Alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s)

Kutoka wikishia

Alama au ishara za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) (Kiarabu: علامات الظهور) ni matukio ambayo yatatokea wakati wa kukaribia kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). Alama za kudhihiri Imamu Mahdi zinagawanyika mara mbili. Kuna ambazo kutokea kwake kuna uhakika na hakuna shaka kwa maana kwamba, zitatokea mia kwa mia na kuna ambazo kutokea kwake hakuna uhakika mia kwa mia. Alama na ishara ambazo kutokea kwake hakuna shaka ni matukio ambayo bila shaka yatatokewa kabla ya kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). Tukio la ngurumo au sauti kali kutoka mbinguni, Khasf Bayda' (kumezwa eneo la Bayda'), Harakati za al-Yamani, kuuawa nafsi takasifu (nafs Zakiyyah) na kutokea Sufyani ni mambo ambayo yametajwa kuwa ni katika alama za wazi kabisa na zisizo na shaka ambazo zitatokea kabla kudhihiri Imam Mahdi mtarajiwa (a.t.f.s). Ama ishara na alama ambazo kutokea kwake hakuna uhakika mia kwa mia ni matukio ambayo hata bila ya kutokea kwake, kuna uwezekano wa kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). Katika baadhi ya vyanzo vya hadithi alama na ishara za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) zimechanganyika na alama za kutokea Kiyama.

Baadhi ya wasomi wametambua baadhi ya ishara na alama za kudhihiri Imamu Mahdi kama Sufyani na Dajjal kuwa ni ishara maalumu na nembo. Kwa mfano wanatambua kuwa, Dajjal ni nembo ya kukengeuka na kuacha Uislamu na Sufyani ni nembo ya kukengeuka na kuwa na upotofu katika jamii ya Kiislamu.

Utambuzi wa maana

Alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) ni yale matukio ambayo kutokea kwake yanaashiria kukaribia kudhihiri mwokozi wa ulimwengu Imamu Mahdi (a.t.f.s). Inaelezwa kuwa, kupitia matukio haya ambapo Imamu Mhadi atafahamika kunako wale wanaodai Umahdi. [1]

Wakati na jinsi ya kutokea

Kwa mujibu wa hadithi, kuna baadhi ya alama na ishara ambazo zitatokea kabla ya kudhihiri Imamu Mahdi na kuunganika na kudhihiri kwake na mengine yatatokea katika kipindi chote cha Ghaiba Kubwa (Ghaibat al-Kubra). [2] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Kamal al-Din cha Sheikh Saduq ni kuwa, ngurumo au sauti kali kutoka mbinguni, Khasf Bayda' (kumezwa eneo la Bayda'), Harakati za al-Yamani, kuuawa nafsi takasifu (nafs Zakiyyah) na Kutoka Sufyani ni matukio ambayo yatatokea kabla ya kudhihiri Imamu Mahdi na kuungana na kudhihiri kwake. [3] Sheikh Mufid ameyataja matukio hayo kama alama za mapinduzi au harakati ya Imamu Mahdi. [4] Kwa msingi huo, alama na ishara hizi zimetajwa pia kwa jina la ishara za mapinduzi na harakati ya Imamu Mahdi (a.t.f.s). [5]

Baadhi ya ishara zitatokea katika hali ya kawaida huku matukio mengine kama ngurumo na sauti kali kutoka mbinguni haiwezekani kutokea katika hali ya kawaida bali yatatokea kimuujiza. [6]

Ishara za uhakika na zisizo za uhakika

Ishala na alama za kudhihiri Mahdi zinagawanyika mara mbili. Kuna ambazo kutokea kwake kuna uhakika na zingine kutokea kwake hakuna uhakika mia kwa mia; [7] ishara ambazo ni za uhakia ni zile ambazo kutokea kwake hakuna shaka na madhali matukio hayo hayajatokea, basi Imamu Mahdi hatodhihiri. Ama alama na ishara ambazo sio za uhakika ni yake matukio ambayo kutokea kwake sio jambo lenye uhakika wa mia kwa mia kwa maana kwamba, hilo halijathibiti mia kwa miaka na inawezekana Imamu Mahdi akadhihiri bila ya kutokea alama na ishara hizo. [8]

Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa na Sheikh Saduq ni kwamba, ngurumo au sauti kali kutoka mbinguni, Khasf Bayda' (kumezwa eneo la Bayda'), Harakati za al-Yamani, kuuawa nafsi takasifu (nafs Zakiyyah) na kutokea Sufyani ni matukio ambayo yatatokea kabla ya kudhihiri Imamu Mahdi na ni katika ishara zisizo na shaka za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). [9] Sheikh Mufid katika kitabu chake cha Irshad ameorodhesha alama za kudhihiri Imamu Mahdi na baadhi yake ni: kupatwa kwa jua, kupatwa kwa mwezi, vifo, vita, machafuko makubwa, bendera nyeusi kutoka mashariki na mvua mtawalia. [10] Baadhi wakitumia ibara ya “Wallah A’lam” (Mola ndiye mjuzi zaidi) iliyotumiwa na Sheikh Mufid mwishoni mwa orodha tajwa [11] wamesema kuwa, Sheikh Mufid alikuwa na shaka kuhusiana na baadhi ya alama hizi. [12]

Imetajwa katika baadhi ya vyanzo kwamba, baadhi ya alama na ishara zisizo za uhakika za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) ni:

 • Hitilafu baina ya Bani Abbas katika uongozi wa dunia na kusambaratika utawala huo.
 • Kuuawa mfalme wa mwisho wa Bani Abbas kwa jina la Abdallah.
 • Kupatwa kwa jua katikati ya mwezi wa Ramadhani, kinyume na ada.
 • Kutoka mtu kutoka Qazvin ambaye jina lake linafanana na jina la mmoja wa Mitume na atafanya dhulma nyingi dhidi ya watu.
 • Kuzama sehemuya magharibi ya Masjid Dimashq.
 • Kuzama moja ya viji vya Sham.
 • Kusambaratika Basra.
 • Kuuawa mtu aliyeanzisha uasi dhidi ya Sufyani nyuma ya Kufa pamoja na masahaba zake 70.
 • Kubomoka ukuta wa Masjid Kufa.
 • Kutundikwa bendera nyeusi na Khorasani. Jeshi hili litapigana na jeshi la Sufyani katika eneo moja jirani na Shiraz na litapata kipigo cha kwanza. Bendera hizi hazitateremka mpaka watakapofika Baytul-Muqaddas.
 • Kuchomoza nyota ang’avu upande wa mashariki ambayo itakuwa iking’ara kama mwezi; kisha pande zake mbili zitainama kwa namna ambayo zitakaribia kukutana.
 • Kujitokeza wekundu mbinguni ambao utatanda sehemu zote.
 • Uharibifu mkubwa Sham na Iraq.
 • Vuta nikuvute baina ya makundi matatu huko Sham (As’hab, Ablaq na Sufyani).
 • Kujaa maji ya Mto Furati kiasi kwamba, yatamiminika katika mitaa ya mji wa Kufa.
 • Kutokea watu 12 kutoka katika ukoo wa Abu Talib ambao wote watakuwa wakiwalingania viumbe kuwatii.
 • Kujitokeza upepo mweusi huko Baghdad mwanzo wa siku.
 • Kupungua nafaka na bidhaa za majani na kutokea ukame.
 • Hitilafu na mzozo baina ya makundi mawili yasiyo ya Waarabu na kutokea mapigano na umwagaji damu mkubwa baina yao.
 • Kuharabika mji wa Rey.
 • Vita baina ya vijana wa Kiarmenia na Azerbaijan.
 • Kubadilishwa kundi la waleta bidaa na uzushi na kuwa katika sura ya nyani na nguruwe.
 • Mwito usio wa kawaida kutoka mbinguni kwa ajili ya walimwengu wote na kila mtu atausikia kwa lugha yake.
 • Kiujumla kutasikika sauti tano kutoka mbinguni ambapo sauti ya nne tu (ambayo itatokea na kusikia katika mwezi wa Ramadhani) ndio ambayo kutokea kwake hakuna shaka. Sauti tatu za mwanzo zitatokea katika mwezi wa Rajab na zitakuwa kwa namna hii:
 • Mwito wa kwanza: ((ألا لعنة الله علی القوم الظالمین ; Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu))
 • Mwito wa Pili: ((یا معاشرالمؤمنین أزفة الآزفة ; Enyi kundi la waumini! Kiyama kimekaribia)).
 • Mwito wa tatu: (utaambatana na mwili wa dhahiri na unaoonekana): ((ألا إن الله بعث مهدی آل محمد للقضاء علی‌الظالمین ; Tambueni kwamba, hakika Mwenyezi Mungu amemtuma Mahdi kutoka katika kizazi cha Mtume (s.a.w.w) ili atoe hukumu kwa madhalimu)).
 • Sauti ya nne ambayo itasikika katika mwezi wa Ramadhani (kuna uwezekano usiku wa Ramadhani 23) na ambayo itatoka kwa Jibril, itatoa ushahidi wa kuwaunga mkono Ahlul-Bayt (a.s).
 • Sauti ya tano ambayo itatoka kwa shetani (kuna uwezekano ikawa ni magharibi ya Ramadhani 23) itakuwa ikionyesha ufuasi kwa Sufyani.
 • Wafu watatoka makaburi wakiwa hai na kurejea duniani na watajishughulisha na kutembeleana. [13]

