Jihadi ya Kujihami
Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Jihadi ya kujihami (Kiarabu: الجهاد الدفاعي) maana yake ni kupigana na adui yeyote mwenye nia ya kuangamiza dini ya Kiislamu au mwenye nia ya kuvamia ardhi za Kiislamu. Madhumuni ya jihadi ya kujihami ni kuhifadhi na kulinda Uislamu na pia kuhifadhi maisha, mali na heshima ya Waislamu. Jihadi ya kujihami ni mkabala wa jihadi ya kuanzisha vita ambayo ni Waislamu kuwa ndio waanzishaji wa vita na lengo ni kupanua Uislamu. Baadhi ya Maulamaa wa Kishia wameitambua jihadi ya kujihami kuwa ni bora kuliko jihadi ya kuanzisha vita. Kwa mujibu wa fatwa ya mafakihi ni kwamba, ni wajibu kwa Waislamu wote kutetea na kulinda ardhi iliyovamiwa na kushambuliwa na sharti pekee la hilo ni nguvu na uwezo wa mtu wa kuhami na kusimama kidete mbele ya adui. Kuhusiana na wajibu wa jihadi ya kujihami, kinyume na jihadi ya kuanza kushambulia si sharti la kuweko Imamu Maasumu (as) au naibu wake. Mafakihi wanaamini kuwa, endapo jihadi ya kujihami itasadifiana na wajibu au haramu ya Mwenyezi Mungu kama kusadifiana na ibada ya Hija au kupigana vita katika miezi ya haramu (miezi ambayo kupigana vita ndani yake ni haramu), basi katika hali hii jihadi ya kujihami itatangulizwa mbele ya mambo haya.
Maana na umuhimu wa Jihadi ya Kujihami
Makusudio ya Jihadi ya Kujihami ni kukabiliana na maadui ambao wameshambulia ardhi za Kiislamu. [1] Aina hii ya jihadi lengo lake ni kutetea na kuhami Uislamu [2] na ardhi za Kiislamu. [3] Jihadi ya kujihami ni mkabala wa jihadi ya kuanzisha vita ambayo ni Waislamu kuwa ndio waanzishaji wa vita na lengo kuwalingania Uislamu makafiri na washirikina. [4] Ja’far Kashif al-Ghitaa mmoja wa wanazuoni wa Fiq’h wa karne ya 13 Hijria, ameitambua jihadi ya kujihami kuwa ni bora kuliko jihadi ya Waislamu kuanzisha vita. [5] Akthari ya mafakihi wanaamini kwamba, wanaouawa katika vita vya Jihadi ya Kujihami wanahesabiwa kuwa ni mashahidi sawa na wale wanaouawa katika vita vya Waislamu kuanzisha vita na hukumu za shahidi zinatekelezwa kwao. [6]
Wajibu wa Jihadi ya Kujihami na Masharti Yake
Kwa mujibu wa fatwa ya mafakihi ni kuwa, Jihadi ya Kujihami ni wajibu kifai (wajibu ambao wakifanya baadhi unaowandokea wengine) kwa mtu ambaye ana nguvu za kupigana (mwanaume, mwanamke, mkubwa, mdogo, mzima, mgonjwa, aliye mbali na karibu na mahali panapopiganwa vita). [7] Hivyo basi sharti pekee ni “nguvu na uwezo wa mtu wa kujihami na kusimama kidete”. [8] Wajibu wake kinyume na Jihadi ya Waislamu kuanzisha vita, [9] sio lazima kuweko Imamu Maasumu (as) au idhini ya naibu wake. [10] Hoja na dalili ya kuwa wajibu Jihadi ya Kujihami bali na hoja ya kiakili, [11] ni kuzuia kuangamizwa mataifa ya Kiislamu na kupata ushindi kufru na shirki dhidi ya Uislamu. [12] Sahib al-Jawahir, mmoja wa mafakihi wa Kishia amesema, Jihadi ya Kujihami ni wajibu ambapo ili kuthibitisha hilo ametumia Aya za Qur’ani, hadithi [13] na ijmaa (itifaki ya wanazuoni). [14] [15].
Hukumu
Baadhi ya hukumu za Jihadi ya Kujihami ni:
• Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri baina ya mafakihi ni kwamba, Jihadi ya Kujihami sio wajibu kwa Waislamu tu ambao wamevamiwa na maadui; bali ni jukumu la Waislamu wote kuhami na kutetea ardhi za Kiislamu ambazo zimeshambuliwa na maadui [16] na madhali hawajajitokeza watu kwa kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kuhami ardhi hizo, taklifu hiyo haitamuondokea yeyote. [17] • Endapo jihadi ya kujihami itasadifiana na wajibu zingine za Mwenyezi Mungu kama kusadifiana na ibada ya Hija basi katika hali hii jihadi ya kujihami itatangulizwa. [18] Kadhalika kama jihadi ya kutetea na kuhami ardhi za Kiislamu itasadifiana na mambo ya haramu kama kushirikiana na mtawala dhalimu, [19], vita katika miezi ambayo ndani yake kupigana vita ni haramu [20] au kumuua Muislamu ambaye amefanywa kuwa kinga ya binadamu [21] inajuzu kufanya jambo hili. Kwa maana kwamba, Jihadi ya Kujihami inatangulizwa mbele ya mambo haya.
