ikiwa na sherhe na ufafanuzi wa Allama Hilli 1311 Hijria Shamsia. [16] Kuna chapa mbalimbali za kitabu hiki; miongoni mwazo ni nakala iliyosahihishwa na Muhammad-Jawad Husseini Jalali ambayo ilichapishwa na kusambazwa 1407 Hijria katika mji wa Qum. Sherhe ya Allam Hilli (Kashf al-Murad) ilitarjumiwa mwaka 1351 na Abul-Hassan Sha’rani na ikachapishwa sambamba na shrhe yake. [17] Kadhalika nakala iliyosahihishwa na Hassanzadeh Amoli ilichapishwa mwaka 1407 Hijria katika mji wa Qom. [18] Agha Bozorg Tehrani [19] na Haji Khalifa [20] wametambulisha idadi kubwa ya sherhe na ufafanuzi ulioandikwa kuhusiana na kitabu cha Tajrid al-I’tiqad. Kadhalika Ali Sadrai Khui na Sayyid Mahmoud Mar’ashi wamefanya utafiti na uchunguzi kuhusiana na nakala ya hati ya mkono ya Tajrid al-I’tiqad pamoja na sherhe na ufafanuzi uliuoandikwa kuhusiana na kitabu hiki na wakazitambulisha athari zote zilizoandikwa kuhusiana na kitabu hiki katika kitabu walichokipa jina la “ Utambuzi wa Kitabu cha Tajrid al-I’tiqad”. Kitabu hiki kinapatikana katika maktaba ya Umma ya Ayatullah Mar’ashi Najafi. [21]