Kuchanganyika na alama za Kiyama

Katika baadhi ya vyanzo vya hadithi, alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) zimechanganyika na alama za kutokea Kiyama. Kwa mfano, kuchomoza jua kutoka Magharibi ambako kumetajwa katika hadthi kwamba, ni katika alama na ishara za Kiyama [14] katika baadhi ya vyanzo tukio hilo linatajwa kuwa ni katika alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). [15]

Kadhalika kumetajwa baadhi ya ishara na alama za kudhiiri Imamu Mahdi kama kutoka Sufyani kando ya alama za Kiyama kama mnyama katika ardhi, kurejea Nabii Issa, harakati ya Imamu Mahdi na kuchomoza jua kutoka magharibi. [16] Imeelezwa kwamba, kwa kuwa katika vyanzo vya dini, harakati ya Imamu Mahdi imehesabiwa kuwa ni katika ishara na alama za Kiyama, [17] kuna baadhi ya alama za kudhihiri Imamu Mahdi zinahesabiwa kuwa ni katika ishara za kutokea Kiyama. [18]

Alama za kudhihiri Imamu Mahdi ni halisi au nembo?

Sayyid Muhammad Sadr (1943-1999), mmoja wa Marajii Taqlid anasema katika kitabu chake cha Tarikh al-Ghaibat al-Kubra kwamba, baadhi ya ishara za kudhihiri Imamu Mahdi kama Sufyani na Dajjal kuwa ni ishara maalumu na nembo. Anaamini kwamba, Dajjal ni nembo ya kukengeuka na kuacha Uislamu na Sufyani ni nembo ya kukengeuka na kuwa na upotofu katika jamii ya Kiislamu. [19] Katika kumjibu mwanazuoni huyo imeelezwa kuwa, kuzitambua alama za kudhihiri Imamu Mahdi kuwa ni nembo naishara maalumu ni kinyume na dhahiri ya hadithi. Kadhalika hilo linapelekea kufutwa utendaji wa alama za kudhihiri Imamu Mahdi; [20] kwani utendaji wa alama za kudhihiri Imamu Mahdi zinasaidia kumtambua Imamu Mahdi (a.t.f.s) kunako waongo wanaodai Umahdi. [21]

