Nenda kwa yaliyomo

Hukumu ya Jihadi

Kutoka wikishia

Hukumu ya Jihadi au Fat'wa ya Jihadi (Kiarabu: حكم الجهاد أو فتوى الجهاد) ni amri (hukumu) ya kiongozi wa juu wa dini inayohusiana na kuanzisha vita vya Jihadi dhidi ya maadui. Kigezo kikuu cha hukumu hii kinakuwa ni kuilinda dini pamoja na jamii ya Kiislamu. Hukumu hii pia huainisha vigezo na masharti yanayotakiwa kutimizwa, ili kupata uhalali kamili wa vita hivyo. Kwa mtazamo wa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia kuhusiana na muktadha huu, kule kutoa fat'wa ya Jihadi katika kipindi cha ghaiba (kipindi cha kutowepo Imamu Maasumu), kunaamsha hisia za Waislamu kuhisi uwepo wa nguvu za kiongozi wa kidini, ambapo fat'wa za maulamaa (katika masuala ya kijeshi), zinaweza kuwa ni miongoni mwa nyenzo, na ni njia muhimu ya kulinda dini pamoja na usalama wa jamii ya Kiislamu dhidi ya maadui za. Kwa mujibu wa fiq’hi ya Kiislamu, hukumu ya Jihadi inatoa amri kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kujilinda kushiriki katika vita dhidi ya maadui zao ili kulinda heshima, uhuru, na ardhi ya Kiislamu. Hukumu hii hutolewa hasa wakati wa uvamizi wa ardhi ya Kiislamu, kutokea kwa tishio dhidi ya dini, au kuibuka kwa hatari inayoweza kudhoofisha heshima, hadhi na uhuru wa Waislamu. Fatwa hii hutolewa na mujtahid mwenye sifa na ujuzi wa kifiqhi unaostahili, hii ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Jihadii hiyo inafanyika kwa kuzingatia misingi ya haki na uadilifu kulingana na sheria za Kiislamu.

Wanazuoni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wameonekana kutoa fatwa za Jihadi katika nyakati mbalimbali za kihistoria. Kuanzia mwaka 1241 hadi 1243 H, wanazuoni maarufu wa Shia kama Ja'far Kashif al-Ghita, Sayyid Ali Tabatabai, Mirza Qumi, Mulla Ahmad Naraqi na Sayyid Muhammad Mujahid, walitoa fatwa za Jihadi dhidi ya vikosi vya Urusi ili kuunga mkono utawala wa Qajar na kulinda ustawi wa Waislamu wa Iran. Baadhi ya watatafiti wanadhani kuwa hizi ndizo fatwa za kwanza kutolewa kama hukumu ya Jihadi katika historia ya fiqhi ya Shia Imamiyya, na zilikuwa ni hatua muhimu katika kulinda na kudumisha umoja wa jamii ya Kiislamu dhidi ya hatari za kigeni.

Huko Iraq, pia kulitolewa fatwa ya Jihadi iliyotolewa na Muhammad Taqi Shirazi mnamo mwaka 1337 Hijiria. Fatwa hii ndio iliyosababisha kuanzishwa kwa mapinduzi ya Thawrat al-‘Ishrin dhidi ya ukoloni na vikosi vya Uingereza, hasa katika maeneo yanayokaliwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mnamo mwaka 1948 M/1327 Shamsia, Abdul Karim Zanjani mmoja wa wanazuoni wa Shia wa karne ya 14 Hijiria, pia naye alitoa fatwa ya Jihadi dhidi ya Israeli. Aidha, mwaka 2014 Miladia, Sayyid Ali Sistani alitoa hukumu ya Jihadi ili kukabiliana na hujuma za vikosi vya wanamgambo wa ISIS nchini Iraq.

Kitabu «Rasa’il wa Fatawa Jihdiy» kilichoandikwa na Muhammad Hassan Rajabiy, kinajumuisha ndani yake majina 95 ya tasnifu na fatwa mbali mbali zilizotolewa na wanazuoni kuanzia mwaka 1200 hadi 1338 Hijiria.

