Al-Ajal

Kutoka wikishia

Al-Ajal (Kiarabu: الأَجَل) ni mwisho wa kila kitu na ina maana ya wakati wa kifo cha mwanadamu. Neno al-Ajal na yanayotokana nalo limetumika mara 56 katika Qur’an katika maudhui mbalimbali. Kwa mfano imekuja kuwa, kila umma una muda wake maalumu ambao haupungui wala kuongezeka.

Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani tukufu wanaamini kwamba, kwa mujibu wa Aya za Qur’an mwanadamu ana aina mbili za ajal (muda wa kifo chake): Al-Ajal al-Musamma ambayo ina maana ya mwisho maalumu na usio na shaka wa kitu fulani yaani muda wa kufa kwake ambao haubadilika na kutokea kwake hakuna shaka. Kwa maana kwamba, kutokea kwake ni lazima. Na Kuna Ajal Mu'allaq ambayo huambiwa mwisho wa kitu ambacho yumkini muda wake ukapungua au kuongezeka. Kwa maana kwamba, muda wake wa kifo chake unaweza kubadilika kutokana na sababu mbalimbali.

Uambuzi wa maana na nafasi yake

Kipindi fulani cha kitu au mwisho wa kipindi cha kila kitu kinajulikana kwa jina la Ajal: [1] neno hili kuhusiana na mwanadamu lina maana ya mwisho wa kipindi chake cha kuishi yaani kifo chake. [2]

Neno al-Ajal na yanayotokana nalo limetumika mara 56 katika Qur’an katika maudhui mbalimbali [3] ambapo miongoni mwazo ni:

  • Kuumbwa kwa mbingu na ardhi kuna muda maalumu (Musamma) na maisha yake yatakwisha baada ya muda maalumu. [4]
  • Mzunguko wa jua na mwezi ni wa kipindi maalumu. [5]
  • Mwenyezi Mungu anaahirisha adhabu ya dhambi hadi wakati fulani, ambao ni wakati wa kufa au ufufuo. [6]
  • Mimba na mtoto ndani ya tumbo la mama ana muda fulani wa maisha. [7]
  • Kila umma una muda wake maalumu ambao haupungui wala kuongezeka. [8]
  • Mwenyezi Mungu amemuwekea kila mwanadamu umri maalumu na kipindi maalumu cha kuishi. [9]

Migawanyiko ya Ajal

Kadhalika angalia: Al-Ajal al-Musamma na Ajal Mu'allaq

Baadhi ya wafasiri wakitegemea Aya ya pili ya Surat al-An’am inayosema: ((هُوَ الَّذِى خَلَقَكُم مِّن طِينٍ ثُمَّ قَضىَ أَجَلًا وَ أَجَلٌ مُّسَمًّى عِندَهُ ; Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha akakuhukumieni ajali, na muda maalumu uko kwake tu)), wanasema kuwa, mwanadamu ana Ajal (muda maalumu) mbili Ajal Musamma na ajal Mu’allaq. [10] Al-Ajal al-Musamma ina maana ya mwisho maalumu na usio na shaka wa kitu fulani. Kwa maana kwamba, kutokea kwake ni lazima na ni Mwenyezi Mungu tu ndiye ajuaye hilo. Al-ajal al-Mu'allaq ni kipindi cha kifo cha kila mtu kulingana na hali yake ya mwili ambapo kutokana na sababu za nje yumkini kifo chake kikatokea haraka au kwa kuchelewa. [11]

Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai akibainisha na kufafanua ajal hizi mbili ameandika: Ajal Mu'allaq ni kipindi cha kifo cha kila mtu kulingana na hali yake ya mwili ambapo kutokana na sababu za nje yumkini kifo chake kikatokea haraka au kwa kuchelewa. Anaamini kwamba, kipindi cha kuaga dunia mtu ni kwa mujibu wa hali yake ya mwili (afya ya mwili) ambapo yumkini kwa kuzingatia sababu za nje, umri wake ukapungua au kuongezeka. Yaani kwa mujibu wa hali ya mtu ya mwili wake, mtu anaweza kuishi kwa mfano miaka 100, hivyo Ajal Mu'allaq yake (wakati wa kifo chake) ni miaka 100; lakini mtu huyu huyu kutokana na sababu za nje inawezekana kifo chake kikawa haraka au kikachelewa na hii ni Ajal Musamma yake. [12]