Ishara za kudhihiri mwokozi katika dini zingine

Katika Uyahudi na Ukristo kumebainishwa ishara na alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) ambapo baadhi yake zinashirikiana na ishara za kudhihiri Imamu Mahdi katika hadithi za Kiislamu. Mayahudi wanaamini kuwa, kuenea ufisadi, vita na machafuko ni miongoni mwa ishara za kudhihiri Masih. [22]

Kadhalika kwa mujibu wa itikadi ya Wakristo aliye dhidi ya Masih au Dajjal ni mtu au watu ambao wanakana na kukadhibisha kwamba, Issa ndiye Masih. [23] Dajjal ataanzisha harakati mwishoni mwa zama (Akher Zaman) na wakati Masih atakapodhihiri atamsambaratisha. [24] Kuenea ufisadi, vita, machafuko, vurugu, zilzala, maradhi, ukame na kutokea ishara katika jua, mwezi na nyota ni katika ishara na alama zingine ambazo kwa mujibu wa imani ya Wakristo zitatokea kabla ya kurejea Masih Issa bin Maryam. [25]

Kuoanisha alama za kudhihiri Imamu Mahdi kwa watu wasiokuwa Imamu Mahdi

Katika zama mbalimbali kulioanishwa na kutabikishwa na watu au na matukio ishara za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). Utabikishaji au uoanishaji ulifanywa na watu au tawala kwa malengo tofauti. Kwa mfano, kuchomoza jua kutoka magharibi kulitabikishwa na kuanzishwa utawala wa Fatimiya nchini Misri na Nafs Zakiyyah kwa Muhammad bin Abdallah bin Hassan Muthanna. [26]

Bibliografia

Chanzo cha dalili za kudhihiri ni hadithi ambazo zimenukuliwa katika vyanzo vya hadithi za Shia na Sunni. Hata hivyo baadhi, wametilia shaka itibari yake na wakasema kwamba baadhi ya hadithi hizi hazikutoka kwa Maasumu. [27] Katika vitabu vya al-Ghaibah cha Nu’mani, [28] Kamal al-Din cha Sheikh Saduq, [29] al-Ghabah cha Sheikh Tusi [30] na al-Irshad cha Sheikh Mufid [31] vimetenga sehemu maalumu na kuzunguzia hadithi za alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). Katika vyanzo vya Ahlu Sunna kuna sehemu zinazofahamika kwa jina la Malahim wa fitan ambapo maudhui hii imezungumziwa. Kadhalika kumeandikwa vitabu kwa jina hili kama al-Malahim wal-Fitan cha Ibn Hammad. [32]

Kuhusiana na ishara za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) kumeandikwa vitabu vya kujitegemea. Baadhi ya vitabu hivyo vimejihusisha na kukusanya hadithi tu zinazohusiana na maudhui hii na vingine vimetoa tathmini na uchambuzi wa mada hii. Miongoni mwavyo ni:

 • Dirasatun fi alaim al-Dhuhur, mwandishi Ja’far Murtadha al-Amili. [33]
 • Nawaib al-Duhur fi Alaim al-Dhuhur, mwandishi: Muhammad Hassan Mirjahani.
 • Ma’tam wa Khamsun Alamah; mwandishi Muhammad Ali tabatabai. [34]
 • Ta’mull dar Nishanehaye hatmi zuhur; mwandishi Nasrullah Ayaati. [35]

Kadhalika na vitabu vingine kama Iqd al-Durar fi Akhbar al-Muntadharm, al-Urf al-Ward fi akhbar al-Mahdi na Al-Burhan fi alaamat Mahdi Akher al-Zaman ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na waandishi wa Kisunni kuhusiana na alama na ishara za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s).