Umuhimu na Nafasi ya Hukumu ya Jihadi

Hukumu ya Jihadi inarejelea amri rasmi (Hukumu za kisheria) inayotolewa na kiongozi wa juu kidini wa dini ya Kiislamu, kwa madhumuni ya kuanzisha vita dhidi ya maadui wa wafwasi wa dini hiyo, huku ikiainisha vigezo na masharti ya vita hivyo. [1] Katika zama za kipindi cha ghaiba (kipindi cha kutowepo Imamu), hukumu ya Jihadi huashiria ushawishi mkubwa wa nguvu za fatwa zinazotolewa na maulamaa wa Kishia, ikionesha nafasi ya kipekee ya viongozi wa kidini katika kuongoza na kulinda jamii ya Kiislamu. Hukumu hii ina umuhimu wa kipekee katika kulinda uhai, mali, heshima, na uhuru wa Waislamu, pamoja na ardhi zao, dhidi ya mashambulizi ya maadui. [2] Aidha imeelezwa ya kwamba; katika zama za ghaiba, fatwa ya Jihadi yenye lengo la kujihami, huhisabiwa kama silaha muhimu ya kuihami dini pamoja na usalama wa jamii ya Kiislamu dhidi ya wavamizi. [3]

Wanazuoni (mafaqihi) wa Kishia wamekuwa na mchango mkubwa katika historia ya Kiislamu kwa kuhamasisha mapambano dhidi ya maadui kupitia utoaji wa hukumu za Jihadi. Fatwa hizi zimekuwa zikitolewa hasa wakati ambapo ardhi za Kiislamu zilipokuwa zikivamiwa, au pale ambapo dini, heshima, na uhuru wa Waislamu ulipokuwa ukikabiliwa na hatari za viwango vya juu. [4] Mfano maarufu wa kihistoria katika hili, ni fatwa ya Jihadi ya mwaka 1337 Hijiria, iliyotolewa na mwanazuoni mashuhuri aitwaye Muhammad Taqi Shirazi. Fatwa hiyo ilichochea vyema harakati za mapinduzi ya silaha zilizojulikana kwa jina la Thawrat al-‘Ishrin dhidi ya ukoloni wa Uingereza nchini Iraq. Kwa sehemu kubwa mapinduzi haya yaliyoongozwa na maulamaa wa Kishia, yaliyo hamasisha jamii ya Kiislamu, hasa katika maeneo yenye Waislamu wa madhehebu Shia. [5]

Wanazuoni wa Shia hawahusishi moja kwa moja uwepo au ruhusa ya Imamu (a.s) au mwakilishi wake wa moja kwa moja kama ni sharti msingi kwa ajili ya kuanzisha Jihadi ya kujihami. [6]

Kwa mujibu wa maoni ya Ja'far Kashif al-Ghita, mwanazuoni maarufu wa madhehebu ya Shia wa karne ya 13 Hijria, ni kwamba; Jihadi ya kujihami inayofanywa kwa muundo rasmi na uongozi wa Kiislamu katika kipindi cha Ghaiba Kubra (kipindi kirefu cha kutowepo Imamu), huhitajia ruhusa kutoka kwa mujtahid maalumu mwenye sifa zinazostahili kumpa yeye mamlaka ya kutoa fatwa mbali mbali. [7] Kwa upande mwingine, Hussein Ali Muntadhiri, mwanazuoni wa Kishia wa karne ya 14 Hijria, yeye pia hakuichukulia ruhusa hiyo kama ni sharti la msingi katika kuanzisha Jihadi ya kujihami. Yeye dhana hiyo alisema kwamba; Ingawa ruhusa hiyo si sharti ya kupigana Jihadii ya kujilinda, ila ni muhimu kupata amri ya Walii Faqihi (kiongozi wa juu wa Kiisamu) kwa ajili ya utekelezaji na usimamiaji wa Jihadi hiyo ya kujihami. Kwa mujibu wa mtazamo wake, Jihadi ya kujihami ni jukumu la kila Muislamu, linaloamriwa moja kwa moja katika kipindi cha wakati wa matokeo hatari dhidi ya dini, jamii, au ardhi za Kiislamu. [8]

Fatwa Maarufu za Jihadi

Makala Asili: Orodha ya Fatwa za Jihadi

Katika historia ya Kiislamu, wanazuoni wa Shia wamekuwa wakitoa fatwa mbali mbali za Jihad kwa ajili ya kujihami dhidi ya maadui wa Uislamu. Zifuatazo ni baadhi ya fatwa maarufu zaidi miongoni mwazo:

