Aya ya Nushuz

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Aya za Nushuz)
Makala hii inahusiana na Nushuzu katika Qur’an. Ili kujua maana ya Nushuzu na hukumu zake rejea makala ya Nushuz.

Aya za Nushuz (Kiarabu: آية النشوز) ni sehemu ya Aya ya 34 na 128 za Surat al-Nisaa ambazo zinazungumzia Nushuzu na hukumu zake. Maana ya Nushuz ni ile hali ya mume au mke kukwepa na kutotekeleza majukumu ya kisheria yaliopo juu ya shingo yake. Aya ya 34 inazungumzia mke kukwepa kutekeleza majukumu ya kisheria kama mke kwa mumewe na Aya ya 128 ya Sura hiyo hiyo ya al-Nisaa inazungumzia mume kukwepa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa mkewe. Mbali na Aya hizo, vitabu vya tafsiri na vya fikihi vimejadili na kuzungumzia maudhui hii kwa mapana na marefu.

Mafakihi wakitumia kama hoja Aya ya 34 wanaamini kwamba, endapo mke atakwepa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa mumewe, awali mume anapaswa kumnasihi mkewe huyo na kama hilo halikusaidia ampe mgongo wakati wa kulala kitandani au amhame kitanda na kama hayo pia hayakusaidia amuadhibu kimwili kwa adhabu nyepesi.

Kwa mujibu wa Aya ya 128 pia, endapo mume atakwepa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama mume kwa mkewe, basi mke anaweza kusamehe na kufumbia macho baadhi ya haki zake kwa ajili ya kuleta amani na kumfanya mumewe ampende zaidi.

Andiko la Aya na tarjumi yake

Katika aya za 34 na 128 za Surat al-Nisaa kumezungumziwa suala la Nushuzu (kukwepa mume au mke kutekeleza majukumu yao ya kisheria): Aya ya kwanza ni kuhusiana na mke na Aya ya pili inazungumzia Nushuz ya wanaume.

  • Aya ya 34 ya Surat al-Nisaa:
وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا


Na ambao mnachelea kutoka katika ut´iifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu.



(Qur'an: Surat al-Nisaa: 34)


  • Aya ya 128 ya Surat al-Nisaa:
وَإِنِ امْرَأَةٌ خَافَتْ مِنْ بَعْلِهَا نُشُوزًا أَوْ إِعْرَاضًا فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا أَنْ يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحًا وَالصُّلْحُ خَيْرٌ وَأُحْضِرَتِ الْأَنْفُسُ الشُّحَّ وَإِنْ تُحْسِنُوا وَتَتَّقُوا فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا


Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.



(Qur'an: Surat al-Nisaa: 128)


Sababu ya Kushushwa Kwake

Kila Aya miongoni mwa Aya hizi mbili yaani Aya ya 34 na 128 za Surat al-Nisaa, kumebainishwa sababu za kushukwa kwake.

Sababu ya Kushuka Aya ya 34 ya Surat al-Nisaa

Kwa mujibu wa wafasiri, Aya ya 34 ya Surat al-Nisaa iliteremka kuhusiana na mmoja wa masahaba wa Mtume wa Uislamu, aitwaye Saad bin Rabi', na mkewe.[1] Mke wa Saad aliamuasi mumewe na hivyo Saad akampiga. Kwa sababu hii, alikwenda na baba yake kwa Mtume (s.a.w.w) na kulalamikia kitendo cha Saad. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kulipizwa kisasi, lakini mkewe akajiepusha kulipiza kisasi na Aya hii ikateremka.[2]

Sababu ya Kushusshwa Aya ya 128 ya Surat al-Nisaa

Kwa mujibu wa riwaya iliyosimuliwa katika kitabu cha Tafsir Qomi kuhusiana na kuteremshwa kwa Aya hii, Rafi bin Khadij, mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w), alikuwa na wake wawili, mmoja wao alikuwa mzee na mwingine alikuwa kijana. Kutokana na kutofautiana, alimpa talaka mke wake mkubwa kiumri na wakati wa kipindi cha eda alimwambia ukitaka, nitarudiana na wewe, kwa sharti kwamba ikiwa nitamtanguliza mke wangu mwingine mbele yako usipinge hilo. Ukipenda pia nitasubiri hadi eda iishe ili tutengane. Mwanamke huyo alikubali pendekezo la kwanza na wakapatana. Kisha Aya hii ikateremka.[3]

