Kuwa na wivu (Kiarabu: الغِيْرَة) ni katika wasifu na sifa za kimaadili ambazo humfanya na kumsukuma mtu mwenye nazo kutetea heshima, hadhi, familia, dini, imani, itikadi na vilevile mali na nchi yake. Kwa mujibu wa hadithi na riwaya mbalimbali, kuwa hali na tabia ya ghera na wivu wa mahali pake ni katika sifa za Mwenyezi Mungu.

Hadithi ya kiakhlaq

Mulla Ahmad Naraqi amesema katika kitabu chake cha Mi’raj al-Saadah kwamba: Waumini hawapasi kughafilika na familia zao na haipasi kufumbia macho na kufanya uzembe katika jambo ambalo hatima yake ni ufisadi. Yeye anaamini kuwa, kufanyia kazi suala la kuamrisha mema na kukataza maovu sambamba na kukabiliana na bidaa na uzushi katika dini ni katika vielelezo na mifano ya kuwa na ghera.

Katika hadithi zilizopokewa na Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kwamba, usafi na utakaso ni nguzo na uthabiti wa familia na zuio la ufisadi na hayo yametajwa kuwa ni katika athari na faida za kuwa na ghera. Wakati huo huo, kuchanganyika maharimu na wasiokuwa maharimu, muziki wa haramu, kumuangalia asiyekuwa maharimu na kunywa vileo ni katika sababu zilizotajwa ambazo zinapelekea kupatikana hali ya ukosefu wa ghera na wivu.

Kwa mujibu wa hadithi iliyopekewa kutoka kwa Imam Ali (a.s) ni kuwa, kufurutu ada (kuchupa mipaka) katika ghera kunaweza kuleta natija kinyume chake na kupelekea ufisadi. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maan Imam Ali akatahadharisha juu ya suala la kufanya na kuonyesha ghera mahali ambapo si pake.


Utambuzi wa maana

Ghera katika utamaduni wa Kiislamu inahesabiwa kuwa fadhila moja muhimu ya kiakhaqi na kimaadili [1] ambayo humsukuma mwenye nayo kutetetea heshima, hadhi, familia, dini, imani, itikadi na vilevile mali na nchi yake. [2]

Neno ghera halijaja katika kitabu kitakatifu cha Qur’an kwa sura ya moja kwa moja, lakini Sheikh Nassir Makarim Shirazi mmoja wa Marajii Taqlid wa Kishia na mfasiri wa Qur’an tukufu anasema kuwa, Aya ya 60-62 za Surat al-Ahzab zinabainisha mafuhumu na maana ya ghera ambapo ndani yake wanafiki, wenye maradhi ya nyoyo na waeneza fitna kuhusiana na wanawake watakasifu na wenye kujiheshimu wanatishiwa kupatiwa adhabu kali, kubaidishwa na kuuawa. [3]

Kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa na Waislamu wa Kishia, kuwa na ghera ni katika sifa za Mwenyezi Mungu na Mola muumba hapendi hali ya kutokuwa na ghera. [4] Ghera katika hadithi tajwa imekuja pamoja na izza, heshima na utukufu. [5] kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, wanaume wasio na ghera wamelaaniwa. [6]

Aina na vielelezo

Mulla Ahmad Naraqi fakihi wa karne ya 13 Hijria, mbali na kubainisha katika kitabu chake cha Mi’raj al-Saadah juu ghera kuhusiana na wanawake, ameelezea pia ghera kuhusiana na dini, heshima na mali. Naraqi anaamini kwamba, waumini hawapasi kughafilika na familia zao na haipasi kufumbia macho na kufanya uzembe katika jambo ambalo hatima yake ni ufisadi. [7] Yeye anaamini kuwa, kufanyia kazi suala la kuamrisha mema na kukataza maovu sambamba na kukabiliana na bidaa na uzushi katika dini, ni katika vielelezo na mifano ya kuwa na ghera. [8]

Hussein al-Madhahiri mmoja wa Marajii Taqlidi wa Kishia mbali na kubainisha ghera ya mtu binafsi, akitegemea hadithi amebainisha aina zingine za ghera; miongoni mwazo ni ghera ya umma na ya kijamii kwa maana ya wanaume wa jamii kuwa na ghera na wanawake wote, [9] kuwa na ghera na nchi na ardhi maana yake ni mtu kupenda nchi yake na kufanya juhudi za kupatikana ustawi na maendeleo. [10] Ama ghera ya dini maana yake ni kutetea Uislamu. [11]

Katika hadithi kumetajwa sababu zinazopelekea kutokuwa na ghera; miongoni mwazo ni: Kuchanganyika maharimu na wasiokuwa maharimu, [12] muziki wa haramu, [13] kumuangalia asiyekuwa maharimu, [14] kunywa kileo [15] na kula nyama ya nguruwe. [16]

Athari za ghera

Kumetajwa athari na faida za ghera kwa kutegemea hadithi za Maasumu; miongoni mwazo ni:

