Hadithi ya Iftiraq

Kutoka wikishia

Makala hii ni kuhusu hadithi ya kugawanyika makundi (Umma wa Kiislamu). Ili kujua sifa ya dhati (halisi) za Kundi la Waliofuzu na kufuzu, angalia maudhui ya kundi ambalo limeongoka na kuokoka.

Hadithi ya Iftiraq (Kiarabu: حديث الافتراق) na kugawanyika makundi Waislamu, ni hadithi ambayo inanasibishwa na Mtume (s.a.w.w) ambayo inahusiana na kugawanyika Umma wa Kiislamu na kuwa zaidi ya makundi sabini. Kwa mujibu wa hadithi hii, ni kwamba: Baada ya Mtume mtukufu (s.a.w.w), Umma wa Kiislamu utagawanyika na kufikia makundi zaidi ya sabini. Katika makundi hayo sabini ni kundi moja tu ndilo litakalookoka kwa kuwa ni kundi ongofu. Ama kuhusiana na sifa za dhati (halisi) za kundi ongofu, kuna hitilafu baina ya Maulama na wasomi wa madhehebu za Kiislamu. Imepokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ya kwamba: Kundi lililo okoka na ongofu ni Mashia (wafuasi) wa Imam Ali (a.s). Hadithi ya kugawanyika (Waislamu) makundi na masuala yanayohusiana nayo katika maudhui na mjadala wa ya kiakida na itikadi, imeakisiwa na wataalamu wa elimu ya utambuzi wa makundi na mivutano (mifarakano).


Madhumuni na ufafanuzi wa hadithi

Hadithi ya kugawanyika makundi ni hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ambayo inaashiria madhumuni ya pamoja yanayo onekana kutoka katika nukuu tofauti tofauti ya kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema: Majusi waligawanyika makundi sabini, Mayahudi wakagawanyika makundi sabini na moja, na Ukristo ukagawanyika makundi sabini na mbili, na umma wangu utagawanyika makundi sabini na tatu na katika hayo ni kundi moja tu ndilo litakalo okoka (kwani ni ongofu) [1]. Lakini katika mapokezi mengine imekuja kwamba makundi sabini na mbili ni yenye kuokoka kwa uongofu na kundi moja tu ndilo la motoni [2]

Katika mapokezi mbali mbali ya riwaya hii, mara nyingine imetajwa na kuashiriwa kwamba, makundi ya Waislamu ni sabini na tatu [3], mara nyingine imetajwa kuwa ni makundi sabini na mbili [4], mara myingine ikasemwa ni makundi sabini na moja [5] Katika ufafanuzi wa hadithi ya kugawanyika umma wa Kiislamu katika makundi, imetajwa kwamba, makundi mengi ya Kiislamu ni makundi potovu isipokuwa kundi moja tu lenye kuongoka na kuokoka na chimbuko la hilo ni hitilafu za kiitikadi ambazo zinapelekea kukufurishana na kufanyiana uadui wao kwa wao, na hii haihusiani na hitilafu za kifikihi kwa mafakihi ambao wao wote wanarejea katika Qur’an na Sunna, na wao wakawa ni wenye udhuru (wanapofanya kosa katika kuichambua sheria na kutoa fat'wa) [6]. (Yaani wao hawawezi kuwa wakusudiwa wa riwaya kuwa ndio kundi la wenye kuongoka). Kuhusu hadithi, baadhi ya (wasomi) wengine wamesema, kuna uwezekano kwamba; inahusu hitilafu na migawanyiko ya kidunia baina ya Waislamu katika masuala ya kimali, kinafsi na kiutawala hali ambayo itapelekea wao kufanyiana uadui na kugawanyika makundi kwa makundi. [7]

Itibari

Umuhimu na itibari ya hadithi ya kugawanyika makundi, haijanakiliwa wala kupokelewa katika Kutub al-Arba’a (vitabu vinne) vya Kishia vya hadithi wala katika vitabu vya Sahihain (sahihi mbili) vya Kisuni. Wahakiki na watambuzi wa makundi kama Nawbakhti katika kitabu chake kiitwacho firaq Shia, na Abul Hassan Ash’ari katika Maqalat al-Islamiyin hawakuitaja hadithi hii wala kuiashiria. Ibn Hazm Andalusi (aliyefariki dunia 456 H) ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kisuni, ambaye yeye ameitaja na kuizingatia hadithi hii kwamba haiwezi kuwa hoja na sio sahihi [8] na kwa mtazamo wa Ibn Wazir fakihi na msomi wa Madhehebu ya Zaydiyah (aliyefariki dunia 840 H), yeye amekiashiria kipengele cha mwisho cha hadithi hii (makundi yote yataingia motoni ispokuwa kundi moja lenye kuongoka) kwamba ni bandia na ya kutengeneza. [9]

Pamoja na hali hii, lakini baadhi ya vitabu vya hadithi vya Kishia [10] na vya Kisuni [11], na baadhi ya waandishi wa mataifa na kaumu [12] wameinakili hadithi hii na kuikubali. Na baadhi ya watafiti na watambuzi wa makundi kama Abdul Qahir bin Twahir Baghdadi [13] Shahfur bin Twahir Esfraini [14] na ibn Abdu Rahman Mulati Shafi’I [15], wao pia wameyagawanya makundi ya Kiislamu kwa kuzingatia makundi sabini na tatu (yaliyotajwa katika hadith). Hivyo basi kwa sababu hii imesemekana kwamba hadithi ya kugawanyika (Waislamu) makundi sio tu mashuhuri na mustafidh (yaani mpokezi wake ni zaidi ya mtu mmoja lakini haijafikia kiwango cha kuwa mutawatir yaani mapokezi mengi) [16], bali pia ni mutawatir [17] au inakaribia kuwa mutawatir [18].