Matumizi ya Kifikihi

Kadhalika angalia: Nushuzu

Mafakihi wanatumia maudhui iliyoko katika Aya za 34 na 128 za Surat al-Nisaa kubainisha hukumu za kukwepa mume au mke majukumu yake ya kisheria.[4] Nushuz maana yake ni uasi na kukwepa mume au mke majukumu yake ya kisheria.[5]

Aya ya 34 inazungumzia kukwepa mke majukumu ya kisheria na majukumu ya mume. Kwa mujibu wa Aya hii, mafakihi wametoa fat’wa wakisema kwamba, kama mke atakwepa majukumu yake ya kisheria na kutoyatekeleza, katika hatua ya awali inapasa kumnasihi. Kama hilo halikusaidia ampe mgongo wakati wa kulala kitandani au amhame kitanda na kama hayo pia hayakusaidia amuadhibu kimwili kwa adhabu nyepesi.[6]

Imeelezwa kwamba mume anaweza kumuadhibu mke kimwili ikiwa tu anaogopa kuabudu matamanio kwa mke wake baada ya kumnasihi na kujitenga naye kitandani, na hukumu hii si wajibu na mume anaweza kufumbia macho hilo na kumtaliki mke katika tukio lolote la haramu.[7]

Aya ya 128 imazungumzia suala la wanaume kukwepa majukumu yao ya kisheria. Mafakihi wakitegemea Aya hii wamesema kuwa, endapo mke ataona alama za kutotekeleza majukumu ya kisheria kutoka kwa mumewe basi mke anaweza kusamehe na kufumbia macho baadhi ya haki zake kwa ajili ya kuleta amani na kumfanya mumewe ampende zaidi na kwa njia hiyo kuzuia talaka.[8]

Maana ya Neno Dharb

Makala kuu: Kumuadhibu Mwanamke Kimwili

Kwa mujibu wa mtazamo wa wafasiri na mafakihi (wanazuoni wa elimu ya fikihi) wa Kishia na Ahlu-Sunna, neno "Dharb" lililokuja katika Aya ya 34 ya Surat al-Nisaa lina maana ya kupiga.[9] Hata hivyo kupiga huku kumeainishiwa mipaka; kama vile kupiga huku kuwe ni kwa ajili ya kurekebisha na kutokuuwa na aina yoyote ile ya kulipiza kisasi[10] na upigaji wenyewe uwe hafifu na mwepesi.[11] Pamoja na hayo, Ayatullah Marifat, mtafiti wa masuala ya Qur'ani wa zama hizi anaamini kuwa Aya hii imefutwa akitaja ushahidi kama vile adhabu ya viboko kwa wanawake kwa fimbo za mswaki na kuharamishwa kuwapiga wanawake na kuagizwa kulinda heshima yao. [12] Kwa mtazamo wake ni kuwa, katika Aya hii kumetumika mtindo wa kufuta kwa utangulizi.[13] Katika mtindo huu, mtungaji sheria akiwa na lengo la kuondoa na kung'oa mizizi ya baadhi ya ada za kiijahilia, awali anajuzisha hukumu ambayo inaendana na jamii na kisha huifuta hatua kwa hatua.[14]

