Hirizi

Kutoka wikishia

Hirizi au taawidh (Kiarabu: حرز) (kinga) ni Aya, dhikri na dua za kujikinga na mabalaa. Katika vyanzo vya hadithi vya Shia, hirizi za dua zimekuwa zikizingatiwa kutokana na athari zake zilizotajwa. Ayat al-Kursi na Aya ya Wa In Yakad ni miongoni mwa Aya ambazo zina matumizi ya hirizi na kinga. Hirizi ya Imam Jawad (as) na Hirizi ya Yamani ni miongoni mwa hirizi mashuhuri za dua. Katika kitabu cha al-Kafi na Muhaju al-Da’awat kumetengwa mlango maalumu wa kutaja hirizi zilizonukuliwa kutoka kwa Maasumina 14. Kuamini kinga na taathira yake mbali na hilo kuweko katika Uislamu linapatikana pia katika dini na mila zingine. Katika dini ya Uislamu kinga za upotofu zinapigwa marufuku na badala yake kunazungumziwa hirizi na kinga kwa mujibu wa Aya za Qur’ani na dua za Kitawhidi. Kwa mujibu wa baadhi ya mafakihi haijuzu kujikinga na vitu ambavyo havitambuliki.

Maana ya hirizi na aina zake

Hirizi au kinga ni Aya, dhikri na dua ambazo husomwa ili kulinda dhidi ya mabalaa, maadui, wanyama, au jicho baya. [1] [2] Baadhi ya wakati hirizi huandikwa katika kitu na mtu kutembea nayo ikiwa katika mkono au shingo au hutundikwa na kuwekwa katika sehemu fulani katika nyumba. [3] Baadhi ya kinga hazitokani na dua au dhikr bali zinatokana na vitu kama chuma, ngozi ya swala, au majani ya miti fulani. [4] Inasemekana kuwa sababu kuu ya kutumia hirizi ni kuzuia na kujikinga na jicho baya. [5] Kulingana na baadhi ya watafiti, hirizi na taawidh (kinga) hazina tofauti sana na kila moja kati ya maneno haya mawili hutumiwa badala ya jingine. [6] ] Katika baadhi ya vitabu vya hadithi pia hirizi na taawidh vimetajwa katika mlango mmoja na katika orodha moja. [7]Hata hivyo, wengine wanaamini kwamba ingawa mpaka kati ya hirizi na taawidh hauko wazi sana, lakini haiwezekani kuyatambua maneno hayo kuwa yako sawa. [8] Kadhalika imesemekana kuwa kumekuwa na mabadiliko katika maana ya hirizi na katika kipindi fulani ikawa sawa na maana ya taawidh na katika kipindi kingine ilikaribia maana ya uchawi. [9] Tamima, [10] Hikal na Hamail ni miongoni mwa maneno na mafuhumu (maana) zenye uhusiano na Taawidh (kinga) ambayo yana utendaji unaofanana na kushabihiana. [11]

Umuhimu wa hirizi katika mijadala ya Kiislamu

Hirizi za dua ni sehemu ya turathi za dua ambazo daima zimekuwa zikizingatiwa kutokana sifa maalumu na athari zilizotajwa kuzihusu. [12] Neno hirizi halikutajwa katika Quran; lakini limetumika katika riwaya na hadithi nyingi zilizopokewa na Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni. [13] Ayat al-Kursi na Aya ya Wa In Yakad, ni miongoni mwa Aya za Qur’an ambazo zina matumizi ya hirizi na ni kutokana na sababu hiyo zimeondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Ayaat al-Hirz (Aya za Hirizi). [14] Kulayni (aliaga dunia: 329 H) katika kitabu cha al-Kafi [15] na Sayyid bin Tawus (aliaga dunia: 664 H) katika kitabu cha Muhaj al-Da’awat wamekusanya hirizi zilizonukuliwa kutoka kwa Maasumina 14 na kuziweka katika mlango maalumu. [16] Kwa mujibu wa kile kilichonukuliwa na Sheikh Abbas Qumi (aliaga dunia: 1359 H) katika kitabu cha Safinat al-Bihar, Mtume (s.a.w.w) akiwa na lengo la kuwakinga Hassan na Hussein alikuwa akisoma Muawadhatein (kinga mbili) ambazo ni Sura mbili za al-Falaq na al-Nas. [17]. Miongoni mwa hirizi mashuhuri ambazo tunaweza kuziashiria ni hirizi ya Imam Jawad (as), hirizi ya Yamani, Hirz Abudajanah na hirz Yassin [18] Wahakiki wanasema kuwa, kutozingatia hirizi zenye itibari sana na kutokuweko kwa hirizi (kinga) hupelekea kutokea matatizo. Ni kwa muktadha huo ndio maana inaelezwa kwamba, inapaswa kutumia tu hirizi ambazo zimetajwa katika riwaya na hadithi za Maasumina (as) na kujiepusha kutumia hirizi ambazo hazina chimbuko la hadithi. [19] kitabu cha “Hirzihaye Maasumina” yaani ‘Hirizi za Maasumina’ kilichoandikwa na Sayyid Ali Lavasani ni miongoni mwa vitabu ambavyo vimeandikwa kuhusiana na maudhui ya hirizi zilizonukuliwa kutoka kwa Maasumina. [20] Kitabu hiki kilichapishwa na Dar al-Sibtein mwaka 1401 Hijria Shamsia kikiwa na kurasa 488. [21]

Historia yake

Kuamini hirizi na taawidh (kinga) pamoja na athari zake kunazingatiwa kuwa ni miongoni mwa mafundisho yasiyo na shaka ya Uislamu; lakini inaelezwa kuwa si suala mahususi kwa Uislamu bali imani hii ipo pia katika dini zingine [22] na mila na mataifa mengine. [23] Katika hadithi limetajwa suala la kusoma kinga katika dini zingine. [24] Baadhi ya wahakiki wanasema kuwa, dini ya Uislamu imepinga na kukataa kinga za zama za ujahilia zilizokuwa zimechanganyika na upotovu na badala yake ikatengeneza kinga ambazo aghalabu zinajumuisha Aya za Qur’an na dua za kitawhidi.[25]

Itibari ya hirizi kwa mtazamo wa kisheria

Baadhi ya watafiti, baada ya kuchunguza idadi ya hadithi zinazohusiana na hirizi na kinga, wamezingatia baadhi yao kuwa zenye itibari na zingine hazina itibari. [27] Kwa mujibu wa Kashif al-Ghitaa ni kwamba, kujinga na Aya za Qur’an na dhikr ni jambo ambalo limenukuliwa katika hadithi kutoka kwa Maasumina (as) na jambo hili linajuzu; lakini haijuzu kujikinga na vitu visivyofahamika. [28] Hirizi na kinga mbali na kuzungumziwa katika mijadala ya kidini na Kiislamu, zinazungumziwa pia katika ulum ghariba (elimu za ajabu kama uchawi). [29] Baadhi wanasema kuwa, ni haramu kwa mtazamo wa kisheria kutumia kinga na hirizi hizi kutokana na mtazamo wa shirki na mbinu zisizo za kiungu zilizotumika katika hirizi za elimu za ajabu. [30]

Rejea

Vyanzo