Fatwa ya wanachuoni wa Kishia juu ya Jihad dhidi ya Israel
  • Fatwa Dhidi ya Urusi (1241-1243 Hijiria): Katika kipindi cha miaka ya 1241 hadi 1243 Hijria (1825–1828 Miladia), wakati jeshi la Urusi liliposhambulia Iran na kuteka baadhi ya maeneo yake, baadhi ya wanazuoni wa Shia walijitokeza na kutoa fatwa za Jihad ili kuunga mkono utawala wa Qajar na kulinda jamii ya Kiislamu ya Iran dhidi ya uvamizi huo wa Urusi. Wanazuoni kama Ja'far Kashif al-Ghita, Sayyid Ali Tabatabai, Mirza Qumi, Mulla Ahmad Naraghi na Sayyid Muhammad Mujahid, walitoa fatwa hizi muhimu kama ni sehemu ya juhudi za kidini na kijamii za kupinga uvamizi na kulinda ardhi ya Kiislamu. [9] Fatwa hizi zilikusanywa sambamba na tasnifu nyengine zinazohusiana na sheria za Jihad, kwa amri ya Abbas Mirza, mwana na mrithi wa Shah Fath Ali. Hatimaye fatwa hizo za Jihadi zilirikodiwa na Mirza Isa Qa'im Maqam Farahani katika kitabu kiitwacho Ahkam al-Jihad wa Asbab al-Rashad. [10] Kitabu hichi kinajumuisha miongozo ya kisheria na maelezo ya Jihad, amabacho kinatambulika kama ndiyo chanzo cha kihistoria kinachoelezea fatwa za kwanza kabisa za Jihad katika historia ya Shia. [11]
  • Fatwa ya Muhammad Taqi Shirazi (1337 Hijiria): Fatwa ya Jihadi ya Muhammad Taqi Shirazi ni moja ya fatwa muhimu na iliyoacha athari kubwa katika historia, fatwa ambayo iliyotolewa dhidi ya ukoloni na utawala wa Uingereza nchini Iraq. Fatwa hii ilitolewa mnamo tarehe 20 Rabi' al-Awwal mwaka 1337 Hijiria. [12] Katika fatwa hii, Muhammad Taqi Shirazi alisisitiza akisema kuwa; Ni wajibu kwa watu Iraq kudai haki zao na, pia ni jukumu lao kuzingatia amani na usalama wa taifa lao katika kudai haki zao. Hata hivyo, aliongeza kuwa, ikiwa Uingereza itakataa kutekeleza matakwa yao, basi ni halali kwao kutumia nguvu ya kujihami na kujilinda kutoka na dhulma hizo. [13]
  • Fatwa Dhidi ya Italia (Wakati wa uvamizi wa Libya): Katika kipindi cha uvamizi wa Italia dhidi ya Libya, Akhund Khorasani, pamoja na Sayyid Ismail Sadr, Sheikh Abdullah Mazandarani na Sheikh al-Shari'a Isfahani, walitoa tamko la Jihadi wakiwahimiza Waislamu kujihami ili kulinda nchi za Kiislamu. [14] Katika tamko lao, walieleza wakisema kuwa; Uvamizi wa Urusi dhidi ya Iran na uvamizi wa Italia dhidi ya Tripoli unaleta madhara makubwa kwa Uislamu, na ni tishio dhidi ya Qur'ani na Sheria. Hivyo ni jukumu la Waislamu wote kujikusanya na kudai haki zao kupitia serikali zao, ili kuondoa uvamizi wa Urusi na Italia. Wala wao hawapaswi kupumzika hadi tishio hili kubwa litapomalizika. Walieleza kwamba hatua hii inapaswa kuchukuliwa kama Jihad katika njia ya Allah, na inapaswa kuonekana ni Jihad kama ilivyokuwa Jihad ya Vita vya Badri na Hunain. [15]
  • Fatwa Dhidi ya Uingereza (Vita vya Kwanza vya Dunia): Katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914–1918), Sayyid Abd al-Hussein Mousawi Lari alitoa maagizo kwa kiongozi wa kabila la Qashqai, aitwaye Sultan al-Dawlah, akisisitiza juu ya umuhimu wa Jihad dhidi ya Uingereza. Katika ujumbe wake, Sayyid Abd al-Hussein alisisitiza kuwa, yeye kama mujtahidi na mrithi wa Mtume wa Uislamu, alihisi kuwa na jukumu la kutoa fat’wa ya Jihad dhidi ya Wazungu, akisema: Mimi, ambaye ni mujtahidi na mrithi wa Mtume wa Uislamu, kwa njia hii natangaza fatwa ya ulazima (wajibu) wa Jihad dhidi ya hawa makafiri (maadui wa kivita), Wazungu. [16]
  • Fatwa Dhidi ya Mawahabi (1217 H): Kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, fatwa ya Sheikh Ja'far Kashif al-Ghita iliyotolewa wakati wa mashambulizi ya Wahhabi dhidi ya Najaf na Karbala mwaka 1217 Hijria (1802 Miladia) ilikuwa na mchango mkubwa katika kuwaondoa Mawahabi kutoka katika maeneo hayo matakatifu. Sheikh Ja'far Kashif al-Ghita, akiwa na wanazuoni 200 na waumini na wajihadi shupavu, aliongoza mapambano dhidi ya Mawahabi na kuwang’oa katika katika maeneo hayo. [17]
Jumbe wa kijihadi na fatwa zilizoandikwa na Muhammad Hassan Rajabi.
  • Fatwa ya Jihad Dhidi ya Israel: Fatwa ya Jihad dhidi ya Israel ilitolewa na wanazuoni kadhaa mashuhuri, akiwemo; Muhammad Hussein Kashif al-Ghita, [18] Sayyid Hussein Borujerdi, [19] na Imamu Khomeini. [20] Wao walitoa fatwa za Jihadi li kuwalinda na kuwatetea watu wa Palestina. Hii ni pamoja na fatwa ya Abdul Karim Zanjani, mmoja wa wanazuoni wa Shia kutoka karne ya 14 Hijria, aliyetangaza fatwa ya Jihad dhidi ya Israel baada ya kuanzishwa kwa dola la Israel na vita vya Israel dhidi ya Waarabu vya mwaka 1948 (1327 Hijria). [21]
  • Fatwa ya Sayyid Ali Sistani (2014 M): Baada ya ISIS kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya magharibi na kaskazini mwa Iraq mnamo mwaka 2014, kisha kuelekea maeneo mengine, Sayyid Ali Sistani alitoa fatwa ya Jihad ili kukabiliana na tishio la kuenea kwa kundi hilo. [22] Fatwa hii ilieleza ikisema kuwa; Ni wajibu kwa raia wa Iraq wenye uwezo wa kubeba silaha kushiriki katika mapigano dhidi ya magaidi wa ISIS, kujiunga na vikosi vya kijeshi, na kujitolea kwa ulinzi wa nchi, taifa, na maeneo matakatifu. Fatwa hii ilikuwa ni Wajib Kifai kwa watu wa Iraq kuungan dhidi ya vitendo vya kigaidi na kulinda ardhi yao na mali zao. [23]