Kwa mtazamo wa Ayatullah Ja’afa Sobhani kuwa hadithi hii ni mustafidh (yaani mpokezi wake ni zaidi ya mtu mmoja lakini haijafikia kiwango cha kuwa mutawatir yaani mapokezi mengi) na kuwepo mapokezi mengi ya hadithi hii katika vitabu vya Kishia na vya Kisuni, kunafidia udhaifu wa sanadi (mapokezi) yake, na kunakiliwa kwake kwa sanadi mbali mbali katika vyanzo hivi, kunapelekea kuaminika na kutegemewa kwa hadithi hii. [19]

Halikadhalika Muhammad bin Ahmad Muqaddasi (aliyefariki dunia baada ya mwaka 381H) mwandishi wa kitabu kiitwacho Ahsan al-taqaasim fi ma’rifatil- Aqaalim, yeye ameitaja riwaya hii kwamba ni mashuhuri zaidi kuliko riwaya zingine, na kwamba idadi ya makundi yenye kuongoka ni makundi sabini na mbili, na kundi lenye kuangamia ni moja tu. Lakini anaamini kuwa riwaya ya pili ni sahihi zaidi. [20]

Kundi Ongofu

Makala asili: Kundi Ongofu

Ni wazi kwamba baina ya Maulama wa madhehebu mbali mbali kuna hitilafu ya maoni na nadharia kuhusiana misdaq na mfano wa kundi ongofu na lenye kufuzu. Kiasi kwamba kila mmoja wao miongoni mwao anaamini kwamba madhehebu yake ndio kundi ongofu na lenye na kufuzu, na makundi mengine sabini na mbili (ya madhehebu) ya wengine ni yenye kuangamia:[21]

Jamaludin Razi ni katika maulama wa madhehebu ya Imamiya (Shia Ithnaasharia) katika kitabu kiitwacho: Tabswiratul Awami fi ma’rifat Maqalaatil-Anaam [22], Ja’far bin Mansur Al- Yaman miongoni mwa Maulama wa Ismailiyah katika kitabu kiitwacho: Sara’ir wa Asrar al- Nutwaqa [23], na Shahristani miongoni mwa Maulamaa wa madhehebu ya Kisuni katika kitabu kiitwacho: Al-Milal wa Nihal [24] Maulamaa hawa katika vitabu vyao wameandika hali ya kuwa wanaamini na kuitikadi kwamba madhehebu yao ndio (yenye) kilelezo na mfano wa (kundi ongofu na lenye kufaulu.

Shekh Swaduq mpokezi wa hadithi mkubwa na mashuhuri wa Kishia katika karne ya nne, katika kitabu kiitwacho Kamalu al-Din wa Tamam al-Ni’mah akitumia hadithi ya Hadith ya Thaqalain (Vizito Viwili) kama hoja na nyaraka ameitakidi kwamba, kila mtu atakayeshikamana na Qur’an tukufu na kizazi cha Mtume (s.a.w.w) basi atakuwa miongoni mwa kundi ongofu [25]. Halikadhalika Allama Muhammad Baqir Majlisi amenukuu hadithi katika chake cha Bihar al-Anwar iliyopokelewa kutoka kwa Imamu Ali (a.s) akisema kwamba: Mashia wangu ni wenye kuongoka (kufuzu). [26]. Allama Hilli pia akitegemea hadithi mbalimbali amewatambulisha Maimamu kumi na mbili na wafuasi wao kwamba, ni kielelezo na mfano wa wazi wa kundi ongofu. [27] Kisha akabainisha na kutaja hoja za kuthibitisha kuwa madhehebu ya Shia Imamiya ndio yaliyo katika haki. [28]

Pamoja na hayo, wafuasi wa madhehebu ya Sunni wao wakigemea hadithi zingine, wanaamini kwamba, kundi ongofu na lenye kufuzu ni jamaa [29] na mkusanyiko mkubwa, au waliowengi miongoni mwa watu [30] au wafuasi wa Khulafaa Rashidun (kwa mujibu wa Masuni ni viongozi wa awali waliotawala baada ya Mtume). [31] Kadhalika kuna mapokezi kuhusiana na hadithi ya kugawanyika umma wa Kiislamu katika makundi ambapo kwa mujibu wake, makundi yote ya Kiislamu ni (makundi yenye) kuongoka na kufuzu isipokuwa kundi moja tu la wazandiki. [32]

Kundi Lililoangamia

Maulamaa wa madhehebu ya Kiislamu wanaamini kwamba makundi yote sabini na mbili yameangamia isipokuwa madhehebu yao tu: [33] Hata hivyo Ibrahim bin Musa Shatwibi (aliyefariki dunia mwaka 790 H), na ambaye ni miongoni mwa Maulamaa wa madhehebu ya Maliki ambayo ni katika madhehebu ya Kisuni, yeye anaamini kwamba; hakuna hoja ya kiakili na nakili inayozungumzia kundi moja lililoangamia katika idadi ya makundi 72. [34]

Ibn Hazm alimu na mwanazuoni wa Kisuni (aliyefariki dunia mwaka 456 H.) katika kitabu cha fiqhi; Al-Muhalla Bil- A’thar akitegemea hadithi ambayo imepokekelewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) isemayo: {Umma wangu utagawanyika na kuwa makundi sabini na kadhaa, kundi la wengi wao ni fitna juu ya umma wangu, na wao ni kundi linalofanya mambo kwa qiyas (kulinganisha jambo ambalo halikutajwa katika hukumu na jingine lililotajwa kutokana na kuwa na sababu moja)…..}[35], anaamini kwamba: Watu wanaofanya mambo kwa qiyas katika fikihi ni katika makundi yaliyopotea na kuangamia.[36]