Rejea

  1. Tabrisi, Majma' al-Bayan, juz. 3, uk. 68. 1408 H.
  2. Sheikh Tusi, at-Tibyan, juz. 3, uk. 189; Tabrisi, Majma' al-Bayan, juz. 3, uk. 68. 14108 H.
  3. Qummi, Tafsīr Qummī, juz. 1, uk. 154. 1404 H.
  4. Tazama: Muhaqiqi Ardabili, Zubdah al-Bayan, uk. 536-538. Najafi, Jawahir al-Kalam, juz. 31, uk. 205-208, 1362 S. Saduq, Man La Yahdhuruh al-Faqih, juz. 3, uk. 520-521, 1413 H. Shahid Thani, Masalik al-Afham, juz. 8, uk. 355-363, 1413 H.
  5. Shahid Thani, ar-Raudhah al-Bahiyyah, juz. 5, uk. 427, 1386 H. Muhaqiqi Hilli, Mukhtasar an-Nafi', uk. 191, 1410 H.
  6. Tazama: Najafi, Jawahir al-Kalam, juz. 31, uk. 205-207, 1362 S. Shahid Thani, Masalik al-Afham, juz. 8, uk. 356-357, 1413 H.
  7. Nasari «Tahqiqi Darboreye Ma'anaye Dharaba dar Ayat Nushuz», uk 40
  8. Tazama: Najafi, Jawahir al-Kalam, juz. 31, uk. 207-208, 1362 S. Shahid Thani, Masalik al-Afham, juz. 8, uk. 363, 1413 H.
  9. Tazama: Tabrasi, Majma' al-Bayan, juz. 2, uk. 69, 1372 S. Abul Futuh Razi, Raudh al-Jinan, juz. 5, uk. 350, 1408 H. Tabataba'i, al-Mizan, juz. 4, uk. 345, 1390 H. Makarim Shirazi, Tafsir Nemune, juz. 3, uk. 372, 1371 S. Fakhrurrazi, Tafsir al-Kabir, juz. 10, uk. 72, 1420 H. Saduq, Man La Yahdhuruh al-Faqih, juz. 3, uk. 521, 1413 H. Shahid Thani, Masalik al-Afham, juz. 8, uk. 356, 1413 H.
  10. Najafi, Jawahir al-Kalam, juz. 31, uk. 207, 1362 S. Khansari, Jami' al-Madarik, juz. 4, uk. 437; Imam Khomeini, Tahrir al-Wasilah, juz. 2, uk. 273, 1390 H.
  11. Makarim Shirazi, Ahkam Khanewade, uk. 219, 1389 S.
  12. Ma'rifah, Shubhat Wa Rudud Haul al-Qur'an al-Karim, uk. 158, 1388 S.
  13. Ma'rifah, Shubhat Wa Rudud Haul al-Qur'an al-Karim, uk. 158, 1388 S.
  14. Ahamdi Nejad, Va Digeran, «Ma'na Shenasi Naskh Tadriji. Mashrut Wa Tamhidi Az Manzar Ayatullah Ma'refat», uk. 18.

Vyanzo

  • Abul Futuh Razi, Husain bin Ali. Raudh al-Jinan Wa Ruh al-Jinan Fi Tafsir al-Qur'an. Tehran: Bunyad Pajuhesh haye Islami, 1408 H.
  • Ahmadi Nejad, Fateme & Digaran. «Ma'na Shenasi Naskh Tadriji. Mashrut Wa Tamhidi Az Manzar Ayatullah Ma'refat». Tahqiqat Ulum Qur'an Wa Hadith. juz: 1, Bahar, 1397 S.
  • Imam Khomeini, Sayyid Ruhullah, Tahrir al-Wasilah. Najaf: Matba'at al-Adab. juz. 2, 1390 H.
  • Ansari, Muhammad Baaqir, «Tahqiqi darbareye ma'anaye dharaba dar Ayat Nushuz» Tarjaman Wahyi, juz. 26, 1388 S.
  • Khansari, Sayyid Ahmad. Jami' al-Madarik. Tehran: Maktab al-Saduq, 1405 H.
  • Shahid Thani, Zainuddin bin Ali. Masalik al-Afham. Qom: Muasese al-Ma'arif al-Islamiyyah, 1413 H.
  • Sheikh Saduq, Muhammad bin Ali. Man La Yahdhuruh al-Faqih. Qom: Entesharat Islami, 1413 H.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin Hassan. At-Tibyan Fi Tafsir al-Qur'an. Beirut: Dar at-Turath al-'Arabi. Bita.
  • Tabataba'i, Sayyid Muhammad Hussain. Al-Mizan Fi Tafsir al-Qur'ān. Beirut: Muasese al-A'lami Li al-Matbu'at, 1390 H.
  • Tabrasi, Fadhl Bin Hassan. Majma' al-Bayan Fi Tafsir al-Qur'an. Beirut: Dar al-Ma'rifah, 1408 H.
  • Fakhrurrazi, Muhammad bin Umar. Tafsir al-Kabir. Beirut: Dar Ihya' at-Turath al-'Arabi, 1420 H.
  • Qummi, Ali bin Ibrahim. Tafsir Qummi. Qom: Dar al-Kitab, 1404 H.
  • Muhaqqiq Ardabili, Ahmad bin Muhammad. Zubdah al-Bayan Fi Ahkam al-Qur'an. Tehran: Al-Maktab al-Murtadhawiyah Li Ihya' al-Athar al-Ja'fariyyah, Bita.
  • Ma'rifah, Muhammad Hadi. Shubhat Wa Rudud Haul al-Qur'an al-Karim. Muasese at-Tamhid, 1388 S.
  • Makarim Shirazi, Nashir. Tafsir Nemune. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiyyah, 1374 S.
  • Makarim Shirazi, Nashir. Ahkam Khanewade. Qom: Imam Ali bin Abi Thalib (as). juz. 2, 1389 S.
  • Najafi, Muhammad Hassan. Jawahir al-Kalam. Qom: Muasese Nashr Islami, 1417 H.