Bibliografia

Kitabu cha Rasa'ili wa Fatawa Jihadiy: Ni kitabu kinachohusisha tasnifu na fatwa za wanazuoni wa Kiislamu kuhusiana na Jihad dhidi ya madola ya Kikoloni. Kitabu hichi kinajumuisha ndani maudhui 95 ya tasnifu na fatwa zilizotolewa na wanazuoni wa Kiislamu kati ya miaka 1200 na 1338 Hijria. Muandishi wa kitabu hichi, (Muhammad Hassan Rajabi), ameziandaa tasnifu hizi katika kitabu chenye muundo wa juzuu moja, ambacho kilichapishwa na Wizarate Farhange wa Irshade  Islamiy(Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu) mwaka 1378 (Shamsi). [24]

Kuna vitabu vingi vilichapishwa kwa jina la Jahadiyya katika kipindi cha utawala wa Qajar ambachi ni kipindi cha vita vya Iran na Urusi. Vitabu ambavyo vilibeba ndani yake fatwa za jihadi na kuelezea umuhimu wa jihad dhidi ya majeshi ya Urusi. Miongoni mwa vitabu hivyo ni; Al-Jihad al-Abbasiya cha Sayyid Muhammad Mujahid na Jami' al-Shatat cha Mirza Qummi, ambavyo ni baadhi ya mifano ya maandiko yaliyoandikwa kuhusiana na wajibu wa kupigana dhidi ya uvamizi wa Urusi. [25]

Maudhui Zinazo Husiana

Rejea

Vyanzo