  • Utakaso na usafi: Inaelezwa kuwa, kama mtu atakuwa na ghera kwa familia yake hawezi kuruhusu nafsi yake kuwa na jicho (kuangalia) familia za wengine. [17] Kuhusiana na hili imetumiwa kama hoja hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s) inayosema: (ما زنیٰ غیورٌ قطُّ ; Mwenye ghera katu hazini). [18]
  • Kuzuia ufisadi: Kwa kiwango kile kile ambacho kutokuwa na ghera na mtu kutokuwa na tofauti kwake kwa matukio yanayojiri ndivyo kunavyoandaa uwanja wa mambo machafu na ufisadi; kuwa na ghera na unyeti maalumu mbele ya mambo ya munkari (yaliyokatazwa kufanywa) kuna nafasi muhimu katika kuzuia ufisadi na mambo machafu na yasiyofaa.
  • Uthabiti wa familia: Kuwa na ghera na kujipamba kwa sifa hii kunapelekea kupatikana uthabiti na uimara katika familia; kwa sababu mabinti na wanawake huwa na amani na usalama kutokana na jamii kuwa wanaume wenye ghera na ambao hawaruhusu watu wenye tamaa zisizo na mipaka ya kisheria, wenye kutaka kufanya ufuska na ambao dhati zao ni chafu kuwaudhi wanawake wenye heshima na utakaso na ambao wenye kujisitiri na kujiheshimu. [20]


Kuchupa mipaka katika ghera

Kumenukuliwa hadithi kutoka kwa Maasumina ambazo zinakataza ghera isiyo ya mahali pake, dhana mbaya na visingizio visivyo na maana vya mwanaume kuhusiana na mwanamke; hii ni kwa sababu haya ni mambo ambayo huwa na matokeo ya kinyume na yenyewe hupelekea ufisadi. [21] Kuhusiana na hili zimetumiwa kama hoja ibara zilizoko katika barua ya Imam Ali (a.s) kwa mwanawe Imam Hassan (a.s); jiepushe na kuwa na ghera katika sehemu ambayo si sahihi, kwani ghera isiyo ya mahali pake inawasukuma wanawake wasafi na watakasifu katika madhambi na mambo machafu. [22]

Kadhalika kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) kumekatazwa kufanya ghera katika jambo la halali; (لا غیرة فی الحلال ; Hakuna ghera katika halali). [23]


Monografia

Kumeandikwa vitabu vinavyozungumzia maudhui hii; miongoni mwavyo ni:

  • Gohar Gherat, mwandishi: Fatma A’zami.
  • Maghame gherat dar akhlaq va erfan eslami, mwandishi: Ali Akbar Iftikharfar.
  • Gherat dar maktabat etrat, mwandishi: Farid Najafniya.
  • Gherat Hosseini va effat Zainabi, mwadishi: Hassan Vakili.
  • Rabiteh Gherat dini ba amr be maaruf va nahi az monkar, mwandishi: Reza Ali Karami.


Vyanzo

  • Akbari, Mahmud, Ghairatmandi wa Asibha, Qom,: Fityan, 1390 S
  • Burujerdi, Sayyied Muhammad Ibrahim, Tafsir Jami', Teheran: Intisharat Shadr, 1366 S.
  • Hurr Amuli, Muhammad bin Hassan, Wasail al-Shiah, Qom: Ali al-Bait, 1414 H.
  • Jazairi, Muhammad Ali, Durus Akhlak Islami, Qom: Markaz Mudiriyat-e Hauzeh-e Ilmiah, 1388 S.
  • Kulaini, Muhammad bin Ya'qub, Al-Kafi. Beirut: cet. Ali Akbar Ghiffari, 1401 H.
  • Makarim Shirazi, Nashir, Akhlak Dar Quran, Qom: Madrasah al-Imam Ali bin Abi Thalib as, 1387 S.
  • Nahjul Balaghah, Penyunting: Shubhi Shaleh, Beirut: Dar al-Kitab al-Lub nani, 1980 M.
  • Nahjul Fashahah, Sukhanan-e Payambar, Abu al-Qasemi Paindah, Riset: Abdul Rasul Paimani dan Muhammad dan Amin Shariati, Isfahan: Khatam al-Anbiya, 1383 S.
  • Naraqi, Ahmad, Mi'raj al-Sa'adah, Qom: Hijrat, 1377 S.
  • Naraqi, Mahdi bin Abi Dzar, 'Ilm-e Akhlaq-e Eslami, diterjemahkan dari Jami' al-Sa'adat, penerjemah: Jalaluddin Mujtabawi, Teheran: 1381 S.
  • Nuri, Mirza Hussein. Mustadrak al-Wasail, Beirut: Muassasah Ali al-Bait li al-Ihya al-Turath, 1408 H
  • Tabataba'i, Sayyied Muhammad Hussein. Al-Mizan fi Tafsir al-Quran, penerjemah: Muhammad Bagir Musawi, Qom: Daftar Nasr-e Eslami, 1374 S.