Aina za Jihadi ya Kujihami
Kwa mtazamno wa Ja’far Kashif al-Ghitaa ni kwamba, Jihadi ina vigawanyo vitano ambapo aina zake nne kati ya hizo tano ni kujihami na aina moja ndio jihadi ya kuanzisha vita. Aina nne ya jihadi ya kujihami ni:
1. Jihadi kwa ajili ya kuhifadhi misingi ya Uislamu mbele ya hujuma na mashambulio ya makafiri dhidi ya ardhi za Waislamu ambayo yanafanyika kwa lengo la kuangamiza na kufuta Uislamu na kisha kuufanya ukafiri na ishara zake kutawala na kuwa na mamlaka.
2. Jihadi kwa ajili ya kukabiliana na wavamizi wa damu na heshima ya Waislamu.
3. Jihadi kwa ajili ya kuwahami Waislamu ambao wanapigana na kundi la makafiri na kuna wasiwasi na hofu ya makafiri kuwashinda Waislamu hao.
4. Jihadi yenye lengo la kuwafukuza makafiri ambao wamekuwa na udhibiti na mamlaka kwa ardhi za Waislamu. [22] Aina hii ya jihadi ni bora kuliko aina zingine. [23]
Tofauti ya Jihadi ya Kujihami na Jihadi ya Kuanzisha Vita
Mafakihi wakiwa na lengo la kuweka wazi mafuhumu, maana na mipaka ya Jihadi ya Kujihami na Jihadi ya Waislamu kuanzisha vita, wametaja mambo yanayotofautiana na jihadi hizi mbili. Miongoni mwazo ni:
• Lengo la Jihadi ya Kujihami ni kuzuia kuangamizwa na kufutwa Uislamu na kuzuia kutokomezwa jamii ya Kiislamu na kulinda mamlaka, roho na heshima ya Waislamu; [24] lakini Jihadi ya Waislamu ya kuanzisha vita hufanyika kwa lengo la kupanua Uislamu na kuongeza wigo wake wa mamlaka na udhibiti. [25]
• Hakuna sharti lolote miongoni mwa masharti yaliyotajwa ya kuwa wajibu jihadi ya Waislamu kuanzisha vita ambalo ni la lazima katika Jihadi ya kujihami na uwezo katika Jihadi ya Kujihami mo jambo lisilotosheleza. [26]
• Jihadi ya Waislamu kuanzisha vita hufanyika kwa ajili tu ya kukabiliana na makafiri; lakini katika Jihadi ya Kujihami hufanyika kwa ajili ya kukabiliana na adui yeyote yule; awe kafiri au Muislamu. [27]
• Katika jihadi ya Waislamu ya kuanzisha vita (kwa ajili ya kuwalingania makafiri ili kupanua Uislamu), haijuzu kwa mtawala wa Kiislamu kufanya mkataba na makafiri Ahlul-Kitab wanaoishi katika ardhi za Waislamu, amani, suluhu na mkataba; lakini katika Jihadi ya Kujihami kama kutajitoleza hofu ya adui kupata nguvu, haijuzu kuhalifu mambo haya na mfano wake. [28]
• Katika Jihadi ya Kujihami, endapo hakutakuwa na bajeti ya kutosha ya Beitul Maal (Hazina ya Dola), inajuzu kwa mtawala wa Kiislamu kuwalazimisha watu kutoa gharama za vita vya kujihami. Kinyume na Jihad al-Ibtida’I (Jihadi ya Waislamu kuanzisha vita) ambapo sharti la kuwa kwake wajibu ambalo limetajwa ni uwezo wa kifedha wa Waislamu. [29]
Monografia
Kitabu cha “Rasail Wafatawa Jihadi” (Risala na Fatwa za Jihadi) kinajumuisha risala na fatwa za Maulamaa wa Kiislamu kuhusu jihadi na madola ya kikoloni. Ni dondoo za anuani 95 za risala (makala na vitabu) na fatwa ambazo zilitolewa na mafakihi kuanzia 1200-1338 Hijria. Majimui hii ilikusanywa na Muhammad Hassan Rajabi katika kitabu kimoja na kusambazwa na Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu ya Iran mwaka 1378 Hijria Shamsia. [30]